Njaa mwana malegeza, shibe mwana malevya

Disemba 10, 1963 ndio siku ya Uhuru wa Zanzibar lakini imekuwa haiadhimishwi kabisa

JAN 19, 2017 

SINA tena haja ya kushawishiwa.  Sasa ninaamini kwamba ni kweli baadhi ya viongozi wetu ni miongoni mwa wale wanaotajwa kwenye Qur’ani kuwa ni “summun, bukmun, umyun” (wasiosikia, wasiosema na wasioona). 

Qur’ani inaendelea kuwaelezea kuwa hawatoweza tena kurudi katika njia iliyonyoka. Kwa ufupi, wameangamia.

Tunapowaangalia na kuwatathmini baadhi yao kinachodhihiri ni mwelekeo wao wa kuliangamiza taifa. Sidhani kama wanafanya hivyo kwa kusudi ila ni kwamba hayo ndiyo majaaliwa ya wale wasiosikia au wasiokubali kusikia.

Wanasemeshwa kila uchao. Wanaambiwa: “Jamani, hivi sivyo! Nchi haiendeshwi namna hii kwa kibri, vitisho na ujuaji mwingi.”  Hawasikii. Utadhani masikio yao yamezibwa kwa vizibo vyenye kuzuia nasaha zisipenye.

Hawa huwa wanajiona kuwa wako juu ya jamii.  Na kweli wako juu ya jamii kwa sababu wameikalia kichwani na huku wanashindana nayo.  Waonavyo wao ni kwamba jamii haijui kitu na ikijua basi haina haki ya kutamka inachokijua.

Hivi sasa wananchi, ambao ndio jamii yenyewe, wanajua kwamba wanakabiliwa na njaa lakini hawana ruhusa ya kuyasema hayo. Wanakatazwa.

Baadhi ya hao viongozi wanashikilia kwamba hakuna mwenye haki ya kutangaza kwamba kuna njaa nchini isipokuwa Rais.  Ni kama kuwaambia abiria walio garini kwamba walionapo shimo kubwa mbele yao hawana haki ya kumtahadharisha dereva.

Wanavyoamini wao ni kwamba haki ya kusema kuna shimo mbele ni ya dereva tu. Mantiki hii haiingii akilini.  Kwa hakika, ni wazimu mtupu.

Jingine wanaloliamini ni kwamba mambo yote yasemwayo si lazima yawe sahihi. Yenye hakika ya kuwa sahihi ni yale wayasemao wao.  Wayasemayo wengine katika jamii, hususan, katika kuukosoa mwenendo wa serikali, huwa ama ni chokochoko au ni uchochezi.  Kwa mujibu wao siku zote wananchi wenye kuikosoa serikali huwa “wanatumiwa” ama na watu wa nje, wafanyabiashara au wanasiasa wenye uchu wa madaraka.  Utafikiri kama vile wao hawana uchu wa madaraka.

Kwa wao uongozi si namna ya kulichunga taifa na kulielekeza kwenye mustakbali mwema. Wanavyofikiri wao kuongoza ni kuwatia mikiki wananchi au kuzusha mapambano na wale wenye kuwaelekeza wanapopotea njia, wanaowasemesha wanapokosa na wanaowaonyesha makosa yao.

Katika nchi zenye mfumo wa demokrasia iliyokomaa, uongozi ulio imara na wenye nia safi huuona upinzani kuwa ni mshirika wake mkuu katika harakati za kuleta maendeleo na si kuwa ni adui wa taifa.

Kiongozi anapoanza kumfikiria kila anayemkosoa au amwambiaye ukweli kuwa ni adui na akamchukulia hatua za kimabavu huwa anazifuata nyayo za madikteta wengine waliotangulia duniani.

Mengi yamekuwa yakisemwa Tanzania siku mbili hizi kuhusu kuwapo kwa njaa nchini.  Wananchi wa kawaida, wanasiasa na hata mashekhe na mapadri wamekuwa wakilizungumzia suala hili. Wote wamekubaliana kwamba njaa iko nchini. Watawala hawataki kuzisikia habari hizo.

Kichwa cha maneno cha makala haya ni usemi ambao kwa maneno mepesi una maana ya kwamba, njaa inamlewesha mtu. Ni kusema kwamba mtu akiwa na njaa kubwa basi hiyo njaa humvunjavunja viungo akawa hajifai, huwa hana nguvu ya kufanya kitu, na akishiba sana hiyo shibe humlewesha.

Uwezo wa njaa wa kumlegeza mwenye nayo umegusiwa na mshairi Sarahan bin Matwar bin Sarahan al-Hudhry Hinawy, (1841-1926) mzalia wa Pondeyani, Chake Chake, Pemba.

Anasema kuhusu njaa kwenye shairi lake  “Njaa hailei mwana”. Shairi hilo limo katika kitabu cha mkusanyiko wa mashairi kiitwacho “Kale ya Washairi wa Pemba: Kamange na Sarahani”, kilichohaririwa na Abdilatif Abdalla na kilichochapishwa 2011 na Mkuki na Nyota.  Tunazinukuu beti mbili tu hapa:

“Njaa khaswa ukishiba, wasema hutaiyona
Njaa ina taghiliba, si mkongwe si kijana
Njaa yavunja mahaba, mkeo mkipendana
Njaa hailei mwana, nifanyeje hali sina!

Njaa haina huruma, japokuwa kitu huna
Njaa haina uzima, pale utapoiyona
Njaa mara hukukama, ukaona nguvu huna
Njaa hailei mwana, nifanyeje hali sina!..”

Sarahani amesema humo kwamba njaa ina taghiliba, yaani udanganyifu, kwa mzee na kwa kijana.  Na inapokukama, yaani inapokubana, utaona nguvu huna.

Utaishiwa.  Lakini haya ni kwa wale wanaobanwa na njaa.

Kwa upande mwingine, mwenye kushiba huwa haijui njaa. Madhali yeye anakula na anashiba, njaa kwake huwa ni kitu au jambo geni.

Njaa imezungumzwa na wengi na mwenye nayo humuuma.  Mwenye kushiba na asiyeijua njaa huwa kama mtu aliyeingiliwa na maruhani kichwani; husema mambo ya ajabuajabu.  Kwa hivyo, haishangazi tunapowasikia baadhi ya
viongozi wa Tanzania wakikana kama kuna njaa nchini.

Marie Antoinette, malkia wa mwisho wa Ufaransa kabla ya Mapinduzi yaliyozusha machafuko ya kisiasa na ya kijamii toka 1789 hadi 1799, anajulikana sana kwa usemi ambao pengine hata hakuusema yeye.

Inavyosemekana ni kwamba alipoambiwa ya kuwa wakulima wadogo vijijini hawana mikate na wana njaa, alisema:  “Waachie wale keki”.

Ama kweli mwenye kushiba haijui njaa. Watu wasioweza kumudu unga na maji ya kuokea mkate watawezaje kumudu hamira, mayai na vinginevyo vya kufanyia keki?

Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambaye baada ya kuundwa Muungano alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania, alikuwa na usemi kuhusu njaa aliokuwa akipenda kuudhukuru mara kwa mara. Akipenda kusema: “Hakuna ulevi mbaya, kama ulevi wa shibe.”

Nadhani wenye kukana kama kuna njaa ndio miongoni mwa hao waliolewa shibe. Hao ndio wenye kukana kwa nguvu kwamba hii leo kuna njaa Tanzania.

Tukiwaacha hao wenye kuyakana ya leo wapo na wengine miongoni mwao wenye kukana na ya kale pia. Zanzibar, kwa mfano, kuna wanaoshikilia kwamba si kweli ya kuwa Zanzibar  ilipata uhuru Desemba 10, 1963.  Tena hawa ni viongozi waliosoma walioiona dunia; wenye kuijua historia.

Juu ya yote hayo wanawaambia wananchi wenzao wasidanganywe, kwamba Zanzibar haikupata uhuru 1963.  Wanachofanya ni kujaribu kuificha historia na kukighilibu kizazi cha sasa.

Hawaoni haya kwamba wanayakana mambo ambayo baadhi yetu tuliyashuhudia katika sherehe za Uhuru zilizofanywa kwenye uwanja wa Cooper’s Ground, ambao siku hizi unaitwa uwanja wa Maisara.

Tena hayo ni mambo yaliyo kwenye kumbukumbu za ndani na nje ya nchi licha ya jitihada zao za kuzifuta kumbukumbu hizo.

Wangetaka wangeliweza labda kusema kwamba uhuru huo ulikuwa wa bendera tu na haujaikomboa  kikweli Zanzibar.  Na hapo uhuru huo wa Zanzibar ungekuwa sawa na uhuru wa nchi nyingi nyingine za Kiafrika, ikiwemo Tanganyika, kwani unaweza kuhoji kwamba nchi zote hizo zilikuwa na uhuru wa bendera tu kwa sababu nyenzo za kiuchumi zilikuwa bado mikononi kwa watawala wa kikoloni.

Lakini kukanya kwamba Zanzibar ilikuwa haikukabidhiwa hati za uhuru Desemba 1963 ni kichekesho na upotoshaji wa historia.  Swali kuu la kuulizwa hao watawala wetu ni hili: ingelikuwa Zanzibar haikupata uhuru 1963 kweli mgeliweza kumpindua Mwingereza aliyekuwa akiitawala nchi?

Ninavyokumbuka ni kwamba mkesha wa kuamkia 10 Desemba, 1963, watu walimiminika kwa mkururo  katika uwanja huo kusubiri kulishuhudia tukio hilo la kihistoria.

Miongoni mwao alikuwa Karume, kiongozi wa chama cha upinzani cha Afro-Shirazi Party (ASP), ambaye kabla ya sherehe hizo alikwishatoa taarifa ya kuukaribisha uhuru. Na si Karume peke yake aliyehudhuria sherehe za uhuru.  Viongozi wenzake wengine wa ASP nao walihudhuria.

Ilipogonga saa sita za usiku juu ya alama, tuliiona bendera ya Uingereza ikiteremshwa kwenye mlingoti mmoja na ya Zanzibar huru ikipandishwa kwenye mlingoti mwingine.  Nukta hiyo, pale bendera ya Uingereza ilipofika chini na ya Zanzibar huru ilipofika juu ya mlingoti na kuanza kupepea ndipo Zanzibar mpya — na huru — ilipozaliwa.

 Mkuu wa dola aliyekuwa mtawala wa kikatiba alikuwa sultan Seyyid Jamshid bin Abdullah bin Khalifa, aliyekabidhiwa hati za uhuru na Duke wa Edinburgh, Prince Philip,  mume wa Malkia wa Uingereza.

Serikali mpya ya Zanzibar ikiongozwa na Sheikh Muhammed Shamte Hamadi, kiongozi wa chama cha Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP).   Ilikuwa serikali ya mseto wa chama hicho cha ZPPP, kilichokuwa kidogo, na kile kikubwa cha Zanzibar Nationalist Party (maarufu Hizbu).

Na ni Shamte, ambaye siku chache baada ya uhuru, aliongoza ujumbe kutoka Zanzibar kwenda makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, kukabidhiwa kiti cha Zanzibar katika Umoja huo. Kiti hicho kilikuwa alama ya kwamba Zanzibar ni dola huru iliyokuwa sawa na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa.

Bendera ya Zanzibar katika Umoja wa Mataifa ilipandishwa siku ileile ilipopandishwa ya Kenya katika sherehe iliyohudhuriwa na aliyekuwa makamu wa Rais wa Kenya wakati huo, Jaramogi Oginga Odinga.

Wenye shibe si kwamba huwa hawaijui njaa tu, lakini shibe huwalevya na kuwafanya wayakane mambo ambayo ni hakika yalikwishakutokea, kwa mfano uhuru wa Zanzibar wa Desemba 1963.

Chanzo: Raia Mwema

Baruapepe: ahmed@ahmedrajab.com

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s