Wanaoendelea ni watu waliohuru

03

Na Juma Duni Haji

KATIKA makala zangu mbili nimeeleza maana ya uhuru na kwa nini tumedai uhuru. Nimejitahidi kufanya uchambuzi wa kina kwamba ili tupate maendeleo lazima sote watawala na watawaliwa tuwe huru, tujielewe maana sote tunahitajiana.

Rais anaitwa Rais kwa sababu kuna watu, si kwa sababu kuna wanyama au kuna mafuta ardhini. Tukizinduka na kukubali hali hiyo ndipo,tutatoka katika hali ngumu ya kihistoria ambayo imeufanya ulimwengu uwe na mabwana na watwana, uwe na wamiliki na wamilikiwa, uwe na wenye amri na wa amriwa, uwe na wenye haki ya kuishi na haki ya kufa.

Huwezi ukaelewa maana halisi ya amani na utulivu kama hujielewi na hujui maana ya uhuru. Hivyo tujiulize kwanza maana ya maendeleo na ni nani anaendelea: jee ni watu au vitu ndivyo vinaendelea, na hivyo watawala wanapaswa wathamini vitu au watu, maana bila ya watu hakuna watawala wala watawaliwa. Watu kwanza mengine yote hufuata.

 Lazima nikiri kwamba pale Mwalimu Nyerere aliposema “fedha si msingi wa maendeleo ila ni matokeo ya maendeleo” nilikawia kumfahamu. Sasa nakubali mambo yote haya tunayoyaona mbele yetu si maendeleo bali ni matokeo ya maendeleo. Katika haja ya kuonesha kwamba vitu ni matokeo ya maendeleo Mwalimu alisema.

 “Maendeleo ni kitendo chochote kile ambacho binaadamu kinamuongezea uwezo wa kutawala mazingira yake hata kama kitendo hicho hakimuengezei shibe” (Mwalimu Nyerere: kitabu cha Uhuru na Maendeleo).

 Hawezi mwanadamu kuyatawala mazingira yake kama hayaelewi. Hawezi kuyaelewa kama hana elimu nayo. Kwa hivyo kutawala mazingira maana yake ni kuwa na elimu ya mazingira hayo.

Maendeleo ni uwezo wa mwanaadamu aliyehuru, aliyezinduka na anayejielewa, wa kuyatawala mazingira yake akishapata elimu ya kuyageuza au kuyasarifu mazingira hayo ya dunia au ya jamii aliyo yeye pale alipo au anapoishi ili kumuwezesha kuishi maisha mazuri na yenye amani leo na kesho:

Mazingira ya kuishi maana yake ni jinsi raslimali za dunia iliyomo juu na chini ya ardhi inavyobadilishwa au inavyotumika kumrahisishia mwanaadamu wa leo na yule atakaezaliwa, kuishi maisha mema ya wema na mazuri zaidi.

 Tangu dunia iumbwe kinachofanywa na binaadamu ni kusindika maliasili na kuzifanya zitumike kurahisisha mai­sha yake. Kila unapoongezeka utaalam wa watu wake kusarifu maliasili na kuzigeuza katika maumbile yanayorahisisha maisha yake ndipo nchi husika huonekana au kuelezwa kuwa imeendelea.

 Maendeleo ni jinsi gani na kwa kiasi gani watu wameweza kubadilisha mfumo mmoja wa maliasili kwa kuzisindika kuwa katika mfumo mwengine bidhaa ghafi na kuwa bidhaa inayoweza kutumika ili kurahisisha maisha ya wanaadamu wake.

 Kwa mfano binaadamu wa awali walikuwa wakitembea kwa miguu tu. Kwa sababu ya uwezo wa akili ya mwanaadamu huyo aliweza kumfuga punda, ngamia na farasi na akawatumia kumsafirisha yeye na mizigo yake kwenda atakako kwa urahisi zaidi.

Baada ya kuvumbua chuma binaadamu alianza na gari za mkokoteni, akavumbua baskeli, akavumbua mutusekeli na kuendelea kuvumbua gari na hatimae ndege na hadi kufikia roketi kwenda mwezini na kwengineko anga za mbali.

 Binaadamu wakiwasiliana kwa alama ya moto, kupuliza barugumu au kupiga ngoma, na baadae kuanza simu za waya, zikaja za upepo na kuvumbuliwa simu za maneno, na kufuatiwa na simu za maandishi hadi leo simu za kompyuta za mtandao.

 Zama za kale msafiri alihitaji miezi sita hadi mwaka kutoka Ulaya ya Uingereza kufika Zanzibar. Leo anahitaji saa 12 tu. Kilichoendelea ni uwezo wa akili ya mwanaadamu wa kizungu kufanya jidudu linaloitwa ndege wa chuma na kumchukua hadi Zanzibar.

 Watu kwanza vingine vyote baadae

Kwa hivyo ni ukweli uliowazi kwamba kuna vitu vya aina mbili tu duniani: Binaadamu na vitu ambavyo vipo kwa ajili ya kumtumikia. Kwa lugha nyingine katika dunia aliye muhimu kuliko vyote ni binaadamu aliehuru, ambae kufanikiwa kwake na kuangamia kwake kunategemea ni kiasi gani anauwezo wa kubadilisha mazingira aliyonayo kumfanya aendelee kuishi na kuwepo duniani.

Viongozi na watawala wetu wajue kwamba watu ndio wanaoendelea si vitu… lazima wawathamini watu ili wathaminiwe na waweze kuwatawala. Na ndiyo maana husemwa kwamba binaadamu ndiye mfalme wa ulimwengu. Anauwezo wa kuvitawala vyote viliomo duniani.

 Ufalme wa mwanaadam

Watu wa dunia ya tatu na hasa wa bara la Afrika huwaonea choyo watu wa bara la Ulaya pale wanapoona miji yao ni mizuri, wana viwanda, majumba makubwa na wana magari na mawasiliano ya kisasa. Watu wa nchi hizo wana maisha mazuri kiasi cha Waafrika wengi kukimbilia huko. Watu hawa husema Marekani imeendelea baada ya kuona mambo kama hayo.

 Wengi wetu hushindwa kuona kwamba kilichoendelea si vile vitu ila ni wale watu waliopata uwezo wa kuvifanya vitu vile. Watu hawa wenye akili kama sisi wanayatumia mazingira waliyokuwa nayo na kuyabadilisha kwa faida yao na kuwarahisishia maisha yao.

 Kwa hivyo binaadamu ni raslimali kubwa na muhimu zaidi kuliko maliasili nyingine katika nchi yoyote ile. Katika kupima utajiri wa nchi au taifa lolote, lazima upime maliasili mbili. Maliasili watu na maliasili vitu.

Binaadamu ana utajiri wa kuwa yeye ni binaadamu mwenye uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi kwa uwezo wake wa elimu ya maumbile na viumbe, maamuzi ambayo hupima matokeo yake. Binaadamu ndiye pekee anayeweza kukiamrisha kiwiliwili chake kifanye kazi za kuzalisha kwa faida yake.

 Ni kweli punda hubeba mzigo lakini baada ya kutwishwa na binaadamu na habebi mzigo ule kwa faida yake. Nguvu kazi ya punda hutumika kwa faida ya binaadamu si yake punda. Hata n’gombe huvuta mkokoteni lakini baada ya kufundishwa na binaadamu na wala haiwi kwa faida yake.

Pia mbwa hufundishwa kumuongoza mtu asiyeona lakini baada ya kufundishwa na binaadamu. Katika viumbe wote ni bi­naadamu pekee anayeweza kufundishwa kitu leo na akaweza kukirudia tena na tena leo na kesho na keshokutwa na mtondogoo. Kiumbe kingine hakiwezi kufanya hivyo hadi kiongozwe na binaadamu.

Watu wengi duniani ni matajiri kwa sababu ya sauti zao tu. Matajiri kwa sababu ya miguu yao tu. Watu wengi duniani ni matajiri sana kwa sababu ya mikono yao.

Mifano hai ni Ronaldo wa Brazil, marehemu Michael Jackson wa Marekani na Serena na Venus Williams wa Marekani. Leo msanii wa Tanzania anaeitwa Diamond Platinumz anasifika kwa kuimba na kucheza muziki wa Bongo flavor na ametoka kwenye kundi la umasikini wa kutupwa wa familia yake.

 Kwa hivyo kilicho muhimu kuliko vyote duniani ni bi­naadamu. Anaeendelea ni binaadamu. Suala na shida kubwa ni kwamba watawala wetu hawawathamini watu, wanathamini vitu na ndiyo maana hawaoni hasara kuwauwa watu hata kama hawana hatia yoyote ile.

Madaraka yanawafanya wasahau kwamba ni madaraka kwa sababu kuna watu. Watu ndipo vingine. Ili jambo hili tulielewe jinsi ya kumuendeleza binaadamu huyo ni vyema tujue utajiri wake uko aina ngapi, utajiri wa binaadamu ni wa aina tatu.

 Nguvu kazi (Raw labour)

Ubinaadamu ni utajiri kwa sababu ni binaadamu mwenye akili na kwamba kiwiliwili chake chote ni zana za msingi zinazotumika kubadilisha raslimali nyingine za dunia zilizo nje ya kiwiliwili chake. Kwa lugha ya siku hizi uwezo wa mwanaadam wa kuzalisha mali bila kuwa na utaalarnu wowote huitwa nguvu kazi.

Unapomwambia mchukuzi akupelekee kigunia cha mchele na kukubaliana kumlipa fedha maalum huwa umekubali kulipa nguvukazi yake. Nguvukazi hii ndiyo hujenga ngome ya pamoja na kudai malipo zaidi dhidi ya malipo madogo yalipwayo na matajiri wa viwanda, kwa dhamiri na kulinda faida kubwa.

 Mfano halisi wa uwezo wa nguvu kazi ni kwamba pamoja na binaadamu kuiunda ndege, ni lazima aiendeshe kwa kutumia mkono wake, akili yake na au kiwiliwili chake.

Pamoja na uwezo mkubwa wa kompyuta kama zana ya maendeleo, lakini imeundwa na mwanaadam na haiwezi kufanya kazi zake kama haikusaidiwa na kuendeshwa nae.

Tunahitaji kuuthamini ubi-naadamu wenyewe kwanza kabla yote maana ndiyo chanzo na matunda ya mengine yote. Ndio asili ya watu kupigania haki ya kuishi badala ya kupewa haki ya kufa.

 Ndiyo maana katika haja ya kulinda nguvukazi hiyo kwa kila mtu husema, “sisi ni watu tunaostahiki kuheshimiwa.” Ubi­naadamu na nguvu itokanayo na binaadamu ndiyo huzalisha mali za aina zote duniani akiwemo binaadam mwenyeywe. Binaadam ndiye huzaa mashine ya kuzalisha mashine.

Binaadam ndiyo bidhaa mtaji kuliko nyingine yoyote. Mama mjamzito ni mwenye kubeba mwanaadam ambae baadae huweza kuwa uwezo pengine hata kuliko wa huyu mzazi.

Ninaamini Bill Gate mmoja wa matajiri wakubwa duniani kwa sababu ya utaalam wake wa komputa atakuwa na akili zaidi kuliko mama yake aliyemzaa.

Chanzo: MwanaHalisi

Advertisements

One Reply to “Wanaoendelea ni watu waliohuru”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.