Wanaye rais wao wa moyoni

Maalim Seif Sharif Hamad
Maalim Seif Sharif Hamad

VIONGOZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameishiwa hoja. Wanapojitokeza mbele ya umma wa Wazanzibari na Watanzania, na kokote waendako, hawawezi kuzungumza kwa ujasiri na uchangamfu kile hasa kilichotokea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 wa Zanzibar.

Yeyote miongoni mwao akitaka kusema, atalitafuta la kusema, na akilipata, atalisema katika lugha ya kulazimisha aaminike. Atajibaraguza tu. Ni kwa sababu kubwa moja – wanajua kwa uhakika wanaiongoza Zanzibar kwa mabavu.

Wanaongoza kwa mabavu maana hawana ridhaa ya wananchi kupitia uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015. Wananchi wa Zanzibar wangekuwa wametoa ridhaa kwa uongozi wa CCM, isingekuwepo sababu ya kulazimishwa kumridhia Dk. Ali Mohamed Shein.

Pale rais wa jamhuri, Dk. John Magufuli alipotoa matamshi ya kuwataka wamtii Dk. Shein kwa kusema “ndiye rais wa Zanzibar na hakuna wa kumuondoa mpaka uchaguzi mwingine ufike mwaka 2020,” alikuwa analazimisha wananchi wamkubali kiongozi wasiyemchagua.

Alifanya hivyo, tena katika lugha ya kusononesha wananchi, kwa kujua huyo anayetaka wananchi wamridhie hawakumchagua. Labda rais alijuilishwa na wasaidizi wake wa kiusalama kwamba Zanzibar kungali na upinzani mkali kwa umma kumkubali Dk. Shein, na hiyo imetokana na ukweli kuwa hakuwa chaguo lao kupitia uchaguzi ule.

Hata pale alipoamua kumuita Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), na kumpongeza na kumtakia tuzo kwa alichosema “amefanya kazi yake vizuri kwa asilimia zote,” alijua anajitoa kimasomaso katika dhana ile ya ‘funika kombe mwanaharamu apite.’

Tuseme itokee Dk. Shein amemtunuku tuzo Jecha, kama alivyosikia rai ya Rais Magufuli kwenye mkutano wa hadhara Septemba mwaka jana, ninaamini Jecha ataendelea kuumia moyo.

Mtumishi mstaafu huyu serikalini anayefahamika kuwa kada wa CCM, anaumia moyo kwa sababu anajua alikanyaga haki. Mwenyewe alikiri mbele ya makamishna wa Tume kuwa alilazimika kufuta uchaguzi ili “kukiokoa Chama cha Mapinduzi.” Kumbe alikistiri chama chao.

Jecha alitangulia kuomba msamaha makamishna hao akiwepo makamu mwenyekiti Jaji Abdulhakim Ameir Issa, alipokutana nao mara ya kwanza Novemba mosi 2015, tangu alipoutangazia umma tarehe 28 Oktoba 2015, kuwa “nimeufuta uchaguzi na matokeo yake yote na utaitishwa uchaguzi mpya baadaye.”

Jecha alitoa tangazo hilo siku ambayo kisheria alitakiwa kutangaza matokeo ya urais ambayo yalishakuwa tayari. Kura zote zilishahesabiwa vituoni na kuidhinishwa na watendaji wa Tume, sehemu kubwa ya kura zilishahakikiwa.

Wakati huo Jecha akitangazia akiwa mafichoni, baada ya kutelekeza kazi aliyoahidi kuifanya kwa kisheria, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walishakabidhiwa hati za ushindi.

CCM ilikuwa imeangushwa na umma. Badala yake, kwa mara nyingine, Chama cha Wananchi (CUF) ndicho kilipewa ridhaa. Yaliyofanyika baada ya kufutwa uchaguzi, yanabakia haramu kisheria.

Ina maana ule ulioitwa “uchaguzi wa marudio” uliofanyika 20 Machi 2016, kisheria ulikuwa na mpaka leo hii, batili. Na huu ndio uchaguzi ambao CCM kilitangazwa mshindi.

Rais anajua Jecha haishi kwa raha. Anahofu. Anakijua anachohofia. Sasa ni kwa nini aishi kwa hofu kama hakutenda lolote baya? Jecha ataishi kwenye kwapa za dola hadi lini?

Binafsi ninamuonea huruma kwa namna anavyoishi katika utaratibu wa kupakwa mafuta kwa mgongo wa chupa; na wafanyao hivyo wakiwa ni viongozi wa CCM, chama kilekile kilichomteua kugombea ubunge mwaka 2010.

Wiki iliyopita, akasikilikana kiongozi mwingine wa ngazi ya juu wa CCM akiendelea kuthibitisha walivyoishiwa hoja. Uovu wa kuhujumu maamuzi ya wananchi wa Zanzibar unawaandama kisawasawa.

Kanali mstaafu Abdulrahman Kinana, katibu mkuu wa chama hicho, kwenye jukwaa la kampeni ya uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Dimani, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, alisema, “Hakuna nchi yoyote yenye ubavu wa kumtangaza Maalim Seif Shariff Hamad kuwa rais Zanzibar.”

Alisema wapinzani wamekosa la kufanya na wamebakia kudanganya wananchi kuwa kuna rais mwingine atakayetangazwa. “Nawaambia acheni kudanganywa, hakuna rais mwingine atakayetangazwa badala ya Dk. Shein hadi mwaka 2020.”

Anaibua maswali. Ni kwanini hasa Kanali Kinana aseme hivyo leo? Hivi amemsikia nani akiwaambia watu Maalim Seif atatangazwa rais na nchi fulani? Tangu lini kiongozi akatangazwa na nchi? Je kwa kauli yake hiyo anamaanisha CCM inatapatapa?

Huko ni kutapatapa. Uongozi uliojiweka madarakani kama hauna hofu yoyote, ya nini watu wazima kupiga mayowe wakati unashika serikali?

Upo huogopi yeyote na chochote, si unaendesha mambo yako kwa raha; yanakusumbuaje maneno ya mitaani? Viongozi wa CCM kwani wanahofia kitu gani? Haoni kanali kuwa huko ni kule kujitekenya wakacheka wenyewe?

Labda watu wamesahau hulka ya Kanali Kinana anapoandamwa na wakati mgumu kisiasa. Huhangaika na hatimaye kujitengenezea kivuli. Akitupa kombora, anakiona kivuli chake.

Ndiye huyuhuyu ambaye Septemba 2015, alijitokeza hadharani na kuandika makala kwenye jarida la Hill, akisema upinzani unaoongozwa na Edward Lowassa na wenzake hauwezi kuruhusiwa kushika dola.

Alisema Tanzania haiwezi kuachiwa kuwa makazi ya makundi ya Waislam wenye misimamo mikali kama kundi la Uamsho lililojipatia umaarufu mkubwa Zanzibar kwa kutaka Muungano wa maridhiano.

Kanali Kinana kuitaja Zanzibar si kwa bahati mbaya; anaijua ni nchi ambayo Uislam sio tu dini inayotawala imani za Wazanzibari karibu wote, bali kwa kweli ndio staili ya maisha hata kwa wasioifuata. Hawafuati mpangilio wa ibada zake, bali wanapenda utamaduni wa Kiislam.

Lakini pia, anajua Zanzibar ndiko serikali ya CCM imekuwa ikipata shida kubwa kuhimili nguvu ya maoni ya wananchi wake waliothibitisha pasina shaka kuwa hawawezi tena kuishi chini ya utawala wa CCM.

Ndio maana makala yake ilijibiwa na wengi wakiwemo waandishi wa kizungu. Majibu yakawa kwamba kiukweli, utawala wa CCM unaendesha serikali kwa mfumo wa kuchochea migawanyiko na Uislam ukitumika kama kivuli.

Aliiandika makala baada ya kujionea muamko mkubwa wa wananchi kisiasa na kiukombozi. Anajua kilichomsibu (marehemu) Samuel Sitta alipokwenda kushawishi katiba mpya. Sheria ilichanwa akishuhudia.

Akiwa kwenye ziara aliyofuatana na Nape Nnauye, aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Kanali Kinana alisema kwa hali aliyoiona, atalazimika kuhamia Zanzibar wakati wa uchaguzi ili kukisaidia chama chake. Alibaini ugumu wa CCM kushinda uchaguzi Zanzibar.

Ripoti zinasema wakati wa ziara yake, mara kadhaa alishangazwa kuwaona watu walewale kila mkutano aliohutubia. Alipouliza, wasaidizi wake walimwambia, “kama si hivyo katibu, huku hutapata watu wa kukusikiliza.”

Makundi ya watu huhamishwa huku na kule kujaza mikutano ya CCM. Ni tofauti na CUF ambako wananchi huchangishana fedha kugharamia usafiri ili kufika kwenye mikutano ya hadhara kote Unguja na Pemba.

Pita mitaani Zanzibar, wananchi wanasema “tunae rais wetu wa moyoni.”

Maoni: 0774/0713 226 248

Chanzo: MwanHalisi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s