JPM: Hakuna fedha za bure

magufuli

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, amesema katika utawala wake hakuna kupata pesa kwa njia rahisi kwani lazima watu wafanye kazi kweli ili kupata pesa halali.

Alisema hayo Handeni wakati anaelekea mkoani Tanga kwa ajili ya uwekaji jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima Uganda hadi Chongoleani Tanga.

Hafla hiyo inatarajiwa kufanyika Agosti 5 mwaka huu.

“Kuna watu walikuwa wamezoea vya bure wanapiga ‘disco’ tu wanapewa hela nyingi, sasa hazipo pesa za namna hiyo, hivi sasa watu wanataka ufanye kazi uzalishe mali ili upate fedha za kweli na asiyefanya kazi asile na usipokula maana yake ufe,” alisisitiza.

Mbali na hilo alisema uchumi wa Tanzania unakuwa kwa kasi kubwa na kwa Afrika katika nchi tano ambazo uchumi wake unakuwa kwa kasi kubwa Tanzania ipo nafasi ya pili nyuma ya Ethiopia.

“Ikiwa uchumi wetu unakuwa kwa asilimia 7.2, wapo watu watakuja na kulalamika hela zimepotea, hao walikuwa wamezoea vya bure na hao ndio mnawaona wanapiga kelele,” alisema.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia katika nchi ambazo uchumi wake unakuwa kwa kasi Tanzania imekuwa nafasi ya tano chini ya India, Nepal, Uzbekistan na Ethiopia.

Wakati huo huo, Rais Magufuli ameliagiza Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kurejesha eneo la eka 50 walilopewa na kijiji cha Mkata, baada ya kushindwa kuliendeleza kwa miaka saba.

Magufuli alitoa agizo hilo jana wakati alipokuwa akizungumza na wakaazi wa Mkata akiwa njiani kuelekea mkoani Tanga, ambapo alimwita Mkuu wa JKT wa eneo hilo na kumhoji kuhusu kuendeleza eneo hilo.

“Hili eneo tangu mmepewa ni miaka mingapi sasa? mliomba ili muwekeze kwa kujenga kiwanda, lakini mmeshindwa, sasa leo hii mrejeshe kwa wananchi ili waweze kumpa hata mwekezaji mwingine,” aliagiza Rais Magufuli na kushangiriwa na wananchi.

Alimweleza mkuu wa JKT kwamba wakajenge kiwanda hicho kwenye kambi yao kwa kuwa wana eneo kubwa ambalo linatosha pia kwa uwekezaji huo.

Awali aliwataka wananchi hao kuwa na subira kuhusu ujenzi wa hospitali katika eneo hilo, kwa kuwa kuna shaka kwamba shilingi 500 milioni zilizotolewa kwa awamu ya kwanza zilitafunwa, hivyo kabla ya kuleta nyingine wanapaswa kujiridhisha na matumizi yaliyofanywa.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alipopewa nafasi ya kulitolea ufafanuzi jambo hilo alisema wanaunda kamati ambayo itachunguza matumizi ya fedha hizo ndipo waweze kuruhusu fedha zingine zipelekwe ili kuendeleza mradi huo.

Akizungumzia shamba la katani linalomilikiwa na mwekezaji Chavda lililopo katika wilaya ya Korogwe, Magufuli alisema tayari notisi ya siku 90 imekwisha hivyo anachosubiri ni kuletewa taarifa mezani kwake.

“Niwahakikishie wananchi muwe na amani hiyo ardhi faili lipo kwa kamishna wa ardhi namsubiri Waziri wa Ardhi anilitee tu niweze kufanya maamuzi yangu,” alisisitiza.

Aidha alisema kama kutawasilishwa mapendekezo ya mwekezaji kukubali kugawa sehemu ya ardhi kwa wananchi wanaweza kuelewana lakini akiwa hataki lazima atalifuta.

“Mimi ni Rais wa wanyonge hivyo sitavumilika kuona wananchi wangu wanalalamika kwa kukosa maeneo kwa ajili ya kilimo, huku kuna watu wanamiliki maeneo ambayo wameyaacha mapori tu,” alisema.

Awali Mbunge wa jimbo la Korogwe Vijijini, Steven Ngonyani, alimuomba Rais Magufuli kuangalia namna ya kulifuta shamba la katani lililoko Hale ili kusaidia wananchi kupata maeneo ya kilimo.

Rais Magufuli yupo safarini ambapo Agosti 5 atakutana na Rais Yoweri Museveni kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga.

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s