Suali kwa Rais Magufuli

john-magufuli

Jaji Warioba alipotoa hoja zake ikiwa ni kutetea rasimu ya katiba alijibiwa kwa matusi badala ya hoja. Rais alipoulizwa maswali na waandishi Ikulu baadhi alijibu kwa hasira na mengine aliyakwepa pamoja na kuwadhihaki waliouliza maswali yaliyoonekana wazi kumkera. Sasa huyu sijui atajibiwa kwa hoja, au naye atadhihakiwa kama wenzake

Jaribu kusoma mpaka mwisho utajifunza kitu.

Rais John Magufuli mimi ninaitwa Padri Privatus Karugendo ni mwandishi na mchambuzi wa masuala ya kijamii na kisiasa kwa miaka mingi sasa.

Bahati mbaya wiki iliyopita ulipokutana na waandishi wa habari Ikulu, sikupata mwaliko. Yawezekana mwaliko ulikuwa wa maelekezo.

Au ni mwaliko ambao ulifuata vigezo ambavyo viliniacha mimi na wengine wengi nje? Vyovyote vile ni kwamba sikupata nafasi ya kuuliza swali langu juu ya mwaka mmoja wa uongozi wako kama Rais wetu wa Serikali Awamu ya Tano.

Siyo lengo langu kumshtaki yeyote kwenye makala haya, bali ni imani yangu kwamba vigezo na masharti yenye kuzingatia kazi na mchango mkubwa wa waandishi wa habari yakifuatwa, siku itakuja, nitaweza kuingia Ikulu, kukutana na wewe na kuungana na waandishi wenzangu kuuliza maswali na kujadiliana na wewe juu ya mwelekeo wa Taifa letu.

Kwa vile umesema utakuwa ukikutana na waandishi wa habari mara kwa mara, basi navuta subira.

Nimekusikia ukisema unasoma magazeti yote. Hivyo nimeamua kuandika swali langu kwenye makala haya, nikiamini utalisoma na kulipatia majibu.

Kwanza kabisa niungane na waandishi wenzangu kukupongeza kwa kutimiza mwaka mmoja kwenye uongozi wa Taifa letu.

Nakumbuka tarehe kama ya leo, mwaka jana nilikuwa miongoni mwa watu walionyeshewa mvua pale Uwanja wa Taifa, nikishuhudia ukiapishwa kuliongoza taifa letu la Tanzania. Hongera kwa kutimiza mwaka mmoja.

Nyakati tofauti nimekuwa nikitoa maoni yangu juu ya uongozi wako na hasa nikijikita kwenye hoja ya utumbuaji, ukarabati na uponyaji.

Kusema ukweli maswali ninayo mengi, lakini kwa leo niulize swali moja tu: Rais Magufuli, yako wapi maandishi yako? Tujuavyo sote ni kwamba maandishi ni kitu kinachomtambulisha mtu, fikra zake, maono yake na wakati mwingine uwezo wake wa kufikiri na kuchambua masuala mbalimbali katika jamii.

Uko wapi mwongozo wako? Uko wapi mfumo wako ambao ungependa Watanzania waufuate? Tulizoea huko nyuma, Mwalimu Julius Nyerere, akitoa tamko lolote la kisiasa, kesho yake tunapata mwongozo, tunapata maandishi na maelekezo.

Akisema siasa ni kilimo, vitabu vinafuata. Akisema ujamaa na kujitegemea, vitabu vinafuata. Vitabu hivi vinakuwa kama mwongozo na mfumo ambao Watanzania walifuata.

Wewe unasema Hapa Kazi tu! Je, hii ni falsafa au ni kaulimbiu? Vyovyote vile, uko wapi ufafanuzi wake? Yako wapi maandishi, ili watu wasome, wajifunze na kufuata mkondo?

Wewe ni mwalimu, unafahamu jinsi ilivyo vigumu kufundisha tu bila kuandika ubaoni, ili wanafunzi wakaandike kwenye vitabu vyao na kwenye akili zao. Mwanadamu daima anahitaji mwongozo.

Wasaidizi wako wanafanya nini? Au umewazuia wasiandike? Kumbuka kilichoandikwa kimeandikwa na kilichoandikwa huwezi kukipindisha au kukizulia uongo.

Tunahitaji vitabu vyako. Vitabu vya zamani na vya sasa. Mtu mwenye maono, kiongozi ni lazima kuandika. Tunahitaji vitabu vinavyoelezea yale yote ambayo umeyafanya kwa kipindi hiki kifupi cha mwaka mmoja. Hili linawezekana kabisa na wala si jambo la kujadili kwa muda mrefu.

Hoja hapa ni kwamba wewe una maono na mwelekeo ambao ungependa taifa lifuate. Maono haya yako kichwani mwako.

Ili uyashirikishe kwa Watanzania wenzako ni lazima uyaandike na kuyapanga kwa kufuatana. Ili Watanzania wasome, wajifunze na kuyatekeleza.

Tunaamini unaanzisha mambo ya kudumu ambayo hata ukishaondoka madarakani yatabaki nyuma kama urithi wa uwepo wako. Tunajifunza mengi kutoka kwa wanafalsa wa kale ni kwa vile mawazo yao yaliandikwa.

Tunaweza kuyasoma, kuyakubali, kuyapinga au kuyaboresha. Viongozi wengi duniani wanakumbukwa kwa vile matendo yao na mawazo yao yaliandikwa. Tunajifunza kutokana na kazi zao kwa vile ziliandikwa kwenye vitabu. Tunahitaji vitabu vyako.

Katiba mpya

Nimekusikia ukisema, suala la Katiba mpya likae kwanza pembeni ili tuijenge nchi kwanza? Hapana! Itakuwa ngumu kuijenga Tanzania mpya, kwa Katiba ya zamani.

Nyakati zinabadilika ni lazima kutembea na nyakati. Katiba ya zamani haiwezi kukuruhusu kujenga Tanzania unayoitamani. Tanzania ya watu wote?

Wakati vyeo na nafasi nyingine za utendaji zinakwenda kwa chama kilichoshinda uchaguzi? Wakati Rais wa nchi ni lazima atoke kwenye chama cha siasa? Unasema kwamba wewe ni Rais wa watu wote?

Hata hivyo, ukweli ni kwamba wewe ni mwenyekiti wa CCM na unatenda ki-CCM. Unatekeleza sera za chama cha CCM. Mfumo huu umepitwa na wakati, lakini huwezi kuachana nao mpaka kariba ibadilike. Hakuna njia ya mkato.

Nimetaja kasoro ndogo tu kwenye Katiba ya zamani ambazo haziwezi kukusaidia wewe kujenga Tanzania mpya, lakini ziko nyingine nyingi kiasi kwamba kama kweli una nia ya kuleta mabadiliko na unaiweka kando Katiba mpya, basi kuna kitu bado kimejificha na unataka usitake, unahitaji msaada wa mawazo.

Usitake kutembea peke yako kama ule mto wa kule kwetu ambao kwa kutembea peke yake nyikani, ulipoteza mwelekeo.

Nimekusikisa ukisema uchaguzi umekwisha siasa tuziweke pembeni. Ukazuia mikutano ya vyama vya siasa. La kushangaza, wewe ukakubali kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama cha siasa.

Maana yake ni nini?

Ina maana siasa inazuiliwa kwa Watanzania wengine isipokuwa wewe? Unasema tuweke siasa pembeni, wewe unakiongoza chama cha siasa. Hivi huwezi kuwa rais mzuri bila kuwa mwenyekiti wa chama cha siasa?

Kama kweli unayasoma magazeti yote, mimi ni miongoni mwa watu waliokushauri usikubali kuwa mwenyekiti wa CCM.

Maana, nimetokea kufahamu mweleko wako. Kinyume na mategemeo yangu na ya wengine, ukakubali kuwa mwenyekiti.

Unategemea kuleta mabadadiliko gani? Unalalamika kwamba ndani ya CCM kuna mambo ya ovyo. Kumbuka hicho chama kina wenyewe.

Wamekijenga chama hicho kwa nguvu zao na jasho lao. Kwa vile ulikubali kuwa mwenyekiti ni lazima ufuate mkondo. Ukitaka chama kizuri, safi na cha kisasa anzisha chako au endesha nchi bila chama cha siasa.

Huwezi kuzuia shughuli za kisiasa, wakati wewe ni mwenyekiti wa chama kikongwe.

Nimesikia ukisema kwamba muswada wa huduma za habari utauwekea sahihi, pale ukiletwa mezani kwako. Pamoja na ukweli kwamba kuna dalili za muswada huu kutokupokelewa vizuri na wadau na walikueleza wewe, kama waandishi hawaupendi, ni wa nani?

Ninapoandika makala haya, tayari muswada huu umepitishwa na wabunge ambao wanatanguliza masilahi yao binafsi na kuiangalia nchi hii zaidi ya Tanzania mpya ya miaka mingi ijayo.

Wabunge wasiopenda kukosolewa, wasiopenda changamoto, wabunge wa chama kinachotamani kuitawala Tanzania milele. Wanafikiri kwa kuwabana waandishi wa habari ni njia ya kudhibiti habari.

Wanajidanganya kwa kupambana na wakati ambao tunaambiwa ni ukuta.

Ukweli ni kwamba sheria hizi ambazo zinatungwa kuwalinda na kuwatetea viongozi, sheria hizi zinazotungwa kuvilinda vyama vya siasa ili viendelee kutawala milele, sheria hizi zinazotungwa kuhakikisha zinazima uhuru wa kujieleza, zimepitwa na wakati.

Teknolojia

Teknolojia inaendelea kwa kasi na kutufundisha msemo wa wakati ni Ukuta. Inashangaza vijana ambao wako mstari wa mbele kutumia mitandao ya mawasiliano ya twitter, facebook, whatsapp na mingine wanashabikia sheria hizi za ovyo.

Teknolojia hii, iko mbele yetu na sheria hizi za kuwanyanyasa na kuwafunga waandishi wa habari ni za kuwalinda viongozi hawa wasiojiamini kwa muda mfupi. Ina maana gani kupitisha sheria ambayo kesho, tutalazimishwa kuifuta tunataka tusitake?

Daima, unasema tumtangulize Mungu. Uko wapi mfumo wako wa kuwafundisha Watanzania kumtanguliza Mungu. Somo hili la kumtanguliza Mungu ni pana.

Wewe unajua fika kwamba hata majambazi, magaidi na mafisadi, wanamtanguliza Mungu katika shughuli zao na wanafanikiwa.

Tunajua wewe unalenga kumtanguliza Mungu, katika kutenda haki, wema na huruma. Unalenga kumtanguliza Mungu kwenye mambo chanya na si hasi.

Wewe unalenga kumtanguliza Mungu, katika kulijenga taifa letu. Pamoja na kwamba kila Mtanzania ana namna yake ya kumwabudu Mungu wake, bado wewe kiongozi wa nchi ambaye umeamua kuunganisha theolojia katika kuliongoza taifa lako, huna budi kuwatafuta wanatheolojia wakakuandalia mfumo na mafunzo ya kuwaelekeza watu kumtanguliza Mungu.

Maana yake ni kwamba hata hapa tunaihitaji maandishi yako. Tunahitaji vitabu vya kusoma ili kupata mwongozo wa kumtanguliza Mungu.

Haitoshi kusema kwenye hotuba na kesho yake watu wakajenga tabia na utamaduni wa kumtanguliza Mungu.

‘Kubeep’ urais

Nimesikia unasema kuutafuta urais wa taifa letu uli ‘beep’ na simu ikapita? Sasa basi kaa kitako, omba msaada wa mawazo kutoka kila sehemu, uandike vitabu, utunge mwongozo na kuandaa mfumo.

Kufundisha ni lazima. Haiwezekani ukaambukiza roho ya kuchapa kazi bila kufundisha na kelekeza, haiwezekani ukaujenga uzalendo na moyo wa kulitanguliza taifa bila kufundisha na kuelekeza.

Hoja hapa ni kwamba kazi iliyo mbele yako ni zaidi ya kutumbua majipu ni zaidi ya vitisho na madaraka makubwa ya urais uliyo nayo ni zaidi ya hotuba na ziara za kushutukiza.

Unahitaji kujenga chuo cha mawazo, chuo ambacho hata kama hakitakuwa na kuta nne, lakini kiwe na vitabu, kiwe na mfumo na kiwe na mwongozo.

Chuo ambacho kitafundisha pamoja na mambo mengine umuhimu wa kufuata sheria, utaratibu na Katiba.

Mungu huyu unayesisitiza tumtangulize ameumba watu totafuti na kila mtu na uhuru wake, mawazo yake na maonjo yake.

Ili kuwaleta pamoja, wakaishi pamoja na kukubaliana kwa kiasi fulani ni lazima ziwepo sheria, taratibu na kwa mafanikio zaidi Katiba. Haya ni mambo ya msingi ambayo kuyapuuza ni kujidanganya.

Rais Magufuli nakutakia afya njema na Mungu akuongoze katika kuliongoza taifa letu. Hongera kutimiza mwaka mmoja.

+255 754 6331 22

pkarugendo@yahoo.com

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s