“Uandishi kweli una mizungu yake…”

Mwandishi na Mhadhiri mkongwe wa Kiswahili - Ali Attas. Picha: Hisani ya BBC
Mwandishi na Mhadhiri mkongwe wa Kiswahili – Ali Attas. Picha: Hisani ya BBC

NOV 03, 2016  

KUNA lulu ya Waswahili iliyopotelea Japani kupindukia miaka 20 sasa.  Kwa hakika, lulu hiyo imepotea na haikupotea kwa sababu ukitaka kuiona unaweza kuiona, na hata kuishika, lakini sharti wende nje kidogo ya Yokohama, ufike Fujisawa, mji ulio kilomita 50 ushei kutoka Tokyo.

Fujisawa ni mji kama wa Malindi, Kenya, ila una tafauti kubwa. Haupo ufuoni bali kiasi cha maili mbili kutoka Enoshima, kisiwa kilichoungana na bara kwa barabara ya lami iliyojengwa juu ya bahari.

Fujisawa ni mji wa kihistoria. Wanadamu wamekuwa wakizaliana huko kwa miaka elfu kadhaa. Siku hizi viwanda vya kila aina vimeingia mjini humo, tangu vya kuundia magari, vya kufulia chuma, na vya kutengenezea zana za aina kwa aina. Kampuni ya Sony nayo imestakimu humo.

Lakini si viwanda vilivyoivutia lulu yetu.  Hiyo lulu yetu, fahari yetu imevutiwa na upepo wa bahari na mandhari ya karibu yanayoshabihi ilikotokea. Chimbuko la lulu hiyo, yenye jina liitwalo Ali Attas, ni Mombasa, Kenya, alikokulia.

Attas amekuwa akiishi Fujisawa kwa zaidi ya miaka 13.  Kabla ya hapo, aliishi miaka tisa jijini Tokyo. Akitaka kwenda Tokyo kutoka Fujisawa hupanda treni moja yenye mwendo wa dakika 40 hivi. Yokohama hadi Fujisawa ni mwendo wa dakika 20.

Attas amenambia kuwa tangu atue Tokyo, miaka zaidi ya 20 iliyopita, hadi leo nauli ya treni toka Yokohama hadi Tokyo imesalia ileile, dola mbili na nusu.

Ingawa mandhari ya Enoshima, karibu na kwake Fujisawa, yanamkumbusha alikokulia, hata hivyo amenambia kwamba kuna mengi ya nyumbani anayoyatamani.  Hayo ni pamoja na mbaazi za nazi na mahamri, samaki wa kupaka na muhogo wa nazi pamoja na burudani za baharini huko Bamburi na Diani.

Ali Attas si jina geni kwa mashabiki wengi wa redio za kimataifa na kwa wasomaji wa vitabu.

Aliwahi kufanya kazi BBC, London, kwa miaka kadhaa na halafu alikuwa mtangazaji wa Redio Japani (NHK). Mara kwa mara amekuwa akihojiwa na Sauti ya Ujerumani.

Nilijuana naye katika miaka ya 1970 kabla hajajiunga nasi London alipokuwa Nairobi akifanya kazi katika Shirika la Uchapishaji la Oxford University Press (OUP). Kabla ya hapo alikuwa mwandishi wa magazeti.

Kazi kubwa anayoifanya Attas siku hizi ni kuwafundisha Kiingereza na Kiswahili Wajapani, wakiwa pamoja na wanabalozi wanaopelekwa katika balozi zao Afrika ya Mashariki.  Sura yake si ngeni katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Japani kwani anasaidia sana kuyakuza mafungamano baina ya Japani na bara la Afrika. Pia ana jarida la mtandaoni, “afrikakiboko”.

Jumamosi iliyopita ilinikuta katika School of Oriental and African Studies (SOAS), Chuo Kikuu cha London, ambako kulikuwa na mkutano wa siku nzima kuhusu Kiswahili.

Mimi na mhadhiri wa lugha ya Kiswahili tulimzungumza pembeni mwanafunzi wake mmoja, binti wa Kijapani, aliyefundishwa Kiswahili awali na Attas.

Huyo mhadhiri alinambia kwamba yeye hamjui Attas lakini wanafunzi wake, huyu wa sasa na mwengine wa zamani, si tu kwamba ni mahodari wa Kiswahili lakini wana adabu na heshima kubwa. Kwa hivyo, alisema huyo mhadhiri, lazima na mwalimu wao naye ni mtu mwenye adabu.

Hakukosea kwani Ali Attas ni mtu mahashumu, mwenye adabu na hishma zake. Pia ni mchoraji wa haja na ni fundi wa uandishi. Ni mhunzi wa maneno. Huyachukua akayachonga na kuyapachika panapostahili.

Ametunga vitabu vinavyokaribia 20 vilivyokwishachapishwa na vilivyo mekoni.

Miongoni mwa vitabu hivyo ni vile vya kuwasomeshea wanafunzi lugha ya Kiswahili, kuna vya hadithi za watoto na kamusi zaidi ya moja.  Attas ni mmoja wa watunzi sita wa “Kamusi Elezi” lililochapishwa mwaka huu.

Hivi majuzi aliamua kupiga mbizi katika bahari nyingine — ya tamthilia.  Hii ni mara yake ya kwanza kuandika tamthilia na, kama kawaida yake, alichoandika kimeandikika.

Nimebahatika kwamba alipokuwa anaiandika tamthilia hiyo iitwayo “Mabandia” alikuwa akinitupia muswada wake kunidodesha.

Nasema akinidodesha kwa sababu hakunipa muswada mzima ila vipande vya muswada huo.

Katika tamthilia hiyo, itayochapishwa Januari 2017, mna mazungumzo ya vikaragosi na ya soga la barazani wakati wa mchezo wa karata wa “wahed wa sitini”.

Kutokana na vipande nilivyovisoma ningeielezea tamthilia ya “Mabandia” kuwa ni tashtiti au mzaha wa kisiasa (political satire) lakini mwenyewe amenieleza kwamba imepindukia tashtiti ya kisiasa.  Amenambia kuwa ubandia anaoupepeta na kuupekechua umo katika mazingira mengi ya maisha.

Amenieleza: “Labda usemi wa kimukhtasari ni huu: Maisha ni Karata!”

Kilichonichochea kuandika makala haya ni matamshi ya Tunduizi, mmoja wa wahusika katika tamthilia hiyo, alipokuwa barazani na wenzake wakicheza karata.

Tunduizi alisema: “Uandishi kweli una mizungu yake…”

Matamshi hayo yalinitwanga mara tu nilipoyasoma kama wiki mbili zilizopita na yamekataa kunitoka kichwani hadi sasa.  Kila nikikaa hunijia tena na tena na huwa sina budi ila kujiuliza iwapo baadhi ya waandishi wetu wanautambua ukweli huo.

Mimi ninaamini kwamba kila mtu ana haki na uhuru wa kuandika. Lakini ninawapinga wale wenye kufikiri kwamba kukaa mbele ya kompyuta, au kuchukua kalamu na karatasi,  na kuandika kunampa mtu haki ya kujiita “mwandishi”.

Uandishi una mizungu yake, chambilecho Tunduizi.  Ni tasnia au fani yenye miko yake ambayo mwandishi hapaswi kuivunja.  Una kanuni na miongozo yake ambayo mwandishi anatakiwa aifuate.

Kuna waandishi wa aina kwa aina; kuna wanaotokwa jasho wanapoandika. Kila makala wanayoyaandika kwao huwa kama ni kibarua.

Na kuna wanaoandika kwa raha bila ya sulubu.  Maneno hutiririka kutoka kwenye vidole vyao wanapogonga herufi za kompyuta au wanapoandika kwa kalamu, na mawazo yao pia hutiririka kutoka kichwani kupitia kwenye vidole hadi kufikia katika ukurasa.

Kuna uandishi wa kifasihi, sizungumzii riwaya bali huu huu uandishi wa habari isipokuwa hutumia nyenzo za kifasihi.

Uandishi aina hiyo unakuwa kama unamwekea msomaji kioo ayaone yote yale aliyoyaona mwandishi na ambayo mwandishi anayaandika kutokana na kumbukumbu zake.

Si kwamba mwandishi anayatia nakshi maandishi yake au anayatia nakshi aliyoyaona lakini huwa anaandika kama anachora taswira ya aliyoyaona.

Baadhi yetu tumejaa sauti tele vichwani mwetu zinazotuchagiza tuziachie huru kama ndege waliofungwa katika tundu. Hizo ni sauti za fikra zinazoutamani uhuru ili ziruke na kuwafikia wengine.  Haziwezi tena kuvumilia kufungwa na zimechoka kuwavumilia wenye kuzifunga.

Wakati mwingine huwa ni sauti za mazungumzo anayoyasikia mwandishi peke yake yakiwa yanakolea kichwani mwake.

Kuna wakati ambapo mazungumzo hayo huwa kama ya soga la barazani, la kuhadithia tukio au matukio au kumbukumbu au kuelezea historia.

Lengo ni kuyachukua ya jana na kuyafanya yawe na maana kwa leo. Kuyachukua ya kale na kuyafanya yalingane na ya leo au yawe ni funzo kwa yanayojiri leo, na pengine kesho.

Wakati wote lengo linakuwa kumuelimisha msomaji, kumpa taarifa mpya.  Msomaji hafaidiki anapokuwa mwandishi anayakariri yale ambayo ulimwengu umekwishayasoma kwenye magazeti mengine ya nchi za nje au uliyoyasikia na kuyaona kwenye vyombo vingine vya habari.

Ikiwa mwandishi hana budi kuzitumia habari chapwa kama hizo basi angalau azihusishe na matukio mingine.

Na kuna nyakati ambapo mwandishi anakuwa na mjadala yeye mwenyewe kwa wenyewe. Anakuwa unaupima ukweli; anaangalia ikiwa, kwa mfano, serikali imetenda haki katika kadhia fulani.

Kichwa cha mwandishi kinakuwa kama mezani ya kupimia dhana mbalimbali kama vile, kwa mfano, haki, utawala bora, uungwana wa viongozi au ufisadi wao.

Wengine tumejitolea kazi yetu iwe ni kufichua na kuzibua.  Kuyafichua yaliyofichika na kuyazibua yaliyozibika.

Kadhalika kuliondosha wingu la vumbi la uongo lililotanda juu ya siasa za nchi zetu.

Tuna wajibu wa kuonyesha kwa mifano iliyo dhahiri jinsi mambo yanavyoendelea kusalia kama yalivyo licha ya kwamba tunaambiwa ya kuwa kumefanyika mabadiliko au kwamba kumekuwako na mageuzi katika mfumo wa utawala. Inatupasa tueleze kwa vipi bado mambo ni yayo kwa yayo maji ya futi kwa nyayo.

Katika jamii hizi zetu za kileo watawala wetu wamebobea kutumia ala mbili kuu za kuwawezesha kuendelea kutawala. Silaha zenyewe ni uongo na hongo.

Watawala wetu siku hizi wana hulka ya kutapakaza uongo wakizidanganya nafsi zao, zetu na za walimwengu wengine, kwa jumla.

Huwa hawaoni haya kufanya ghilba na vitimbi vya kukirihisha madhali kufanya hivyo kutawahakikishia utawala endelevu. Ndipo wanapokuwa tayari hata kuwahonga waandishi.

Kuna makosa ya jinai katika uandishi. Mfano ni mwandishi kuiba yaliyokwishaandikwa na wengine na kujidai kuwa ni yake, hata kama ni kwa kuyatafsiri. Uungwana wa uandishi unamwajibisha mwandishi kumtaja aliyemdokolea maandishi au kupataja alipopadokoa.

Halafu kuna na lugha na namna ya kuisarifu  na kuichezea hiyo lugha.  Wenye kuisarifu lugha vizuri ndio wale wanaozifanya fikra zao ziwe kama zimeota mbawa; ziwe zinaonekana zinaruka huku na kule kwa madaha ya kushangaza na kumfanya msomaji apate ladha isiyoikata kiu yake anapoyasoma maandishi.

Hata kama hana jipya la kusema mwandishi aliyebobea, kwa matumizi tu ya maneno, anaweza ama kumstarehesha msomaji au kumchochea auangalie ulimwengu kwa jicho jipya.

Namna ya kuitumia lugha ni muhimu kwa sababu lugha inaweza kuwa chombo cha ugandamizi au chombo cha ukombozi, cha kuwafumbua macho wanaodhulumiwa.

Ndio maana lugha ni nguvu.  Mwenye kujua kuitumia huwa na nguvu za aina; huwa na uwezo wa ajabu.
Mwandishi mahiri hulipima kila neno analolitumia na hulitumia kama lina uzito unaostahiki. Kwanza hulilinganisha na maneno mingine katika kundi la maneno yenye maana moja au yanayofanana.

Hujiuliza, kwa mfano, inatosha kumuelezea mtawala kuwa mbaya tu? Ni mbaya ni muovu? Neno lipi lenye uzito zaidi ya jengine? Au ni afiriti ama ni firauni?

Anaweza pia akaamua kulichukua na kulitumia neno katika muktadha usiozoea kutumia neno hilo. Mfano,  katika “Mabandia” Ali Attas amemlisha mhusika Sungusungu maneno yafuatayo:

“demokrasia iliyouumuka”.

Kila mwandishi anawajibika kwa maandishi yake.  Anawajibika awe mkweli kwa anayoyaandika na awe na ujasiri wa kuyaandika anayoyaamini.

Kadhalika, anawajibika kumfanya msomaji ajifunze walau jambo moja katika makala yake kwani maisha huwa hayana maana iwapo mwanadamu anaishi tu, siku nenda siku rudi, bila ya kugundua  au kujifunzaa japo jambo moja jipya kila siku.


Baruapepe: ahmed@ahmedrajab.com

Chanzo: Raia Mwema

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s