Msajili azuia ruzuku ya Sh468 milioni za CUF

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad,
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad,

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amezuia ruzuku yao tangu Agosti na akataja matukio tisa ambayo amesema yanaonyesha jinsi mlezi huyo wa vyama vya siasa na Jeshi la Polisi wanavyomlinda Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye ana mgogoro na chama hicho

Chama hicho kiliingia kwenye mgogoro wa kiuongozi baada ya Profesa Lipumba kuandika barua ya kujivua uenyekiti wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu uliopita na mwaka huu akaandika barua nyingine ya kufuta uamuzi wake, lakini chama hicho kikaendelea na mchakato wa kujadili uamuzi wa kujiuzulu na kuupitisha

Hata hivyo, alipinga uamuzi huo na juhudi za kuondoa utata huo zilifika kwa Msajili ambaye alitangaza kuwa bado anamtambua Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti, hatua ambayo imezua mgogoro wa kiuongozi kutokana na chama hicho kupinga uamuzi wa kumtambua

Jana, Maalim Seif aliwaambia waandishi wa habari kuwa tangu Agosti Msajili amekuwa hawapi fedha zao za ruzuku kwa maelezo kuwa chama hicho kina mgogoro

Nilimuandikia kumweleza kuhusu ruzuku, lakini akasema fedha hizo zitatolewa mgogoro utakapoisha. Nilimuuliza ‘sasa mbona ulitaka kumpa Lipumba?’” alisema Maalim Seif jana jijini Dar es Salaam

Maalim Seif, ambaye alisema CUF hupata Sh117 milioni kwa mwezi, alidai kwamba Msajili alitaka kuidhinisha fedha hizo zitolewe kwa Profesa Lipumba anayetambuliwa na ofisi yake, lakini mpango huo uligonga mwamba

Akizungumzia ruzuku, Naibu Katibu Mkuu wa CUF-Bara, Magdalena Sakaya, ambaye amesimamishwa uongozi, alisema ni kweli chama hicho hakijapokea ruzuku kutokana na mgogoro unaoendelea

Sakaya alibainisha kuwa hivi sasa kinajiendesha kwa michango ya wabunge na wanachama wake

Akizungumzia mikutano ya chama, Maalim Seif alisema Profesa Lipumba amekuwa akifanya mikutano kwa baraka za Jeshi la Polisi na Msajili, huku wao wakinyimwa haki hiyo

Katibu huyo alisema hayo yote yametokana na safari yake nchini Marekani ambako alikwenda Juni mwaka huu, kuieleza jumuiya ya kimataifa kilichojiri kwenye Uchaguzi Mkuu hadi kusababisha CUF kususia uchaguzi wa marudio wa Rais Zanzibar

Wakubwa hawakufurahia ziara  yangu ya nje. Wanasema nimekwenda kuwavua nguo nje. Nimekwenda kuwavua nguo au wamejivua wenyewe?” alihoji Maalim Seif ambaye alikuwa mgombea urais Zanzibar katika Uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana kabla ya matokeo kufutwa

Mambo wameyafanya wazi wenyewe, yameonekana na kila mtu. Sasa ni mimi, ni wao?” alihoji Maalim Seif

Hizi ni njama za kurudisha nyuma jitihada zangu mimi. (Wanataka) Wanifunge na mgogoro ili nisiendelee. Lakini hakuna, nitaendelea.

Maalim Seif alisema tangu chama hicho kiingie kwenye mgogoro, kumekuwa na matukio ambayo yamedhihirisha kuwapo na hujuma dhidi ya CUF

Katibu huyo alitaja matukio aliyodai kuwa chama chake kinafanyiwa hujuma na polisi kwa kushirikiana na Jaji Mutungi kuwa ni kuvamia na kusababisha vurugu kwenye Mkutano Mkuu Maalumu kwa CUF uliofanyika Agosti 21 kwenye ukumbi wa Hoteli ya Blue Pearl jijini Dar es Salaam

Mkutano huo ndiyo uliokubaliana na uamuzi wa Profesa Lipumba kujiuzulu, lakini ulipofikia hatua ya kumchagua mwenyekiti mpya, vijana wanaomuunga mkono msomi huyo waliingia na kuibuka vurugu zilizosababisha mkutano kuvunjika

Maalim Seif alisema wajumbe 476 waliridhia kujiuzuru kwa Profesa Lipumba dhidi ya 16 ambao hawakuridhia

Profesa Lipumba na wafuasi wake walivamia mkutano na kufanya vurugu wakishuhudiwa na askari polisi bila kuchukuliwa hatua zozote,” alisema makamu huyo wa kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) iliyoongoza Zanzibar kwa kipindi kimoja (2010-2015).

Alisema tukio la pili ni utekaji wa wanachama na viongozi wa CUF, akisema licha ya matukio hayo kuripotiwa polisi na ushahidi usiokuwa na shaka, hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya wahusika

Katibu huyo alidai Septemba 16, kaimu naibu katibu mkuu, na mkurugenzi wa uchumi na fedha, Joram Bashange alitekwa wakati akitoka nyumbani kwake na watu aliosema wako upande wa kundi la wapinzani wao

Alitaja tukio la tatu kuwa ni uvamizi wa ofisi kuu ya makao makuu ya CUF aliodai umefanywa na kundi la wafuasi wa Profesa Lipumba

Maalim Seif alidai kuwa wafuasi wa Profesa Lipumba walivunja na kupiga walinzi waliokuwapo katika ofisi hizo zilizopo Buguruni jijini Dar es Salaam.

Wakati wanatakeleza hayo, walikuwa na ulinzi wa polisi,” alidai Maalim Seif

Maalim Seif alitaja tukio la nne kuwa ni uvamizi wa ofisi za CUF wilaya ya Mkuranga na Bagamoyo, ambako amedai wafuasi wa Profesa Lipumba walivunja makufuli ya milango ya ofisi hizo na kuweka ya kwao ili kuzuia shughuli za ofisi zisiendelelee

Maalim Seif alisema tukio la tano ni kuzuiwa kwa wajumbe na wabunge wa chama hicho wasifanye mkutano mkoani Mtwara bila ya kupewa sababu, wakati Profesa Lipumba akiruhusiwa kufanya mikutano yake

Jeshi la Polisi limekuwa likimlinda na kumkingia kifua Lipumba,” alisema

Tukio la sita ni jeshi la polisi kuzuia kufanyika kwa mkutano wa CUF mjini Tanga bila ya kutoa sababu ya zuio hilo, wakati akitaja tukio la saba kuwa ni kutekwa kwa mlinzi wa chama hicho, Mahamed Said

Kiongozi huyo alidai kuwa mlinzi huyo alitekwa mbele ya walinda usalama, lakini hawakuchukua hatua zozote

Tukio la nane ni zuio la polisi la kufanyika kwa mkutano wa ndani wa CUF, Mtwara na Lindi licha ya kuomba kibali kwa jeshi hilo

Tukio jingine kwa mujibu wa mwanasiasa huyo mkongwe ni lile lililotokea Novemba 24, siku ambayo anadai walinzi wanaomuunga mkono Profesa Lipumba walitaka kuwazuia baadhi ya viongozi wa chama hicho wasiingie Mahakama Kuu kusikiliza kesi iliyofunguliwa dhidi yake pamoja na Msajili

Akizungumzia madai hayo, Kamishna wa Polisi, Operesheni na Mfunzo, Nsato Marijani alisema Jeshi la Polisi halina upendeleo kwa upande wowote

Alisema jeshi hilo linatambua kuwa kuna mvutano kati ya pande mbili za uongozi wa CUF, na kwamba upande moja ukitaka kufanya mkutano, upande mwingine unapanga kufanya vurugu

Hatuna upendeleo ila hali halisi ndiyo inatufanya tuzuie. Ndiyo maana tunahimiza wakae na wazungumze,” alisema Kamishna Marijani.

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s