Siri nzito CCM, ACT

Tanzania's President elect Magufuli addresses members of the ruling CCM at the party's sub-head office on Lumumba road in Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu

UTEUZI wa viongozi wawili wa ngazi ya juu wa Chama cha ACT-Wazalendo uliofanywa na Rais John Magufuli sasa huenda ukaibua mgogoro kati ya kiongozi huyo na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, MwanaHALISI imebaini.

Aidha, uteuzi huo ambao vyanzo vya habari vya gazeti hili vinaueleza kama uliofanywa bila ya Zitto kushauriwa, unaelezwa pia kwamba unajenga picha ya muendelezo wa mtazamo wa Rais kuashiria kudhoofisha siasa za upinzani.

Zitto ni Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo, chama alichokianzisha wakati taifa likikabiliwa na uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2015. Wakati huo Zitto alikuwa anatekeleza mkakati wa kubaki kwenye siasa za kitaifa baada ya kulazimika kuondoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alichokitolea jasho tangu akiwa kijana mdogo.

Lakini wakati akiwa anaongoza chama kichanga kilichotoka na mbunge mmoja tu kwenye uchaguzi mkuu, Zitto anajikuta jitihada zake zikivurugwa kwa viongozi wenzake wanaounda Kamati Kuu, kuteuliwa na Rais Magufuli kuwa watendaji serikalini.

Juzi Jumamosi, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais (Ikulu), ilitangaza kwamba Rais amemteua mwenyekiti wa ACT Wazalendo Anna Mghwira, kuwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro. Anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Said Meck Sadik aliyejiuzulu kwa sababu ya kuchoka.

Rais Magufuli ambaye naye anaonekana kubadilisha dhamira yake ya awali ya kutoteua alichoita “mtoto wa kambo” kwenye serikali anayoongoza – alimaanisha hatoshirikisha asiyekuwa mwanachama kindakindaki wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) – alianza kumteua Profesa wa Sayansi ya Siasa, Kitila Mkumbo, kuwa katibu mkuu.

Katika uteuzi uliofanywa Aprili 4, 2017, Rais alimteua Prof. Kitila kuwa katibu mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, kujaza nafasi iliyoachwa wazi baada ya Mhandisi Mbogo Mfutakamba kustaafu utumishi serikalini.

Prof. Kitila aliteuliwa wakati wiki kadhaa kabla, mwenyewe alilaumu hatua ya Rais Magufuli kuteua wahadhiri wanaofundisha vyuo vikuu na kuwaingiza serikalini kuwa watendaji.

Alisema utaratibu huo haufai kwa sababu unaondoa wataalamu katika kazi muhimu ya kuwajenga vijana kuja kuwa wataalamu wa baadaye katika taifa.

Pamoja na Prof. Kitila, uteuzi ulifanywa pia kwa Dk. Leonard Akwilapo anayekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Kabla alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo.

 

Pia alimteua Maimuna Tarishi kuhamia Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge) kama katibu mkuu akitokea Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Kabla yake, katibu mkuu wizara hiyo alikuwa Mussa Uledi ambaye Rais alitengua uteuzi wake.

 

Rais Magufuli alimteua Dk. Ave Maria Semakafu kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kujaza nafasi iliyoachwa na Dk. Akwilapo aliyepandishwa. Kabla ya uteuzi huo, Dk. Semakafu alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).

Gazeti hili limefahamishwa na mtoa taarifa ndani ya serikali kwamba katika uteuzi wa viongozi hao wawili wa ACT-Wazalendo, Rais Magufuli anaelekea katika kujiandaa na uchaguzi mkuu ujao wa 2020.

“Hili unalolisema wewe naliamini, lina mantiki yake. Lakini huku tunavyochukulia hatua hii ya mkuu kuteua watendaji wa ngazi ya juu kutoka chama kama ACT-Wazalendo, ni ya kujenga mazingira mazuri ya uchaguzi ujao,” amesema mtoa taarifa huyo.

Alikuwa ameulizwa kama kwa hatua hiyo ya kuteua viongozi kutoka ACT-Wazalendo, Rais amekusudia kumdhoofisha Zitto kwa sababu ya kinachoelezwa kuwa “hawaivi.”

Zitto amekataa katakata kuzungumzia suala hili. Alipoulizwa anajisikiaje kukuta chama alichokianzisha kwa nguvu kubwa kinamegwa kwa viongozi wenzake “kuchotwa na rais” na kupewa nafasi za uongozi serikalini, alisema, “Niachieni. Naona sina la kuzungumza katika jambo hili.”

Lakini, kutoka ndani ya chama hicho, msiri mmoja ameitonya MwanaHALISI kuwa tangu kusikia tangazo la uteuzi, Zitto amebadilika. “Amekuwa mkimya kuliko kawaida. Lakini ukimuangalia kwa mbali, unabaini kama ameguswa na suala hili.”

Yapo maoni ndani ya ACT-Wazalendo kuwa Rais Magufuli ameamua kukidhoofisha chama hicho huku akilenga hasa “kumkomoa Zitto binafsi.”

Mwandishi wa gazeti hili alipouliza kwani Zitto amefanya lipi baya kwa uongozi wa Rais Magufuli, msiri huyo alisema, “mara kadhaa kiongozi wetu mkuu amekuwa akiikosoa serikali mpya ya CCM.”

Alitoa mfano wa matukio yaliyosababisha Zitto aonekane kama mpinzani mahsusi wa Rais Magufuli na utendaji wake; suala la uhaba wa chakula ulioikumba sehemu kubwa ya nchi tangu mwishoni mwa mwaka jana.

Zitto alifikia hatua ya kujiapiza kwamba serikali haina chakula cha akiba kwa sababu imeshindwa kununua msimu uliotangulia. Serikali ilitangaza inacho chakula cha kutosha kwenye maghala ya akiba, Zitto alisema anauweka rehani ubunge wake iwapo ataoneshwa tani zipatazo milioni 1.5 za chakula kinachotajwa kuwepo maghalani.

Serikali ilishindwa kuonesha chakula hicho na Zitto akapata nguvu ya kusema, iwapo mwananchi yeyote atafariki dunia kwa njaa, Rais na serikali yake watabeba lawama hizo.

Zitto pia alikuwa mmoja wa wanasiasa wachache nchini waliothubutu kuzungumzia mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar baada ya uchaguzi mkuu. Alipata kusema mgogoro huo uliotokana na kufutwa kibabe kwa matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25, 2015, utatuliwe kwa Rais Magufuli kusimamia utangazaji wa matokeo ya uchaguzi uliokwishafanyika.

“Suala la Zanzibar lisidharauliwe. Matokeo yatangazwe na mshindi aapishwe. Hatuwezi kutazama tu Katiba inakanyagwa. Vinginevyo Maalim Seif (Maalim Seif Shariff Hamad wa CUF) apate Jaji amwapishe na aunde serikali mara moja na kuanza kutumikia Wazanzibari, serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar,” alisema katika andiko lake la Novemba 9 mwaka 2015.

Alisema haikuwa sahihi kwa Jecha Salim Jecha, mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufuta hata matokeo ya wawakilishi Oktoba 28, 2015, ambayo yalishatangazwa na washindi kukabidhiwa vyeti vya ushindi. Sehemu kubwa ya kura za urais zilishahakikiwa na kuonesha Maalim Seif alikuwa anaongoza.

Licha ya kuahidi kushughulikia mgogoro huo wakati analihutubia bunge kwa mara ya kwanza, Rais Magufuli hakuchukua hatua yoyote kumaliza tatizo.

Lakini alichokifanya baadaye, ni kutamka kuwa hana la kufanya kwa sababu kila kitu kilifanyika kwa mujibu wa sheria na katiba. Alithubutu kumsifia Jecha kuwa alifanya kazi kwa asilimia 100 na angekuwa yeye Rais wa Zanzibar, angemtunuku zawadi Jecha.

Kuna siku Rais Magufuli alisema uchauzi umekwisha na Dk. Shein ndiye rais wa Zanzibar, hakuna atakayembadilisha. Alimtaka Dk. Shein kufanya kazi bila ya hofu na akitokea anayemsumbua, amwambie atamdhibiti mara moja.

Rais Magufuli anaonekana kukengeuka kauli yake ya kutoteua viongozi kutoka upinzani kuwajumuisha katika serikali anayoiongoza. Akiwa ziarani Zanzibar mwaka jana, alisema kwenye mkutano wa hadhara: “Sijawahi kuona rais umechaguliwa upate asilimia 92, bado uwachukue watu wa vyama vingine unawaingiza kwenye serikali yako.

 

“Mimi nilipata asilimia 58, hakuna wa chama kingine kuingia na wala hataingia. Lakini baba huyu kwa upole wake amepata 92 bado analeta wengine kwenye serikali yake mimi nimepata 58 hakuna atakaekanyaga mguu kwenye serikali yangu.”

 

Swali muhimu katika hatua hiyo mpya, ni nini kimetokea kati yake, CCM anachokiongoza, na ACT-Wazalendo?

Anna Mghwira ameteuliwa wakati hayupo nchini. Jitihada za kumpata ili kueleza kama ameridhia uteuzi uliofanywa, hazikufanikiwa. Inaelezwa yuko nchini Marekani kuhudhuria mkutano wa wanawake duniani.

Mghwira ndiye aliyekuwa kiongozi wa juu kabisa wa chama hicho. Lakini baada ya uchaguzi mkuu, chama kilifanya mabadiliko ya Katiba yake na kuunda nafasi ya “kiongozi mkuu” ambayo alivikwa Zitto.

Zitto alianzisha chama hicho na baadhi ya vijana aliotoka nao Chadema, akiwemo Habibu Mchange na Samson Mwigamba. Wote wameachia ngazi.

Kitu kingine ambacho huenda kimemkera Rais Magufuli ni hatua ya Zitto kujitokeza bega kwa bega kukaa na Freeman Mbowe, baada ya mwenyekiti huyo wa Chadema kutangazwa kama mmoja wa viongozi wa kisiasa wanaokabiliwa na tuhuma za kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya.

Katika kauli iliyoonesha mshikamano imara wa Mbowe na kambi ya upinzani, Zitto alisema kama “Mbowe angekuwa ni muuza madawa ya kulevya, basi mimi ningekuwa punda wake.”

Alichomaanisha Zitto ni kwamba ana historia ya miaka mingi ya uhusiano wa kikazi na Mbowe, hasa kwa kuwa ndiye aliyemwezesha kufikia hatua aliyoifikia kisiasa. Zitto alipatwa mkasa wa kukorofishana na Chadema wakati akiwa Naibu Katibu Mkuu na mjumbe wa Kamati Kuu.

Hata katika mvutano ulioibuka hivi karibuni baada ya Rais kukabidhiwa ripoti ya kamati aliyoiunda kuchunguza kiwango cha madini kwenye mchanga unaotoka kwenye migodi ya dhahabu nchini, Zitto alisema kinachotatiza ni sheria ambazo zinaruhusu rasilimali za Watanzania kusafirishwa nje ya nchi.

Alisema hata kama Rais Magufuli anasema ana nia njema, alichotakiwa kuanza nacho katika kudhibiti kufisidiwa kwa rasilimali za Watanzania, ni kubadilisha sheria. Itamkwe wazi rasilimali zote nchini ni mali ya Watanzania.

Uteuzi wa Mghwira unafanyika huku Zitto akiongoza kongamano la “Rasilimali za Madini” kwenye ukumbi wa Makumbusho ya Taifa, Dar es Salaam.

Hatua hiyo imezidi kumuonesha Zitto kuwa hakubaliani na alichokifanya rais kwa kuwa anaamini chanzo cha matatizo yote ni serikali ya CCM kuidhinisha sheria inayoruhusu kuwepo usiri mkubwa wa mikataba ya madini kati ya serikali na wawekezaji.

Mtumishi wa Bunge ameliambia gazeti hili kuwa anakumbuka Zitto alimshika koo Magufuli alipokuwa waziri wa ujenzi, baada ya kuibuka kashfa ya wizara hiyo kupata hati chafu kutokana na Sh. 253 bilioni ambazo wizara iliziomba kwa ajili ya utekelezaji wa miradi maalum, kutumiwa isivyostahili.

Wakati huo akiwa mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia Chadema, Zitto aliibebea bango kashfa hiyo hadi kushikilia mshahara wa waziri Magufuli. Kashfa hiyo ilitokana na ugunduzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

“Hili suala inawezekana halijasahaulika mawazoni mwa mkuu. Alimhangaisha sana kutoa maelezo ya kujiokoa.

Akiwa Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Zitto aliwakataza wabunge wa Chadema kumsifia waziri Magufuli.

“Wabunge wengi wa Chadema walikuwa wakisimama wanamsifu Magufuli kwa utendaji wake, Zitto akawaonya kuwa Magufuli alizitumia vibaya sifa hizo kwa kuushusha hadhi upinzani. Haya mambo si rahisi kuyasahau na hasa mtu akiwa amefikia hatua ya maamuzi ya mwisho katika nchi,” alisema kada wa CCM.

Mhariri wa gazeti la kila wiki ambaye ametaka asitajwe jina, alisema, “Kimsingi Magufuli na Zitto hawajawahi kuiva chungu kimoja. Ni Zitto aliyeahidi kuwa Magufuli atakuwa Rais wa muhula mmoja. Kwamba mwaka 2020 atakataliwa na wananchi.”

Leo hii Magufuli ndiye Rais wa Tanzania. Zitto ni Kiongozi wa ACT-Wazalendo, chama kichanga ambacho kinahitaji uwekezaji mkubwa ili kiimarike na kukua. Unafikiri inakuaje.

Mwandishi wa makala za uchambuzi nchini, Lukman Maloto anasema “Kitila na Mghwira walikuwa nguzo hasa za ACT. Magufuli kawatwaa na kukiachia pengo chama, kisha kukijaza kashfa kuwa viongozi wake wana nasaba na CCM.

Kipindi hiki Zitto lazima ajue Magufuli ni nani. Magufuli ni Rais. Anatumia mamlaka yake kisayansi kukidhoofisha na kukipa wasifu mbaya chama cha ACT. Watu wakione chama ni ndugu na CCM, jambo ambalo ni sumu mbaya kwa siasa za upinzani Afrika.”

Zitto wewe endelea kukomaa na usahihi wa sheria za madini, endelea kupambana kudai utawala wa sheria, endelea kunadi maono yako kuwa Magufuli ni Rais wa muhula mmoja, halafu yeye anakupiga kwa vitendo tu.

Mwandishi mmoja wa habari wa gazeti la Uhuru amesema anasubiri kuona itakujae kwa kuwa kwa utaratibu wa CCM, mtu anayeteuliwa mkuu wa wilaya au mkuu wa mkoa anakuwa pia mjumbe wa kamati ya siasa ya eneo hilo. “Huyu dada ataingiaje kwenye kikao hicho wakati yeye ni ACT-Wazalendo?” Anauliza.

Chanzo: MwanaHalisi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s