Jecha ataishi hivyo hivyo…

jecha-kituoni

KALAMU 364

AMESIKIKA Rais Dk. John Magufuli akishikilia msimamo kuwa Dk. Ali Mohamed Shein, ndiye rais wa Zanzibar. Anarudia kauli hii wakati huu anapotimiza miezi 12 ya kuwepo mamlakani.

Dk. Magufuli, aliyekuwa waziri katika serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu mwaka 1996 alipoanzia naibu waziri, alikula kiapo cha utii cha kutumikia uongozi wa juu nchini, baada ya uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba 2015.

Kwa hatua yake hiyo ya kushikilia msimamo wa kumridhia Dk. Shein, na hiyo kuwa na maana ya kuendelea kulazimisha wananchi wamkubali, kumtii na kumuunga mkono, anazidi kuthibitisha kuwa hajabadilika.

Kwamba kiongozi huyu wa jamhuri na pia mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), hatabadilika au kubadilisha msimamo na anawaambia wanaomsubiri labda atabadilika, wasimshughulishe, wanajisumbua.

Huyu kiongozi anataka ieleweke kwa asilimia zote 100 kuwa hata Wazanzibari wakiendelea kutoamua kumkubali, kumtii, kumridhia na kumuunga mkono Dk. Shein kama kiongozi wao, basi wanajihangaisha tu. Kwamba anawaambia hakuna manufaa yoyote watakayoyapata.

Rais Magufuli anasema Zanzibar ni shuwari. Hali ya usalama wa sehemu hii ya jamhuri, ni nzuri isiyokuwa na hata chembe ya tatizo.

Anajiamini kwa mara nyingine na kusema kama kiongozi mkuu wa taifa, anatekeleza ipasavyo jukumu la kuhakikisha Dk. Shein anaendesha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) vizuri na hakuna anayemshughulisha.

Ikumbukwe kuwa miezi ya nyuma hapo, Rais Magufuli alipata kumtoa hofu Dk. Shein kuhusu hatima yake. Alimwambia awe na amani, yeye anamuunga mkono kwa hali zote na kama kuna anayemhofia, amtajie tu “nitachukua hatua muda mfupi.”

Katika kilichoonekana kama kuchoma msumari jeraha bichi, Rais Magufuli akawageukia wananchi wasiomridhia Dk. Shein akisema hata wakimpinga na kuchoma samaki na nini, “uchaguzi ulishafanyika, huyo ndiye amechaguliwa rais halali na ataendelea kuwepo.”

Wakati akitoa kauli kwenye mahojiano yake na wahariri Ikulu jijini Dar es Salaam juzi Ijumaa 4 Novemba, Rais Magufuli, usoni alionesha kukasirika. Alikasirika kuulizwa swali lililohusu msimamo wake huo. Kwa kweli sitokuwa namkosea nikisema alimkasirikia muuliza swali.

Hali hiyo ina maana kubwa moja: Rais hapendi kuulizwa kuhusu mgogoro wa Zanzibar. Hapendi na laiti angeweza, pengine angetangaza hadharani kuwa ni marufuku kwa mtu yeyote kumuulizia masuala ya Zanzibar yanayohusu kilichotendwa Oktoba mwaka jana.

Kadiri anavyoshikilia msimamo wake huo, kwa upande mwingine, ajue ndivyo anavyozidi kuwasukuma wasioamini hicho anachokishikilia kama ni haki, kujenga chuki. Chuki inajengwa dhidi ya huyo anayemkingia kifua; na hata yeye mwenyewe.

Labda niseme hapa, tangu Rais Magufuli alipomsifia Jecha Salim Jecha hadharani kwamba ametimiza jukumu lake vizuri kwa asilimia zote, kada huyo wa CCM hajabadilisha staili ya kuishi. Baada ya kutangaza kufuta uchaguzi na matokeo yake pale 28 Oktoba, 2015, hayuko huru.

Jecha hana amani hata kama atakanusha akishasoma hapa rafiki yangu huyu. Anaendelea kuishi kwa hofu. Hajarudi kuishi kwenye makazi yake na familia yake, yaliyozoeleka na kujulikana kuwa ndio mji wake, Bububu, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Jecha anaishi kwa siri, tena chini ya ulinzi mahsusi anaopewa na walinzi wa serikali. Hajathubutu kutembea kwa uhuru, popote atakapo na kwa wakati wowote autakao.

Mara moja alitoka na kwenda ofisi kuu za kampuni ya simu ya mkononi ya Zantel, eneo la viwanda vidogo la Amani, mjini Zanzibar. Mtumishi mmoja wa Zantel aliniambia Jecha alikwenda kubadilisha laini ya simu yake. Ndani alifuatana na mtu mmoja aliyehisiwa ni askari kanzu.

Alipata bahati kukutana haraka na mtumishi anayemfahamu. Walikuwa peke yao wawili wakati akihudumiwa, huku wakiongea kwa maneno machache. Walikuwa Jecha na mtumishi anayemhudumia.

Watumishi wengine walitoweka eneo hilo mara tu alipotokea mbele yao; mmoja akisema kwa sauti ya chini, “roho yangu nzito kuendelea kumuona usoni pangu.”

Hata mwenyewe Jecha alibaini amezusha hofu. Alipomaliza kuhudumiwa, aliharakia kutoka na hatimaye akaondoka pale Zantel kwa kasi akiendeshwa. Sema wewe kama anatembea kwa uhuru.

Jecha tangu alipojidharau, kama vile mtu aliyepoteza fahamu zake, amekuwa akijitokeza hadharani pale panapokuwa na hafla ya kitaifa, tena ile ambayo anakuwepo Rais Magufuli.

Hajawahi kujitokeza kwenye hafla ambayo Dk. Shein ndiye kiongozi mkubwa, ndani ya Zanzibar. Kila kitu kinaonekana kupitia kamera za televisheni ambazo hazina kawaida ya kupotea njia.

Kibarua mmoja kwenye Bandari ya Zanzibar, iliyopo Malindi, ameniambia kuwa Jumamosi iliyopita asubuhi changa, Jecha aliingia bandarini na kwenda kupanda boti iliyokuwa inapakia abiria wa kwenda jijini Dar es Salaam. Alipopanda akaenda moja kwa moja sehemu ya juu wanakokaa abiria wa daraja la juu.

Lakini naambiwa alikurupuka huko na kushuka daraja la chini baada ya kumuona Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), yule ambaye Jecha aliapa kuwa ulimi wake hautathubutu kumtangaza kuwa ndiye mshindi wa uchaguzi.

Hapana shaka Jecha aliogopa fadhaa. Wiki iliyopita Maalim Seif alimtaja kuwa ndiye mtu aliyehujumu uchaguzi na kuitia nchi kwenye msukosuko, ili nini; chama chao CCM kibaki madarakani.

Ipo kwenye rekodi kuwa Jecha alijiapiza kipindi cha baada ya kuteuliwa kuwa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) mwaka 2013, na kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015. Hapana shaka alijua chama chao kitaendelea kushindwa kura halali.

Haya mazingira anayoyaishi Jecha yanamdhoofisha afya yake. Anaumia rohoni na akilini. Anaumia kwa sababu anajua hakutenda sawa kwa alichokitenda.

Anajua hata alipokutana na wajumbe wa tume Novemba mosi 2015, siku chache baada kufuta kibabe uchaguzi, alikuwa anajaribu tu kujisahihisha lakini ni kwa utaratibu wa kurekebisha makosa kwa kutenda makosa mengine.

Ndani ya kikao kile alianza kwa kuwataka radhi wajumbe akiwemo Makamu Mwenyekiti Abdulhakim Issa Ameir. Eti anasema alifanya vile kunusuru balaa Zanzibar. Tena akanukuliwa kusema “nilinusuru CCM kuanguka.”

Jaji Abdulhakim wa Mahakama Kuu Zanzibar siku ile ya 28 Oktoba, alitekwa kinamna muda mfupi kabla ya Jecha kutoa tangazo la kuhujumu uchaguzi. Alitangazia mafichoni chini ya ulinzi mkali.

Jaji yeye alipelekwa Ziwani, yalipo Makao Makuu ya Polisi upande wa Zanzibar. Alikaa huko kwa saa tatu hivi kabla ya kupelekwa nyumbani kwake. Hakudhuriwa.

Hali hii ya maisha ya hofu kwa Jecha, itaendelea mpaka 2020 iwapo haki ya wananchi iliyoporwa kwa nguvu ya dola haitarudishwa kunakostahili. Ni haki ya kuongozwa na yule waliyemchagua.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s