Ujenzi wa mahkama ya watoto Mahonda kukamilika mwezi ujao

Mhandisi Mkuu wa Jeshi la Polisi Mrakibu wa Polisi Paschal Macorwa akimpatia maelezo Balozi Seif hatua iliyofikia ya ujenzi wa jengo la Mahakama ya watoto Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja
Mhandisi Mkuu wa Jeshi la Polisi Mrakibu wa Polisi Paschal Macorwa akimpatia maelezo Balozi Seif hatua iliyofikia ya ujenzi wa jengo la Mahakama ya watoto Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja

Mrajis wa Mahkama Kuu ya Zanzibar Jaji George Kazi amesema mtoto anapaswa kuandaliwa mazingira maalum yatakayo muwezesha kutoa ushahidi ulio huru endapo atafanyiwa vitendo vya udhalilishaji au kujitetea kama amefanya makosa ya jinai akiwa chini ya Umri wa miaka 18.

Alisema Serikali imeanzisha Sheria ya Mtoto nambari 6  ya Mwaka 2011 kwa madhumuni ya kuipa mamlaka Mahakama kusikiliza na kuamua makosa ya Jinai dhidi ya Mtoto kwa kosa lolote linaloshukiwa kutendwa kabla ya Mtoto hajafikia umri huo isipokuwa makosa ya Uhaini, Kuua na Kubaka.

Jaji George Kazi alisema hayo wakati akitoa ufafanuzi mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefanya ziara fupi ya kukagua hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa Jengo la Mahakama ya Watoto liliopo Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema mfumo sasa ndani ya Mahakama nyingi Nchini umekuwa na mchanganyiko wa Kesi kiasi kwamba inaleta usumbufu kwa zile kesi zinazowahusu Watoto jambo ambalo huwapa kigugumizi watoto wanaohusika na kesi hizo wakatiwa kutoa ushahidi au kujitetea.

Jaji George Kazi alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba mfumo mpya wa uanzishwaji wa Mahakama za Watoto utawapa nafasi Majaji au Mahakimu waosikiliza Kesi zinazowahusu Watoto kuzihamisha kutoka Mahakama za kawaida na kuzipeleka Mahakama maalumu za Watoto.

Naye Mhandisi Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania anayesimamia ujenzi huo Mrakibu wa Polisi { S.P } Paschal  Macorwa akimkaguza Balozi Seif  kuangalia maeneo mbali mbali ya Jengo hilo alisema kazi halisi za ujenzi huo zinatarajiwa kukamilika kati kati ya Mwezi ujao wa Disemba.

Kamanda Paschal alisema ujenzi wa Kituo hicho unaotekelezwa na Jeshi la Polisi kama Taasisi kwa kutumia vifungu vyake vya kawaida vya matumizi umechelewa kukamilika kutokana na  kupanda kwa gharama za vifaa vya ujenzi.

Hata hivyo kamanda Paschal alieleza kuwa juhudi zinafanywa na jeshi hilo kuhakikisha kwamba ujenzi huo unakamilika ifikapo Tarehe 15 Disemba  kwa kumalizia kazi za uwekaji wa huduma za Umeme pamoja na Maji ili Mahakama hiyo ianze kutoa huduma kama ilivyokusudiwa.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  alilipongeza Jeshi la Polisi Nchini kwa kazi kubwa inalochukuwa licha ya ulinzi wa Raia lakini pia kujihusisha na Miradi inayotoa huduma kwa Jamii akiutolea mfano Ujenzi huo wa Mahakama ya Watoto Mahonda.

Balozi Seif alisema udhalilishaji wa Watoto kwa sasa umekuwa tishio kwa Jamii kiasi kwamba Serikali kupitia Taasisi mbali mbali imefikia hatua ya kuanzisha Mahakama ya Watoto kwa lengo la kukabiliana na vitendo hivyo vinavyovuruga ustawi wa Jamii Nchini.

Wakati huo huo

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikitembelea Kituo cha Afya cha Mahonda kinachojitayarisha kupokea Wataalamu wa Afya kutoka India watakaopiga kambi kwa ajili ya kuwafanyia uchunguzi  wananchi kwa maradhi ya meno, kisukari pamoja na sindikizo la damu (Blood Pressure)

Kambi hiyo awali ilikuwa imepangwa kufanyika katika Kituo cha Afya Kitope lakini kutokana na sababu za kimsingi zilizotolewa na Wataalamu wa Sekta ya Afya wamependekeza uchunguzi huo ni vyema ukafanyika katika Kituo cha Afya cha Mahonda  kutokana na kubahatika kuwa na vifaa vingi vya uchunguzi vitakavyorahisisha kazi zao.

Balozi Seif katika mazungumzo yake ya awali na  Wagonjwa na Wafanyakazi wa Kituo cha Afya cha Kitope juzi aliwahamasisha Wananchi wote wa Wilaya ya Kaskazini “B” kushiriki katika kufanya uchunguzi wa Afya zao utakaotolewa na Madaktari hao Mabingwa kutoka Nchini India.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s