Wapinzani waiunge mkono Serikali

DSC_4070

Jumuiya ya Madola kuendelea kuiunga mkono Z’bar

Yasifu mapinduzi ya uchumi yanayofanywa

JUMUIYA ya Madola imeahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo kama ilivyo kwa wanachama wengine wote 52 wa Jumiya hiyo.

Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Patricia Baroness Scotland, aliyasema hayo wakati akizungumza na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ikulu mjini Zanzibar.

Katika maelezo yake, Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa Jumuiya ya Madola inaendelea kutekeleza mipango na mikakati kabambe ambayo imeiweka kwa wanancha wake ikiwemo Tanzania ambapo Zanzibar pia, ni miongoni mwao.

Alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa juhudi kubwa anazozichukua kuhakikisha Zanzibar inakuza uchumi na kuimarisha amani na utulivu na kusisitiza kuwa Jumuiya anayoiongoza haitokuwa nyuma kumuunga mkono.

Aidha, alimueleza Dk. Shein miongoni mwa mipango ya Jumuiya hiyo kwa nchi wanachama wake ni pamoja na kuongeza fursa katika sekta ya biashara na uchumi, kuwasaidia wanawake, vijana, upatikanaji ajira kwa vijana, elimu, kutunza mazingira, uwezeshaji na mengineyo.

Aliongeza kuwa uchumi kwa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo umekuwa ukiimarika kwa kiasi kikubwa kwa zile nchi za Afrika na hata nchi za Asia uchumi wake umeimarika kwa asilimia 5 hadi asilimia 8.

Katika mazungumzo hayo, Scotland alimueleza Dk. Shein kuwa miongoni mwa maeneo yaliopewa kipaumbele na Jumuiya hiyo ni katika kuhakikisha nchi zake wanachama zinaimarika kiuchumi ni pamoja na miundombinu na nishati.

Akieleza juu ya Jumuiya hiyo ilivyoweka mikakati katika kusaidia kupambana na changamoto ya hali ya mabadiliko ya tabianchi hasa kwa nchi za visiwa, alitoa mfano wa nchi yake ya kisiwa cha Jamhuri ya Dominica jinsi ilivyopata athari zilizotokana na hali hiyo.

Nae Dk. Shein kwa upande wake alitoa pongezi kwa kiongozi huyo kwa ujio wake Zanzibar sambamba na juhudi kubwa zinazochukuliwa na Jumuiya hiyo katika kuendelea kuiunga mkono Zanzibar.

Alimueleza kiongozi huyo kuwa Zanzibar iko salama kutokana na kuwepo kwa amani na utulivu mkubwa hatua ambayo inapelekea hata uchumi wake kuzidi kuimarika siku hadi siku.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepata mafanikio katika kuimarisha uchumi wake kutokana na sekta ya utalii, sekta ambayo bila ya kuwepo kwa amani na utulivu ni vigumu kuimarika.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza juhudi za serikali jinsi inavyochukua hatua kuimarisha sekta za maendeleo na kueleza azma ya ujenzi wa bandari mpya ya Mpigaduri pamoja na kuuimarisha uwanja wake wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume kwa kujenga jengo jipya la abiria.

Aidha, alieleza mafanikio yaliopatikana katika kuimarisha demokrasia na utawala bora nchini huku akimueleza juhudi zilizochukuliwa na serikali katika kutunga sheria ya maadili kwa viongozi wa umma.

Alitumia fursa hiyo kumueleza Katibu Mkuu huyo hatua zinazochukuliwa na serikali anayoiongoza katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa akina mama na watoto sambamba na juhudi za kuanzisha pensheni jamii kwa wazee kuanzia miaka 70, jambo ambalo Katibu Mkuu alilipongeza.

Pia, alimueleza hali ya mabadiliko ya tabianchi jinsi inavyoathiri mazingira ya Zanzibar hasa katika kasiwa cha Pemba na sehemu nyenginezo na kueleza hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Jumuiya za Kimataifa katika kupambana na hali hiyo huku akitolea mfano mkutano wa nchi zinazoendelea za visiwa (SIDS) uliofanyika mwaka 2014 Samoa na maazimio yake juu ya hali hiyo.

Akijibu masuali ya waandishi wa habari baada ya mazungumzo hayo, Scotland alivitaka vyama vya upinzani kushirikiana na serikali anayoiongoza Dk. Shein kwa lengo la kuwaletea maendeleo endelevu wananchi wa Zanzibar na kusisitiza kuwa Zanzibar inafaidika na misaada ya Jumuiya hiyo kupitia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Jumuiya ya Madola  ilianzishwa karne ya 20 kwa lengo la kuikutanisha Uingereza na yaliyokuwa makoloni yake duniani kwa jukumu la kuhakikisha wanachama wake wanajikwamua katika Nyanja mbali mbali za kimaendeleo ikiwemo kisiasa, kiuchumi, kijamii, michezo na burudani huku Malkia wa Uingereza akiwa ndiye Kiongozi Mkuu wa Jumuiya hiyo.

Pia Katibu Mkuu huyo alitembelea mji mkongwe wa Zanzibar na shamba la viungo Kizimbani na kueleza kuvutiwa kwake na mazingira ya Zanzibar.

 

 

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s