Mpaka lini Trump ataipuuza Afrika?

Rais Mteule wa Marekani, Donald Trump
Rais Mteule wa Marekani, Donald Trump
Nov 24, 2016

SIKU hizi tukitaka tusitake hatuwezi kumuepuka Donald Trump, Rais mteule wa Marekani.  Hizi ni zama zake na hatujui huko mbele tutakabiliwa na nini.

Hata hivyo, vyovyote iwavyo, jambo moja ni la hakika. Nalo ni kwamba huu ndio mwisho wa dunia kama tuijuavyo na kama tulivyoizoea.

Trump ni mfanyabiashara na ni mfanyabiashara aliyefanikiwa katika biashara zake, ingawa alipata kufilisika. Uzoefu wake ni katika  shughuli za kibiashara.   Hakuwahi kuendesha hata idara moja ya serikali.

Wala Trump si mwanasiasa wa kawaida.  Hakuwahi kuwa mbunge, hakuwahi kuwa meya, hakuwahi kuwa chochote katika serikali kuu ya Marekani au ya majimbo au hata ya kitongoji.

Juu ya hayo, kutokuwa na uzoefu huo hakukumzuia asijinate kwamba yeye ndiye mwenye uwezo wa kuiokoa Marekani na kuifanya nchi hiyo iwe adhimu tena, iwe nchi yenye hadhi kubwa duniani.

Hivyo ndivyo alivyokuwa akijinata wakati wa kampeni nzima ya kuwania urais.  Wapiga kura wa Marekani walimwamini, wakampa kura zao na ameibuka mshindi.

Trump hatokuwa rais wa kwanza wa Marekani aliyewahi kuwa mfanyabiashara.  Tangu karne ya 20 Marekani imekuwa na Marais  wasiopungua saba waliokuwa wafanyabiashara kabla ya kuingia Ikulu ya White House.

Ushindi wake Trump umewashangaza wengi Marekani na nje ya Marekani si kwa sababu yeye ni mfanyabiashara lakini kwa sababu ya alivyo.  Trump ni mbaguzi, fidhuli na mtovu wa adabu.

Chambilecho Rais Rodrigo Duterte wa Philippines aliyesema kwamba yeye na Trump ni chapa moja kwa sababu “sote tunapenda kutukana”.

Trump ana dalili za kifashisti, ana viashiria vionyeshavyo kwamba atatawala kimabavu ingawa hatoweza kufanya hivyo kwa sababu Marekani ni nchi yenye demokrasia ya kibwanyenye na taasisi zake za kuilinda demokrasia hazitomruhusu.

Jambo lake jengine lenye kushangaza ni kwamba hana itikadi ya kisiasa inayotambulika.

Anajiendea tu akisema maneno ya ovyo na ya ajabuajabu.  Maneno hayo yanatuwezesha tuagulie ni sera gani atazozitekeleza atapoushika usukani wa utawala.

Matamshi yake tangu siku za kampeni hadi sasa yamekuwa yakiwatisha Wamarekani Weusi, watu wenye asili za kigeni waliohamia Marekani pamoja na Waislamu wazalia wa huko na wale waliohamia huko.

Sababu ya Trump kushinda ni Hillary Clinton, mshindani wake mkuu katika mbio za kuukimbilia urais.  Waliokuwa wakimpendelea Hillary waliathiriwa zaidi na mambo ya hisia na sio ya sera.  Kwa mfano, kuna waliomuunga mkono kwa sababu yeye ni mwanamke na walikuwa na shauku ya kutaka Rais mpya wa Marekani awe mwanamke.

Kwa hakika, ingekuwa jambo zuri kabisa lau ingekuwa hivyo kwamba Rais ajaye wa Marekani angekuwa mwanamke. Lakini si mwanamke huyu.  Huyu, Hillary Clinton, ni bidhaa mbovu iliyokwishaharibika. Hivyo, ndivyo wengi wamuonavyo.

Lakini hata angekuwa mwanamke mwenye uadilifu isingetosha kwamba achaguliwe kwa sababu ya jinsia yake tu kama vile ambavyo haitoshi mgombea wa kiume achaguliwe kwa misuli yake au jinsia yake tu.

Kuna waliokuwa wakihisi ya kuwa itapendeza iwapo Hillary angeibuka mshindi kwa sababu ushindi wake ungekuwa wa kihistoria si tu kwamba ni mwanamke lakini kwamba ni mke wa aliyekuwa Rais.

Na lau angelikuwa Rais basi bao lingegeuka na mumewe, Rais wa zamani Bill Clinton, angekuwa “Mume wa kwanza” wa Marekani.

Yote hayo ni mambo ya hisia, ya matamanio yasiyohusika na sera na hayajibu swali la msingi la: “nini maana ya Hillary kuwa Rais?”  Angewafanyia nini wafanyakazi na wasio na kazi wa Marekani, angeufanyia nini ulimwengu na Afrika yetu ingefaidika vipi kwa ushindi wake?

Hisia hizo za waliompendelea Hillary hazikuwavutia waliomchagua Trump. Wako miongoni mwa waliomuunga mkono Hillary waliolijua hilo lakini maoni yao yalipuuzwa.  Mmojawao alikuwa mumewe mwenyewe Hillary, Rais mstaafu Clinton.

Sasa yaliyokuwa yakifichwa yameshaanza kuibuka na tunasikia kwamba hata yeye alikasirika sana na jinsi mkewe, Hillary, alivyokuwa akiendesha kampeni yake.

Wakati mmoja inasemekana Bill Clinton alighadhabika na kufoka alipokuwa akizungumza kwa simu na mkewe.

Mtu mmoja aliyekuwa naye wakati huo anasema aliingiwa hofu kwamba Bill angeweza kupata mshtuko wa moyo. Inasemekana hamaki zake zilimfanya airushilie mbali simu hadi sakafuni.

Kisa hicho kilitokea baada ya Hillary kuanza kumlaumu Mkurugenzi wa FBI (Shirika la Uchunguzi la Marekani), James Comey, alipoona kwamba huenda akashindwa katika uchaguzi. Comey ndiye aliyeamrisha Hillary achunguzwe, kwa mara ya pili, kwa ile kashfa ya baruapepe zake alipokuwa waziri wa mambo ya nje.

Sababu ya Hillary kushindwa ni Hillary mwenyewe.  Bill Clinton ananukuliwa akisema kwamba wa kulaumiwa alikuwa  Hillary pamoja na mwenyekiti wa kampeni yake, John Podesta, na meneja wa kampeni hiyo, Robby Mook.

Bill alizidi kukasirika kwa sababu Hillary akimpuuza. Hakutaka kusikiliza maoni yake na akimwambia kwamba fikra zake zilipitwa na wakati.

Kumbe ni yeye Bill aliyekuwa akiujuwa wakati ulivyo na nani aliyekuwa akilia na wakati na aliyehitaji kufuatwa na kubembelezwa na  kampeni ya Hillary.

Kwa mfano, Bill alitambua kwamba wengi wa Wamarekani wenye asili ya Kiafrika wamevunjika moyo sana na miaka minane ya utawala wa Rais Barack Obama kwa sababu ijapokuwa serikali yake ilizidi kuwapa misaada maisha yao bado yangali magumu.

Tathmini hiyo inaungwa mkono na wasomi wawili wa Kimarekani wenye asili ya Kiafrika, Profesa  Michael Eric Dyson na Profesa Eddie Glaude Jr.

Hivi karibuni kila mmojawao alichapisha kitabu juu ya namna utawala wa Obama ulivyowaathiri Wamarekani wenye asili ya Kiafrika.

Cha Dyson kinaitwa “The Black Presidency” na cha Glaude kinaitwa “Democracy in Black”.  Ukivisoma vitabu hivyo utaona kwamba havitafautiani na Bill Clinton kwamba sera za Obama hazikuwanyanyua Wamarekani Weusi.

Kuna na wasemao kwamba sera hizo ziliwatumbukiza katika nakama baadhi ya Wamarekani weusi.

Isitoshe, Bill pia akihisi ya kuwa Hillary hakuwashughulikia wazungu walio kwenye tabaka la wafanyakazi.

Profesa Noam Chomsky, yule msomi maarufu wa umma, naye anaamini vivyo hivyo.  Anasema kwamba Trump alipata ushindi alioupata kwa sababu chama cha Democratic cha mshindani wake mkuu kiliwatupa watu walio katika tabaka la wafanyakazi.

Tangu baada ya mumewe kuuacha urais, Hillary amekuwa akihisi kwamba zamu ni yake na ni haki yake kuingia Ikulu ya White House.  Kadhalika, kampeni yake nayo ilijikita zaidi juu ya yeye kuwa mwanamke.

Swali zito linalotuhangaisha sisi, bila ya shaka, ni: nini zitakuwa sera za Trump kuhusu nchi zetu na bara letu?

Kwa sasa, hatuwezi kulijibu swali hilo kwa sababu inavyoonyesha ni kwamba Trump hakulitia maanani bara la Afrika alipokuwa akizizingatia sera zake au mambo gani atayotaka kuyatekeleza atapokuwa Rais.

Kwa ufupi, tunaweza kusema kwamba Trump hana sera mahsusi kuhusu Afrika, pengine hana sera zozote zile kulihusu bara letu. Au pengine kutokuwa na sera ndiyo sera yake kuhusu Afrika.

Kwa hakika, hatutoweza kujua Trump ana dhamira na makusudio gani kuhusu Afrika mpaka labda pale atapomteua waziri atayelishughulikia bara hili na wasaidizi wake wengine pamoja na wakuu wa mambo ya usalama.

Nionavyo serikali ya Trump itajishughulisha na mambo matatu kuhusu Afrika. La kwanza ni mkakati wake wa vita dhidi ya ugaidi wa kimataifa, mkakati ambao utazidi kulitegemea jeshi la Marekani la AfriCom, linalozidi kujitanua barani humo.

La pili ni mahusiano ya kibiashara kati ya Marekani na nchi za Kiafrika na la tatu ni msimamo wa serikali hiyo juu ya suala la kuimarisha demokrasia barani Afrika.

Ama kuhusu vita dhidi ya ugaidi haielekei kwamba Trump atauacha mkakati huo au kwamba atalifanyia mageuzi makubwa jeshi la AfriCom, licha ya kwamba amekuwa akipiga kelele kuhusu ubadhirifu wa fedha za serikali na umuhimu wa kubana matumizi.

Nionavyo ni kwamba atawasikiliza wakuu wa majeshi na atawakubalia wazidi kuliingiza kwa kishindo jeshi la Marekani barani Afrika.

Haielekei, kwa mfano,  kwamba Marekani chini ya Trump itafikiria kuifunga kambi yake ya kijeshi iliyo Agadez, Niger, au ile ya Lemonnier iliyo Djibouti.

Serikali ya Trump inaweza hata ikazidi kuziimarisha kambi hizo na ikatafuta vijisababu vya kuwa na kambi zaidi za kijeshi barani humo.

Kisingizio chake kikubwa kitakuwa kuupiga vita ugaidi, hasa sasa ambapo ugaidi wa kimataifa unazidi kushamiri katika maeneo ya Sahel na Afrika ya Magharibi.

Kwa mujibu wa wenye kufuatilia nyendo za magaidi wanasema kwamba sura za magaidi na ya ugaidi katika maeneo hayo zinabadilika.  Mkuu wa jeshi la Nigeria, Luteni-Jenerali Tukur Yusuf Buratai alinukuliwa hivi karibuni akisema kwamba ingawa chimbuko la magaidi wa Boko Haram ni Nigeria lakini asilimia isiyopungua 60 ya magaidi hao ni watu wasio na asili ya Nigeria.  Ni wazalia wa nchi zilizo jirani ya Nigeria.

Magaidi hao wamekuwa pia wakifanya mashambulizi nchini Niger na Cameroon.  Mali nayo ina magaidi wake Kaskazini mwa nchi hiyo na jangwa la Sahara limekuwa likizidi kutumiwa na magaidi katika miaka ya karibuni kusafirishia silaha zilizoporwa Libya.

Kwa vile ni mfanyabiashara nadhani kwamba serikali ya Trump itazidisha kiwango cha biashara ya baina ya Marekani na Afrika. Itakuwa muhali nafikiri kwa serikali ijayo ya Marekani kuifuta ile Hatia ya Sheria ya AGOA inayorahisisha bidhaa kutoka Afrika ziingie katika soko la Marekani.

Wakati wa kampeni ya kugombea urais, Trump hajaidhukuru Afrika hata mara moja. Mshindani wake Hillary Clinton naye pia hakuitaja.

Trump amekuwa akisema kwamba vipaumbele vyake ni kuirejeshea Marekani hadhi yake na kuifanya sera yake ya mambo ya nje iyaweke mbele maslahi ya Wamarekani na usalama wa Marekani.

Trump huenda akataka kuendelea kuipuuza Afrika lakini nadhani akishaingia Ikulu tu washauri wake watamkumbusha kwamba Afrika ina umuhimu mkubwa kwa maslahi ya Marekani na hata kwa usalama wake.

Kwanza atakumbushwa kwamba asilimia kubwa ya madini yaliyo muhimu sana duniani yanapatikana Afrika.

Halafu atakumbushwa kwamba Afrika inakaribisha biashara kutoka Marekani ilimradi biashara hizo zisiwe zinazinyonya nchi za Kiafrika.

Ikiwa Trump atazinyima misaada nchi za Kiafrika basi atazifanyia fadhila kubwa nchi hizo kwani zitalazimika kuiacha ile tabia ya kuyaomba omba mataifa makubwa.

Chanzo: Raia Mwema

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s