Operesheni kamata ‘bodaboda’

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassan Nassir Ali

JESHI la Polisi limeendesha operesheni ya kukamata pikipiki zinazotumika kusafirisha abiria maarufu kama ya ‘bodaboda’, zinazofanyakazi hiyo katika  Mkoa wa Mjini Magharibi.

 

Operesheni hiyo ilianza jana asubuhi katika maeneo mbalimbali ikiwa ni utekelezaji wa amri ya Kamishna wa Polisi Zanzibar, ambaye aliwaagiza watendaji wa jeshi hilo, kuhakikisha hakuna kituo cha bodaboda katika Mkoa wa Mjini.

 

Akizungumza na Zanzibar Leo, Ofisini kwake Mwembemadema, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Hassan Nassir Ali, alisema vyombo hivyo vimeonekana kwa kiasi kikubwa kufanya matendo ya kihalifu ambayo hayapendezi katika jamii.

 

Alisema, operesheni hiyo imeanzia maeneo ya Michenzani, Darajani, Malindi na sehemu nyengine katika Mkoa huo, ambayo hutumiwa zaidi na madereva wa usafiri huo kama vituo vyao ambavyo haviko kisheria.

 

Aidha, alisema ni dhahiri kuwa vyombo vya bodaboda vimekuwa vikwanzo vikubwa barabarani pamoja na kufanya matukio ya kuuwa huku  mmoja wao kuuliwa katika siku za hivi karibuni.

 

“Sisi jeshi la polisi hatupendi mtu auwe au auliwe bali tunataka watu waishi kwa salama na amani,” alisema.

 

Kamanda Nassir, alisema vyombo hivyo vimekuwa vikikiuka sheria za barabarani ikiwemo madereva kukosa leseni zao na vyombo vyao kukosa leseni za njia.

 

“Tulimkamata juzi mmoja wa madereva hao hata leseni hana na chombo chake hakina chochote, hawajui kuendesha lakini wanaendesha na kuwapakia wananchi, jamii ifahamu kuwa vyombo hivyo havifai kusafirisha abiria,” alibainisha.

 

Sambamba na hayo, alibainisha kuwa vyombo vingi aina ya bodaboda vinaonekana kuwa vibovu, madereva kuvaa nguo ambazo hazipendezi na hata kupakia abiria bila ya kuvaa kofia ngumu jambo ambalo linaweza kusababisha ajali.

 

Hata hivyo, alisema ni vyema kwa wamiliki wa vyombo hivyo kutambua kuwa vespa na bodaboda sio vyombo vya biashara huku akisisitiza kuwa Zanzibar haijafikia kuwa na biashara hiyo.

Alisema pamoja na kusaidia vijana hao kupata ajira lakini ni jambo la msingi kuendelea na ombi lao la kuishauri serikali kupitia idara ya Usafiri na Leseni kuomba kibali cha kufanya biashara hiyo.

 

Hivyo, alihakikisha kuwa jeshi lake litaendelea kusimamia zoezi hilo la kisheria kupambana na wamiliki hao kwani wanavunja sheria na kuleta uvunjifu wa amani nchini.

 

Katika hatua nyengine, alimpongeza Mkuu wa usalama barabarani, Mkadam Khamis Mkadam, kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuhakikisha ajali za kizembe hazijitokezi katika mkoa wao.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s