Dk. Shein:ZECO jiandaeni kushindana.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amelitaka Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kufanya biashara isiyo na hasara na kuhakikisha linatengeneza faida.

Aliyasema hayo Ikulu mjini Zanzibar wakati akizungumza na  uongozi wa Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira pamoja na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) na uongozi wake.

Alisema umefika wakati kwa shirika hilo kuhakikisha linafanya biashara zake kwa lengo la kuleta tija na hilo linawezekana  kama litafanya juhudi.

Aidha, alisema lazima shirika hilo lihakikishe linaendesha vyema huduma zake kwa wananchi na wale wote wanaodaiwa ni vyema wakalipa madeni yao na wakishindwa kulipa hatua zichukuliwe ikiwemo kuwakatia umeme.

Alisisitiza kuwa iwapo watafanya kazi vizuri mafanikio yatapatikana na kusisitiza kuwa ni lazima deni linalodaiwa na TANESCO lilipwe ambapo serikali kwa upande wake itaendeleza utaratibu ulioweka kuhakikisha kila mwezi deni hilo linalipwa.

Alieleza haja ya kushughulikiwa wafanyakazi wakorofi ambao wamo ndani ya shirika hilo ambao hulisababishia shirika kukosa mapato huku akitumia fursa hiyo kueleza matumaini yake makubwa aliyonayo kwa Bodi ya Wakurugenzi ya ZECO.

Alilitaka shirika hilo kujitayarisha kufanyakazi katika mazingira ya ushindani kibiashara kutokana na mpango wa serikali wa kuishirikisha sekta binafsi katika miradi mbali mbali ya maendeleo ambapo wawekezaji wengi wameonesha nia ya kuwekeza kwenye sekta hiyo.

Nae Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, alieleza haja kwa shirika hilo kuhakikisha linakusanya vyema mapato hasa katika hoteli kubwa kwani zipo nyingi lakini mapato yanayotokana na hoteli hizo ni madogo.

Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, alilitaka ZECO kuangalia vyema ubora wa vifaa vya umeme inavyovitoa ikilinganishwa na bei zake huku akieleza haja ya kuondosha ubinafsi ambao hupelekea kufanya kazi kwa mazoea na hatimae kulitia hasara shirika.

Nao uongozi wa ZECO ulieleza hatua inazochukulia katika kuhakikisha inakusanya mapato yake sambamba na hatua za kusambaza huduma ya umeme kwa wananchi.

Meneja Mkuu wa shirika hilo, Hassan Ali Mbarouk, alieleza hatua zilizofikiwa kati ya shirika hilo na kampuni zitakazouza umeme kwa kufungua vituo katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma kwa ufanisi tofauti na ilivyo hivi sasa.

Alitumia fursa hiyo kueleza mafanikio na changamoto zilizopo katika shirika hilo ikiwa ni pamoja na zile za matumizi ya umeme na kueleza haja ya kuendeleza utaratibu wa kuwepo umeme mbadala hasa wa gesi.

Nao uongozi wa wizara ulieleza hatua za makusudi zinazoendelea kuchukuliwa katika kuhakikisha shirika linapata mafanikio na kuimarisha uhusiano na bodi ya ZECO.

Mapema Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa ZECO, Shafi Mussa Haji, alieleza majukumu, utendaji kazi wa bodi hiyo, mafanikio pamoja na changamoto zilizopo.

Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja wa bodi, shirika limesambaza umeme katika vijiji 47 Unguja na Pemba pamoja na kufungua vituo vya Gamba na Makunduchi vinavyotoa huduma za kiufundi kwa wateja wa maeneo ya karibu na hivi karibuni shirika linatarajia kufungua vituo kama hivyo eneo la Dunga, wilaya ya Kati.

Wakati huo huo, Dk. Shein alisema mabadiliko yaliyofanywa na serikali ndani ya Shirika la Biashara la Taifa la Zanzibar (ZSTC) ikiwemo kutunga sheria yamelifanya shirika hilo kupata mafanikio ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa biashara ya karafuu.

Aliyasema hayo alipokutana na uongozi wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, Bodi ya Wakurugenzi ya ZSTC na uongozi wake.

Alitumia fursa hiyo kulipongeza ZSTC kwa mafanikio iliyopata ikiwa ni pamoja na kutunga sheria ya shirika ya ZSTC namba 11 ya mwaka 2011 na ile sheria ya maendeleo ya karafuu namba 2 ya mwaka 2014.

Alisema azma ya serikali ya kurekebisha vituo vya kununua karafuu na kuimarisha miundombinu ya barabara kwa maeneo yanayozalisha karafuu kwa wingi ni miongoni mwa hatua muhimu za kuliimarisha zao hilo na kukuza bishara ya karafuu.

Alisema kuwepo sheria hizo zitalisaidia kufikia lengo la kuimarika kwa biashara ya karafuu pamoja na biashara nyenginezo ambazo zina maslahi na wananchi huku wananchi na wauzaji wa karafuu nao wakiendelea kufaidika.

Aliutaka uongozi wa ZSTC kutambua kuwa maghala yote ya shirika hilo ni mali yao hivyo ni lazima wayasimamie vyema na kuyatunza.

Nae Balozi alilipongeza ZSTC kwa kuendelea kufanya vizuri na kueleza haja ya kuendelea kufanya vizuri kwani ni shirika la zamani na lina historia yake.

Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Balozi Amina Salum Ali, alisema shirika hilo ni miongoni mwa mashirika yaliyopata mafanikio nchini Tanzania ambalo halijawahi kupata misukosuko.

Alisema masoko ya bidhaa zinazozalishwa na ZSTC yapo hata nje ya nchi na kusisitiza haja ya kuongeza uzalishaji wa bidhaa kwa kuwashirikisha wakulima na vijana kulima mazao ya biashara yakiwemo ya viungo huku akieleza uwezekano wa kuzalisha asali, mbaazi na dengu badala ya karafuu pekee.

Aidha uongozi wa ZSTC ulieleza changamoto zilizopo sambamba na mafanikio yaliopatikana.

Umesema bidhaa za kiwanda cha makonyo zimepata mnunuzi nchini China ambaye ameahidi kunua tani 40 kila mwezi.

Nae Dk. Abdulhamid, alieleza haja ya kukiangalia kwa mtazamo wa uzalishaji wenye tija kiwanda cha makonyo Wawi kwa kukifanyia matengenezo ama kukijenga upya ikiwa ni pamoja na kuweka mashine za kisasa kwa lengo la kuzalisha bidhaa kwa wingi.

Mapema Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya ZSTC, Kassim Maalim Suleiman, alisifu ushirikiano uliopo kati ya bodi na uongozi wa wizara.

Alisema miongoni mwa mafanikio yaliopatikana ni pamoja na kuwa na hakiba ya shilingi bilioni 5.2 kuanzia Julai 2016 hadi Machi 2017.

Alisema kwa mwaka 2016 hadi 2017 Shirika limeuza karafuu tani 2156 zenye thamani ya shilingi bilioni 36.6 huku akieleza haja ya kutotegemea zao hilo peke na badala yake kutafuta mazao mengine ambayo yatalipunguzia mzigo zao hilo.

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s