Hawaikubali kweli, watasaliti tu umma

Muwakilishi Jimbo la Paje kupitia CCM Mhe. Hashim Jaku(aliyevaa kofia) akiwa na Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shain
Muwakilishi wa Jimbo la Paje kupitia CCM Mhe. Hashim Jaku(aliyevaa kofia) akiwa na Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shain wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa Zanzibar mwaka jana

SIKU zote nimekuwa nikitamani kuona Baraza la Wawakilishi likijitokeza katika uasili wa kuanzishwa kwake – kuwa kiwakilishi cha mitazamo ya umma – zaidi kuliko kuwa kifuataji amri za serikali.

Kila kilipojitokeza kujitambua hivyo, nilikitambua. Kila kilipojiachia na kuamua kujiegemeza ubavuni mwa serikali, nilikisema. Nilikilalamikia. Kuwa hakiwatendei haki wananchi. Kinakengeuka jukumu lake kuu la kuibana na kuisimamia serikali kuhusu matumizi ya raslimali za nchi.

Hili Baraza limekuwa likienda na kurudi. Mara nyingi linachukua mkondo wa kuwa kisaidizi cha setikali (utawala). Limekuwa likitumika kupitisha matakwa ya watawala, mara nyingi pasina kuhoji vizuri mantiki ya kilichofikishwa mezani kujadiliwa.

Kama inavyokuwa mara nyingi kwenye Bunge la Jamuri ya Muungano wa Tanzania, mijadala kwa Baraza la Wawakilishi, nayo hudhibitiwa na mkalia kiti. Hali hujionesha hasa kuwa yapo maelekezo mahsusi ya ni mwakilishi gani aseme, na aseme wakati gani.

Mara kadhaa kwa mfano, baraza limejikuta likiwa uwanja wa kupashana michapo na kupigana vijembe. Hali huzidi pale suala linalojadiliwa linapokuwa limeleta hisia na misimamo ya kiitikadi inayohusisha mitizamo ya kisiasa.

Kwa kuwa mara zote kiti hukaliwa na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho kinaongoza serikali, basi utashi wa matakwa yake hutawala mijadala. Kwa kuwa kwao wengi kuzidi wale wawakilishi wa upinzani, ambao mara zote huwa ni Chama cha Wananchi (CUF), wanachokitaka ndio mwishowe huwa.

Na wanachokitaka huwa hata kama hakiakisi kile wanachokitaka wananchi. Au kwamba kilichoidhinishwa kuwa tofauti na matumaini ya sehemu kubwa ya umma.

Wawakilishi wa CCM hulenga zaidi kushambulia upinzani. Wakati mwingine hushuhudiwa wakitajwa viongozi wa CUF ambao hata si wajumbe wa Baraza la Wawakilishi. Kwa CCM, imekuwa kawaida kupeleka mashambulizi kwa wakuu wa CUF, lengo likiwa ni kuwakashifu na kutekeleza mbinu za kudhoofisha sauti ya upinzani barazani.

CCM imezoea kuwa ikitumia udhibiti wake barazani – kuwa na wajumbe wengi kuzidi upinzani, na kuwepo mkalia kiti ambaye ni kada wake kiitikadi – kupitisha maamuzi hata yasiyo na maslahi ya kweli na nchi. Wakati mwingi maamuzi yanayopitishwa kwa hakika huwa ni kwa ajili ya kutimiza maslahi ya kisiasa zaidi.

Kumekuwa na shida kubwa katika kutarajia maendeleo kupitia baraza hili, ambalo kikatiba ni moja ya mihimili mitatu inayojenga dola. Mingine ikiwa ni ile Serikali na Mahakama.

Nimetumia maneno “mara nyingi” au “wakati mwingi” kwa sababu ipo katika historia ya utendaji wa Baraza la Wawakilishi, kupata kupitishwa maamuzi ya maana na yenye maslahi ya kweli na nchi.

Yapo maamuzi yametarajiwa hasa kwani yalielekea katika kukidhi matumaini ya umma na kuzingatia mustakbali mwema wa nchi yao.

Yalionekana katika vikao vya baraza hili vilivyofuatia tukio adimu la kusainiwa kwa makubaliano ya kuendeshwa siasa za maridhiano mwaka 2009, mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu wa 2010. Makubaliano hayo yaliyolenga kufutwa kwa siasa za chuki, fitna na majungu, yalifanywa kati ya Amani Abeid Karume, aliyekuwa rais, na Maalim Seif Shariff Hamad, katibu mkuu wa CUF.

Hapo nyuma niliwahi kujadili kwamba baada ya CCM, ikisaidiwa na dola, kuvuruga uchaguzi kwa kuhujumu matakwa ya wananchi, na kwa vile ilivyojiundia serikali itakavyo, hata Baraza halitakuwa na jipya zaidi ya kupitisha wanachokitaka watawala.

Sijafuta msimamo huu. Lakini kimeibuka kitu nisichokitarajia – mgawanyiko wa mawazo kwa wawakilishi wenyewe wa CCM. Ama hili ni jambo jema kwa mustakbali wa Zanzibar. Ndani ya mgawanyiko, tatizo kubwa linaloisibu nchi, linaelezwa bayana.

Wapo wawakilishi wa CCM, wameamua kujivua gamba. Wanasema kweli, na wanayoisema ni kweli tupu. Wanaelezea kinachoonekana dhahiri kuikumba Zanzibar – mgogoro wa kisiasa. Wanasema mgogoro unatokana na ubinafsi katika siasa, ambao matokeo yake ni kukwamisha nchi kuendelea.

Kwa namna wanavyolalamika na kutanabahisha, wameanza kuonywa. Msimamo wao mkali unawatia hofu watawala; labda utabadilisha mwelekeo wa upepo. Utaamsha waliolala na kuhamasisha chuki dhidi ya kilichopo.

Msimamo wa Jaku Hashim Ayub (Paje), Simai Mohamed Said (Tunguu), Hamza Hassan Juma (Shaurimoyo), Hassan Khamis Hafidh (Welezo) na Nadir Abdulatif Jussa (Chaani) unawaumbua wakubwa kwa kuwaonesha ni watu wasiojali nchi, bali maslahi binafsi. Wanajali chama kwanza, nchi shauri yake.

Si wazalendo kweli, bali wanasiasa fitina na wapaliliaji migawanyiko kwa visingizio vya kutengeneza.

Wanasiasa wenye maamuzi CCM wanashutumiwa ni wakorofi. Hata pale kunapofanywa muafaka wa masuala yanayoijenga Zanzibar, wao hukubali shingo upande. Bali wakikaa faraghani, wanafikiria kukaidi walichoamua na wenzao.

Unakumbuka walichokifanya wakati wa kuelekea Bunge Maalum la Katiba mwaka 2013? Walishiriki majadiliano na wawakilishi wenzao kutoka CUF, wakiwa mstari wa mbele kuitetea Zanzibar.

Katika majadiliano yaliyotangazwa moja kwa moja na vyombo vya habari vya serikali (televisheni na redio), waliinua sauti kulalamikia matatizo yanayoiumiza Zanzibar.

Walilalamikia kwa maneno makali na makavu uendeshaji mbaya wa mambo ya nchi kwa kuzingatia mfumo wa Muungano wa Zanzibar na Tanganyika, na wakataka Zanzibar ipewe nafasi yake ya haki ya kujiendesha ili nayo ipige hatua mbele kama ilivyo kwa mshirika wake Tanganyika.

Aah wapi; sikio la kufa halisikii dawa. Wakadhihirisha usaliti wao. Wakaisaliti nchi yao. Wakajivika ukichwa ngumu na undumi la kuwili. Hawakujali kisasi. Wakatukana wenzao, wale waliokuwa pamoja kutoa ya mayoni yanayoijenga Zanzibar.

Huku ikiaminika watashikilia msimamo ule popote watakapopata nafasi, wanasiasa wakorofi na wabinafsi wa CCM walibadilika. Wakapayuka na kufyatuka.

Wakajidhalilisha kwa kuyakanyaga maneno mazuri waliyoyasema katika Baraza la Wawakilishi, na kusimama upande wa kuihujumu dhamira ya mabadiliko ya mifumo ya uendeshaji, ambayo ndiyo waliyotoka nayo barazani.

Wakafyatukia wawakilishi wenzao wa CUF kama vile ndio tatizo la Zanzibar kuendelea. Wakaanzisha mashambulizi ya nguoni dhidi ya viongozi wakuu wa chama hicho ambao hata hawakuwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba.

Mjadala wa bunge lile wala haukupaswa kugusa viongozi wa vyama. Wana-CCM waliugeuza kwa makusudi ya kukidhi matakwa ya kuisaliti Zanzibar.

Matokeo yake, yalipokuja maamuzi kuhusu maoni ya wananchi juu ya katiba gani wanaitaka, wakayaponda maoni ya umma na kuungana na wanachama wenzao upande wa Tanganyika, kupandikiza maoni wayatakayo wao.

Masikini roho zao, kama vile hawakujua wenzao wa Tanganyika walikuwa wanaitafuta nafasi ya kushindilia msumari wa moto kwenye jeneza la “maiti Zanzibar.”

Kama vile wana-CCM wa Zanzibar kuambiwa na wenzao hao “mumeyataka wenyewe, tunakusaidieni mupate mkitakacho. Ila mtakipata kwa vile “tunavyoamini sisi ndicho mnapaswa kupata.”

Hawa ndio CCM hasa, wakiipata tu nafasi ya kusaliti dhamira yao, hawahofii chochote, watasaliti na umma wenyewe wanaopaswa kuukomboa. Ndani ya nyoyo zao, wao ni wasaliti tu. Hawapikiki chungu kimoja na kina Nadir.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s