Salma

Salma Said

ASALAMU ALAYKUM WARAHMATULLAH  TAALA WABAKAATUH.

Mpendwa Msomaji wa weblog hii, ninakukaribisha katika jukwaa hili la Salma Said

Mawasiliano baina yangu, kama msimamizi na mwendeshaji wa weblog hii, nawe mpendwa msomaji. Pamoja na hayo, weblog hii inatarajiwa iwe jukwaa baina ya Zanzibar na ulimwengu huu mpana ambao sasa umefanywa uwe mwembamba kutokana na njia kama hizi za mawasiliano ya mtandao. Mimi naitwa Salma Hamoud Said. Ni Mzanzibari niliyezaliwa Hurumzi Mji Mkongwe, Zanzibar, mji ambao sasa ni urithi wa kimataifa. Familia yangu inatokana na ukoo wa Al Marhuum Rashid Bin Slim Al-Ghaithiy wa Mwera Kiongoni. Nina fakhari ya kuzaliwa, kukulia na kuipenda Zanzibar. Kwangu Zanzibar sio tu kwamba ni nchi yangu ya uzawa, bali ni heshima yangu.

Mimbar ya Msikiti Mkongwe wa Kizimkazi unaoaminika kuwa wa mwanzo katika upwa wa Afrika ya Mashariki

Nchi hii ya Visiwa imekuwepo kwa karne na karne huku watu wake wakiishi pamoja kwa masikilizano na upendo hata pale inapotokea pana tafauti za kidini, kisiasa au kiuzawa. Kwa mfano, licha ya kuwa Uislam ndio dini kuu ya Zanzibar huku zaidi ya asilimia 99 wakiwa ni waumini wa dini hiyo, nimezaliwa na kukulia katika Zanzibar inayotambua uwepo wa dini nyengine kama vile Ukristo, ambao ulifika Zanzibar kabla ya nchi yoyote ya Afrika Mashariki na Kati. Ushahidi wa ukongwe wa Ukristo Zanzibar ni kanisa la Minara Miwili lililopo Mji Mkongwe, mji ambao nimezaliwa.

Nimekuwa mwandishi wa habari tangu mwaka 2000. Ninaandikia magazeti ya Mwananchi na The Citizen na pia naripoti kwa Sauti ya Ujerumani (DW)kutokea Zanzibar. Pia nimewahi kufanya kazi na Radio ya Voice Of America (VOA) na BBC Monitoring na pia hadi sasa nimekuwa mchangiaji wa makala kwa magazeti mbali mbali kama An Nuur la Dar es Salaam na Dira Zanzibar. Gazeti la Dira lilisimama kama sauti ya Wazanzibari lakini likaja kupigwa marufuku na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa madai kwamba lilikuwa likikiuka maadili ya uandishi.

Baada ya kuona njia mpya ya mawasiliano imeanza kukuwa kupitia Social Media nimeamua kuanzisha blog hii mwaka 2008 lengo likiwa ni kueneza habari mbali mbali kwa njia za mtandao na kwa haraka zaidi kama ambayo tunavyofahamu umuhimu wa matukio muhimu na upatikanaji wake kwa wakati.

Kanisa la Minara Miwili, Shangani, Zanzibar. Nalo ni katika majengo makongwe ya ibada katika Afrika Mashariki

Baada ya kufanya uandishi wa habari wa kimapokeo kwa miaka kadhaa, sasa nimeamua kuongeza ufanisi katika fani hii ya khabari kupitia kuchapisha kwenye mtandao, ambako jukwaa na hadhira itaongezeka hasa kwa wale walio nje ya Zanzibar na Tanzania.Kwa Kiswahili kibovu, njia hii ya mawasiliano huitwa gazeti tando, yaani gazeti linalochapishwa mtandaoni. Pamoja na kutokukubaliana na tafsiri hiyo, lakini dhana ipo pale pale kwamba ninatumia njia hii ya mawasiliano kuchapisha habari, makala, tafiti, na maoni mbali mbali kuhusu mada tafauti kama zinavyojitokeza katika jamii yangu ya Zanzibar.Kupitia weblog hii, msomaji ataweza kusoma khabari mbali mbali za Zanzibar kama zilivyotokea.

Jua likituwa Magharibi ya kisiwa cha Unguja. Mandhari nzuri na adimu

Kutokana na ukweli kwamba mimi mwanzilishi na muendeshaji wa weblog hii ni mwandishi wa khabari, msomaji ategemee kuzipata khabari moto moto kama zinavyotokea kwa njia zote mbili: kuzisoma kupitia magazeti ya Mwananchi na The Citizen na kuzisikiliza kupitia Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani (Deutsche Welle).

Saa kongwe kwenye Mjini Mkongwe

Vile vile kutakuwa na makala na taarifa za Uchambuzi kuhusu hali ya kijamii, uchumi na maisha ya Zanzibar. Hali halisi ya hali za maisha ya watu wa Visiwa vya Unguja na Pemba, matarajio yao, misimamo yao, imani zao na ustaarabu zitachambuliwa katika ukurasa huo.Pamoja na hayo, kutakuwa pia na ukurasa maalum kuhusu siasa za Zanzibar, .

Hii ni mada inayovutia wachambuzi wengi wa siasa za ndani na nje na weblog hii inakaribisha michango ya wachambuzi hao.Weblog hii pia ina ukurasa maalum kuhusu taarifa na makala mbali mbali zilizokuwa zimetayarishwa na kutolewa na katika Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani Deutshe Welle (DW) ambazo zinahusu maisha ya kila siku ikiwemo siasa, utamaduni, jamii pamoja na makala za wanawake na maendeleo, mazingira, haki za binaadamu utamaduni na sanaa na mengi zaidi kutoka Zanzibar.

Zanzibar Yetu

Lakini suala la uchumi nalo halikuwachwa nyuma katika blog hii hasa kwa kuzingatia Visiwa vya Zanzibar vinategemea sana bahari na biashara za mpito katika uchumi wake. Zao la karafuu limeporomoka na utalii bado haujakidhi haja ya kuwa muhimili wa kiuchumi kwa Wazanzibari wenyewe. Hizo ni baadhi ya mada ambazo weblog hii itazichambua.Kuna safu ya Makala na Uchambuzi ambayo baadhi ya mambo yanayojitokeza hapa Zanzibar huandikwa katika safu hii kwa urefu zaidi ikiwa ya kisiasa, kidini au kiuchumi kwa lengo la kuwapa nafasi wasomaji wa blog hii kuweza kufahamu zaidi kwa kuwa taarifa zinazoendikwa huandikwa kwa ufupi lakini makala na uchambuzi hutolewa ufafanuzi zaidi.Nina heshima kubwa kukaribisha maoni ya kila mchangiaji na naahidi kuheshimu mawazo hayo. Hata hivyo, kwa ajili ya kulinda mila na desturi adhimu za Kizanzibari, sitachapisha maandishi yoyote yanayokwenda kinyume na utamaduni wetu.Kwa mawasiliano zaidi na mwenye Blog hii tafadhali tumia barua pepe: muftiiy@yahoo.com au simu nambari +255777477101

37 Replies to “Salma”

    1. ALLAH akuzidishie ujuzi wa mambo ya habar, na pia akufanyie wepec kwakila jambo lako unalolikusudia. lkn lapili nna swali kwenye hii sentence yako uloiandika hivi: “NIMEZALIWA NAKUKULIA KATIKA ZANZIBAR INAYOTAMBUA UWEPO WA DINI NYENGINE KAMA VILE UKRISTO”. swali langu ni je unao ushahidi wauhakika kua UKRISTO ni dini km ulivoandika kua zanzibar intambua uwepo wa DINI nyengine kana UKRISTO?

  1. Asalaam alaykum, tunataraji kupata habari zenye mtazamo wa kizanzibar (Kiislamu) na si za kimagharibi kama ambavyo huwa mnatupa kuptia DW!

  2. Bi Salma MwenyeziMungu akuzidishie imani ya kuipenda na kuipigania nchi yako ya Zanzibar. Wasioitakia mema Zanzibar wanajitokeza kwa kusema japo kuwa ni kwenye makongamano yao kwamba Zanzibar iendelee hivi hivi. Hii ni sawa na kusema kwamba Zanibar kuwa na mamlaka kamili si jambo la muhimu. Tunawashangaa sana watu wenye msimamo huu.
    Tunakushukuru kwa kuiweka hadharani makala ya mzee wetu Mzee Ibrahim Hussein. Wale wenye imani na nchi hii na kuona hapa ndio pao na hawana pengine watajifunza mengi na makala hiyo.
    itakuwa vyema kama na pia utaitowa na humu kwenye “Zanzibar Yetu”
    asante kwa moyo wko huo

  3. Nimefurahishwa sana na mori yako ya kuwatumikia wazanzibari. Allah akujaze nguvu zaidi na akuoneshe njia sahihi ya kuwatumikia wazanzibari.

  4. Salma I like your introduction about you and your country Zanzibar is commendable.My advise is to request you to increase your knowledge in mass communication at the Open University of Tanzania.We also have a branch in Zanzibar.Please well-come Salma Said.
    Best Regards
    Hamza.

  5. Assalam_alykum
    Allah akupe nguvu,moyo wa subra pamoja na ari ya kutupasha habari tofauti duniani kote na hususan za hapa kwetu Zanzibar, japokua utakutana na vikwazo vingi sana vya kukuvunja moyo au kukukatisha tamaa but jitahidi Mungu atakusaidi na tuko pamoja.

  6. Bi salma nakujali sana na nathamini utendaji wako wa kazi kwani wewe ni muandishi wapekee hapa zanzibar ambae unajali utendaji wa kazi bila ubaguzi wowote unamthamini kila mtu Namuomba ALLah akupe uzima na umri mrefu uzidi kututeteea

  7. Nadhani Ndugu yangu Salma Wazanzibari wanakuhitaji sana katika kupata taarifa za ukweli hasa wakati huu ambapo propaganda ni kubwa kuliko ukweli Mwenyenzi mungu akuwezeshe, tuko pamoja nawe.

  8. Safi sana dada Salma,hivi ndo uislam unavohimiza lazima tuendane na changamoto za dunia kwa njia za kileo bila ya kukengeuka mipaka ya Mungu.

  9. mimi nakuombea dua na naitakia sana Zanzibar irudi kama ilivyokua zamani pigana kuitangaza Zaznibar na in shaa Allah Mungu atakupa fungu lako

  10. Ahsante dada salma sisi tulio nje inakuwa ngumu kupata habar zinazoendelea nyumbani lkn kwa kupitia blog hii basi tunapata habar vizur.
    Pia nafrahi kukuza habar zako kwa njia ya mtandao na kuweza kuanzisha mada mbalimbali zinazohusu visiwa vyetu vya znz.
    Pia naomba uwe za kisiasa ktk kipindi hiki cha kuelekea ktk uchaguz mkuu ili kila mtu aweze kutoa maoni yake kuhusu znz yetu.
    Naipenda znz na najiona fakhar kuwa ni mzanzibar tena khalis.
    Allah ibariki znz na uipushie na lolote lililobaya kwa watu wasiotakia mema nchi yetu.

    1. Nashukuru sana, usiwe na shaka yoyote na yale ambayo Mwenyeenzi Mungu ameshayasema kwamba hakika subira huvuta kheri na kila jambo hupangwa na Muumba hivyo basi mbele ya uwezo wa Allah hakuna mtu ambaye ana uwezo wa kumshinda na hakuna kinachoharibika ikiwa Mwneyeenzi Mungu kaamua kukitengeneza. Shukran

  11. nonsense naona unajilabu kwa ukoo wako tu ila katika hiyo makala sioni impact naona majisifu yaso faida tu urojo mtupu, hivi dada nikuulize uandishi umejifunza wai naona kama huko kiproffedion unaipenda tu iyo kazi lkn hujabobea, rudi darasani kwanza mie nimekuwa nikiifatilia blog yako lkn haifunzi kitu uko kisiasa zaidi, nakushauri badilika ili sio tulokuwa sio wanasiasa tuweze kukusoma kupitia blog yako, blog inajulikana kama znz yetu ila nikuulize kwani znz ndo siasa tu hakuna mengine, fanya vitu vya kutuvutia

    1. Asante sana Salma nimependa kwa jitihada zako na mwelekeo wako wa kuwa na ujasiri wa kizanzibari. Nakupongeza kwa weblog yako na nataraji wazanzibari wote watapenda kuwa pamoja na wewe na kwa kupata habari za zanzibar . Najiproud kuwa mzanzibari japo kuwa niko mbali lakini mimi ni MZANZIBARI.

    2. we jamaa vipi, bwege nin kila habar zinaendana na wkati, wakati huu zanzibar kinaendelea nin kwani kama si siasa tu, au unataka matangazo ya biashara na vyakula? fela wew, nenda blog nyengine si zko nyingi. Achana na blog hiii wew

  12. Habari.

    Nashukuru kwa kuweka taarifa yetu mtandaoni. Ila mimi Abdallah Ally Mtolea Naibu Mkurugenzi mambo ya Nje ni Mbunge wa Temeke sio Kinondoni.

    Asante.
    0758811110

  13. Mama Mola Atakuzidishia nguvu,uwezo na arri juu ya kaziyako ya kulisukuma mbele gurudumu la kudai haki ya wa Zanzibari.

Leave a reply to salum attar Cancel reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.