Mbunge, Mwakilishi wasaidia Tunguu

 NO. 1

WAVUVI wa kijiji cha Unguja Ukuu Tindini, hatimaye wamepata faraja baada ya uongozi wa jimbo la Tunguu kuanza kuukwamua ujenzi wa soko lao uliokwama kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.

 

Mwakilishi na Mbunge wa jimbo hilo Simai Mohammed Said na Khalifa Salum Suleiman, walikabidhi mabati na vifaa vyengine kwa uongozi wa kamati ya maendeleo Tindini ili kuanza hatua ya kuliezeka jengo hilo.

 

Vifaa vyote hivyo vimegharimu shilingi 3,500,000.

 

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo yaliyofanyika kijijini hapo, Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kusini Unguja Sauda Ramadhan Mpambalyoto, alisema hatua hiyo inapaswa kuwahamasisha wananchi kujitolea katika shughuli za kumaliza ujenzi wa soko hilo.

 

Alisema, ushiriki wa vijana kuchangia nguvu katika ujenzi huo, ni muhimu kwa ajili ya kuwatia moyo zaidi viongozi wa jimbo hilo katika kuleta maendeleo endelevu kwa manufaa ya wananchi wote wa kijiji hicho na vijiji vya jirani.

 

Aidha aliwaomba viongozi wa jimbo hilo kuwajengea mazingira mazuri vijana ili waweze kuendesha uvuvi wa kisasa utakowavutia wahitaji wa samaki kutoka maeneo mbalimbali hasa katika ukanda wa utalii.

 

Kwa upande mwengine, alisema ili vikosi vya ulinzi na usalama vya taifa viweze kufanya kazi kwa ufanisi, ni lazima wananchi wawe tayari kutoa ushirikiano kuwabaini na kuwafichua watu wenye nia mbaya na wasiopenda maendeleo, amani na utulivu.

 

Naye Mwakilishi wa Tunguu Simai Mohammed Said na Mbunge Khalifa Salum Suleiman, walisema mikakati yao ni kuhakikisha wanazimaliza kero zote zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo.

 

Walieleza kuwa, baada ya kukamilika ujenzi wa soko hilo, ni wazi wananchi kutoka sehemu mbalimbali watakuwa wakimiminika kijijini hapo kwa ajili ya kujipatia mahitaji ya samaki.

 

Kwa hivyo walisema wako tayari kuwaunganisha wananchi wa Unguja Ukuu yote na wawekezaji wa ukanda wa utalii Mkoa wa Kusini, ili kuhakikisha wanapata soko la uhakika la samaki watakaovuliwa.

 

Viongozi hao pia walieleza dhamira yao ya baadae ni kujenga soko kubwa la kisasa katika eneo la makutano ya barabara ya Unguja Ukuu, Makunduchi na ile inayoelekea Cheju ambayo hivi karibuni imemaliza kuwekewa lami.

 

“Eneo hilo linaweza kuwa kiungo cha wafanyabiashara na wananchi wa mikoa mingine, kwani kuwepo barabara nzuri ndiko kunakovutia wawekezaji na hivyo kusaidia kukua kwa uchumi,” alisema Simai.

 

Hawakusita kumshukuru Mwakilishi wa Viti Maalumu Mkoa wa Kusini Wanu  Hafidh Ameir, kwa mchango wake alioutoa kufanikisha ujenzi wa soko hilo.

 

Katika risala yao, wananchi wa Tindini walitaja chanagomoto kadhaa zinazohitaji kushughulikiwa, ili kuwapa nguvu ya kushiriki kazi za amali na kujikwamua na umasikini.

 

Baadhi ya changamoto hizo ni ulinzi wa uhakika ili kudhibiti uhamiaji holela wa watu kutoka maeneo ya mbali, ambao hujihusisha na vitendo viovu na kukipa jina baya kijiji hicho.

 

Katika hatua nyengine, viongozi hao wa jimbo la Tunguu walifanya ziara fupi katika kijiji cha Mwera Kiongoni na kushuhudia wananchi wakifurahia kupatikana kwa huduma ya maji ya bomba ambayo kwao ilikuwa ndoto ya miaka mingi.

 

Kupatikana kwa maji katika kijiji hicho alichozaliwa Rais wa kwanza wa Zanzibar marehemu Abeid Amani Karume, kumetokana na viongozi hao kupeleka mipira ya kusambazia maji pamoja na mifereji miezi miwili iliyopita.

 

Diwani wa wadi ya Ubago Usi Ali Mtumwa, aliwashukuru viongozi hao, akisema kitendo hicho cha kihistoria, kitawapumzisha na matumizi ya maji ya visima na mashimo ambayo si salama.

Chanzo: Tunguu

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s