Kiswahili kipewe hadhi yake

ikulu.jpg

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amelitaka Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) kuwasaidia waandishi wa habari hapa nchini kuitangaza na kuiandika vyema lugha ya kiswahili kwenye vyombo vyao.

 

Dk. Shein aliyasema hayo jana, alipokutana na uongozi wa Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo pamoja na Bodi yake ya Baraza la Kiswahili na Uongozi wa Baraza hilo huko ikulu mjini Zanzibar.

 

Alisema miongoni mwa mambo muhimu katika kukienzi na kukitunza Kiswahili ni kukiandika na kukizungumza kwa ufasaha. Hivyo, ni vyema kwa (BAKIZA) kutoa elimu kwa waandishi wa habari, watangazaji na wanaosimamia kada hiyo kwani kuna baadhi yao hawakipi heshima yake.

 

Aliongeza kuwa kuna wanahabari wanakiandika Kiswahili vibaya na wengine wanakitamka sivyo inavyopaswa, hivyo ni jukumu la (BAKIZA) kuchukua hatua za kufanya jitihada hizo ili Kiswahili kiweze kubakia na sifa yake.

 

Aidha, alisema kuwa habari, utamaduni na utalii haviendi bila ya Kiswahili hivyo Wizara ina jukumu la kuhakikisha Kiswahili kupitia (BAKIZA) kinalindwa na kinaenziwa.

 

Dk. Shein alisema lugha hiyo lazima iendelezwe na kueleza kuwa miongoni mwa mambo anayoyapenda ni watu kusoma hivyo anafarajika kuona kuna mabingwa waliobobea kwenye fani ya Kiswahili hapa nchini wakiwemo waliopata Shahada ya Uzamivu na wanaoendelea na Shahada hiyo kwani hilo ndio lengo la Serikali.

 

Alisema BAKIZA ni lazima ibadilishwe na ibadilike kwani ni Baraza muhimu hapa nchini na kuahidi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar italisimamia hilo huku akieleza haja ya kulienzi Kamusi la Kiswahili la BAKIZA ambalo lina sifa zote za Kiswahili sanifu na fasaha.

 

Dk. Shein pia, aliahidi kuwa Serikali itayanunua makamusi yote yaliochapishwa na BAKIZA kwa lengo la kutatua changamoto ya uchache wa mauzo ya makamusi hayo 25,000 yenye thamani ya milioni 375 ili fedha hizo pia zisaidia kuliimarisha Baraza hilo.

Nae Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo Rashid Ali Juma alieleza kuwa Kiswahili bado hakijatendewa haki na kusisitiza kuwa Bodi na Wizara ina jukumu kubwa la kukitunza Kiswahili ndani na nje ya nchi.

 

Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee kwa upande wake alieleza haja ya kujitangaza zaidi kuwa Zanzibar ndio chimbuko la Kiswahili kwani fursa zipo kwa kila kona ya dunia.

 

Alieleza kuwa kuna haja ya Bodi hiyo kukaa na Wahariri na waandishi wa Habari wakiwemo wa vyombo vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwapiga msasa juu ya matumizi ya lugha ya Kiswahili ili kiendelee kuchukua nafasi yake.

 

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Kiswahili Mohammed Seif Khatib alisema kuwa Kiswahili hivi sasa kinatumiwa na wapatao milioni 150 duniani na ni lugha ya kwanza ya Kiafrika kwa ukubwa.

 

Aliongeza kuwa nchi jirani za Uganda na Rwanda zinajiandaa kukifundisha Kiswahili katika skuli zao na kusisitiza kuwa Bunge la Afrika Mashariki limeamua Kiswahili kitumike kwenye vikao vyao.

 

Akitoa mapendekezo yake Mwenyekiti huyo wa Bodi alieleza umuhimu na haja kwa wanafunzi wanaosoma elimu ya juu na ambao wanachukua somo la Kiswahili kupewa mikopo kwani mahitaji makubwa ya wataalamu wa lugha hiyo.

 

Nao uongozi wa Baraza hilo ulieleza kuwa Baraza limekuwa likiandaa vipindi kwa kushirikiana na vyombo vya habari vya redio na televisheni za Serikali na zile binafsi kuhusu maendeleo ya Kiswahili.

 

Aliongeza kuwa BAKIZA lina ushirikiano na taasisi za serikali na za binafsi zikiwemo BAKITA, Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki na Vyuo na kueleza jinsi linavyoshirikiana na wataalamu katika makongamano yalioandaliwa ndani na nje ya Tanzania.

 

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s