Dk. Shein tulia, ICC nini kiongozi…

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein na Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Haukeland Bw. Eivend Hansen wakikata utepe kuzindua jengo la wodi ya watoto
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein na Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Haukeland Bw. Eivend Hansen wakikata utepe kuzindua jengo la wodi ya watoto

Na. Jabir Iddrissa

AKIWA ziarani kisiwani Pemba, Dk. Ali Mohamed Shein amewaambia wananchi: Siwezi kuondolewa madarakani na Mahakama ya ICC. Haina uwezo huo. Hata mimi nasema, ni kweli mahakama hii haina uwezo huo. Wala mahakama hii haishughulikii kesi zinazohusu uchaguzi. Hata mara moja.

Mahakama ya Uhalifu wa Kivita – International Criminal Court – inashughulikia mashitaka yanayohusu vitendo vya uhalifu kama lilivyo jina lake. Vitendo vyenyewe ni vile vinavyohusu matendo ya watu wakiwemo wanasiasa nyakati za migogoro au hata penye amani.

Pale palipotokea matendo yaliyosababisha madhara ya uhai kwa binaadamu, na hata kusababisha raia kukimbilia maeneo ya nje ya makazi yao ya kawaida kwa lengo la kutafuta hifadhi salama, ndipo mahakama hii huingia. Itatuma wapelelezi wake hapo, na kuangalia kwa ukubwa gani matendo hayo maovu yametendwa.

Hata huko nyuma uzoefu wa utendaji kazi wa mahakama hii haujaonesha kujikita kufuatilia masuala ya uchaguzi. Hufuatilia uhalifu dhidi ya binaadamu na ubinaadamu.

Lakini ni jambo la wazi, na uzoefu wa mambo unathibitisha pasina shaka yoyote, kuwa uchaguzi ni miongoni mwa matukio makubwa yanayochangia uvunjaji wa haki za binaadamu nchi mbalimbali. Ni uchaguzi unaotumika kudhuru wananchi kwa sababu za kisiasa.

Uchaguzi unapovurugwa na kuhujumiwa, kama ilivyotokea Zanzibar, migogoro hutokea. Ni bahati tu kukuta safari hii kwa Zanzibar, tofauti na ilivyotokea baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2000, hakukutokea machafuko. Watu hawakupigana au kuingiana mwilini.

Lakini ipo kwenye rekodi kwamba wakati wa kampeni ya uchaguzi wa Oktoba mwaka jana, vyombo vya dola vilikuwa vinawapiga wananchi. Askari waliojifunika nyuso zao kwa kutumia vitambaa vyeusi walionekana wakizunguka mitaa ya mji wa Zanzibar na kupiga raia, wengine wakiwa wametulia kwenye baraza za majumbani kwao.

Wananchi wengine walipigwa na kudhalilishwa kwenye baraza za mazungumzo wanamokaa baada ya mahangaiko ya mchana kutwa ya kutafutia riziki familia zao na kujenga taifa lao. Watu waliokuwa wakipiga wananchi, wakiwa wamebeba silaha za moto na za jadi, walikuwa wamepakiwa kwenye gari za serikali.

Matukio kama haya ya askari wa serikali kupiga na kudhalilisha wananchi, ikiwemo kuwajeruhi kwa kupata majeraha makubwa, yakaongezeka baada ya tarehe 28 Oktoba 2015, siku ambayo uchaguzi mkuu wa Zanzibar ulivurugwa kufuatia tangazo la kuufuta na matokeo yake yote. Jecha Salim Jecha, aliyeongoza Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ndiye alitoa tangazo hilo.

Ni tangazo baya kiusalama na kidhamira, lililotolewa wakati kada huyu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiwa mafichoni, kule ambako yeye binafsi pamoja na wale waliomtuma wanakujua vizuri. Alilitoa baada ya kukimbia au kutelekeza majukumu yake ya kusimamia kazi ya kuhakiki na kutangaza kura za uchaguzi wa rais, akiwa amewaacha kwenye mataa wajumbe wa tume hiyo.

Wakati akitangaza, Jecha alikuwa anajua vizuri akitekeleza mpango wa kuhujumu haki ya wananchi kuchagua viongozi wawatakao. Alijua vizuri kuwa kisheria hakuwa na mamlaka ya kufanya alichoshikwa kufanya. Alijua fika kwamba akishafanya hivyo, atakuwa ametengeneza mazingira ya hofu katika nchi na vifuani mwa wananchi. Kadhalika alijua kuwa atakuwa ameiangamiza haki na kuzua tafrani kiusalama.

Waliolazimisha Jecha kutoa tangazo lile wapo. Wanajulikana. Wapo. Na ndio hawa ambao walishikilia pawari kwamba askari walioamua kufanya uharamia dhidi ya wananchi waendelee kuzunguka mitaa na kupiga na kudhalilisha wananchi. Ndio wale waliosimamia kuhakikisha Jecha huyohuyo anatangaza siku ya kufanyika uchaguzi ambao wameuita “uchaguzi wa marudio.”

Uchafuzi wao ukashuhudiwa kwa mara nyingine. Vituo vya uchaguzi havina watu, lakini kura zilizokuja kutangazwa na Jecha zikawa nyingi zisizokubalika hata kwa macho ya kinda wa darasa la tatu. Televisheni ziliwaumbua wapangaji ubaya ambao ni kweli kama ilivyosema huko nyuma, wanapenda namba lakini hawajui hisabu. Hawaijui desturi ya namba kuwa haikosei popote inapowekwa.

Baada ya uchafuzi na matangazo ya sherehe na kuapishana, vikosi vya ujahili vikatumwa kuendelea kupiga wananchi. Wanaopigwa mpaka siku hizi ni wale walioaminika (hapana wamehisiwa) walipigia kura wagombea wa upinzani dhidi ya CCM. Kwa hivyo wapangaji ubaya na uchaguzi kuvurugwa, wanajua hali haijatulia. Hawajatulia na wenyewe.

Katika kujikusuru wanapayuka. Wanasema ovyo. Wanakaa vikao visivyokwisha. Imekuwa ada siku hizi viongozi wa CCM kukaa vikao zaidi nyakati za usiku, kinyume na mazoea. Si wanasema uchaguzi umekwisha, sasa vikao visivyokwisha vya kazi gani?

Watu waliotulia hawana sababu ya kuwa na vikao kila wakati hata usiku wa manane. Ni wachawi tu wenye desturi ya kukutana muda huo. Lakini yaonesha ni kweli, wapanga ubaya wameingia katika ushirikina.

Dk. Shein anaposema mahakama ya uhalifu wa kivita haiwezi kumuondoa madarakani, anayo sababu ya kusema hivyo, ingawa kimantiki, anazidi kujiumiza. Hivi ni nani amepata kusema ICC itamuondoa madarakani? Kwani aondolewe hapo kwa makosa gani? Yeye ameshasema hajafanya kosa na amekaa hapo kihalali kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, sasa shida iko wapi hata aondolewe?

Tena, amepata uungaji mkono wa kiongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, ambaye katika kuonesha dharau ya utaratibu wa kikatiba na kutambua mamlaka ya wananchi, hakusita kumhakikishia kuwa afanya kazi zake bila hofu, na hakuna atakayemuondoa. Alimwambia akiwepo anayemhisi anamsumbua, amtajie tu, “nitamshughulikia dakika chache tu.”

Basi Dk. Shein asihofu kitu. Aendelee tu kudunda katika kiti cha enzi. Wala asijali kama ni kweli amekaa hapo kwa haki au kwa kudhulumiwa haki ya wananchi. Asijali chochote. Nataka kumsihi daktari kwamba kwa namna ilivyo, kitakachomuondoa alipo ni dhamira yake mwenyewe.

Ndivyo ilivyo, Dk. Shein amebeba mzigo wake na atautua chini atakapochoka kuubeba. Hana msaidizi wa mzigo huo, ni mzigo wake mwenyewe. Peke yake. Ndo mwenye dhima. Dhima yake peke yake. Kwa hakika hana msaidizi katika hilo.

Lakini kwa upande mwingine wa shilingi, katika kutohofu kitu, basi asihangaike kutoa maneno ambayo hajawahi kuyasikia yakisemwa popote. Haya maneno ya kwamba ataondolewa na ICC ameyasikia wapi?

ICC haitamuondoa Ikulu. Lakini mahakama hii inazo rekodi na vielelezo vya udhalilishaji na unyanyasaji wananchi uliofanywa na askari wa serikali chini yake. Wananchi wamedhalilishwa kwa maelekezo ya serikali yake, wasaidizi wake, mawakala wa serikali na chama chao.

Mimi sitaji majina maana sinayo. Bali kule The Hague, nchini Uholanzi kwenye makao makuu ya mahakama hii ya ICC, kwa taarifa za uhakika nilizonazo, yako majina yametajwa. Ni majina ya watu wake, watu kibao waliohusika kuelekeza vitendo vya udhalilishaji na unyanyasaji wananchi ambao hawakuwa na lolote la kujitetea. Wananchi hohehahe.

Ijulikane wazi kwamba mkono wa sheria zinazosimamiwa na ICC – ambao hautumiki kuondoa mtu ikulu, haukwepeki. Na wabaya waliohusika kudhalilishwa na kuumizwa wananchi wa Zanzibar, hawatasalimika. Watakumbwa tu na mkono huu. Ndivyo utaratibu wa kidunia ulivyo. Angalau mpaka pale Tanzania nayo itakapoondoa wino kwenye uanachama wa kuanzishwa mahakama hii.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s