Vipi CCM, hakiliki tena nini?

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mh. Jecha Salim Jecha akitoa taarifa za uchaguzi
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mh. Jecha Salim Jecha akitoa taarifa za uchaguzi

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimejitega, ndivyo ninavyoweza kusema kwa sasa. Ni vigumu kujua kwa uhakika ni nani atanasa kupitia mtego wao. Ila ni lazima awepo wa kunasa. Atakayenasa atakuwa mtu. Yawezekana ni watu. Lakini wa kunasa, itakuwa kutokea ndani ya chama chenyewe.

Wasiwasi wangu ni kuwa hwenda uongozi wa juu, ukajikuta unaopaswa kukubali kitakachokuja mbele, kama si hapo karibuni, basi hata ikifika uchaguzi mkuu mwingine. Wenyewe wanashikilia hautakuwepo isipokuwa itakapofika Oktoba 2020. Hebu wakubaliwe.

Hiki chama kimetangaza kuunda “Kamati Maalum ya kufanya tathmini ya kina kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar kwa ujumla na masuala yanayohusu uchaguzi wa Zanzibar 2015.”

Nimeyachukua maelezo haya kutoka blogi ya CCM inayoandaliwa na Bashir Nkoromo, mwandishi wa habari na mpigapicha ambaye tulikuwa pamoja kikazi name nilipokuwa mwajiriwa wa lililokuwa likiitwa Shirika la Magazeti ya Chama kwa umaarufu “Uhuru na Mzalendo.”

Maelezo zaidi kwa mujibu wa yaliyomo blogini ambayo kama yanavyothibitisha, yanatokana na taarifa aliyotoa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi, anayeondoka, Nape Nnauye, yanasema imekuwa ni utamaduni wa CCM kufanya tathmini kila baada ya uchaguzi mkuu.

Lakini kwa mujibu wa yaliyomo ndani ya kota za chama hiki, tathmini ya uchaguzi ilishafanyika. Hii inayokusudiwa kufanywa sasa, ni “tathmini ya kina.” Inamaana Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (CC-CCM) haikuridhika na “tathmini” iliyofanyika kabla.

Ninajiuliza kisichowaridhisha wakubwa wa CCM ni hadidu rejea za vipi tathmini yenyewe ifanywe (ilivyofanyika), au matokeo ya tathmini?

Hapa ndipo panaponisukuma kuomba Mwenyeezi Mungu atie nguvu zake. Ninaomba aishushe kadari yake juu ya makada watakaopewa kazi ya kufanya “tathmini ya kina” wawe wepesi wa kuridhia watakachokiona. Wawe wepesi wa kukieleza na kukiwasilisha hicho walichokiona kwenye ripoti watakayoitoa.

Ninakusudia kumuomba Allah, na hapa ninakupa wajibu mwenzangu unayesoma haya, nawe mwelekee muumba na kumuomba awafanyie wepesi wanakamati hawa katika kuifanya kazi waliyokabidhiwa na viongozi wao. Najua kazi yenyewe ni nyepesi kwa maumbile yake, maana kila kitu kipo. Watauliza maswali machache tu ya vitu ambavyo havijakaa sawa. Vingi vingine vipo mikononi, sina shaka.

Kada wa chama hiki ameniambia muda mfupi kabla sijaingia ofisini Jumamosi, kwamba wakubwa wanalo wanalolitafuta, kwa sababu, “kila kitu kipo mikononi mwao. Wanaujua ukweli na wanajua kila kilichotokea. Wanajua hali yetu kama chama. Wanajua tulichokifanya hata tukawepo tulipo sasa. Wanajua kila kitu, hakuna kilichojificha.”

“Tathmini hizi hutusaidia sana, kujua wapi tulifanya vizuri na wapi hatukufanya vizuri na mengineyo yote yaliyokuwa sehemu ya ushiriki wa Chama katika uchaguzi mkuu, na tumekuwa tukifanya hivi katika chaguzi zote hali ambayo imeifanya CCM kuimarika zaidi,” amesema Nape.

Kumbe mara zote baada ya uchaguzi, na ikishafanyika “tathmini” chama kinapata nguvu – kinaimarika. Tatizo chama safari hii kimeanguka. Ugumu upo hapo.

Mwenezi anatoa maelezo haya huku akijua kuwa ngome zao zinazidi kunyofolewa. Halmashauri nyingi zimewatoka. Majimbo-ngome kwao yako UKAWA. Kwa ujumla, mwenezi na wenzake wanajua chama kishidani.

Nguvu zinazotumika mpaka kutangazwa kushinda urais, majimbo na kata kadhaa, si ndogo. Nguvu kubwa. Nguvu zinazoonekana hadharani. Kwa kweli ni “maguvu makubwa hasa” hushuhudiwa vyombo vya dola wakitumia kuokoa CCM.

Nguvu kubwa imetumika Zanzibar kwa mara nyingine. Hapo ilipo CCM kwa sasa, ni matokeo ya “maguvu makubwa.” Baada ya kuona hawana pa kutokea, anguko limedhihiri, CCM walichagua kufisidi. Wakubwa wakaagiza matumizi ya “maguvu makubwa.”

Siku ya Jumanne ya 27 Oktoba 2015, walishajua wameanguka. Wakafanya jitihada za kuinuka, ikashindikana. Jopo la viongozi lilifika mbele ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na malalamiko. Walilalamikia matokeo kwenye baadhi ya majimbo. Awali walitaka wanaposikilizwa wawe wao tu na Tume.

Wakubwa hawa akiwemo Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Vuai Ali Vuai, walitaka vyama vingine visiingie wanaposikilizwa. Basi vyama vingine vikazuiwa, lakini Tume iliruhusu wawakilishi wachache wa makundi ya waangalizi wa uchaguzi.

Ni hapo ilidaiwa walionesha ushahidi kuwa uchaguzi ulivurugwa. Wakadai mawakala wao walizuiwa kushiriki uhakiki wa kura kwa baadhi ya maeneo kisiwani Pemba. Mpaka leo akili yangu haikubali – mawakala wa CCM wazuiwe? Ni msimamizi gani mwenye ubavu wa kumzuia mtu wa CCM? Uzoefu haukubali.

Malalamiko ya CCM yakashindwa. Hayakuwa na nguvu. Wakubwa wakatoka nje, nyuso zikionesha “hali ni ngumu.” Nyuso zilithibitisha walikosa walichokitaka.

Baada ya hapo, au kabla kidogo, walitumwa makada wanaoaminika waende Pemba kufanya jitihada. Nako walichokitaka kikashindikana. Walitaka baadhi ya mawakala wa Chama cha Wananchi (CUF) kama ilivyothibitishwa na baadhi ya familia za mawakala wenyewe, hawakuwapata.

Kutumia uzoefu wa miaka iliyopita, walishatafutiwa hifadhi nje ya Pemba.

Hapo ndipo pakabuniwa pigo la mwisho. Hii wenyewe wanaita Tsunami. Wanademokrasia wanaita “Mapinduzi ya uchaguzi.” Uchaguzi ukatangazwa kufutwa 28 Oktoba 2015, kiasi cha saa 6 mchana wakati Tume ikisubiriwa kutoa matokeo ya mwisho.

Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Na. 11 ya Mwaka 1984, matokeo ya urais yanapaswa kutangazwa ndani ya siku tatu tangu uchaguzi ulipofanyika. Uchaguzi ulikuwa tarehe 25 Oktoba. Ikitokea haja, muda huongezwa usiozidi siku nyingine tatu baada ya sababu ya nyongeza kuelezwa hadharani.

Utata kuhusu mazingira ya tamko la Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa ZEC, kufuta uchaguzi haujatatuka hata leo. Alikimbia kazi 27 Oktoba 2015; jioni alipoarifiwa kazi imesita kutokana na tatizo la umeme, akaagiza “fungeni kazi mpaka kesho.” Tarehe 28 Oktoba hakuonekana kazini.

Kila alipopigiwa simu ili afike na kuongoza kikao, alitoa sababu nyepesi. Mara moja alisema, “nina kikao muhimu.” Hakueleza wapi au anakutana na nani. Hakutokea. Aliyekuwa akimpigia zaidi ni Jaji Abdulhakim Ameir Issa, Makamu Mwenyekiti. Waliporidhika kuwa ni lazima waendelee na kazi, wakakubaliana makamu aongoze kikao cha kazi. Sheria inakubali maana ndiye msaidizi mkuu wa mwenyekiti.

Kazi ilianza. Mara kukatokea “wito mahsusi” ukimtaka Jaji Abdulhakim atoke kwenda kumpitisha aliyetajwa kama “mtumishi wa Tume” aliyezuiwa getini na nyaraka muhimu. Ni getini ambako tayari walikuwepo JWTZ, mbali na Polisi. Eti mtumishi ana nyaraka zinatakiwa zifikishwe Tume wakati huu ikiwa ukumbi wa Salama wa Hoteli ya Bwawani ambako ndiko ofisi zake zilihamishiwa kipindi cha uchaguzi.

Saa chache baada ya Jaji Abdulhakim kutoka, akasikika Jecha, kupitia kituo cha televisheni cha Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) au TVZ akitoa tangazo.

Ona tukio lilivyojaa sura ya kupangwa. Jecha hayupo kazini. Makamu mwenyekiti anaongoza kazi, kwasababu ilikuwa siku ya mwisho lazima matokeo yatangazwe, anaitwa getini kumpitisha mtu, anachukuliwa yeye na kupelekwa makao makuu ya Polisi Zanzibar.

Huko aliwekwa kwa saa tatu hivi. Aliondolewa kizuizini na kusindikizwa na polisi hadi nyumbani kwake. Jecha alitoa tangazo akiwa mafichoni, inasemekana alikuwa ofisi asili za tume Maisara, wakati makamu wake amezuiwa Polisi. Aliuliza sababu, akajibiwa, “Usihofu kitu mheshimiwa, hutadhurika… utaruhusiwa mambo yao yakikamilika.” Msiri aliyekuwa ndani aliniambia.

Mpaka leo, CCM haikuonesha ushahidi kuhusu madai yake kuwa uchaguzi ulivurugwa. Mwanabalozi Mark Green, alithibitisha hili alipohutubia kongamano lililoandaliwa na Centre for Strategic and International Studies (CSIS) jijini Washington, Marekani Juni 12, mwaka huu.

Maalim Seif Shariff Hamad, anayeshikilia ndiye rais mchaguliwa kwenye sanduku la kura, akiwa mgeni maalum siku hiyo, alieleza kwa upana hujuma iliyofanywa. Akatahadharisha watu wamechoka kuzibiwa mlango wa demokrasia.

Kwa hayo yaliyotokea, CCM imejitega. Inacho chakula inakila, inakila kwa hofu, au labda hakiliki tena. Ndio maana ya kweli, ikidhihiri uongo hujitenga.

Chanzo: MwanaHalisi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s