Raza awapaka mawaziri wa SMT

Mohammed Raza Hassanali, mwakilishi wa Uzini
Mohammed Raza Hassanali, mwakilishi wa Uzini

Katika hali ambayo Wazanzibari wamechoka nayo kuona wanaamuliwa mambo na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania badala ya kupanga pamoja kama nchi mbili huru zilizoungana kwa  hiari.

Akizungumza katika semina iliyofanyika kwenye ukumbi wa baraza la wawakilishi Chukwani Zanzibar. Raza alisema Zanzibar sio ya kupewa taarifa bali ya kukaa pamoja na Tanzania bara na kuamua kwa pamoja.

Semina hiyo ambayo mjadala wake haukuzidi nusu saa na  ambayo iliitishwa ghafla na mawaziri wawili waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais Muungano Bi.Samia Suluhu Hassanna Naibu Waziri wa Fedha Adam Kighoma Malima kuja kutoa taarifa kuhusiana na hatua ya Tanzania kusaini itifaki ya kujiunga na umoja wa sarafu wa Afrika Mashariki.

Raza aliwa-challenge kwamba kwa nini waje watoe “taarifa” tu kwa suala kubwa kama hilo? Nini nafasi ya Zanzibar? Akasema kwamba Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi zote ni nchi moja hivyo zinaweza kujiunga lakini Tanzania ni nchi mbili zilizo huru na sawa. Vipi Tanzania itajiunga bila ya ushirikishwaji mpana wa Zanzibar?

Akawaeleza kwamba Dkt. Salmin Amour akiwa Rais aliandika barua rasmi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, wakati huo Benjamin Mkapa kueleza msimamo wa Zanzibar kutaka ijiunge na Jumuiya ya Afrika Mashariki kama mwanachama peke yake. Akahoji vipi leo Zanzibar iburuzwe tu?

Akauliza iwapo suala hilo lilizungumzwa na Baraza la Mapinduzi au Baraza la Wawakilishi kupata msimamo tofauti na huo wa Zanzibar?

Mwisho, akawaambia kama wamekuja kutembea Zanzibar ni sawa lakini kama ni kutafuta ridhaa wasahau. Akasema yeye kama Raza anapinga na wananchi wa Zanzibar wanapinga suala hilo.

Katika kubabaika kujibu, Malima alisema kwamba mambo hayo hayataki jazba na kwamba yeye wakati wa kujadiliana kuhusu suala la mafuta na gesi, alimnasihi Mansoor awache lugha kali lakini hakumsikiliza na matokeo yake mpaka leo limekwama.

Hapo hapo Mwakilishi Hijja Hassan Hijja akasimama na kumtaka afute kauli yake na aombe radhi kwani suala la msimamo wa mafuta na gesi halikuwa la Mansoor binafsi. Akamwambia Mansoor alikuwa Waziri aliyetoa msimamo wa BLM na baadaye kupata ridhaa ya BLW kupitia Azimio lililopitishwa kwa kauli moja na wajumbe wote akiwemo Samia aliyekuwa mbele yao.

Adam Malima ikabidi afute kauli na aombe radhi. Mwisho, akasema kawasikia Wawakilishi na atafikisha msimamo waliompa kwa wakubwa zake.

Leave a comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.