”Hakuna mchele wa plastiki Z’bar”

BODI ya Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar, imesema hadi sasa haijabaini kuwepo mchele wa plastiki ulioingizwa nchini.

Akizungumza na Zanzibar Leo ofisi kwake Mombasa, Mkuu wa Idara na Ubora wa Chakula wa Bodi hiyo, Aisha Suleiman, alisema taarifa za kuwepo mchele huo zinaonekana katika picha zilizorushwa kwenye mitandao ya kijamii lakini hakuna uthibitisho wowote kama umeingia Zanzibar.

Alisema, serikali imeweka utaratibu maalumu wa uingizaji wa chakula ikiwemo mfanyabiashara kusajiliwa na kusajili bidhaa zake mambo ambayo yanafanywa kwa ajili ya kudhibiti ubora wa bidhaa ili kumlinda mtumiaji.

Alisema katika utaratibu wa kuingiza chakula, kama mzigo umeshafika bandarini kontena hukaguliwa na kufanyiwa uchunguzi ikiwemo kuchukuliwa sampuli ambayo itawakilisha kontena zima kwa ajili ya kufanyiwa vipimo katika maabara yao na kutoa majibu kwa mfanyabiashara kama bidhaa yake inafaa kwa matumizi ya binaadamu au la.

Katika hatua nyengine, alisema wananchi hawapaswi kuwa na hofu ya kutumia mchele katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu ya Eid el ftiri.

Alisema bodi imeandaa udhibiti wa michele na wataendelea kufanya ukaguzi katika sehemu zote zinazoingizwa chakula na kinakohifadhiwa.

Aliwaomba, wafanyabishara kukagua bidhaa zao kabla ya kuondoka dukani kwa ajili ya kujiridhisha ili wasiende kuwauzia wananchi bidhaa zisizo na kiwango.

Wakati bodi hiyo ikisema hivyo, Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) imeanza kufuatilia madai kuhusu kuzalishwa na kutumika kwa mchele wa plastiki nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo, alisema mara baada ya kupata taarifa hizo kupitia mitandao ya kijamii mamlaka hiyo iliunda timu kwa ajili ya uchunguzi.

“Mchele ambao upo na ambao TFDA tunautambua ni wa basmati ambao huitwa Sunrice. Huu wa kutengenezwa kwa plastiki tunaendelea kufuatilia kama taarifa hizo ni za kweli au la,” alisema.

“Tayari nimeshatoa maelekezo kwenye kanda zetu za TFDA zikiwamo Mwanza, Arusha, Mbeya kuanza kufuatilia na ninavyozungumza ni kwamba ukaguzi unaendelea. Kama taarifa hizi ni za kweli tunamwomba huyu aliyetuma ‘clip’ (picha) hii kwenye mitandao ya kijamii ajitokeze ili atusaidie ni wapi alikula mchele huu maana clip inaonyesha mkono tu,” aliongeza.

Baada ya picha hiyo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, ikielezea mchele huo kutumiwa na mamalishe Kariakoo jijini Dar es Salaam, kumezua taharuki na gumzo kwa wakazi wa Dar es Salaam ambao asilimia kubwa hula hasa kwa mama lishe.

chanzo: Zanzibar Leo

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s