Hofu inayowaandama madikteta

Baadhi ya Wanaharakati wa Angola wakiwa mahakamani. Picha Jornalf8.net
Baadhi ya Wanaharakati wa Angola wakiwa mahakamani. Picha Jornalf8.net

NOV 10, 2016 

Hii ni hadithi yenye ncha nyingi. Ninaweza nikaianza kwa kitendawili: kuna uhusiano gani kati ya mkusanyiko wa wanaharakati katika duka la kuuzia vitabu Luanda, Angola, na mkusanyiko wa kidini Mji Mkongwe, Zanzibar?

Kwa hakika, wa Zanzibar haukuwa mkusanyiko mmoja bali miwili; wa kwanza wa Mashi’a na wa pili wa Masunni.

Au naweza kuianza kwa kutaja lililo wazi na lisilopingika: kwamba uhuru ni kitu adhimu. Na uwe uhuru wa kukusanyika, wa kufikiri, wa kusema, wa kuabudu, wa kusoma dua, wa kuwakosoa wakubwa, hata wa kuwaapiza. Uhuru wa aina yoyote ile.

Bila ya shaka uhuru una mipaka yake, sikatai. Hii ni mipaka ya uungwana, yenye kutenganisha baina ya yenye kuingia akilini na ya wazimu. Au baina ya ubinadamu na uhayawani.

Naweza pia kuianza simulizi hii kwa kuandika kwamba udikteta, kinyume na uhuru, hauna mipaka. Hauna kabila, rangi wala itikadi moja. Na si watawala peke yao wanaoweza kuwa madikteta. Wamejaa tele majumbani, wa kiume na wa kike.

Tukiyafumbua ya Mji Mkongwe na ya Luanda tunaona kuwa kuna uzi mmoja uliyoyaunganisha miji hiyo miwili. Nao ni uzi wa udikteta ingawa ya Luanda yametokea mwaka jana, miaka 51 baada ya yaliyojiri Mji Mkongwe.

Tuanze na ya Mji Mkongwe, ya mkusanyiko wa Mashi‘a wa madhehebu ya Ithnaasheri Ja’afari. Walikusanyika mahali panapoitwa Hussein Ta‘ziakhana.

Kabla ya Mapinduzi ya 1964, madhehebu matatu ya Kishi‘a yalikutana katika kijipembe kimoja cha Mji Mkongwe, karibu na Hamamni, kwani Hussein Ta‘ziakhana ilikuwa kama pua na mdomo na msikiti wa Mashi‘a wa Kibohora pamoja na iliyokuwa skuli ya Mashi‘a wa Kiismaili wanaoongozwa na Aga Khan.

Ingawa wapo wenye kuiita Hussein Ta‘ziakhana kuwa ni msikiti lakini hasa ni mahali pa taazia ambapo huombolezwa ushahidi wa Imam Hussein, mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), aliyeuliwa na Yazid ibn Muawiya. Kadhalika, watu hukusanyika hapo kwa ukumbusho wa kifo cha Mtume na siku za Milad Nabii husomwa Maulidi humo kusherehekea na kuadhimisha siku ya kuzaliwa Mtume.

Lakini Jumamosi ya Septemba 19, 1964 wakati wa ishaa waumini Wakishi’a walijazana ndani ya Hussein Ta‘ziakhana kwa kumbukumbu nyingine. Ulikuwa ni usiku wa kuomboleza kifo cha Bibi Fatma al-Zahra, binti wa Mtume (SAW).

Wakati huo giza lilikuwa limekwishavigubika vichochoro vya Mji Mkongwe. Majumbani kukiandaliwa chai ya usiku na nje waliokuwa wameteremka misikitini wakielekea makwao. Mheshimiwa mmoja, mjumbe wa Baraza la Mapinduzi, aliyekuwa akiitwa Mohamed Abdalla “Kaojore” alikuwa ndii, tayari amekwishalichapa tembo.

“Kaojore” alifuatana na dereva wake, ambaye pia alikuwa ‘chicha’, wakavikata vichochoro wakifululiza hadi Hussein Ta‘ziakhana. Walipofika hawakuwa na hodi wala sumile. Waliingia ndani kwa vishindo wakaufunga mlango.

Humo ndani walimkuta mwanachuoni Sayyid Abdul Muttalib bin Hashim, akisoma Ziyarat ya kumsalimia Binti wa Mtume kwa kusema:

“Salaam alayki ya Fatima RasuliLlah.”

Kaojore akamuuliza: “Huyu Fatma ni nani?”

Sayyid Abdul Muttalib akamjibu: “Ni binti wa Mtume.”

Kaojore akamuuliza jengine: “Mtume ni nani?”

Kabla hakumjibu Kaojore akamwambia: “Haya mwambie huyo Fatma kwamba nakuua.”

Jibu la Sayyid Abdul Muttalib likawa: “Huyu haambiwi…Haya ni mambo ya Mungu, ukitaka kuniua niue.”

Kaojore akafyetua risasi akiwalenga watu wazima na watoto. Watu watano walikufa wakawa mashahidi. Wengine 20 walijeruhiwa.

Waliouliwa walikuwa Sayyid Abdul Muttalib, Sayyid Ali Asghar bin Hussain, Haji Mohamed Asar, Abdul Hussain Remtullah Tejani, (babake Maalim Ja’afar Tejani, mwalimu wangu wa Kiarabu katika skuli ya sekondari) na Gulamabbas Kassamali.

Huyu wa mwisho alikuwa mtoto wa miaka 14. Babake, Kassu Nahoda, alikuwa rafiki mkubwa wa Rais wa wakati huo, Sheikh Abeid Amani Karume, tangu walipokuwa pwani, wakifanya kazi katika motaboti.

Hakuna lililomfika Kaojore. Sheria hata haikumgusa seuze kumtia nguvuni.

Inasemekana mtu alikwenda kutia fitina kwamba jamaa wa Kiithnasheri walikusanyika wakipanga kuipindua serikali.

Baada ya mauaji hayo, Karume alifanya mkutano wa hadhara na akadai kwamba mkusanyiko huo ulikuwa ni wa kisiasa. Lakini baadaye, aliamrisha kila familia ya waliouawa ipewe fidia ya shilingi elfu kumi. Rais Julius Nyerere wa Tanzania aliyesikia kuhusu msiba huo alikuwa kimya kama hapajatokea kitu.

Miaka minne baadaye palitokea kioja kingine katika nyumba ya bwana mmoja aitwaye Mohamed Said Salim ambaye siku hizi anaishi Oman. Nyumba hiyo iko Malindi nyuma ya msikiti mkubwa wa Ijumaa.

Siku hiyo iliyokuwa Ijumaa kuna wafuasi wasiopungua 14 wa tariqa ya kisufi ya Ba‘Alawi walioendeleza kawaida yao ya kwenda nyumbani humo kusoma Qasidatul Burda baada ya uradi wao wa alasiri kwenye Msikiti wa Ijumaa.

Burda ni shairi refu linaloghaniwa kumsifu Mtume Muhammad na limetungwa na sufi mkubwa wa Misri Imam Busiri.

Walipokuwa wanaendelea na kisomo walijishtukia wamekabiliwa na askari waliopanda juu ghorofani wakiwa na silaha nzito.

Mmoja wao aliwaambia waendelee kusoma mpaka wamalize. Nao wakaendelea mpaka mwisho, wakanywa kahawa yao na halafu wakachukuliwa na kupelekwa kituo cha polisi cha Malindi.

Huko wakatendewa kama watendewavyo wahalifu wa jinai. Waliambiwa watoe vitu walivyokuwa navyo na wakawekwa chumbani toka saa hizo hadi kama nne za usiku.

Halafu wakapakiwa ndani ya magari ya polisi hadi jela kuu la Kiinua Miguu. Huko walitumbukizwa kwa “Ba Mkwe”, sehemu ya mateso. Waliselelea jela kwa takriban mwezi.

Kwa jumla, walikuwa watu wapatao 14. Miongoni mwao walikuwa Sayyid Ahmed bin Hassan, Sayyid Muhammed Abbas, Bwana Kheri, Mzee Mfaume, Sayyid Ahmed Abbas na Maalim Zubeir Rijal, aliyenisomesha baiolojia skuli ya sekondari.

Wiki moja baadaye waliendewa na Ibrahim Makungu, aliyekuwa mkuu wa usalama, akawaambia kwamba uchunguzi uliofanywa ulionyesha kwamba hawakuwa na kosa na kwamba walitiliwa fitina za uongo.

Wakapewa karatasi zilizowataka wasihadithie nje walioyaona Kwa Ba Mkwe na wakaamrishwa watie saini zao kuridhia. Halafu wakachukuliwa kupelekwa kwenye mkutano uliohutubiwa na Karume.

Yeye, kwa upande wake, aliwaambia kwamba uchunguzi uliofanywa ulionyesha kwamba mashekhe hao walikuwa na kikao kikubwa chenye makao yake makuu London na wenzao Dubai na kwamba waliokuwako Zanzibar walikuwa wafanye machafuzi ya kisiasa.

Karume akaamrisha warejeshwe jela na akauliza: “Na wale wengine wako wapi?”

Swali hilo likawa ishara ya kukamatwa mashekhe wengine na kupelekwa jela, akiwemo Sayyid Omar Abdalla (Mwinyi Baraka).

Bwana huyu alikuwa kama taasisi ya mtu mmoja; pamoja na kuwa bahari ya elimu ya dini alikuwa pia mhitimu wa vyuo vikuu vya Makerere, London na Oxford, Uingereza, alikoandika tasnifu ya falsafa juu ya “The Concept of Felicity in Medieval Islam” (Dhana ya Sudi katika Uislamu wa Enzi za Kati yaani miaka 1100 hadi 1500). Aliwasomesha wengi, akiwemo Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi.

Hatimaye mashekhe hao waliachiwa huru. Hata hivyo, wengi wao walidhurika. Maalim Zubeir, kwa mfano, aliingiwa na hofu na wasiwasi mkubwa uliosababisha shinikizo lake la damu lipande na kuwa sababu ya mauti yake miezi kadhaa baadaye.

Kuna mmoja Zanzibar ilimtumbukia nyongo kiasi cha kumfanya asitake tena kuikanyaga nchi yake baada ya kupata fursa ya kuihama. Hadi leo anaishi ughaibuni.

Serikali ilithubutu kuufanya uhabithi huo kwa sababu ilikuwa ya kidikteta. Hapakuwako utawala wa sheria. Aghalabu serikali kama hizo licha ya kuwa zinatisha, nazo pia huishi kwa woga. Huziogopa fikra na huiogopa mikusanyiko ya watu.

Woga wa aina hiyo ndio uliowaponza wanaharakati wa Angola waliobandikwa lakabu ya “Klabu ya Vitabu ya Luanda”.

Kutoka Mei hadi Juni mwaka jana wanaharakati hao wakikutana kila Jumamosi katika “Livraria Kiazele” duka la kuuzia vitabu lililo Luanda. Wakikutana kujadili mbinu za kuleta mageuzi nchini mwao kwa njia za amani.

Juni 20, 2015 walikutana kuusoma na kuujadili muswada wa kitabu ulioandikwa na Profesa Domingos da Cruz, mwandishi wa habari na mhadhiri wa chuo kikuu. Awali ilipangwa Da Cruz awepo lakini siku ilipowadia hakuwepo.

Muswada wa Da Cruz hivi sasa umekwishachapishwa na ni kitabu kinachoitwa “Ferramentas para Destruir o Ditador e Evitar Nova Ditadura: Filosofia Política da Libertação para Angola’’ (Zana za Kumwangamiza Dikteta na Kuepusha Udikteta Mpya: Falsafa ya Kisiasa kwa Ukombozi wa Angola).

Kilichomchoea Da Cruz aandike kitabu hicho ni kile kitabu maarufu cha msomi wa Marekani Gene Sharp, aliyeiasisi Taasisi ya Albert Enstein. Kitabu cha Sharp kinaitwa “From Dictatorship to Liberation” (Kutoka Udikteta Kuelekea Ukombozi).

Moja ya imani za Sharp ni kwamba mapambano yasiyotumia silaha yana fursa kubwa zaidi ya kufanikiwa kushinda yale yenye kutumia nguvu. Sharp anaamini hivyo kwa sababu anasema tawala za kimabavu zinawazidi wapinzani kwa nguvu zao kubwa za kijeshi.

Kitabu cha Sharp kimekuwa kikitumiwa na wanaharakati wa nchi mbalimbali duniani wanaotafuta mbinu za kuleta mageuzi ya amani nchini mwao.

Kitabu cha Da Cruz nacho kinapinga upinzani kutumia nguvu na mapinduzi ya kuupindua udikteta. Da Cruz anahoji kwamba mapinduzi ni hatua inayourejesha nyuma mchakato wa mageuzi na kwamba aghalabu huzusha udikteta mpya. Wala Da Cruz hapendelei wanaharakati wasaidiwe na watu wa nchi za ng’ambo.

Juu ya yote hayo serikali ya Angola inadai kwamba wanaharakati wa “Klabu ya Vitabu ya Luanda” walikuwa wakila njama za kuipindua serikali.

Walikamatwa na Machi 28 mwaka huu, wote 17 walipewa vifungo vya baina ya miaka miwili hadi minane pamoja na kutozwa faini ya kwanza 50,000 (sawa na dola 300 za Marekani). Da Cruz mwenyewe alihukumiwa kifungo cha miaka minane na nusu.

Miongoni mwa wanaharakati hao mna wasomi, dereva, waalimu na waimbaji wa hip hop. Mdogo wao kabisa ana umri wa miaka 19.

Baruapepe: ahmed@ahmedrajab.com

Chanzo: Raia Mwema

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s