Simba SC yaibana Bidvest Wits

MAVUGO-NA-KICHUYA.jpg

SIMBA SC imetoa sare ya kufungana bao 1-1 na mabingwa wa Ligi Kuu ya ABSA Afrika Kusini, Bidvest Wits katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Sturrock Park, Chuo Kikuu cha Afrika Kusini.

Katika mchezo huo wa kujipima nguvu kujiandaa na msimu mpya, Simba SC walikuwa wa kwanza kupata bao, lililofungwa na beki anayeweza kucheza kama kiungo pia, Erasto Edward Nyoni dakika ya 33 kabla ya wenyeji kusawazisha.

Huo ulikuwa mchezo wa pili wa kirafiki wa Simba katika kambi yake Afrika Kusini kujiandaa na msimu, baada ya Jumamosi kufungwa 1-0 Orlando Pirates.

Baada ya mchezo huo, Simba SC inatarajiwa kurejea nyumbani Tanzania kwa ajili ya mchezo mwingine wa kujipima nguvu dhidi ya Rayon Sport ya Rwanda Agosti 8, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar  es Salaam.

MWISHO

Ligi Kuu Tanzania bara yazinduliwa

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya soka ya Tanzania Bara umezinduliwa rasmi jana  kwa timu  zote 16 zitakazoshiriki ligi hiyo msimu ujao.

Zoezi hilo limefanyika mjini Dar es Salaam  na Vodacom wanaodhamini Ligi  hiyo wamekabidhiwa vifaa mbalimbali zikiwemo jezi, viatu, mipira na suti za kimichezo.

Akikabidhi vifaa hivyo, Mkurugenzi wa Idara ya Masoko ya Vodacom, Hisham Hendi alisema kwamba, kwa mara nyingine tena katika kuhakikisha Ligi Kuu ya soka hapa nchini inaenda vizuri wanakabidhi vifaa vya ubora wa hali ya juu.

Hemedi alisema kwamba pia Vodacom imefurahishwa na klabu zilizopanda Ligi Kuu msimu huu kutoka Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, Singida United, Lipuli na Mji Njiombe FC kuwa zimejiandaa vizuri kwa ushindani.

“Tunajisikia furaha kukabidhi vifaa hivi tukiwa tunatakeleza matakwa ya mkataba wa udhamini  na ni imani yetu kwamba timu zitakazoshiriki Ligi Kuu zimejiandaa vya kutosha kwa msimu mpya wa Ligi,” amesema Hendi

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniphace Wambura ameishukuru  Vodacom Tanzania na kuzitaka klabu zinazoshiriki Ligi Kuu kuzingatia na kuheshimu nembo ya mdhamini wakati wa mechi.

Wambura alisema Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) halipendi kutumia kanuni na sheria kuziadhibu klabu zitazokwenda kinyume na maelekezo hayo.

Aliongeza kwamba, msimu huu wa Ligi Kuu utakuwa bora kutokana na maandalizi yote kukamilika mapema – pia timu zitakazoshiriki kuwa zimejiandaa vizuri.

Timu nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu ni mabingwa, Yanga SC, washindi wa pili, Simba SC, wa tatu, Kagera Sugar, wa nne Azam FC, wa tano Mtibwa Sugar, wa sita Stand United, wa saba Ruvu Shooting, wa nane Tanzania Prisons, wa tisa Maji Maji, wa 10 Mwadui, wa 11 Mbeya City, wa 12 Mbao FC na wa 13 Ndanda FC.

MWISHO.

Wachezaji Zenj wazidi kutimkia Bara

 

MCHEZAJI Majid Khamis ‘Dudu’ amesaini kandarasi ya mwaka mmoja kuichezea klabu ya Ndanda FC ya Mtwara akitokea Black Sailors.

Dudu ambae anacheza nafasi ya kiungo mshambuliaji ameelezea kufurahishwa na  kusajiliwa na timu inayoshiriki ligi kuu soka Tanzania bara.

“Unajua Zanzibar kuna vipaji vingi sana, naamini nitaonesha kipaji changu katika ligi kuu ya bara, malengo yangu ni kufika mbali zaidi ya hapa nilipofika sasa, nawashukuru Black Sailors kwa kunilea vizuri hasa hasa kocha wangu Juma Awadh pamoja na benchi zima la ufundi na wachezaji wenzangu wote wa Sailors”. alisema.

Idadi ya Wachezaji kutoka Zanzibar kwenda kucheza ligi kuu soka Tanzania bara inazidi kuongezeka baada ya wachezaji kadhaa wakiwemo Abdallah Haji Shaibu “Ninja” aliyesajiliwa Yanga akitokea Taifa ya Jang’ombe, Ibrahim Mohammed “Sangula” aliyesajiliwa Ndanda akitokea Jang’ombe Boys, Ali Hamad “Kidimu”  amekwenda Stand United akitokea Gulioni FC pamoja na Dudu kutoka Black Sailors kujiunga na Ndanda FC.

MWISHO

Mwenge yairipua Okapi

Jang’ombe Boys, JKU zakabana koo

 

KARAMU ya mabao kwenye michezo ya Ligi Kuu Zanzibar hatua na nane bora imeendelea kuliwa baada ya jana timu ya Mwenge kuibuka na ushindi mtamu wa mabao 5-0 dhidi ya Okapi.

Mchezo huo ambao ulisukumizwa katika dimba la Gombani Kisiwani Pemba, ulikuwa si wa kupendeza sana kwani Mwenge walitawala mchezo katika vipindi vyote, na Okapi kuonekana wazi kuwa imeshindwa kuhimili vikumbo vya Mwenge.

Katika mchezo wa jana Mwenge ilianza kula pweza kizani kwa kupachika bao la kwanza lililofungwa na Abdul Yussuf dakika ya sita, na bao la pili lilifungwa dakika ya tisa na mchezaji Sharif Juma, huku bao la tatu likipachikwa kimiani na mchezaji Humud Abrahaman dakika ya 15.

Wakati Okapi ikijiuliza imefungwa vipi mabao ya haraka haraka na kutafuta mbinu ya kuweza angalu kupunguza idadi ya mabao hayo, walijikuta wakipachikwa bao la nne lililofungwa tena na mchezaji Abdul Yussuf, mabao hayo yaliweza kudumu hadi kipindi cha kwanza kinamalizika.

Kuanza kipindi cha pili timu ya Mwenge iliendelea kuweka kambi langoni mwa Okapi ambayo siku ya jana kamwe haikuweza kafurukuta na kurusu idadi kubwa ya mabao, ambapo katika dakika ya 75 Humud Abrahaman alirudi tena nyavuni kwa kupachika bao la tano.

Mbali na mchezo huo mchezo mwengine ambao ulikuwa mkali na wa kupendeza ulisukumizwa katika uwanja wa Amaan, baina ya maafandi wa JKU na Jang’ombe Boys, mchezo ambao ulimalizika kwa wanaume hao kutoka sare ya bila ya kufungana.

Mchezo huo ambao ulikuwa mzuri kwani timu zote zilishambuliana kwa zamu, lakini JKU inapaswa kujilaumu zaidi kwa kushindwa kuondoka na ushindi baada ya mshambuliaji Amour Omar Janja kukosa penalti baada ya kurusha juu ya lango katika dakika ya 83.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s