Taarifa ya hatua za mchakato wa uuzaji wa meli 3 za Serikali

  • UTANGULIZI

Shirika la Meli ni Taasisi ya umma inayomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa asilimia mia moja. Shirika lilianzishwa upya  kwa Sheria nambari 3 ya mwaka 2013 ambayo pamoja na mambo mengine lilipewa jukumu la kusimamia, kutunza na kuendesha Meli za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Hadi hivi sasa, Serikali kupitia Shirika la Meli inamiliki Meli tano (5), MV Maendeleo, MT Ukombozi, MV Mapinduzi II, MT Ukombozi II na Meli ya Jitihada.

  • MV MAENDELEO

Meli ya MV Maendeleo ni Meli ya Abiria na Mizigo. Meli hii ina urefu wa mita 77.5 na upana wa mita 12.2 na ilijengwa mwaka 1980 nchini Japan. Meli hii ina uwezo wa kubeba abiria 600 na  mizigo tani 690 hivyo, imeshatoa huduma ya usafirishaji kwa zaidi ya miaka 30.

  • Kuharibika na matengenezo ya Meli ya MV Maendeleo.

Meli ya MV Maendeleo ilisita kufanya kazi mwaka 2016 kutokana na uchakavu na hitilafu katika sehemu mbali mbali. Kutokana na hali hiyo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilifanya maamuzi ya kuiuza meli hiyo mwaka 2016. Hata hivyo, Mzabuni aliyeshinda Zabuni ya ununuzi wa meli hiyo, alishindwa kulipa fedha za uuzwaji wa Meli hiyo ambayo ilikuwa USD 500,000. Baada ya hatua hiyo, Serikali iliamua kuifanyia matengenezo makubwa meli hiyo kwa kuipeleka Mombasa nchini Kenya  mwaka 2019 kwa ajili ya matengenezo makubwa.

Kutokana na changamoto mbali mbali ikiwemo changamoto ya kifedha na maradhi ya UVIKO, meli hiyo ilikaa muda mrefu nchini Kenya hali iliyopelekea kuzidi kupoteza thamani kwa Meli hiyo kwa kuendelea kuzidi  kuharibika. 

  • MV MAPINDUZI II

MV Mapinduzi II ni Meli ya abiria na mizigo. Meli hii ina ukubwa wa GRT 5,464, urefu mita 90 na upana mita 17. Meli ina uwezo wa kuchukua abiria 1,200 na mizigo tani 200. Meli hii ilijengwa nchini Korea ya Kusini na Kampuni ya Daewoo International na Kampuni ya Posco Plantec Co. Ltd. Meli hii ilijengwa kwa gharama za USD 30.5 milioni ambapo Ujenzi wa Meli hii ulianza mnamo Julai, 2013 na kukamilika Disemba, 2015 ambapo ilianza kufanyakazi rasmi Januari, 2016. Gharama zote za ujenzi  ziligharimiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Katika kipindi cha miaka sita (2015/2016-2020/2021), MV Mapinduzi II imepata hitilafu za kiufundi na kufanyiwa matengenezo  makubwa mara tano na kusababisha kutumika kwa Fedha nyingi sana kwa ajili ya matengenezo hayo ya mara kwa mara.

  • MT UKOMBOZI

MT Ukombozi  ni meli ya kusafirishia  mafuta kama vile Petroli, Mafuta ya Taa, Diseli na Mafuta ya ndege (Jet A1). Meli hii imeundwa mwaka 1980 nchini Japan na uwezo wa kusafirisha tani 2,300. Meli ina urefu wa mita 74.5 na upana wa mita 12 na ina GRT 1403. Meli ina tabaka moja (Single Hull).

Kutokana na kuwa na umri mrefu, Meli hii imekuwa ikihitaji Vipuri mara kwa mara, aidha Meli hii tayari inaonekana imepoteza sifa kitaifa na kimataifa ya kufanya kazi kutokana na maumbile yake (Single hull).

  • HATUA ZA UTEKELEZAJI WA UUZAJI WA MELI TATU ZA SERIKALI

Mnamo tarehe 5 Mei 2022, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Shirika la Meli  ilitangaza rasmin  Zabuni ya  Uuzwaji wa Meli tatu za Serikali ambazo ni MV Maendeleo, MV Mapinduzi II na MT Ukombozi. Kabla ya kutangaza Zabuni hiyo, meli hizo zilizofanyiwa tathmini na Mthamini Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya Ocean Maritime Services ya Zanzibar kwa gharama ya 28,301,500.

Matangazo ya Zabuni yalitolewa katika vyombo vifuatavyo;

  1. Redio Zanzibar
  2. Televisheni ya Zanzibar
  3. Tovuti ya Shirika la Meli na Tovuti ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano  na Uchukuzi.
  4. Gazeti la Zanzibar Leo
  5. Gazeti la Daily News
  6. Gazeti la Guardian
  7. Gazeti la East Africa  

Jumla ya Kampuni 14 zilijitokeza kununua Zabuni hizo.  Hadi kufika tarehe 15 Juni ambayo ni  siku ya Mwisho ya kurejesha Zabuni hizo, jumla ya Kampuni   10  zilifanikiwa kurejesha Zabuni zao.

Muhtasari wa Zabuni zilizorejeshwa pamoja na mapendekezo ya gharama za bei walizoweka inaonekana kwenye Jadweli hapo chini.

 LOT 1: MV MAENDELEO

NamJINA LA KAMPUNIBEI ELEKEZI USDBEI YA MZABUNI USDASILIMIA
1SAFELINE WORKS LTD. P.O.BOX 32284 DSM296,000230,00077%
2TUDOR LEADS ENTERPRISE P.O.BOX 87704-80100 MOMBASA KENYA296,000199,00067%
3LOFTY SERVICES CO. LTD P.O.BOX 53734-00200 NAIROBI296,000190,68964%
4MARINE STEEL LIMITED P.O.BOX296,000153,39651%

LOT 2: MV MAPINDUZI II

NamJINA LA KAMPUNIBEI ELEKEZI USDBEI YA MZABUNI USDASILIMIA
1HONG YU STEEL COMPANY LTD14,044,800802,6545.7%
2LOFTY SERVICES CO. LTD P.O.BOX 53734-00200 NAIROBI14,044,800514,7013.6%
3MARINE STEEL LIMITED P.O.BOX    KENYA14,044,800400,5342.8%

LOT 3: MT UKOMBOZI

NaJINA LA KAMPUNIBEI ELEKEZI USDBEI YA MZABUNI USDASILIMIA
1NABZUZ MARINE266,400251,00094%
2SAFELINE WORKS LTD. P.O.BOX 32284 DSM266,400175,00065%
3ISLAND MASH CO.LTD P.O.BOX 3667 ZANZIBAR266,400160,00060%
4LOFTY SERVICES CO. LTD P.O.BOX 53734-00200 NAIROBI266,400158,69959%
5IVASSA INVESTIMATE LTD P.O.BOX 31276  DSM266,400155,00058%
6MARINE STEEL LIMITED P.O.BOX 50049-00200  NAIROBI KENYA266,400127,83045%
7SILVER STAR IMPORT AND EXPORT P.O.BOX 75821 DSM266,400104,00039%
8UNITED MARINE SERVICES P.O.BOX 1600 ZANZIBAR266,40050,00018%

Kupitia takwimu hizo za fedha, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeamua kuuza Meli ya MT Ukombozi kwa Kampuni ya NABZUZ MARINE ya Zanzibar kwa kiwango cha Dola za Kimarekeni 251,000 na Meli ya MV Maendeleo kwa Kampuni ya  SAFELINE WORKS LTD ya Dar es Salaam  Dola za Kimarekeni 230,000.

Kwa upande waMeli ya MV Mapinduzi II,Serikali iliagiza kuangaliauwezekano wa kufanya mambo matatu ikiwemo; kuingia Ubia na Kampuni Binafsi (PPP), kukodisha au Kuiuza. Baada ya michakato miwili ya kuingia ubia na Kampuni binafsi na kuikodisha meli ya MV Mapinduzi II kushindikana, Serikali iliingia katika mchakato wa 3 kuiuza meli hiyo. Hata hivyo, kutokana na kiwango kidogo sana cha fedha za ununuzi zilizowasilishwa na Wazabuni, Serikali imeamua kuifanyia matengenezo makubwa Meli hiyo ili iweze kufanya kazi ya kusafirisha abiria na mizigo katika Visiwa vya Zanzibar na mwambao wa Afrika Mashariki.

Katika harakati za kufanya matengenezo ya Meli hiyo ya MV Mapinduzi II, Uongozi wa Shirika la Meli Zanzibar umeshafanya Mawasiliano na Kampuni mbali mbali zinazojihusisha na Mambo ya Meli ikiwemo Kampuni ya Kyros Engineering inayopatikana nchini India na Dubai pamoja na Kampuni ya SYNERGY ya Goa, India ambayo inamiliki Chelezo cha utengenezaji wa meli (shipyard). Aidha, Shirika limewasiliana na Kampuni ya MAN ya Ujerumani kuhusu uwezekano wa kubadilisha mashine za MV Mapinduzi II.

NOTE

  1. Meli ya MV Maendeleo ina jumla ya deni la dola za Kimarekani 525,766 kwa Kampuni ya African Marine na dola 71,107 kwa Kampuni ya Green Island ambayo ni wakala wa meli za Shirika nchini Kenya. Kwa sasa Shirika linatozwa USD 100 kwa siku kwa ulinzi na  umeme (shore power) katika meli hiyo. Kwa upande wa uwakala, Shirika linatozwa dola 100 kwa siku. Hivyo, Shirika linapata gharama ya dola za Kimarekani 200 kwa siku.
  2. Meli ya MV maendeleo imeshatumia jumla ya USD 1,198,124 ikiwa ni gharama za utengenezaji wa meli hiyo. Aidha, Shirika limetumia jumla ya USD 277,244 kwa huduma za uwakala wa meli hiyo kupitia Kampuni ya Green Island Shipping ya Mombasa nchini Kenya.
  3. Kwa hivi sasa, meli hiyo ina jumla ya wafanyakazi wawili ambao wanailinda meli hiyo.

Leave a comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.