Mbinu hii ya Polisi kukabiliana na wahalifu Zanzibar ibadilishwe

IGP Ernest Mangu akimuelezea Balozi Seif Ali Idd mikakati ya Jeshi la Polisi katika ulinzi wa raia na mali zao
IGP Ernest Mangu akimuelezea Balozi Seif Ali Idd mikakati ya Jeshi la Polisi katika ulinzi wa raia na mali zao

Na. Salim Said Salim, Mwananchi

Watanzania mara nyingi tunaambiwa rushwa ni adui wa haki. Kwa bahati mbaya wapo watu walioanza kuamini kuwa rushwa na ufisadi ndiyo adui pekee wa haki.

Ukweli ni kwamba maadui wa haki ni wengi na wapo wa dhahiri shairi. Hawa ni wale wanaoitwa wahalifu, majambazi, wafanyabiashara, wauzaji dawa za kulevya, dawa mbovu zinazohatarisha maisha ya watu, matapeli na kadhalika.

Ni jukumu la kila raia mwema kuwafichua na kupambana na watu hawa kwa kila hali, lakini mzigo mkubwa wa kazi hii umetwishwa Jeshi la Polisi ambalo mbiu yake ya kazi ni usalama wa raia na mali zao.

Uzoefu wangu mdogo unatokana na kufanya kazi karibu na Jeshi la Polisi tangu miaka ya 1960 nilipokuwa nikienda Chuo cha Polisi (PTC) kilichopo Moshi, kuandika habari za uhalifu ndani na nje ya Mahakama na kuwa na mazunguzo na maafande nimejifunza kwamba msako wa wahalifu lazima ufanywe kwa siri kubwa.

Hata sisi wanataluma ya habari tunapofanya uchunguzi wa kufichua maovu hufanya kimya kimya na hatuwaambi tunaowachunguza.

Mambo huwekwa hadharani baada ya uchunguzi kukamilika na kuwaachia waliotuhumiwa kufanya maovu kujibu mashtaka.

Vinginevyo wahalifu wanapata mwanya wa kukwepa kukamatwa na kuwajibishwa kisheria kwa makosa waliyoyatenda au kupanga kuyafanya. Lakini baadhi ya nyakati mwenendo wa utendaji kazi wa Jeshi la Polisi Zanzibar unanishangaza, kunisikitisha na baadhi ya wakati kuniacha nicheke peke yangu.

Hatimaye hubaki nikijiuliza maswali mengi bila ya kupata jawabu kwa kutoamini kinachotokea.

Hivi karibuni viongozi wa Jeshi la Polisi Zanzibar walitangaza kuwa na mpango kabambe wa kuwasaka watu wanaochapisha nyaraka bandia.

Tuliambiwa kwamba watu hawa wanavyo viwanda vya kufanyia uhalifu huo katka sehemu mbalimbali za Zanzibar.

Tujiulize kwa kutoa tangazo hilo kulikuwa na lengo gani kama siyo kuwaambia hao wanaofanya uhalifu huo waingie mitini na kujificha na ikiwezekana wahamishe au kuharibu vitendea kazi za uhalifu wao?

Wapi umesikia mwizi anaambiwa akae hapo alipofanya uhalifu wake na angojee polisi wamkamate na kumtia pingu na baadaye kumwajibisha kisheria?

Hata hivyo, siyo mara ya kwanza wala ya pili kwa Jeshi hili visiwani kufanya makosa (au mzaha) kama huu.

Ninakumbuka safari moja walitangaza kufanya msako wa nyumba zinazouza gongo. Matokeo yake ni kwamba kila walipofika nyumba inayouza gongo na bangi walikuta siyo tu haifanywi biashara hio, lakini hapana vifaa vya kutengenezea wala kuuzia kinywaji hicho haramu wala dawa za kulevya.

Nilielezwa kwamba katika nyumba moja mjini Unguja iliyosemakana kuwa maarufu kwa kuuza gongo walikuta kikundi cha watu waliovalia kanzu na wengine wakiwa wameshika tasbihi pembeni wakisoma maulidi.

Askari waliofika hapo kusaka wauza na wanywaji gongo walikaribishwa kula tende na kahawa na kuambiwa ikiwezekana wajiunge nao kwa kisomo cha maulidi.

Mara nyingine utasikia tangazo kwamba polisi watakuwa na msako wa makahaba au mashoga katka maeneo mbalimbali ya visiwani.

Matokeo yake hao wanaofanya uchafu huo huficha makucha yao na hawaonekani wakati wote msako unapoendelea.

Kwa maana nyingine wahalifu hawa huamua kwenda likizo baada ya kusikia tangazo la Poisi kuamua kuwasaka.

Kwa kweli kwa mwenendo huu Jeshi la Polisi haliwatendei haki Wazanzibari ambao wanawategema kuwalinda na uhalifu na uchafu wa maadili katika jamii.

Tangazo la kusaka viwanda vya kutengeneza nyaraka bandia kama vyeti vya kuzaliwa, leseni za gari na biashara lilitolewa sambamba na mpango wa kusaka vituo vilivyokubuhu kwa kuharibu watoto wa kiume.

Tuliambiwa kwamba Jeshi la Polisi limegundua kuwa miongoni mwa sehemu maarufu ya kuzalisha vijana wenye maadili mabaya visiwani ni Mtaa wa Miembeni, mjini Unguja.

Kama kweli palikuwapo mpango wa kuwabana wanaotengeneza nyaraka bandia, wanaouza dawa za kulevya zoezi hili lingekuwa la siri.

Wahalifu wa aina yoyote ile hawapaswi kupewa onyo la kukamatwa. Kama ni kutolewa onyo basi hilo limeshafanyika kwa muda mrefu kwa kuwepo sheria zinazojulikana kwamba vitendo hivi ni vya uhalifu na havikubaliki.

Ni vizuri kwa viongozi wa Jeshi la Polisi Zanzibar wakatafakari upya mwenendo wao wa utendaji kazi kwa kuelewa kwamba hata wakifanya kazi nzuri katika maeneo mengi lile wanalokosea ndiyo linaloonekana na jamii. 

Kosa moja hutia doa mazuri 11 waliyoyafanya. Huu ndiyo ulimwengu baya huonekana na zuri hufumbiwa macho na kuzibiwa masikio.

Uhalifu kama nilivyoelezea hapo juu ni adui mkubwa wa haki, jamii na nchi kwa jumla na haupaswi kufanyiwa huruma ya aina yoyote ile.

Wanaofanya uhalifu wa aina yoyote ile na wote wanaowasaidia kwa njia moja au nyingine ni maadui wakubwa wa jamii na nchi na lazima wahibitiwe kisheria.

Kinachotakiwa ni kumwona mhalifu ni mhalifu, bila ya kujali yeye ni nani au wazazi, ndugu, jamaa na marafki zake ni nani.

Zanzibar ilikuwa ikisifika kwa watu wake kuwa watiifu wazuri wa sheria na ukiangalia kumbukumbu utaona kesi za mauaji, ujambazi, utapeli na uvunjifu wa sheria mbalimbali ulikuwa wa kiwango kidogo.

Mpaka miaka ya karibuni watu walijihisi salama kutembea hata kwenye maeneo ya kiza na ukahaba ukifanyika kwa siri kubwa, lakini leo hali ni tofauti.

Hata watu kutembea na vichupi ilikuwa siyo jambo la kawaida, lakini leo wengine hufanya hivyo hata kwenye masoko kama vile wapo kwenye fukwe za bahari.

Ni vizuri kwa sheria kusimamiwa. Ni kweli katika dunia ya leo mara utasikia lawama za kuvunja haki za binaadamu, lakini ukweli ni kwamba haki za binadamu ni jambo moja na vitendo vya uhalifu ni jambo jingine tofauti.

Anayefanya uhalifu ndiye hasa anayevunja haki za binaadamu na anapaswa kudhibitiwa na siyo kupewa tahadhari za kujificha wasikamatwe.

Onyo au tahadhari hutolewa kwa masuala kama ya kuweka mazingira safi au kuchukua hatari za kujikinga na maradhi na siyo kwa watu wanaovunja sheria.

Mhalifu hastahiki kupewa tahadhari, bali kubanwa na kuwajibishwa kisheria. Kama walivyo wahalifu kutokuwa na huruma na wanaowatenda vibaya basi na Polisi hawastahiki kuonyesha huruma ya aina yoyote kwa wanaovunja sheria za nchi.

Kilichokuwa muhimu ni kwa Polisi kuhakikisha hakuna anayetumia vibaya sheria zilizopo kuonea watu wenye kutii sheria kwa sababu moja au nyingine.

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii. barasteki@gmail.com

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s