Wanafunzi ni kosa kufanya kazi ugenini- SMZ

"<br

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema itawachukulia hatua wanafunzi wanaokwenda kusoma nje ya nchi kwa kulipiwa na serikali na kisha kufanya kazi katika nchi hizo kwa kwenda kinyume na sheria.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ali Juma Shamhuna bodi ya mikopo ya elimu ya juu ya Zanzibar ina wadhamini wanafunzi 161, wanaosoma katika vyuo mbali mbali vya nje ya nchi vikiwemo Uganda, China, Ukraine, Malaysia na nchi yengine.

Alisema wanafunzi hayo wanalipwa ada ya masomo, gharama za mitihani, chakula, usafiri na bima ya matibabu ambapo kwa mujibu wa viza zao za wanafunzi hawatastahiki kufanya kazi na kama kuna wanaofanya kazi basi watachukuliwa hatua za kushitakiwa na kuadhibiwa.

Majibu hayo ameyatoa Shamhuna katika kikao cha baraza la wawakilishi kinachoendelea Mjini Unguja alipokuwa akijibu suali la msingi la Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni (CCM) Jaku Hashim Ayoub, aliyetaka kujua ni hatua gani serikali inachukua kwa wanafunzi ambao wapo nje ya nchi na wana kilio cha muda mrefu cha kucheleweshewe fedha za masomo hali inayowalazimisha kufanya kazi za vibarua badala ya masomo.

Akimjibu Mwakilishi huyo, Shamhuna alikiri kuidhininishiwa na baraza la wawakilishi bajeti ya mikopo ya elimu ya juu ya shilingi billioni 8 kwa mwaka wa fedha wa 2012-2013, lakini kuidhinishwa kwa fedha hizo haimaanishi kwamba fedha hizo zinapatikana kwa wakati.

Alisema bodi ya mikopo ya elimu ya juu inafanya malipo ya walimu wote kwa kutegemea fedha zilizopatikana na kipaumbele wanapewa wanafunzi wanaosoma vyuo vya nje ya nchi.

Akitoa mfano Shamhuna alisema hadi mwezi machi 2013, bodi ya mikopo ya elimu ya juu imeshapokea jumla ya shilingi 4.3 billioni sawa na asilimia ya 53 ya fedha za bajeti.

Shamhuna alisema kwa kutumia fedha hizo wanafunzi wote wanaosoma katka vyuo vje wameshalipiwa ada ya masomo yao kwa mwaka wa na asilimia 75 ya malipo yao mengine yakiwemo gharama za malazi na chakula.

Malipo ambayo hawajalipiwa wanafunzi hao, Shamhuna alisema 2012-2013 ni malipo ya gharama ya chakula na malazi kwa robo mwaka ya mwisho, yaani kwa kipindi cha mwezi wa Aprili hadi Juni 2013.

alisema wizara inatoa kipaumbele kwa kufanya malipo ya ada ya vyuoni kwa wanafunzi waliopo nje ya nchi kwa kutambua kuwa wao wapo mbali na mara nyengine wanazuwiwa masomo kutokana na kuchelewa kulipa ada ya vyuo.

Alisema licha ya juhudi kubwa ya wizara ya elimu kwa kushirikiana na ofisi ya rais, wizara ya fedha ya kuingiziwa kwa wakati lakini dhahiri kwamba gharama za kusomesha wanafunzi nje ya nchi ni kubwa.

“Mfano mwanafunzi mmoja wa fani ya udaktari amesoma nchini china ameigharimu serikali dola za kimarekani milioni 56 kwa miaka sita, kiwango hicho ni kikubwa sana kwa mhitimu kumudu kukilipa atakapomaliza masomo na kufanya kazi na ndio maana serikikali imezuwia kusomesha wanafunzi kutoka nje ya nchi” alisema Shamhuna.

Alisema kwa fani zinazopatikana kutoka vyuo vya ndani ya nchi, pamoja na serikali kuendelea kuwagharamia wanafunzi waliopo nje ya nchi “napenda kutoa wito kwa wazazi na wanafunzi hao kuwahudumia watoto wao hasa kwa gharama za chakula na malazi pale fedha za serikikali zinapochelewa kupatikana, kwani wajibu wa kuwafundisha vijana wetu ni wetu sote” alisisitiza Shamhuna,.

Akijibu suali la nani wa kulaumiwa ka wanafunzi wa kike wanaocheleweshewa fedha zao, Shamhuna alisema kuchelewa kuwatumia fedha wanafunzi wanaosoma nje ya nchi sio kisingizio cha wanafunzi kufeli au kujiingiza katika mambo yasiofaa na atakayefanya hivyo atastahiki kulaumiwa mwenyewe na wala sio serikali.

Alisema wizara ya elimu wakati wote inafuatilia maendeleo ya wanafunzi ama kwa kuwatembelea au kuwatumia maafisa wa ofisi za wizara hiyo za kibalozi zilizopo nje ya nchi hizo. Ambapo taarifa zinzokuja kupitia vyombo vyao vya uhakika hakuna tabia hiyo ya kukosaq maadili na kujiingiza katika vitendo viovu hata kama fedha zinapochelewa kupelekwa vyuoni.

MWISHO

SMZ YAKIRI ATHARI ZA KIMAZINGIRA

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekiri kuathirika na tabia nchi duniani ambayo kwa kiasi fulani visiwa vya Zanzibar navyo vibakabiliwa na tishio la mmomonyomko wa radhi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Nchi Makamo wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdulhabib Ferej amesema hayo wakati akijibu swali la msingi la Mwakilishi wa Jimbo la Mtambwe (CUF) Salim Abdallah Hamad aliyetaka kujua athari ya mazingira ambayo imeathiri katika maeneo ya visiwa vya Zanzibar.
Mwakilishi huyo pia alitaka kujua ni namna gani wizara imejipanga katika kupambana na uharibifu huo wa mazingira, ili wananchi na sasa wakulima waweze kutumia ardhi yao ipasavyo.

Akijibu suali hiyo waziri Fereji alisema katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo kuingia maji ya chumvi kwenye mashamba ya wakulima, ofisi ya makamo wa kwanza imekuwa ikiwashajiisha na kuwaelimisha wadau na wananchi wa maeneo yalioathiriwa kupanda miti kwa wingi na ikibidi kujenga matuta ili kupunguza athari hizo na kupata nafasi ya kuendelea kuyatumia maeneo hayo kwa shughuli za kilimo.

Waziri huyo alisema maeneo ambayo tayari yamejengwa matuta kwa ajili ya kuzuwia maji ya chumvi ni pamoja na Koowe, Ukele, Tumbe, na kwa Jibwa iliyopo Kengeja.

Sambamba na hilo ofisi ya makamo wa Rais imekusanya taarifa za maeneo yote yanayoingia maji ya chumvi hapa Zanzibar na imebaini kuwa yapo maeneo 148 Unguja na Pemba (123 Pemba na 25 yapo Unguja).

Alisema ofisi hivi sasa imeanza mchakato wa kujitayarisha mapendekezo ya mradi kwa baadhi ya maeneo hayo ili hatua zinayostahiki zichukuliwe.

Akifafanua suala hilo Fereji alisema kisiwa hicho kinakabiliwa na tatizo la maji ya bahari kuvamia maeneo ya makaazi ya wananchi kutokana na wananchi kukata miti aina ya mikoko kwa matumizi ya ujenzi wa nyumba za kuishi.

Alisema miti ya mikoko ni maarufu kwa ajili ya kuzuwia kasi ya maji ya bahari kuvamia maeneo ya wakaazi.

‘Mheshimiwa Spika napenda kusema kwamba nilipata nafasi ya kutembelea eneo la kisiwa hicho na kujionea athari za kimazingira ambapo ni kweli maji ya baharini yanavamia maeneo ya makaazi ya wananchi kwa kasi kubwa’alisema.

Alisema Serikali imechukuwa hatua za awali ikiwemo kutoa ushauri wa kupandwa kwa miti aina ya mikoko pembezoni mwa bahari.

Fereji alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imetafuta mshauri mwelekezi kwa ajili ya kufanya tathmini ya kina ya athari za mazingira zinazotokana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Alisema kazi ya mshauri mwelekezi ni kuangalia maeneo ya athari za mazingira ikiwemo visiwa vidogo vidogo ambavyo vinaishi wananchi ikiwemo Pemba.

Fereji aliwapongeza wananchi ikiwemo vikundi mbali mbali vya kulinda mazingira ambavyo vimekuwa vikifanya kazi ya kulinda mazingira ikiwemo upandaji wa miti aina ya mikoko.

Alisema tayari zipo jumla ya vikundi 11 vinavyotowa Elimu ya kamati ya mazingira nchini.

Aidha alisema Serikali inatarajiwa kupata jumla ya sh.Milioni 546 kutoka katika mfuko wa Kimataifa wa kimazingira kwa ajili ya kusaidia athari za mazingira ziliopo sasa.

Mwisho.

SMZ KUSITISHA VIBALI VYA UJENZI MAHOTELI MJI MKONGWE.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema ipo katika mchakato wa kupunguza utoaji wa vibali vya ujenzi wa hoteli za kitalii katika mji huo ili kuhifadhi mji huo ubakie katika hifadhi ya kimataifa.

Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati,Ramadhan Abdalla Shaaban aliyasema hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini (CCM) Ali Abdalla Ali aliyetaka kujuwa mipango ya Serikali ya kupunguza ujenzi wa majengo ya hoteli za kitalii katika Mji Mkongwe wa Zanzibar.

Mheshimiwa Spika tupo katika mchakato wa kuhakikisha kwamba tunasitisha vibali vya ujenzi wa hoteli za kitalii katika eneo la Mji Mkongwe pamoja na hilo na umepunguza ujenzi wa nyumba na ofisi za Serikali” alisema Shaaban.

Waziri Shaaban alisema Mji Mkongwe upo chini ya Mamlaka ya Hifadhi ya Kimataifa ambayo imepewa majukumu mbali mbali ikiwemo kulinda mji huo na kuuhifadhi.

Alisema katika mikakati hiyo ni kuhakikisha inapunguza utoaji wa vibali kwa ujenzi wa hoteli za kitalii katika mji huo ikiwemo majengo ya Ofisi za Serikali ambapo kwa sasa baadhi ya majengo hupuguzwa na kujengwa nje ya mji.

Aliwambia wajumbe wa baraza la kwamba ni kweli hivi sasa kuna baadhi ya majengo ya hoteli za kitalii katika eneo hilo la Mji Mkongwe na kusababisha msongamano mkubwa ambao unatishia kupunguza sifa za miji yenye sifa za urithi wa kimataifa.

Kwa mfano alisema tayari hivi sasa majengo mengi ya Ofisi za Serikali yanajengwa nje ya eneo la Mji Mkongwe kwa lengo la kuondowa msongamano katika mji huo.

Akijibu suali la msingi la Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni (CCM) Jaku Hashim Ayoub aliteyetaka kujua kazi na mamlaka ya Mji Mkongwe kuingiliana na kazi za Baraza la Manispaa na kumtaka waziri abainishwe mbele ya baraza hilo la wawakilishi ni kwa nini hali hiyo hutokea.

Waziri Shaaban akijibu swali hilo Mji Mkongwe unajengwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa zinazosisitiza uhifadhi wa urithi wa kimataifa na hiyo sheria zote zinayostahiki zinafuatwa kama kawaida na hakuna muingiliano wa kimamlaka kama anavyosema Mwakilishi.

Alisema kazi za Mamlaka ya Mji Mkongwe Zanzibar zimeanishwa kikamilifu katika sheria namba 4 ya mwaka wa 2010, na kwa mpango mkuu wa uhifadhi wa ulioambatana na kanuni zake.

Alisema migongano ya kuingiliana kazi hiyo haupo kwani kila taasisi ina mipaka yake kisheria, pamoja na hayo ikitokezea hali kama hiyo au inayolingana, sheria ya mamlaka ya mji mkongwe ndio iliyopo juu ya mamlaka nyengine.

MWISHO

One Reply to “”

  1. Assalaam Alaaykum, Waungwana

    UMOJA, UHURU, UWADILIFU

    ZANZIBAR KWANZA

    “Usipo ziba ufa, utajenga ukuta”, huu ni msemo maarufu. Haya ndio yanayotufika sisi Zanzibar hii leo. Watawala utadhani hawapo, au hawaoni au hawasikii, maharibiko ya fukwe na nchi nzima kwa jumla si yaliotokea ghafla.

    Maharibiko yametokea na kuonekana, pia imeoonywa athari ya maharibiko haya kwa muda mfupi na kwa muda mrefu, msiba ni kwamba watawala hawakuona dharura ya kulishughulikia suala hili katika wakati, natija ndivyo hivi tulivyofika hii leo. Tumo katika khatari ya visiwa kuwa mafungu ya mchanga na mahandaki ya maji.

    Nilandika maqala humu kukhusu uharibifu wa ardhi, khasa huko Chechele. Nimeshuhudia kwa nafsi yangu mahandaki yaliochimbwa mchanga. Unasikia inasemwa, “Sirikali itachukuwa khatuwa kwa wenye kuchimba mchanga sehemu zisizoruhusiwa na Sirikali”, Hii ni sawa na hii qauli kwamba, “wamekamatwa watu wenye kunywa pombe isioruhusiwa”. Kunywa vodak kunaruhusiwa, kunywa tembo la mnazi hakuruhusiwi!

    Ingelikuwa watawa wametumia nadhari na maarifa, wengelitambuwa mwanzo kabisa kwamba visiwa vya Zanzibar havistahili kuchimbwa mchanga hata wa ujenzi wa nyumba moja. Watawala wengeli fikiria na kupanga kupatikana mchanga na udongo kwa njia nyengine, hata kwa kuagiza kutoka nchi za nje, lakini Zanzibar kusichimbwe mchanga wala udongo.

    Miti, ya matunda, miti ya vivuli na miti ya aina zote imeingiliwa kukatwa, si kwa shoka na panga, kwa misumeno ya moto. Mikarafuu imekatwa na kupandwa hiliki na kufanywa kuni na kuchomwa makaa. Minazi imekatwa na kuuzwa mbao. Mito imekauka, samaki wamekimbilia bahari kuu. Yote haya yamefanywa na yanafanywa na mabwana watawala kama hawayaoni au hawasikii.

    UGAVI WA EKA TATU UMEFISIDI ARDHI
    Mabwana watawala walipo pora ardhi za watu na kuzigawa eka-eka walidhania khasara nI kwa yule mnyonge aliedhulumiwa ardhi yake. Walisahau mawili, walisahau kwanza kwamba dhulma haileti isipokuwa khasara, pili walisahau kwamba kumpa mtu miliki ya kitu bila kukitaabikia ni kukipoteza hicho kiltu. Natija ya ugavi huu mkorofi, ndivyo ardhi ilivyofisidiwa kwa kukatwa miti na kuchimbwa mchanga. Ikifanywa utafiti itabainika kwamba nyingi ya ardhi zilizogaiwa eka zimefisidiwa kwa kujengwa majumba na kuchimbwa mchanga. Mito na visima vimekauka kwa kukatwa miti ya kivuli pembezoni mwa mito na sehemu za mitoni zote.

    Kwa watawala kushindwa kuziba ufa; haitarajiwi kujenga ukuta.

    Wa Billahi Tawfiiq

Leave a comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.