Bara moja, utendaji tofauti Afrika

yahya-jammeh

KINACHOENDELEA nchini Gambia na mjumuiko wa Kanda ya Afrika Magharibi, kinanisukuma katika kuchukia. Ninachukia ninapoiangalia mifumo ya utatuzi wa migogoro inayotokana na uchaguzi wa viongozi wa kuongoza Waafrika, katika bara moja la Afrika.

Gambia, kijinchi kidogo kama uchochoro kikiwa kimemezwa na Senegal pande zake tatu za kijiografia – kusini, kaskazini na mashariki – ina tatizo kubwa ambalo wapo wadadisi wanaothubutu kulifananisha na kilichotokea Zanzibar.

Wagambia walipigakura Disemba mosi kumchagua rais, jukumu la usimamizi wa uchaguzi likiachwa kwa iitwayo tume huru ya uchaguzi – Independent Election Commission (IEC), ikiongozwa na Alieu Momar Njie.

Walikuwepo wagombea wawili wenye ushindani mkali zaidi. Alhaji Yahya Jammeh, rais aliyepo madarakani kwa miaka 22 sasa, aliingia kutetea kiti na Adama Barrow, aliteuliwa kuwakilisha muungano wa upinzani.

Siku tisa baadaye, wakati Alhaji Jammeh alisharidhia kushindwa na mgombea wa upinzani, alibadili kauli na kupinga matokeo. Anaamua kutia ulimi puani wakati umma ulishashikamana kwa sherehe za kufurahia kushindwa kwake.

Kushindwa kwa muumini huyo makini wa Uislam asiyekosa kushika kitabu kitakatifu mkononi kila aendako, kulikuwa na maana ya umma kuangusha utawala wa muda mrefu uliokuwa ukilaumiwa kwa uongozi mbaya.

Alhaji Jammeh, mwenye umri wa miaka 52, sawa na mpinzani wake, Barrow, alipobaini amepoteza mamlaka kupitia uchaguzi huru, aliinua simu na kumjuilisha mwenyekiti wa tume, Njie, kumwambia kuwa anampongeza Barrow kwa ushindi.

Njie alikaririwa akisema tamko hilo lilimpa afuweni kuwa kazi yao imerahisishwa. Aliambiwa Rais Jammeh tayari amempigia Barrow kumjuilisha kuwa ajiandae kuongoza serikali na kwamba atashirikiana naye akimhitajia.

Yote hayo – Alhaji Jammeh kukiri ameshindwa, kupiga simu kwa mwenyekiti wa tume na mgombea aitwaye sasa Rais mteule, kulifanyika hadharani, japo si kwa maana ya umma kushuhudia.

Umma uliripotiwa matukio hayo kwa uharaka na vyombo vya habari, vikiwemo vya kimataifa ambavyo waandishi wake wengi walikuwa wakifanyakazi kwa hofu kufuatia vikwazo vilivyowekwa na serikali ya Alhaji Jammeh.

Hatimaye mwenyekiti Njie alitangaza matokeo. Alimpa ushindi Barrow wa asilimia 45.5 dhidi ya asilimia 36.7 ya rais anayeondoka. Baadaye, katika kilichoelezwa kuwa urekebishaji wa hitilafu ya uhakiki iliyotokea, ushindi wa upinzani ulishuka kuwa asilimia 43.3 ikiwa ni wa tofauti ya kura 20,000 hivi.

Hapo kwenye hitilafu ya uhakiki ndipo Alhaji Jammeh alipatumia kubadilisha kauli. Ilikuwa ni Disemba 9 alipotangaza kukataa matokeo.

Alikataa matokeo, akatangaza kuufuta uchaguzi mzima, na akaahidi uchaguzi mwingine kufanyika ndani ya siku 90 ambao “utampa nafasi kila raia kupiga kura.”

Alisema uchaguzi huo utasimamiwa na tume ya watu tofauti, ambao alisema, “wanahofu ya Mwenyezi Mungu.”

Hatua mpya ya Alhaji Jammeh ilipingwa dunia nzima. Ilisononesha wananchi walioshaamini ushindi wa upinzani umebadilisha kila kitu nchini mwao.

Kwa kuwa amepingwa ndani na nje ya nchi, Jammeh anakabiliwa na mtihani mgumu ingawa mwenyewe juzi tu alisema, “Siondoki hata ikawaje na simuogopi mtu yeyote.”

Ni mazingira yanayoweza kufanana na kile kilichotokea 28 Oktoba 2015 pale Jecha Salim Jecha, mkuu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), alipotangaza kutokea mafichoni kuufuta uchaguzi wote na mpya utaitishwa ndani ya siku 90.

Nasema “yanaweza” kufanana maana hayafanani, kwa sababu: Jammeh aliridhia hadharani kushindwa kwa kumpigia simu mpinzani. Ilikuwa ni baada ya kuelezwa na wasaidizi wake katika chama.

Ni yeye aliyetoka hadharani tena akatangaza kauli mpya, ya kukataa kushindwa. Mara zote mbili – matokeo yalipotangzwa mara ya kwanza na pale yalipotangazwa baada ya kasoro za uhakiki kurekebishwa – Alhaji Jammeh ilionesha ameangushwa na wananchi.

Na mpaka sasa anavyohaha kushikilia hatamu, akiitumia mahakama itengue matokeo ya Njie, mwenyekiti mwenyewe wa tume anasimamia kauli kwamba “Jammeh ameshindwa hata kama watachoma moto rekodi.” Jeshi la Gambia linazidhibiti ofisi za tume.

Hali mbili tofauti. Gambia hakutumika mtu kuvuruga mambo. Ni rais mwenyewe na chama chake. Zanzibar katikati ya mgogoro ni Jecha aliyetumiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuvuruga mambo.

Ingawa huwezi kusema rais aliyeangushwa Zanzibar kwa mujibu wa kura za wananchi sandukuni, hana mkono katika uharamia uliofanywa dhidi ya maamuzi ya wananchi, hakusikika akisema amemshinda Maalim Seif Shariff Hamad ambaye kwa kuridhika amechaguliwa, aliharakia kuisihi Tume isiyumbe.

Ipo kwenye kumbukumbu za simulizi kuwa Dk. Ali Mohamed Shein alivutana na wasaidizi wake katika CCM, baada ya kukubali kuwa amepoteza na kuagiza matokeo yatolewe; wasaidizi wakimbana asiridhie kushindwa.

Zanzibar matokeo hayakuwahi kutangazwa na tume, lakini yanaonekana yote kwenye fomu halali za tume hiyo na zina mihuri na saini za watendaji wake.

Kule Gambia alivuruga rais na Tume imesimamia msimamo wake kuwa rais ameshindwa; huku Zanzibar alivuruga mkuu wa tume akiwa ametumiwa na CCM kilichonufaika na maamuzi yote yaliyofanywa na Jecha.

Shida yangu hapa ni hatua zilizofuata baada ya uvurugaji. Umma wa Gambia unataka mabadiliko, sawa na Zanzibar. Asasi za ndani Gambia zinataka mabadiliko na zinachukua hatua kuyafanikisha.

Asasi mbalimbali, mfano umoja wa vyama vya wafanyakazi, chama cha walimu, mwanabalozi aliyekuwa kwenye serikali ya Jammeh, zinataka mabadiliko na zimetamka kumtaka aondoke ili kuachia utaratibu wa makabidhiano utekelezwe kwa amani.

Gambia haikuachwa peke yake. Jumuiya ya Ushirikiano ya Afrika Magharibi (ECOWAS) inayofanana kimuundo na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na ile ya ushirikiano wa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), inaongoza harakati za kuhakikisha Jammeh anang’atuka, na Barrow anaapishwa ifikapo 19 Januari mwakani.

Katiba ya Gambia imeweka muda wa siku 60 kwa kiongozi mpya kuapishwa ili kushika hatamu na inatambua kamati maalum ya kuratibu makabidhiano ya madaraka.

Zanzibar hayapo hayo. Kiongozi akitangazwa anaapishwa haraka. Asasi za kiraia zimenyamaza, bali hatari zaidi kimya cha kisanii cha asasi za kinchi na kanda.

Wakati ECOWAS imesema itamtoa Jammeh kwa nguvu akigoma kuondoka baada ya ushawishi wao wa awali kushindikana, Afrika Mashariki na SADC zinaridhia tawala za kiimla na kuvumilia uvurugaji wa maamuzi ya wapigakura.

ECOWAS ilituma haraka ujumbe wa marais wanne kwa Jammeh ukiongozwa na Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia, kumshawishi kukubali matokeo, lakini alikataa na kulaumu kuwa walikwenda na msimamo tayari.

Viongozi wengine mbali na Sirleaf ambaye ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, ni Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria, Ernest Bai Koroma na mshindwa wa uchaguzi wa Ghana, John Mahama ambaye amekubali kuachia baada ya kukiri kushindwa uchaguzi na mgombea wa upinzani.

Tatizo hilo ukilichanganya na ukweli kwamba uhuni wa kupindua haki ya wananchi Zanzibar umeungwa mkono kwa nguvu zote na serikali ya Tanzania, linatoa jibu moja tu – bara moja, utatuzi wa mizozo tofauti.

0713/0774 226248

Chanzo: MwanaHalisi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s