Kwa CCM, tatizo Maalim Seif

CUF 000

Na Mwandishi Maalum

MATUKIO mawili yaliyotokea ndani ya vipindi visivyokaribiana sana, yamenisukuma kutotulia; haraka nikae kuyajadili. Ninayajadili kwa muktadha wa kuona athari mbaya za marufuku ya shughuli za kisiasa nchini.

Marufuku hii ya wanasiasa kutoendesha mikutano ya hadhara mpaka utakapowadia uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, ilitangazwa na Rais John Magufuli aliposhika tu hatamu. Baadaye ilikaziwa kwamba hata mikutano ya ndani isifanyike.

Rais Magufuli amekuwa akirudia amri yake hii kila anapojisikia; kama alivyofanya tarehe 4 Novemba akiwa Ikulu wakati akijibu maswali kwenye mkutano na waandishi wa habari, ulioandaliwa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya ofisi yake. Ilikuwa katika hafla ya kuadhimisha mwaka mmoja wa uongozi wake.

Tukio la kwanza ni la kitendo cha Jeshi la Polisi kumzuia kwa mara ya pili Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, kuendesha vikao vya ndani vya chama.

Ilitokea hivyo mara ya kwanza jijini Tanga. Katibu Mkuu wa CUF alizuiwa kushiriki kufungua mkutano mkuu wa wilaya wa chama. Polisi hawakujali kwamba wanazuia utekelezaji wa katiba ya chama cha siasa kilichosajiliwa kisheria.

Safari hii imetokea mkoani Mtwara. Jeshi la Polisi limemzuia tena Maalim Seif kuendesha mkutano wa ndani ambao ungempa fursa muhimu ya kuhutubia viongozi ambao kimuundo, ndio wasaidizi wake wakuu kwenye wilaya katika jukumu la kuongoza chama hicho.

Katika sababu ambazo viongozi wa Jeshi la Polisi wamezitoa kujenga hoja ya uamuzi wao wa kumzuia Maalim Seif kufungua vikao vya ndani ya chama anachokiongoza, wakuu wa jeshi hili wanasema inatokana na taarifa za kiintelijensia walizozipata kuwa kutakuwa na uvunjifu wa amani mikutano ikifanyika.

Kuitafakari hali hii, wanamaana kwamba iwapo wataruhusu viongozi hao wa CUF wakutane, tena ndani ya ukumbi, sio hadharani watu wengine wakishuhudia, na kuzungumza masuala yanayohusu ustawi wa chama chao, basi itakuwa sivyo. Wataibua machafuko, kwa mujibu wa fikra za walinzi wa amani.

Bila ya shaka mazingira ya kuzuia mikutano hii miwili ni yaleyale. Jeshi la Polisi kutumia kigezo cha chama hicho kuwa katika mtafaruku unaohusisha tatizo lililotengenezwa na Profesa Ibrahim Lipumba, baada ya kulazimisha kurudi kwenye uenyekiti, wadhifa alioutema mwenyewe kwa barua ya tarehe 5 Agosti 2015.

Prof. Lipumba, mtaalamu gwiji wa uchumi, aliyepata kufanya kazi Benki ya Dunia, na kuwa mshauri wa Rais Yoweri Museveni nchini Uganda, alijuzulu kwa hiari yake kupitia taarifa aliyoitoa mbele ya waandishi wa habari tarehe 6 Agosti mwaka jana. Alifanya mkutano huo Hoteli ya Peacock, Mnazimmoja jijini Dar es Salaam.

Lakini miezi kumi baadaye, tarehe 10 Juni 2016, alimwandikia Katibu Mkuu Maalim Seif, kumjulisha kuwa ametengua uamuzi wake wa kujiuzulu uenyekiti. Anamjulisha katibu mkuu kwamba yuko tayari kuingia ofisini kuanza kazi.

Hakukubaliwa haraka kuingia ofisini kuanza kazi.

Ni kinyume na matarajio yake ingawa aliridhia kusubiri kwa kadri alivyoelekezwa na katibu mkuu. Alipoona kuwa kimya kimezidi, kama anavyoeleza mwenyewe, akaamua kusikiliza anaoita “wanachama na baadhi ya viongozi” ambao anadai walimuomba arudi kwenye uongozi.

Prof. Lipumba wakati ule 2015, alishikilia na hatimaye kutangaza kujiuzulu licha ya kupata ushauri na nasaha za wanachama wakiwemo wazee walipomuomba afute nia yake hiyo na asubiri kumalizika kwa uchaguzi mkuu. Niseme kwa kifupi, aliwapuuza.

Safari hii anadai ametii ushauri wa “wanachama na baadhi ya viongozi” kumtaka ahudhurie mkutano maalum wa chama uliokuwa umeitishwa kwa lengo la kuchagua nafasi zilizokuwa wazi, ikiwemo ya uenyekiti. Eti ahudhurie ili suala lake lijadiliwe.

CUF iliandaa mkutano huo tarehe 21 Agosti mwaka huu ukumbi wa Blue Pearl, Ubungo Plaza. Ni hapo mkutano ulipolazimika kuahirishwa ghafla baada ya kuzuka mvutano uliohusiana na suala la kujiuzulu kwa Prof. Lipumba. Hapo mkutano ulisharidhia kwa kura kujiuzulu kwake.

Kufikia sasa, Prof. Lipumba anajitambua kuwa yungali mwenyekiti. Ameshikilia msimamo huo kwasababu ametambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini. Utambuzi huu ulikuja baada ya Msajili kuchambua malalamiko ya profesa na majibu ya katibu mkuu ambaye alitakiwa kuwasilisha majibu.

Matukio mawili ya kuzuiwa Maalim Seif kuhutubia vikao vya ndani, sasa yana sura nyingine tofauti. Kwanza ifahamike kuwa hakuna ubishi na uhalali wa Maalim Seif kuwa ndiye katibu mkuu wa CUF.

Yeye hajajiuzulu kama alivyofanya Prof. Lipumba, wala hajafukuzwa kama alivyofanyiwa profesa huyu baada ya kukaidi wito wa chama kumtaka afike mbele ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (BKUT), kilichofanyika mjini Zanzibar.

Katiba ya CUF inatambua kwamba katibu mkuu ndiye msaidizi mkuu wa mwenyekiti katika kulinda katiba ya chama. Ndio maana Prof. Lipumba alipoamua kujiuzulu, alimwandikia Maalim Seif. Ikumbukwe alikuwa maalim aliyetamka wakati ule kuwa kwa kadri anavyojua, Prof. Lipumba alikuwa hajajiuzulu.

Maalim Seif alitoa kauli hiyo alipoulizwa na gazeti la Uhuru, linalomilikiwa na kampuni tanzu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Ni kama vile uamuzi wa profesa kujiuzulu ulishajulikana zaidi CCM kuliko CUF.

Huyu Maalim Seif, kwa sura ya sasa ya utendaji wa jeshi la polisi, kumbe ndio tatizo la watawala wa CCM. Ninaziona sababu kadhaa. Ni kwanini naona hivyo? Mtwara ambako amezuiwa kufanya kikao cha ndani, profesa alifika na kukutana na viongozi wa CUF kwa mapana.

Sio kwamba alizuiwa na polisi, walimlinda asibughudhiwe. Alifanya hivyo Nachingwea na Masasi. Wiki iliyopita, baada ya kushiriki mazishi ya Samuel Sitta, spika wa bunge la tisa, wilayani Urambo, Tabora, profesa alihutubia kikao cha ndani cha viongozi wa CUF.

Maalim Seif ambaye hajajiuzulu wala kufukuzwa ukatibu mkuu wa CUF, anazuiwa kufanya kazi za ukatibu mkuu, hata kwa mfumo ule unaoruhusiwa na serikali ya CCM – kufanya vikao vya ndani.

Picha ninayoiona ni kuwa kwa watawala, Maalim Seif ndio shida. Sababu vilevile inajionesha: Ndiye kinara wa kupigania ushindi wa uchaguzi mkuu upande wa Zanzibar.

Sio kwamba watawala wanamzuia ili kudhoofisha CUF. Au kwamba wanalenga kuzuia ushiriki wake katika vikao vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA). Hapana. Shida yao ni upinzani wake dhidi ya Dk. Ali Mohamed Shein kushika urais.

Kampeni ya kurudisha haki ya Wazanzibari waliyoporwa kwa amri ya CCM anaiongoza yeye Maalim Seif. Sababu kubwa ya kuwindwa na dola. Alihutubia vikao vya ndani vya CUF wilaya zote kumi za Zanzibar. Walimzuia kusema na Waislam baada ya sala ya Ijumaa.

Lakini wanayafanya yote hayo wakati Maalim Seif alishajieleza ulimwenguni kote, alishajieleza kwa mapana Marekani, Uingereza na Canada. Alishafika Umoja wa Mataifa akajieleza. Hata Mahakama ya Uhalifu wa Kivita (ICC) ameacha vielelezo.

Kwa akili zao watawala, hawataki kufanya kosa tena. Njia moja tu – kumzuia asisikike. Habari ya kufunga banda, farasi akiwa ameshatoka.

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s