Siku za madhalimu kitengani

machi-20-2016

KITENDO cha kundi la vijana watiifu kwa Maalim Seif Shariff Hamad, anayeaminika ndiye rais mchaguliwa na wananchi, kukusanyika Mtendeni yalipo makao makuu ya Chama cha Wananchi (CUF), na kumtaka aeleze hatima ya haki yao iliyotokana na maamuzi waliyoyafanya katika uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba 2015, kinaashiria kuchoka uvumilivu.

Vijana wamechoka kuvumilia matendo ya uongozi uliopo chini ya Dk. Ali Mohamed Shein, kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) anayeshikilia hatamu baada ya chama hicho kumlazimisha Jecha Salim Jecha, kufuta uchaguzi katika siku ambayo Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ilikuwa ikisubiriwa kutangaza mshindi wa wadhifa huo wa urais.

Wanaonesha kuchoka wakati kwa namna farasi anayekufa anavyosukuma mateke kwa nguvu zaidi, wanaweza kupinduka na kuzimia watakapoambiwa kuwa sasa wajiandae kuchinja wale mbuzi walioweka kwa ajili ya kushangilia kurudi mikononi haki wanayostahili. Jitihada haiondoi kudura, ilisemwa zamani na wahenga.

Wakati kundi la vijana wa CUF wakijazana Mtendeni ili kumbana Maalim Seif, ambaye pia ndiye Katibu Mkuu wa chama hicho, Bi Fauzia Abdalla Seif el Bahriy, mjane wa marehemu Said Idi Bavuai, mmoja wa viongozi waasisi wa Zanzibar walioshirikiana na mzee Abeid Amani Karume kuunda serikali ya kwanza baada ya mapinduzi ya tarehe 12 Januari 1964, analalamika kutendewa sivyo.

Ni afadhali Maalim Seif anabanwa kwa jukumu analosimamia la kurudisha haki ya wananchi iliyodhulumiwa na CCM, Bi Fauzia yeye anamlalamikia anayeitwa Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, kwa kile anachosema mjane huyo wa marehemu Bavuai, “kudhulumiwa pande kubwa la ardhi kijiji cha Kazole.”

Kijiji cha Kazole kipo eneo la kando ya Bahari ya Hindi, kilomita 20 hivi nje ya mji wa Zanzibar, kwendea kaskazini magharibi mwa kisiwa cha Unguja, ambako viongozi wakubwa wa CCM wameamua kukimbilia kuhodhi maeneo ya ardhi yanayotajwa kuwa yakimilikiwa na Waarabu waliokuwepo kabla ya mapinduzi.

Bi Fauzia katika maneno aliyorekodiwa na mwenyewe kuahidi kuyaeneza dunia nzima ili “somo lieleweke,” anasikika akisema, yeye hajawahi kumdhulumu mtu chochote, lakini anasikitika kuambiwa kuwa amehodhi ardhi kwa miaka mingi bila ya kuiendeleza.

Lakini kwa maneno yake ndani ya simanzi na masikitiko, Bi Fauzia anakiri Balozi Iddi ni mheshimiwa na kiongozi, ni mtu mwenye nguvu, hodari, ni mheshimiwa jeuri.

Lakini anasema, kwa namna alivyokaa na waasisi wa mapinduzi, alifundishwa kuwa likitokea jambo lolote lenye hitilafu, basi ilikuwa panaundwa tume ya kulifuatilia pande zote. Hiyo anasema ilikuwa ndio njia muafaka ya kutafuta ukweli wa jambo lenye hitilafu. Anasema alidhani hata zama hizi viongozi waliopo wanapaswa kutumia njia hiyo kuyaendea mambo yenye hitilafu.

Bi Fauzia analalamika kuwa hajaghili (hajapora) ardhi ya mtu yeyote. Ardhi anayosulubiwa nayo leo, anasema ni yake mwenyewe. Aliipata baada ya kujisalimisha kwa “hao waasisi” walipotakiwa kuridhia kuolewa nao kwa lengo la uongozi wa wakati huo chini ya Mzee Karume, kutaka kutibu majeraha ya ubaguzi kati ya makundi ya kijamii Zanzibar.

Huyu mama ni wa asili ya Kiarabu ambaye ni mmoja wa wanawake wengi wa Kizanzibari kutoka asili ya Bara Arabu walioingia mikononi mwa mkono wa dola wakati huo, na kulazimishwa kuolewa na viongozi wa serikali na Chama cha Afro Shirazi (ASP) katika kile kilichoelezwa kuwa haja ya kuchanganya damu za Wazanzibari kwa kuwa kabla ya hapo, haikuwa rahisi watu wa jamii tofauti kiasili kukubaliwa kuoana.

Bi Fauzia anasema alipata shamba kwa kurithi. Amezungusha ukuta eneo hilo na ndani kuna majengo ikiwemo msikiti. Ndani ya eneo hilo ndimo pia wanazikana ndugu na jamaa zake. Hili eneo analalamika kuwa limetwaliwa kwa nguvu ya Balozi Iddi kwa kisingizio kuwa yeye Bi Fauzia si halali yake.

Analalama: Mheshimiwa haya chukua (hilo shamba), vunja kuta, vunja hata makaburi, na vunja msikiti… vunja kila kilichokuwemo kwenye shamba kwa ujabari wako. Shamba la Kazole ni langu mimi Fauzia Abdalla Seif el Bahriy. Nakwambia hili shamba ni haki yangu, nimerithi kutoka kwa wazazi wangu. Walikuwa ni Wazanzibari, na mimi hapa ni Mzanzibari, sijabadili uraia mimi. Uraia wangu ni Mzanzibari. Watoto wangu ni Wazanzibari, wajukuu zangu Wazanzibari.

“Tulijisalimisha baada ya hao waasisi kutaka sisi kuolewa na watu hao (Waafrika) tukaambiwa ndio kufuta ubaguzi. Kwa hivyo unarejesha ukabila ambao kaufuta Karume 1964. Mapinduzi yalikuwa ya kuondoa fitna hizi za ukabila. Sasa wewe unakwenda dhidi (ya) siasa za Uzanzibari. Unaleta ubaguzi,” anapiga yowe akimgusa Balozi Seif.

Huku akieleza kuwa hajapata kumvunjia heshima kiongozi yeyote, Bi Fauzia anasema amesononeshwa kumsikia Balozi Seif Iddi akimuita yeye mbadhirifu. “Mimi si mbadhirifu… lugha uliyoitumia siifahamu, labda unasema mimi ni dhaalim, mimi si dhaalim hata kidogo. Sijamdhulumu mtu kitu chake mie… ila wewe ambaye ni kiongozi jabari, ukae ujichuje, useme hivo ulivyonavyo umevipata vipi.”

Anasema kwa namna matendo ya viongozi wa sasa yalivyo mabaya, hata shamba aliloacha Bavuai, limechukuliwa kidhuma na viongozi wa serikali. Anasema marehemu hakuacha mali zaidi ya nyumba yake moja aliyokopeshwa na serikali na kuilipia kutokana na makato katika mshahara wake.

“Wao waasisi waliishi kwa mishahara yao tu. Bwana Bavuai hakujenga nyumba nyingine yoyote, lakini hata hilo shamba alilopewa na Mzee Karume amedhulumiwa na viongozi,” anasema kwa sauti ya unyonge huku akisema kwa hayo aliyoyasema, yuko tayari kuchukuliwa na Balozi Seif Iddi na kufungwa.”

Hii ni kadhia nzito. Ni kadhia inayotokana na matendo ya viongozi walioshika serikali baada ya kuhujumu haki ya Wazanzibari.

Baada ya kuvuruga uchaguzi halali uliosifiwa na kila asasi ya waangalizi, walimtumia Jecha na kuitisha uchaguzi mwingine 15 Machi 2016, wakaupa jina la “uchaguzi wa marudio” ambao matokeo yake yalitangazwa siku hiyohiyo, harakaharaka. Dk. Shein alipewa ushindi wa asilimia 90 katika uchaguzi ambao vituo vilikuwa vitupu tofauti na ilivyokuwa 25 Oktoba 2015.

Sasa serikali iliyoundwa kutokana na uharibifu huo, ndio inatuhumiwa kwa maongozi ya kidhalimu. Baadhi ya viongozi wake wakubwa wanatajwa kwa ufisadi na Bi Fauzia yeye akimuelekea Balozi Seif Ali Iddi kwa kumtaja kuwa ametwaa ardhi yake ya halali aliyoirithi kwa wazazi wake.

Malalamiko ya Bi Fauzia yanakuja siku chache baada ya serikali ya Dk. Shein kufanikiwa kulitumia Baraza la Wawakilishi, kutunga sheria ya kunyang’anya maeneo ya ardhi yanayoelezwa kuwa hayajaendelezwa kwa miaka mingi. Kazole ni eneo ambako viongozi wakubwa wamefika na kujitwalia maeneo kwa visingizio mbalimbali.

Haraka hii ya kupora mali za wananchi, inakujaje sasa? Ni kwa sababu wakubwa wanajua siku zao zinahesabika mamlakani.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s