Shein afungukia Pemba

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein akiwahutubia wafanyakazi wa idara za mahakama, wanasheria na wananchi waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa jengo la mahakama kuu Chakechake Pemba. Picha: Haji Nassor
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein akiwahutubia wafanyakazi wa idara za mahakama, wanasheria na wananchi waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa jengo la mahakama kuu Chakechake Pemba. Picha: Haji Nassor
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wananchi kisiwani Pemba kuendelea kufanyakazi kwa bidii kwa kushirikiana na serikali na kuzipuuza taarifa za serikali nyingine kuingia madarakani.

Aliwaambia wananchi kisiwani hapa kuwa serikali anayoiongoza iko madarakani kwa mujibu wa Katiba na inaendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM hadi mwaka 2020 ambako itaeleza namna Ilani hiyo ilivyotekelezwa.
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo na mimi ndie Rais. Ni serikali halali kwa mujibu wa Katiba ya mwaka 1984” Dk. Shein alisisitiza na kutoa changamoto kwa yeyote anayejihesabu kuwa ni Rais ajitangaze.
Aliwahakikishia wananchi hakuna nchi wala taasisi iwe ya ndani au ya nje inayoweza kuiondoa serikali iliyopo sasa na wala hakuna wa kuhoji uhalali na uwepo wa serikali hiyo.
“Hakuna nchi inayoapishwa Rais mara mbili. Mimi sina wasiwasi na Serikali yenu haina wasiwasi na tuko hapa kuwatumikia ili kuendeleza nchi yetu. Maneno haya yanawapotezea muda wetu tu” Dk. Shein aliwahakikishia wananchi hao na kuwataka kuendelea maisha na kuwapuuza wanaoeneza uzushi huo.
Dk. Shein alieleza kuwa wapo baadhi ya watu wanaofika hata kukejeli aya za Mwenyezi Mungu na kubainisha kuwa serikali iliyopo ni ya wananchi kwa sababu ndio waliyoichagua.
“Serikali hii ni ya wananchi; waliyoichagua na wasioichagua; waliopiga kura na wasiopiga kura; wako wanayoitaka na wasiyoitaka wote hao wanafanya kwa hiari yao lakini mwisho wa yote kwa kuwa tayari imewekwa madarakani na wananchi wenyewe kupitia uchaguzi ulioendeshwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar hawana budi kuitii ” Dk. Shein alieleza.
Dk. Shein alibainisha kuwa ni tamaa tu za baadhi za wanasiasa waliowashawishi baadhi ya watu wasishiriki katika uchaguzi wa marudio ambao uliitishwa kwa mujibu wa Katiba lakini sasa baada ya kuona waliyoyatarajia hawakuyapa wanazubaisha wananchi kwa kupita mitaani na maneno yasiyo na msingi.
“Wanapita (baadhi ya wanasiasa) mitaani kueneza maneno ya kitoto – eti Dk. Shein hatafika Julai, mara hatafika Agosti -. Haya ni maneno ya kitoto na wananchi mnapaswa kuyapuuza” Dk. Shein aliwaeleza wananchi hao huku akisisitiza kuwa uchaguzi umekwisha sasa ni wakati wa kutekeleza Ilani ya CCM.
Akionesha kukerwa na uzushi huo, Dk. Shein aliwakumbusha wanasiasa wa aina hiyo kuwa anayetaka ushindi ni lazima ashiriki uchaguzi, achaguliwe na wananchi na atangazwe na Tume ya Uchaguzi vinginevyo kuzunguka nje ya nchi ni kupoteza muda wao tu.

“Wanaisingizia ICC, wanadanganya tu haina uwezo huo wa kuhoji uchaguzi wa Zanzibar ulioendeshwa kwa mujibu wa Katiba yake” Dk. Shein aliwaeleza wananchi hao na kusisitiza kuwa yeye na Serikali  yake anayoingoza wako kwa mujibu wa Katiba.
Dk. Shein aliyewasili kisiwani Pemba jana, hiyo jana alizungumza na wananchi wa mji wa Chake Chake wakati wa uzinduzi wa jengo la Mahkama Kuu na wananchi wa Kengeja wakati alipozindua dakhalia ya wasichana ya skuli ya sekondari ya ufundi Kengeja.
Leo amezungumza na wananchi wa Micheweni wakati wa kukagua ujenzi wa ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya hiyo na wananchi wa Gando wilaya ya Wete wakati alizindua madarasa ya skuli ya Chekechea ya Gando.

Tangu kumalizika uchaguzi wa marudio uliofanyika mwezi Machi mwaka huu, kumekuwepo na uvumi unaoeneza na baadhi ya viongozi wa upinzani kuwa kutafanyika mabadiliko ya uongozi kwa masaada wa mataifa ya nje.
Dk. Shein yupo kisiwani Pemba kwa ziara ya siku tano kukagua shughuli za maendeleo ambapo kesho anatarajiwa kukagua ujenzi wa barabara kadhaa zinazoendelea kujengwa katika mkoa wa Kusini Pemba.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s