ZATI yawashusha presha wanachama wake

BAADA ya Jumuiya ya Wawekezaji wa Sekta ya Utalii Zanzibar (ZATI) kuwasilisha rasmi serikalini mapendekezo kuhusu viwango vipya vya mishahara kwa sekta binafsi, imewasihi wawekezaji wa sekta hiyo kuwa watulivu kusubiri majibu ya serikali.

 

Akizungumza ofisini kwake Malindi mjini Zanzibar, Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Seif Masoud Miskry, amesema ZATI imeshitushwa na namna wawekezaji wa hoteli na maeneo mengine ya kitalii, walivyoupokea uamuzi wa serikali kupandisha kiwango cha mishahara ya kima cha chini kwa wafanyakazi wa sekta hiyo.

 

Aidha, alisema hata ZATI imeona kuwa hatua hiyo inaweza kuleta athari, lakini akaeleza kuwa si busara kwa wawekezaji hao kuanza kuchukua hatua, ya ama kupunguza wafanyakazi au kukata marupurupu wanayowalipa katika utaratibu waliojipangia.

 

Kwa hivyo, amesema kufuatia tangazo la tarehe 30 Juni, 2017 lililotolewa na Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Moudline Castico kupandisha mishahara hiyo, uongozi na wanachama wa ZATI walikutana Juni 6, mwaka huu, kujadili hali hiyo na kutoka na mapendekezo kwa serikali.

 

Alisema tayari jumuiya hiyo imeshawasilisha serikalini mapendekezo ya wanachama wake na ya wadau wa sekta ya utalii, kutaka uamuzi huo upitiwe upya na kuangalia namna nyengine ambayo haitawaumiza waajiri wala waajiriwa, na pia kuzingatia faida ya serikali kupitia kodi zitokanazo na utalii.

 

Alifahamisha kuwa, waraka wa mapendekezo hayo umepelekwa serikalini Jumatatu wiki hii, ukielezea kwa kina mapungufu wanayoyaona kwenye uamuzi wa serikali, huku maoni ya wadau wao yakiwa hayajawasilishwa rasmi wakati wa mjadala uliofanywa kabla ya tangazo la serikali kupandisha mishahara.

 

Hata hivyo, alifahamisha kuwa, kutokana na umuhimu wa sekta ya utalii ambayo alisema inagusa maisha ya wananchi wengi wa Zanzibar pamoja na kuiingizia serikali fedha za kigeni, ni vyema wanachama wake waendelee kuwa na subira wakati mjadala na serikali ukiendelea.

 

Miskry alisema ZATI inaamini kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni sikivu na haiko tayari kuona sekta ya utalii inatetereka, lakini hata jumuiya hiyo haitaki kuwaumiza wafanyakazi kwa malipo kidogo, lakini akasema suala hilo linaweza kujadiliwa kwa pamoja na pande zote husika kwa kuzingatia maslahi ya wote.

 

Alisema linapotokea jambo zito kama hilo, subira na hekima ni muhimu ili kuleta umoja utakaohakikisha uchumi hauathiriki kwa kupunguza wafanyakazi au kupanga mikakati itakayokuja kuumiza uchumi miezi ya baadae.

 

Mwenyekiti huyo alieleza kuwa, ZATI imechukua hatua ya kuwatuliza wanachama wake ili wasifanye haraka ya kuchukua maamuzi yatakayosababisha migongano na suitafahamu baadae, jambo alilosema si malengo ya jumuiya hiyo.

 

Alihitimisha kwa kusema kuwa, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ilizikaribisha wawekezaji wa sekta binafsi kwa nia njema ikiamini katika dunia ya sasa, uchumi wa nchi hujengwa na kuimarika kwa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.

 

Kwa hivyo, alisema kwa sasa ni muhimu kutulia na kuendelea kuchapa kazi na kutoa nafasi ya mjadala, badala ya kufikiria kufunga mahoteli na kupunguza wafanyakazi.

 

Chanzo: Zanzibar Leo

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s