ICC nyumba ya wachochea vurugu

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania, Bahame Nyanduga (katikati) akizundua Ilani ya Uchaguzi. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendani wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Hellen Bisimba. Kulia ni Mratibu wa Mtandao wa Watetea Haki za Binadamu, Onesmo Ngurumwa
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania, Bahame Nyanduga (katikati) akizundua Ilani ya Uchaguzi. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendani wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Hellen Bisimba. Kulia ni Mratibu wa Mtandao wa Watetea Haki za Binadamu, Onesmo Ngurumwa

WAKATI kampeni za uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 zimetimiza wiki tatu, kumeshajitokeza dalili za kukiukwa misingi ya usawa inayoweza kuleta uvunjifu wa amani. Tayari yameshuhudiwa matukio ya matumizi ya lugha zisizo na staha katika kampeni zinazoendelea za kunadi wagombea wa urais, ubunge na madiwani na ilani za uchaguzi za vyama vinavyoshiriki.

Lugha chafu zinazotolewa na wanasiasa mbalimbali, ni viashiria vinavyoweza kuwa chanzo cha vurugu.

Mwenendo huo umeanza kutia hofu wananchi. Wachambuzi na watetezi wa haki za binadamu wameanza kutaharuki, kwa kufikiria kwamba itakuaje iwapo tume zinazosimamia uchaguzi (Tume ya Taifa na ya Zanzibar) hazitachukua hatua haraka kukomesha matukio haya.

Kwa mfano, Juni 22, mwaka huu, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye akiwa jukwaani alisema, “kwa namna yoyote ile, CCM itarudi Ikulu hata kama ni kwa bao la mkono… bao ni bao tu ili mradi refa hajaona.”

Neno “bao la mkono” hutumiwa kama goli lililofungwa kinyume na taratibu za mpira wa miguu kwa kuupiga mpira kwa mkono kinyume cha sheria ya mchezo huu. Lakini goli hilo linaweza kukubalika iwapo mwamuzi wa mchezo hakuona wakati linafungwa au kama alikula mlungula ili kubeba upande mmoja.

Nape alitoa kauli hiyo wakati akihutubia mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Nyehunge, jimbo la Buchosa.

Aidha, tarehe 4 Agosti, mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete akiwa anazungumza kwa nafasi yake ya Mwenyekiti wa CCM taifa, alisema, “Wale wanaodhani CCM ni ya mchezo watakiona cha mtemakuni.”

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo wakati akihutubia wananchi eneo la ofisi ndogo za CCM zilizopo Lumumba jijini Dar es Salaam akimpokea mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Dk. John Magufuli.

Dk. Magufuli alipokewa kwenye uwanja wa barabarani Lumbumba, wakati akitokea Makao Makuu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo.

Mbali na kauli hiyo, pia vipo vitendo vinavyoashiria kuvunjwa amani wakati huu taifa likikabiliwa na uchaguzi mkuu.

Kwa mfano, tarehe 2 Septemba, mgombea ubunge jimbo la Ubungo kwa tiketi ya CCM, Didas Masaburi alituhumiwa kuwashawishi vijana zaidi ya 100 kuandamana katika eneo la Moroco, Dar es Salaam.

Lengo la maandamano hayo linatajwa kuwa ni kushinikiza kurudi kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dk. Willibrod Slaa katika nafasi yake baada ya kujiuzulu, hatua ya kupinga kukaribishwa chama aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kuwania urais akiwakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Hata hivyo Masaburi alikana tuhuma hizo ingawa katika maelezo yake yaliyosambazwa mitandaoni, alikiri kukutana na vijana hao na kuwaunga mkono baada ya kupata maelezo yao.

Tarehe 28 Agosti, mgombea urais kupitia CCM, Dk. John Magufuli akihutubia wakazi wa Mbalizi, mkoani Mbeya alisema, “Msitoe hukumu ya jumla. Zipo nchi zilifanya hivyo zilijuta. Libya ya Gaddafi ilikuwa ukioa unapewa nyumba, unatafutiwa mtaji, elimu na umeme bure, lakini wananchi walichoka raha… wakasema wanaondoka lakini wale vijana waliosema wanataka raha na wale vijana waliosema wanataka ukombozi wa haraka ndio wa kwanza kuvuka bahari kwenda Ulaya.”

Septemba 10, saa 9. 30 alasiri mfuasi wa Chadema, Mwita Bhoke Waitei aliuawa kwa kukatwa mapanga huku Mgesi Bhoke Waitei na Samwel Bali wakijeruhiwa baada ya kuvamiwa na wafuasi walioamini ni wana-CCM.

Mwita aliuliwa kijijini Kegonga, Kata ya Nyanungu, mkoani Mara, baada ya wahuni kuvamia msafara wa mgombea ubunge jimbo la Tarime Vijijini, John Heche na mgombea udiwani Kata hiyo, Mangenyi Ryoba Masiaga.

Ni viashiria vinavyomsukuma Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania, Bahame Nyanduga kuonya kwamba mtu yeyote, awe mpigakura au mwanasiasa mgombea kura na wapambe wake, akibainika kupanga vurugu na kuvunja sheria na baada ya uchaguzi ikabainika kuwa chanzo cha ghasia kubwa wakati na baada ya uchaguzi, atastahili kushitakiwa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC).

Nyanduga hata kabla ya tukio la Tarime Vijijini, alikuwa ameshatoa onyo hilo kwenye ukumbi wa Millenium Tower, Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Ilani ya Uchaguzi ya Asasi za Kiraia (AZAKI).

Anajua Tanzania ni mwanachama wa Mkataba wa Roma ulioanzisha ICC kupitia mwamvuli wa Umoja wa Mataifa. Ieleweke vema yakitokea makosa yanayotajwa na mkataba huo wakati au baada ya uchaguzi, wale watakaothibitika kuhusika kuyatekeleza au kuyapanga, watashikwa na kushitakiwa katika mahakama hiyo.

“Tume inapenda kutoa tahadhari kuhusu kauli ambazo zina viashiria, au vinaweza vikawa vyanzo vya uvunjifu wa amani, zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa kama vile kusema tukiibiwa kura patachimbika, ushindi ni lazima, serikali haitolewi kwa vikaratasi, goli la mkono, au ushindi saa nne asubuhi. Kauli kama hizi zinajenga hisia ambazo zinaweza kudhoofisha utaratibu wa kampeni na uchaguzi wenyewe,” anasema Nyanduga.

Anataja viashiria vingine kuwa ni kuwepo kwa vikundi vya ulinzi vya ndani ya vyama vya siasa.

Uzoefu unaonesha katika nchi mbalimbali vikundi kama hivyo vimekuwa chanzo cha vurugu na kuvunjwa haki za binadamu, hasa baada ya uchaguzi mkuu kumalizika, bila ya kuwepo uwazi na haki.

Vikundi hivi, kwa mujibu wa sheria, haviwajibiki kwa mtu yeyote isipokuwa vinalinda maslahi ya vyama.

“Kwa nafasi yangu kama mwanasheria niliyehusika katika kesi inayohusu mauaji ya halaiki ya nchini Rwanda katika Mahakama ya Mauaji ya Kimbari nchini Rwanda (ICTR) jijini Arusha, na nimekuwa mdau wa masuala ya ICC, napenda kutoa indhari kwamba viongozi wote watakaochochea vurugu, wawe ndani au nje ya serikali, raia wa kawaida au waandishi wa habari, watachukuliwa hatua.

“Wale watakaodhihirika kutumia lugha za uchochezi ama kushiriki kupanga vurugu na uvunjifu wa haki za binadamu, kwa kiwango kitakachoilazimu ICC kuchunguza makosa hayo hapa Tanzania, waweza kufikishwa mbele ya mahakama ya ICC,” amesema Nyanduga.

Katika kuhakikisha haki inatendeka wakati wa uchaguzi mkuu, Nyanduga amehimiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kuhakikisha taratibu za uchaguzi zinaendeshwa kwa uwazi, haki, kwa misingi ya sheria na pia wasimamizi wa uchaguzi wasijaribu kuingiza ushabiki wala hisia binafsi.

Chanzo: Mawio

 

 

Leave a comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.