Samia aapishwa kuwa Rais

SAMIA AANDIKA HISTORIA MPYA TANZANIA

AMEKUWA MAKAMO WA RAIS WA KWANZA MWANAMKE NA RAIS WA KWANZA MWANAMKE TANZANIA

WENGI WAELEZA MATUMAONI YAO KWAKE, WASEMA HODARI, JASIRI NA MCHAPAKAZI

Samia Suluhu Hassan ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyeanzia kukamata wadhifa huo 2015 sasa ameapishwa rasmi na kuwa mrithi wa Rais John Magufuli ambaye amefariki dunia jana Jumatano Machi 17,2021 hapa Tanzania.

Samia ameweka rekodi ya kuwa Mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo wa juu zaidi nchini Tanzania tokea nchi hii kupata uhuru wake kama ambavyo ameshika nafasi hiyo ya Makamu wa kwanza wa Rais Tanzania kuwa wa kwanza.

Samia anatarajiwa kushikilia wadhifa huo kwa kipindi kilichosalia cha muhula wa urais mpaka 2025, kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano Tanzania kama inavyosomeka katika kifungu cha 37 (5).

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kifungu cha 37 (5) inasomeka kwamba “Endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kutokana na Rais kufariki dunia, kujiuzulu kupoteza sifa za uchaguzi au maradhi ya mwili au kushindwa kutekeleza kazi na shughuli za Rais, basi Makamu wa Rais ataapishwa na atakuwa Rais kwa muda uliobaki katika kipindi cha miaka mitano. na kwa masharti yalioelezwa katika ibara ya 40, kisha baada ya kushauriana na chama cha siasa anachotoka Rais atapendekeza jina la mtu atakayekuwa Makamu wa Rais na uteuzi huo utathibitishwa na Bunge kwa kura zisizopungua asilimia hamsini za wabunge wote”.

Samia amekuwa ni Rais wa pili wa Tanzania kutokea katika visiwa vya  Zanzibar, wa kwanza akiwa Mzee Ali Hassan Mwinyi aliyeliongoza taifa hilo la Tanzania kwa miaka 10 kutoka mwaka 1985 mpaka 1995 ambapo pamoja na changamoto nyingi alizokutana nazo lakini aliamaliza muda wake akiacha nchi ikiwa na na amani na uchumi wa wastani na kupewa jina la “Mzee Rukhsa” kutokana na kufungua milango ya biashara nchini.

John Pombe Magufuli ni Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufariki akiwa madarakani kabla ya muda wake kumalizika kikatiba. Mwengine aliyefariki akiwa madarakani ni aliyekuwa Rais wa Zanzibar Abeid Amani Karume alifariki akiwa madarakani baada ya kuuwawa wakati akicheza Zumna katika Afisi kuu ya Cham Cha (ASP) Kisiwandui Zanzibar mwaka 1972 ingawa hakuwa na kikomo cha uongozi wake.

Aidha Makamo wa kwanza kufariki kabla ya kumaliza muda kwa upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Dk Omar Ali Juma naye alifariki kabla ya kumaliza muda wake wa utumishi wa wadhifa hayo mnamo Julay 4 mwaka 2001.

Katika safari yake ya mafanikio kwenye moja ya maelezo yake ambayo amewahi kunukuliwa Samia amewahi kusema safari yake ya kufikia mafanikio haikuwa rahisi na nyepesi alipita kwenye milima na mabonde hadi kufikia hapo alipofikia leo, subira na uvumilivu na kukubali ushauri na maelekezo ndio sababu ya mafanikio yake huku akimtanguliza Mwenyeenzi Mungu katika kila hatua ya maisha yake.

”Safari yangu katika siasa imekuwa njia ndefu na yenye tija. Sio rahisi kuwajibikia familia yako wakati huo huo ukiendelea na maisha ya siasa elimu na majukumu mengine ya kikazi,” anasema Samia.

Leo wakati alipomaliza kula kiapo cha kuiongoza nchi ya Tanzania Samia aliongea na hadhira iliyokuwa mbele yake wakiwemo viongozi mbali mbali ya Zanzibar na Tanzania huku akiwaomba kumuunga mkono katika jukumu kubwa la kiuongozi ambalo analokwenda kulikabili wakati ambao anachukua jukumu hilo akiwa na machungu na wimbi kubwa la huzuni kufuatia kifo cha mtangulizi wake John Magufuli ambaye mwili umehifadhiwa ukisubiri kuangwa na kuzikwa “Nina maumivu makubwa kwa kuondokewa na Rais wetu mpendwa” alisema Samia.

Hata hivyo katika hutuba yake alisema huu ni wakati wa watanzania kuungana na sio wakati wa kunyoosheana vidole na ni wakati wa kurejesha nchi katika utulivu na masikilizano pamoja na kurejesha mahusiano mema kwa kila mtanzania.

Bi Samia Suluhu Hassan alizaliwa Januari 27, 1960 Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja Zanzibar. Alisomea shule za msingi za Chawaka (Unguja), Ziwani (Pemba) na Mahonda (Unguja) kati ya 1966 na 1972 na kisha akasomea masomo ya upili Ngambo, Unguja (1973-1975) na Lumumba, Unguja (1976).

Lakini baadae akajiendeleza na kusomea kozi mbalimbali hadi akafikia kupata shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Southern New Hampshire nchini Marekani. ni mhitimu pia wa Chuo Kikuu cha Mzumbe alikosomea masuala ya utawala na baadae kurudi Zanzibar na kufanya kazi sehemu tofauti.

Ajira yake ya mwanzo Samia aliajiriwa kwenye kiwanda cha uchapishaji akiwa mchapishaji katika ofisi ya serikali ya Zanzibar mwaka 1977 wakatib huo akiwa kijana mdogo na akaanza safari yake ya utumishi hatua baada ya hatua polepole na baadae mnamo mwaka 1987 na 1988 akawa afisa wa mipango serikalini.

Samia aliwahi kuwa Meneja wa Mradi wa Shirika la Chakula Duniani (WFP) Zanzibar kati ya 1985 na 1997, na pia kama Mkurugenzi wa Mwamvuli wa NGOs (ANGOZA) 1998 hadi 1999 akifanya kazi na wanaharakati wengine katika masuala ya kijamii.

Mnamo 2000 Samia alijiunga na siasa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiwa Zanzibar na akateuliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitia viti vya nafasi za wanawake na baadae akateuliwa kuwa waziri Wanawake na Watoto wadhifa uliokuwa ukiongozwa na Bi Asha Bakari (Marehemu) chini ya utawala wa Amani Abeid Karume akiwa Rais wa Zanzibar mwaka 2000 hadi 2005.

Omar Dadi Shajak aliwahi kuwa Katibu Mkuu katika WIzara ya Vijana, Ajira, Maendeleo ya Wanawake na Watoto kati ya mwaka 2000-2005 akiongozwa na waziri wake wa wakati huo Samia Suluhu Hassan.

Shajak ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa wizara ya Afya anasema kufanya kazi na Samia kunaleta faraja kwa kuwa ni mtu anayejituma na kujiamini na anayependa kuona anachokifanya kinatoa matunda na tija katika kazi.

“Ni mtu hodari sana na anayejiamini na anaheshimu maoni ya watu wote bila ya kujali mkubwa na mdogo anayetoa mawazo, msikivu na mwenye hekima kubwa katika kazi” alimuelezea Shajak

Mambo yanayohusu sera alikuwa anasikiliza halafu anatekeleza sifa yake kubwa ana uwezo wa kusikiliza kwanza kabla ya kutoa uamuzi.

Changamoto ukitaka kuichukulia kama ni fursa basi ataweza kukabiliana na changamoto zote ambazo amezipotia

Shajak amesema hakuna anajali wakati bali akijali zaidi kazi na kufanikisha. “ Mimi naungana na wote wanaosema Samia ni mama mkakamavu”.

Mwaka 2005 pia Samia aliteuliwa tena kwa kipindi cha mara ya pili cha utawala wa Amani Karume na akateuliwa tena kuwa Waziri wa Biashara, Viwanda na Utalii Zanzibar na hapo alifanya kazi kwa karibu na jumuiya za wafanyabiashara.

Watu ambao amefanya nao kazi wanamzungumzia Rais Samia kuwa ni mchapakazi, msikivu, mwenye tabia ya kuheshimu maamuzi yanayotokana na vikao na mtoaji maamuzi yasioumiza kutokana na kutumia busara zaidi kwenye uamuzi wake. Professa Mohammed Hafidh Khalfan alikuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Wafanyakazi wa Jumuiya ya wafanyabishara wenye viwanda na wakulima (ZNCCIA).

“Tunamfahamu alipokuwa waziri tulifanya naye kazi vizuri ni muadilifu na mchango wake mkubwa na mchango wake mkubwa kwenye sekta binafsi na alileta mabadiliko makubwa” alisema Professa Hafidh.

Professa Hafidh amesema Samia sio mtu wa kujikwenda wala kujivuna na popote anapokuona anatambua uwepo wako huku akitoa mfano wakati mmoja alipokuwa kwneye maonesho ya sabasaba jijini Dar es salaam ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Samia akiwa makamo wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Tulikuwa tumekaa na mimi kama nimejificha ili nisionekane lakini bahati akaniona na akataja kwa jina kwenye speech yake kuonesha kuutambua uwepo wetu na bahati nzuri baada ya kututaja tukawekwa mpaka kwenye ratiba wakati hatukuwemona pia tukapewa nafasi kutoa neon la shukrani yote ni kutambua ujumbe kutoka Zanzibar” alisema Professa Hafidh.

Baada ya kupata uzoefu wa kutosha kwenye siasa Samia akaamua kwenda jimboni kuwania nafasi ya Ubunge katika jimbo la Makunduchi baada ya kumaliza muda wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Abdusalam Issa Khatib  

Mnamo mwaka wa 2010 alichaguliwa kuwa mwakilishi wa jimbo hilo la Makunduchi ambapo akateuliwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuwa waziri wa maswala ya Muungano katika serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipofanya kazi na Makamu wa Rais Mohammed Gharib Bilal ambaye kwa sasa amepumzika.

Mnamo mwaka 2014, aliwania na kuchaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa Bunge maalum la Katiba mjini Dodoma alichaguliwa kwa kura 390 sawa na asilimia 74.6 na kumshinda mpinzani wake Bi Amina Abdalla Amour (Marehemu) ambaye alipata kura 126 sawa na 24%.

Kutokana na kuliendesha Bunge la Katiba kwa ufanisi na kufanikiwa kusimamia kanuni na utaratibu wa bunge wengi walianza kumtabiria makubwa kuanzia hapo.

Hatimae Julai mwaka 2015, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Pombe Magufuli alimteua kuwa mgombea mwenza katika kipindi chake cha miaka mitano 2005-2010 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano akimsaidia kazi Rais Magufuli ambapo aliwahi kumsifia namna anavyompa mashirikiano aktika jukumu lake la kuwatumia wananchi wa Tanzania.

 

Kwa upande wake Kauthar Khalfan amesema furaha yake ni kuwa Rais mwanamke ameapishwa jambo ambalo hajawahi kuliona tokea kuzaliwa kwake kwa nchi ya Tanzania huku akiamini kwa kuwa Rais ni mwanamke atasaidia kwa kiasi kikubwa shida na matatizo ya wanawake ambayo yanawakabili.

“Ni jambo geni kwetu tumeshangaa kutokana na utaratibu wetu wa marais wanaume tu, lakini naamini kupewa yeye urais basi atazingatia shida nyingi za wanawake zinazowakabili na naamini atazifanyia kazi” alijiaminisha Kauthar

Nikolas Clemency maoni yake Samia ni kiongozi imara na shupavu na kwa Tanzania imepata kiongozi mzuri mwanamke ambaye ana uwezo wa kuongoza na kutoa matumaini kwa wananchi watanzania.

“Muhimu Mama Samia aungwe mkono na kila mtanzania ili kumsaidia katika utekelezaji wa kazi na majukumu yake” amesema Nicolas.

Akitoa maoni yake Abdul Mtulya ni mchambuzi wa masuala mbali mbali akihojiwa na Sauti ya Ujerumani (DW) alisema anapendelea kumuona Samia akiongoza kwa kuendeleza pale alipoachia John Pombe Magufuli.

Lakini anapendelea kuona Samia akiongoza kwa kurejesha mahusiano mazuri na mataifa mengine na kuzingatia suala afya za wananchi kwa kukabiliana na jenga la Corona lakini pia alimpigia mfano kama Canceller wa Ujerumani Angella Michael aliingia madarakani huku baadhi ya wananchi wakiwa na shaka naye juu ya uwezo wake wa kuongoza taifa hilo la Ujerumani lakini wananchi baadae waliona namna ya uongozi huo na khofu yao ikamaliza kutokana na uwezo mkubwa wa kuingoza nchi hiyo ambapo kwa kiasi kikubwa kuongoza taifa hilo kubwa tajiri katika bara la ulaya.

Samia ni mtoto wa tatu kuzaliwa kati ya watoto saba khalisa (Mama mmoja Baba mmoja) kutoka katika familia ya Baba yake Suluhu Hassan (Marehemu) na Mama Mwanamvua Yussuf (Marehemu).

Mwaka 1978 Samia alifunga ndoa na Bwana, Hafidh Ameir, katika maisha yao ya ndoa wamejaliwa kupata watoto wanne watatu wa kiume na mtoto mmoja wa kike ambaye naye ameingia kwenye siasa na sasa ni Mbunge wa kuteuliwa kupitia nafasi za wanawake kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) aitwaye Wanu. Watoto wake wengine ni Ameir aliyepewa jina la abu yake na Abdul na Ahmed ambaye ni mtoto wake wa mwisho.

Wanu ni mtoto wa pekee wa kile na ni wa pili kuzaliwa na Rais Samia na yeye kama Mama yake alivyokuwa kwenye siasa naye amejiunga na siasa kama Mama yake na aliteuliwa kupitia viti maalumu vya wanawake katika kipindi cha miaka mitano ndnai ya Baraza la Wawakilishi mwaka 2010-2015. na baadae mwaka 2020 ameingia kwa mara nyengine katika kinyanganyiro hicho na kukumbana na mchuano mkali wa wanawake wenzake ambao mara hii muamko mlikuwa mkali wa nafasi za wanawake kuwania nafasi za uongozi.