Drop of Zanzibar wagoma

IMG-20170802-WA0017

Washinikiza mshahara mpya

 SHUGHULI za uzalishaji katika kiwanda cha maji ‘Drop of Zanzibar’ kilichoko Hanyegwa mchana Wilaya ya Kati Unguja, zimedorora kuanzia Julai 1, 2017 kufuatia mgomo wa wafanyakazi wakilalamikia kutolipwa mshahara mpya uliotangazwa na serikali.

 

Wafanyakazi hao wamechukua hatua hiyo, wakidai kutosikilizwa na uongozi, ambao ulitarajiwa kuanza kulipa kiwango kipya cha mshahara uliotangazwa kwa sekta bnafsi mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.

 

Itakumbukwa kuwa, tarehe 30 Juni, 2017, Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Moudline Castico, alitangaza kuwa kuanzia mwezi Julai mwaka huu, kima cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi kitakuwa shilingi 300,000 kwa mwezi.

 

Kiwango hicho ni kwa ajili ya wafanyakazi   wenye mikataba, huku vibarua wakipangiwa kulipwa kati ya shilingi 10,000 na 30,000 kwa siku.

 

Akiwa kiwandani hapo jana, mwandishi wa habari hizi alishuhudia kundi kubwa la wafanyakazi wakiwa nje ya kiwanda, ambao walipoulizwa walisema hawatarudi kazini hadi uongozi utakapokubali kuwalipa mshahara mpya.

 

Mbali na kuzikimbia mashine na vitengo vyao mbalimbali vya kazi, wafanyakazi hao walisema pia hawako tayari kuchukua mshahara wa mwezi wa Julai ambao tayari umeingizwa katika akaunti zao za benki bila ya kufanyiwa marekebisho.

 

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mohammed N. Ali, mwendeshaji mashine ya kujaza maji katika chupa, alisema wameamua kugoma ili kupinga kitendo cha mwajiri wao kutokutimiza agizo la serikali lililotaka walipwe nyongeza ya mshahara kutoka shilingi 145,000 hadi 300,000 kuanzia mwezi wa Julai.

 

Alisema mbali na kunyimwa mshahara mpya, alisema kumekuwa na matatizo mengi yanayowakabili ikiwemo kulazimishwa kufanya kazi kwa zaidi ya saa nane, lakini malipo wanayolipwa kwa saa za ziada hayalingani na kiwango wanachostahiki.

 

“Uongozi unatubabaisha tu kwani tukiwauliza wanatuambia eti wameambiwa wasilipe mpaka makampuni yamalize mjadala na serikali ambao unatarajiwa kuleta muafaka,” alieleza.

 

Wakati wakizungumza na mwandishi wetu, wafanyakazi hao walisema tayari wamewatuma wawakilishi wao kwenda kuonana na Waziri mwenye dhamana ya kazi jana, lakini msimamo wao ni kuendelea kupigania haki yao hadi mwajiri wao atakapotekeleza agizo la serikali.

 

Naye Saada Rashid, msaidizi mtunza ghala kiwandani hapo, alisema waliipokea vyema kauli ya serikali kupandisha mishahara katika sekta binafsi, na kwamba walikuwa wakisubiri kwa hamu mwisho wa mwezi ufike ili waanze kutononoka.

 

Zanzibar Leo ilifika ofisini hapo na kukutana na Meneja Mauzo, Othman Shakur ambaye alikiri kwamba uongozi wa kiwanda umeshindwa kutimiza agizo la serikali na hivyo wanaungana na wenzao wa kiwandani kutokufanya kazi wala kuchukua mshahara pungufu walioingiziwa.

 

“Sisi tunatambua kauli ya Waziri kuongeza mishahara lakini hatujasikia tamko jengine la kuifuta, hivyo ofisini tunakuja kama kawaida ila kazi hatufanyi,” alisisitiza.

 

Akijibu madai ya wafanyakazi hao, Meneja Mkuu wa kiwanda hicho Amar Rahman, raia wa India, alisema hatua ya kutolipa mshahara mpya imetokana na maelekezo ya mshauri wao elekezi, kuwataka wasubiri mazungumzo kati ya viongozi wa jumuiya ya sekta binafsi na serikali yamalizike na kuja na jibu jipya.

 

“Sisi hatukatai kuwalipa wafanyakazi wetu mishahara mipya, lakini tunasubiri maelekezo ya wakuu wa sekta watakapomaliza mazungumzo na serikali na tutalipa haraka bila ajizi,” alieleza Rahman.

 

Alieleza kuwa si kawaida ya kampuni yake kuwadhulumu wafanyakazi, lakini akawalaumu kwa kutokufikisha malalamiko yao ofisini kwake kabla kuzungumza na vyombo vya habari.

 

Alitumia fursa hiyo kuwasihi wafanyakazi hao kurudi kazini na kusubiri hatima ya mazungumzo aliyosema yanaendelea ili wasizidi kukitia hasara kiwanda, na kuikosesha serikali mapato ya asilimia 18 kwa kila siku inayopita bila uzalishaji.

 

Alipoulizwa kuhusu kadhia hiyo, Kamishna wa Kazi Fatma Iddi alisema, kauli ya serikali kuwataka waajiri wa sekta binafsi kulipa kiwango kipya kuanzia mwezi Julai, haijabadilishwa.

 

“Agizo hili linatokana na sheria ya kazi namba 11 ya mwaka 2005, kwa hivyo waajiri wanapaswa kulitekeleza na hakuna njia nyengine,” alisisitiza.

 

Kamishna huyo alitahadharisha kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mwajiri yeyote wa sekta binafsi atakaekwepa kutekeleza agizo hilo la serikali lililotolewa ili kuwapa faraja wafanyakazi wa sekta hiyo kama ilivyo kwa waajiriwa wa sekta  ya umma.

Alisisitiza kwamba kiwango cha sasa cha mishahara ya chini kwa wafanyakazi wenye mikataba ni shilingi 300,000 badala ya shilingi 145,000 za zamani kwa waajiriwa wenye mikataba.

 

Chanzo: Maelezo

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s