Nurbhai Issa: Shujaa wa mashujaa.

Na Ahmed Rajab

 

MAALIM Nurbhai Issa Nurbhai, aliyefariki dunia Utaani, Wete, Pemba, Juni 30 alikuwa mwanaharakati aliyejitolea kuutetea ukweli bila ya woga.  Ingawa  alikuwa nje ya Zanzibar 1963 kilipoasisiwa chama cha Umma Party  na kwa kipindi chote cha uhai wa chama hicho, Nurbhai alikuwa mmoja wa vigogo wake na mfuasi madhubuti wa kiongozi wake Abdulrahman Babu.

Akiamini kwa dhati kwamba Babu alikuwa ni mmoja wa wanasiasa wa barani Afrika waliobobea na waliokuwa wakiona mbali.  Alikuwa akisema hajauona mfano wake kwa Zanzibar.

Umma Party kilikuwa chama cha kwanza cha Kimarx katika eneo zima la Afrika ya Mashariki, tukikiacha Chama cha Kikomunisti cha Sudan kilichoundwa 1946.

Ingawa alivutiwa na siasa tangu ujana wake, Nurbhai alizidi kupikika kisiasa alipokwenda China ambako alikaa kwa miaka mitano tangu 1962.  Huko alikuwa mwanafunzi wa chuo kikuu jijini Beijing, alikosomea sayansi ya siasa na sheria ya kimataifa.

Wakati huo huo akiwasomesha Wachina Kiswahili.  Wanafunzi wake walikuwa ni Wachina wa mwanzo katika enzi hizo waliokuwa wakisoma Kiswahili.

Aliondoka China 1967 baada ya kumaliza masomo na kupata shahada yake. Badala ya kurudi nyumbani alifanya mpango na wawakilishi wa Ujerumani ya Mashariki aliokutana nao Beijing na akafululiza kwenda Berlin ya Mashariki.  Huko, alikuwa amekwishatengenezewa mambo na Wajerumani aendelee na masomo ya juu. Lakini ilikuwa kwa sharti kwamba lazima kwanza apewe idhini na serikali ya Zanzibar.

Kwa hivyo, akamwandikia waziri wa elimu wa Zanzibar, ambaye siku hizo alikuwa komred mwenzake, Ali Sultan Issa, kumtaka ampe ruhusa ya kuendelea na masomo ya juu Ujerumani ya Mashariki.  Waziri akamwambia kuwa bora arudi nyumbani ende kujenga nchi.  Hapo ndipo Nurbhai alipoamua kurudi Zanzibar.

Kadhia hiyo inaonesha mambo matatu: kwanza, nidhamu ya hali ya juu ya makomred inayopigiwa mfano na wengi. Pili, uzalendo aliokuwa nao kwamba aliposhauriwa arudi kujenga nchi hakupinga; na tatu, kwamba Ali Sultan hakumlazimisha arudi ila alimshauri tu kwa kumwambia “bora rudi ujenge nchi.”

Baada ya kurudi Zanzibar, Nurbhai alikuwa mwalimu kwanza katika skuli ya sekondari ya Ben Bella na baadaye katika chuo cha ufundi cha Karume Technical College.  Kote kuwili akisomesha Kiswahili lakini zaidi katika chuo cha Karume alikigeuza Kiswahili kiwe siasa.

Kwa mfano, alipokuwa akijadili methali za Kiswahili akipenda kuziunganisha na dondoo za Mwenyekiti Mao, kiongozi wa Kikomunisti wa China. Nurbhai akimpenda Mao lakini pia alikuwa na ujasiri wa kuzikosoa baadhi ya sera zake.  Alikuwa wa mwanzo miongoni mwa makomred kutambua kwamba hali ya mambo China haikuwa kama wengi wetu tulivyokuwa tukifikiria.  Baadhi yetu ilituchukua muda mrefu kung’amua kuwa licha ya ugwiji wake Mao pia alikuwa dikteta.

Pakitokea tukio nchini basi alikuwa akilielezea kwa kuwafahamisha wanafunzi wake athari za kisiasa za tukio hilo.

Safari moja aliwahi kuwaambia wanafunzi kwamba chama cha Afro-Shirazi Party (ASP), kilichokuwa kikitawala Zanzibar, hakikuwa chama bali lilikuwa “genge la wahuni”.

Baadhi ya wanafunzi wakereketwa wa ASP waliwahi kumshitaki kwa Mwalimu Mkuu wa Shule. Alipoitwa ajieleze aliyakariri maneno hayohayo kwa Mwalimu Mkuu na akamwambia anaweza kuyasema, tena na tena, popote pale.

Siku zote akionesha dhahir bila ya kificho kuwa hakuwafikiani na uongozi wa ASP na wakati mmoja aliwahi kusimamishwa kazi asisomeshe.

Katika muktadha wa harakati za kisiasa za Zanzibar,  Nurbhai alikuwa ni mfano mzuri wa walivyotakiwa wawe wafuasi wa Umma Party au  “makomred”, kwa umaarufu wao.

Wengi watamkumbuka Nurbhai kwa mengi mengine.  Kuna ambao hawatochoka kuikumbuka na kuihadithia mikasa yake kwani alikuwa mtu wa mikasa mingi.  Kuna wataoukumbuka ubongo wake ulivyokuwa ukifanya kazi, haraka haraka, kama cherehani.

Kuna wataomkumbuka kwa sauti zake mbili.  Alipokuwa akihadithia mizaha au mikasa alikuwa akizungumza kwa sauti ya kawaida; lakini alipokuwa akilizungumzia jambo lenye uzito au lenye umuhimu mkubwa sauti yake ikibadilika na kuwa nzito kuliko ilivyokuwa kwa kawaida.

Wengine watamkumbuka Nurbhai kuwa hakuwa mtu aliyependa kuropokwa na kuzungumza ovyo. Alipoulizwa jambo alikuwa hafanyi papara kujibu bila ya kulitafakari hilo jambo na kujua anajibu nini.

Wanafunzi wake wa skuli ya sekondari ya Ben Bella alikokuwa akisomesha Kiswahili kuanzia 1968 hadi 1972 watamkumbuka kwa hima yake ya kusomesha, uchangamfu wake uliopita kiasi, ufaswaha wake wa lugha, na kwa mapenzi yake ya tenzi na mashairi ya Kiswahili.  Watamkumbuka kwa mshororo unusu ufuatao aliokuwa akipenda kuwasomea wanafunzi wake waliokuwa watukutu au watoro:

“Mmbeja wangu mmbeja, leo wantenda haya, kesho utantendaje?”

Kuna shairi moja la beti mbili la Muyaka bin Haji Ghassani liitwalo “Utanitendaje?” na nadhani Nurbhai alidokoa mshororo unusu huo kutoka kwenye shairi hilo na akapachika na ya kwake, jambo ambalo linaruhusiwa kwa kukidhi haja ya kuwaasa wanafunzi wake. Kwa wapenzi wa mashairi, hilo shairi la Muyaka lasema hivi:

“Risala alipokuja, na maneno kunambiya

Nalikaa kukungoja, nawe hukunitokeya

Likupeteni mmbeja, lililokukuzuwiya?

Leo wanitenda haya, kesho utanitendaje?

 

Si vyema hivyo si vyema, umekwisha jitendaya

Muungwana ni kalima, lakwe likatimiliya

Na kwamba hutaandama, ujibupo si vibaya

Leo wanitenda haya, kesho utanitendaje?”

Lakini wengi visiwani Zanzibar watamkumbuka Nurbhai kuwa mtu wa msimamo.  Alikuwa hayumbiki wala hakukubali kuyumbishwa.  Wengi zaidi watamkumbuka kwa ushujaa wake wakati wa ile iitwayo “kesi ya uhaini”. Kesi hiyo ilihusika na mauaji ya Aprili 7, 1972 ya Sheikh Abeid Amani Karume, aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Tanzania.

Upande wa mashitaka ulidai kwamba washitakiwa walikula njama ya kuipindua serikali ya Zanzibar iliyopelekea kuuawa kwa Karume.  Takriban washitakiwa wote walikuwa makomred.  Kesi hiyo ilikuwa ya maajabu.  Sitostaajabu akizuka mwandishi wa tamthilia akaandika matini ya tamthilia kuhusu kesi hiyo iliyoendelea kwa miaka.

Kesi iliendeshwa katika yale yaliyokuwa yakiitwa “Mahakama ya Umma”. Ulimwengu haujawahi kushuhudia vioja kama vilivyokuwa vikizuka kwenye Mahakama hayo.  Baadhi ya majaji wake walikuwa watu wasiowahi kusoma skuli. Mmojawao alikuwa muuza njugu.

Washtakiwa hawakuruhusiwa kuwa na mawakili wa kuwatetea.  Mshitaki Mkuu wa serikali, Wolfango Dourado, ndiye aliyewashitaki na wakati huohuo ndiye aliyejidai kuwatetea.

Machi 29, 2012 baada ya kufariki Dourado niliandika makala kwenye gazeti hili (Buriani Wolfango Dourado: Shujaa na mzalendo) ambamo nilieleza jinsi Dourado alivyokuwa akiwadharau na kuwakashifu washitakiwa kwa baadhi ya maswali yake. Hata hivyo, niliongeza kuandika, Dourado aliwapata waliokuwa kiasi chake au waliomzidi kwa maarifa.  Nikamtaja Nurbhai kuwa mfano.

Nurbhai alimtoa jasho kwelikweli Dourado.  Majibizano yao Mahakamani yanaweza yakatungiwa opera au tamthilia ya mtindo-naghama.

Nurbhai alikuwa mshtakiwa namba 14 katika kesi hiyo. Ilipomalizika, aliibuka akiwa shujaa wa mashujaa na mfano wa ushujaa wa makomred. Aliithibitisha ile sifa ya makomred ya kutokubali kutishwa na ya kutoogopa kifo.

Safari moja aliyaambia hivi Mahakama:  “Mimi sikuwa najua huu mpango wa Mapinduzi, abadan, lakini kwa namna nilivyochoka na Serikali hii, yoyote yule angenijia kutaka ushauri wa mabadiliko ningelimuunga mkono.”

Mara nyingine akimzungumza Dourado alimwambia hivi Jaji: “Bwana Jaji inakuwaje huyu Dourado awe kazaliwa Zanzibar hajui Kiswahili? Hata hicho Kiingereza anachozungumza anafanya makosa tele ya grammar [nahau au sarufi]. Nitaomba na miye niruhusiwe nijitetee kwa Kiingereza nipambane naye.”

Dourado hakusema uongo alipomshutumu Nurbhai kuwa akikichukia chama cha ASP na serikali yake.  Alipokuwa akijitetea Mahakamani, Nurbhai mwenyewe aliwahi kusema: “Hakika Serikali ya ASP imejaa majuha ndio matokeo yametufikisha hapa.”

Siku nyingine alisema hivi: “Afro-Shirazi kama jiwe ukilibeba litakufwata, ukiliacha ujihadhari lisije kukubanja kidole.”

Nurbhai hakuwaacha hata Majaji waliokuwa wakiisikiliza kesi yake. Aliwahi kuwaambia: “Tutegemee nini kuhukumiwa na eti majaji wasiokwenda hata skuli”.

Ujasiri aliouonesha alipokuwa akijitetea Mahakamani, ulimfanya Nurbhai  azidi kuteswa alipokuwa anarudishwa jela. Ndipo alipolazimika wakati mmoja kumwambia hivi Jaji: “Bwana Jaji nihakikishie haya nitayoyasema hayatofanya nikirudi huko korokoroni nikageuzwa pweza kutandikwa kwa magongo wala sio bakora.”

Nurbhai aliteswa sana alipokuwa jela.  Yaliyomponza yalikuwa maoni yake dhidi ya ASP na serikali yake, maoni aliyoyaandika kwenye shajara yake, kitabu cha kumbukumbu zake za kila siku kilichogunduliwa nyumba yake ilipopekuliwa alipokamatwa.

Shajara hiyo ilipofikishwa Mahakamani na alipoulizwa kwa nini aliiandika alijibu kwa kusema: “Kila aliyesoma hufanya hivyo na asiyesoma hafanyi hivyo.”  Shajara hiyo ama ilichomwa moto na watu wa usalama au ilichanwachanwa. Haiko tena.

Kuna siku Dourado alidhihirisha wazi jinsi alivyokuwa akikerwa na Nurbhai.  Aliyaambia hivi Mahakama: “Kusema kweli, nilichosema ni kwamba utafika wakati ambapo watabidi wajifunze kuyaheshimu Mahakama na wajue namna ya kujibu.  Kwa sababu ulifika wakati sikuweza tena kuvumilia na mtu niliyemkusudia alikuwa Nurbhai Issa.”

Hapohapo Nurbhai alisimama, akasema: “Nakubali kuwa mimi mhuni.”

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa Mei 8, 1973 watu 81 walipofunguliwa mashitaka. Miongoni mwao 54 walikanusha mashitaka, tisa walikiri na 18 waliokamatiwa Bara walihukumiwa wenyewe wakiwa hawako Mahakamani.  Washtakiwa 34 walipewa hukumu ya kifo, wakiwa pamoja na Nurbhai, Ali Sultan Issa, Badawi Qullatein, Miraji Mpatani na Khamis Abdulla Ameir.

Babu, Kanali Ali Mahfoudh, Amour Dugheish, Hamed Hilal, Hashil Seif  na wengineo waliokuwa Bara walihukumiwa wenyewe wakiwa hawako Mahakamani.

Baada ya kuuawa Karume na kamatakamata ya makomred ilipoanza, zilipita siku nyingi kabla ya Nurbhai kutiwa mbaroni.  Watu wa usalama na askari wakimtafuta lakini iliwachukua muda kumpata.  Kwa vile jina lake ni la Kihindi, babake alikuwa Bohora wa Pemba, wakidhania kuwa atakuwa na sura za Kihindi.

Hawakujua kwamba alichanganya damu.  Ndio maana wakimpita barazani kwake Vuga bila ya kumtambua.  Siku moja askari walimpita mara tatu na wakamuuliza iwapo akimjua Nurbhai. Aliwaambia hamjui.

Ajali yake ilipofika ilikuwa ni bibi mmoja jirani yake (jina tunalihifadhi) aliyemkamatisha.

Baadaye huyo bibi alijitetea akisema kwamba alipoulizwa na askari ikiwa anamjua Nurbhai alijibu kweli kuwa akimjua na alipita kwake na alimkuta barazani amekaa. Askari wakamtaka awapeleke.  Walipotambua kwamba ni yeye waliyekwishampita mara kadhaa walianza hapohapo kumpiga.

Washtakiwa wote pamoja na waliohukumiwa kifo hatimaye waliachiwa huru.  Nurbhai alikuwa wa mwisho kufunguliwa jela 1978. Siku hiyo komred mwenzake Amar Salim (Kuku) akifuatana na wanawe alikodi daladala akenda nao mlango wa nyuma wa jela kumsubiri atoke.  Baada ya muda wakatokea makomred wengine kina Ali Sultan, Said Baes, Miraji Mpatani na wanawe pamoja na Mohamed Abdulla Baramia.

Walipomuona anatoka jela huku akitabasamu Baramia aliwaambia wote wampigie makofi.  Watoto, kwa vile walikuwa watoto, walipiga makofi kwa nguvu. Hawakuwa wakijua kwamba walikuwa wakishuhudia tukio lililokuwa kama pazia, na kwamba nyuma ya pazia hiyo kulifichika historia nyeti.  Kwa vile walikuwa bado watoto hawakujua nini hasa maana ya “historia”.  Ungeliwaambia wakati huo kwamba Nurbhai alikuwa anatoka jela moja na kutia mguu kwenye jela nyingine watoto hao wasingelijua una maana gani.

Nilionana na kuzungumza naye kwa muda mrefu Unguja katika miaka ya 1980 kabla hajahamia Pemba. Nurbhai hakujihusisha na siasa baada ya kurudishwa mfumo wa vyama vingi.  Lakini alikuwa na mawazo sawa na ya hasimu yake Dourado kuhusu Muungano. Wote wakiamini kuwa si wa halali na kwamba kwa namna ulivyo uliizuia Zanzibar isipate maendeleo kwa kuipokonya mamlaka yake.

Baada ya kuhamia Pemba, akiwa Wete akipenda saa za jioni kukaa katika baraza yake nje ya sinema ya huko na  akiwapa “vitu” aliokuwa akiwaamini.  “Vitu” vyenyewe vilikuwa mchanganyiko wa matukio ya kihistoria na darsa za siasa za mrengo wa kushoto.

Chanzo: Raiamwema

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s