RC ataka wahalifu wachukuliwe hatua

IMG-20170117-WA0006

MKUU wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ayoub Mohammed Mahmoud, ameitaka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka kuharakisha uchunguzi wa jalada la mtuhumiwa anayedaiwa kuwajeruhi wageni katika mkahawa wa Lukman ulipo Malindi mjini hapa.

 

Alisema jalada hilo ambalo limekwama kwa Mkurugenzi wa Mashtaka kwa muda mrefu tangu tukio hilo lilipotokea, jambo ambalo limeanza kutia wasiwasi na kusababisha wananchi kukosa imani na vyombo vya sheria.

 

Akizungumza na Zanzibar Leo Ofisini kwake Vuga, alisema imefika wakati kuhakikisha kila aliyepewa jukumu kujiamini katika nafasi yake ya utendaji ili kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati.

 

“Hivi karibuni nilipokea ujumbe wa simu kutoka kwa Balozi wa Ujerumani kulalamikia kuachiwa kwa mtuhumiwa wa tukio hili, nilijisikia vibaya sana kwani tunaonekana kama serikali haifanyi kazi au kesi haijafunguliwa,” alisema.

 

Alisema tukio hilo limetokea mwezi wa Ramadhani na hadi sasa halijafikishwa mahakamani, ambapo alipowauliza watendaji wake aliambiwa mtuhumiwa ameachiliwa kwa dhamana.

 

Alibainisha kuwa, kuna malalamiko mengi ambayo yanajitokeza katika kesi hasa za udhalilishaji kwa hatua za kwenda mahakamani, na hukumu jambo ambalo linasababisha familia kuweka mapatano yanayopelekea kesi kufutwa.

 

Sambamba na hayo alisema matukio mengi yanazidi kuongezeka na kukosekana imani kutokana na kuwepo kwa muhali, rushwa na watendaji kutowajibika ipasavyo.

 

Hivyo alisisitiza kuwa imefika wakati kuona wanashirikiana katika kujenga taifa bila kujali muhimili, kujali nafasi ya mtu kwani ikiwa wengine wanabomoa na wengine wanajenga maendeleo yatachelewa kupatikana.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassan Nassir Ali akizungumzia tukio hilo alikiri kuachiwa kwa mtuhumiwa Mohammed Suleiman Jussa (23) mkaazi wa Kokoni baada ya kugundulika kuwa ni mgonjwa wa akili.

 

Alisema baada ya uchunguzi wa awali uliofanywa kwa mtuhumiwa huyo ilithibitika ni mgonjwa wa akili, ambae aliathirika kutokana na utumiaji wa dawa za kulevya kwa muda mrefu, huku akipata matibabu katika hospitali ya wagonjwa wa akili Kidongochekundu.

 

Kamanda Nassir alibainisha kuwa tayari Jeshi la Polisi limeshakamilisha upelelezi na jalada la mtuhumiwa huyo limeshapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka kwa hatua zaidi, ili aweze kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za shambulio la hatari.

 

Hata hivyo, Kamanda Nassir alisema hali za majeruhi hao zinaendelea vizuri na tayari wameshaondoka nchini.

 

Tukio la kujeruhiwa kwa wageni na watembezaji watalii lilitokea Mei 28 mwaka huu, ambapo walijeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao na kusababishwa kulazwa katika hospitali ya Tasakhataa Global iliyopo mnazi mmoja mjini Unguja.

 

Kijana huyo awali alipatikana kufuatia timu maalum iliyoundwa na Mkuu wa Operesheni wa Mkoa kwa kushirikiana na askari, ambao alibainika kuwa ni mtumiaji maarufu wa dawa za kulevya.

 

Wageni waliojeruhiwa ni Mauget Gerarol (66) raia wa Ufaransa alijeruhiwa pembeni ya jicho la kulia, Jennifer Wolf (24) raia wa Ujerumani ambae alijeruhiwa kichwani sehemu ya nyuma, Anna Catharina Ehlgen (20) raia wa Ujerumani ambae alijeruhiwa kichwani sehemu ya nyuma na Liying Liang (24) raia wa Canada ambae alijeruhiwa sehemu ya shavuni.

 

Wengine ni Hassan Abdalla Abdalla (24) mkaazi wa Kiponda ,ambaye alikuwa ameongozana na raia wa Canada ambapo alipata majeraha mdomoni na Sajad Hussein (55) mkaazi wa Mkunazini.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s