Mapambio hayatasahaulisha haki Z’bar

mpiga-kura

KALAMU OKT17
NDANI ya wiki moja iliyotoka, Dk. Ali Mohamed Shein ameinuliwa kisiasa na kidiplomasia; ingawa ni “humuhumu” kwenye Jamhuri. Amepanda na kuhutubia majukwaa mawili yanayotofautiana hadhi.

Kwanza, alihutubia mkutano wa Bunge la Afrika Mashariki uliopelekwa Zanzibar kama sehemu mbadala wa Burundi ambako kuna hali mbaya ya usalama kutokana na mgogoro uliojengwa na kiongozi wao, Pierre Nkurunziza anayepigania kung’ang’ania madaraka.

Pili, Dk. Shein ameonekana akihutubia taifa tarehe 14 Oktoba mkoani Simiyu kulikokuwa na sherehe ya kilele cha mbio za mwenge.

Hatua hiyo ya kuonekana kwa upana daktari, inajenga picha kuwa anatambulika kuwa kiongozi mkuu hasa Zanzibar. Ninaamini haya haikuja hivihivi, isipokuwa ni matukio yaliyopangwa kwa makusudi ya kumpa hadhi ambayo kiukweli hao wanaompa, wanajua haimstahili.

Hiyo ni kwa Zanzibar, sehemu ya Jamhuri ya Muungano ambayo ina mamlaka yake kwa mambo mbalimbali kama katiba yake – Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 – inavyojieleza.

Lakini pia hatua hiyo imejenga picha ya kumtambulisha Dk. Shein kama msaidizi mkuu halali katika wasaidizi wawakubwa wa Rais John Magufuli kwenye jamhuri.

Hapo panapothibitisha kwa mara nyingine, msimamo wa rais wa jamhuri, kuhusiana na mgogoro wa kisiasa unaoikabili Zanzibar, lakini ambao kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni upuuzi mtupu kwa kuwa viongozi wake wanaona kila kitu ni sahihi, ni halali pasipo shaka yoyote, na kama wanavyosema, “uchaguzi ndio umekwisha tunasubiri wa 2020.”

Kwao, msimamo ni huo anaousimamia Rais Magufuli – Dk. Ali Mohamed Shein ndiye kiongozi wa Zanzibar, na hakuna wa kumuondoa mpaka utakapofika uchaguzi mwingine mwaka 2020.

Rais Magufuli, katika namna ya kubadilisha msimamo alioutoa awali baada ya uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba 2015 aliposema Zanzibar kuna tatizo la uchaguzi wake na atashirikiana na Makamu wake Samia Suluhu Hassan kutatua, ameamua kumhalalisha Dk. Shein, na anasimamia hilo kwa nguvu zote.

Dk. Shein aliipata ridhaa muhula wa kwanza Oktoba 2010, baada ya CCM na Chama cha Wananchi (CUF) kufikia muafaka wa kujenga siasa za maridhiano Zanzibar. Leo anaendelea kupingwa na Wazanzibari wengi na wanashikilia kudai haki ya maamuzi yao.

Haki yenyewe ni ya uamuzi wa kumchagua kwa kura halali Maalim Seif Shariff Hamad, kabla ya CCM kutumia mbinu kwa kinachoweza kuitwa kitaalamu “mapinduzi ya uamuzi wa wananchi” wakimlazimisha Jecha Salim Jecha, mkuu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), atangaze 28 Oktoba 2015, kuufuta uchaguzi licha ya kujua kisheria hana mamlaka ya kufanya hivyo.

Bali kwa upande mwingine, hatua hiyo ya kumuinua Dk. Shein majukwaani, inajenga picha kuwa kwa CCM, na muhimu zaidi, kwa utashi wa kiongozi wake, Dk. Magufuli, ndio kweli ameaminisha ulimwengu kwamba hakuna kitu kama kurudishwa kwa haki ya uamuzi Zanzibar.

Bunge la Afrika Mashariki ambalo vikao vyake hufanywa kwa utaratibu wa kupokezana nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, lingeweza kufanyika popote Tanganyika penye ukumbi stahiki. Tanzania ikaamua likutane Zanzibar.

Lakini, kiongozi gani afungue mkutano wa bunge hili. Tanzania ambayo kwa hakika ni mamlaka ya Rais Magufuli, ikamteua Dk. Shein, anayejulikana anapingwa na umma wa wananchi Unguja na Pemba kwa kuamini hawakumchagua.

Kama hiyo haikutosha, Serikali ya Muungano ambayo kwa hakika ni mamlaka ya Rais Magufuli, ikaamua Dk. Shein huyuhuyu akahutubie taifa katika kilele cha kuzima mwenge. Hatua nyingine inayoonesha ukorofi katika kutii misingi ya demokrasia na haki ya watu kuchagua kiongozi wanayemtaka.

Haya, baada ya kupewa jukwaa, Dk. Shein ameshahutubia majukwaa hayo mawili. Alichokifanya ndicho anachokiamini Rais Magufuli na wenzake katika CCM. Je, nikihoji ndio wanauhakika hicho pia kinaaminiwa na kuridhiwa na Wazanzibari wanaojua haki yao inahujumiwa?

Kwamba kwa kumuinua kwa staili hiyo ya kumpatia jukwaa kubwa zaidi hata nje ya Zanzibar, Dk. Shein ndio anajianika kwa watu na mataifa kwamba ndiye rais halali Zanzibar? Sitarajii nisubiriwe kujibu.

Uzuri ni kwamba kwa jicho langu la kitafiti, kadiri mamlaka inavyozidi kulazimisha Dk. Shein akubaliwe, ndivyo kwa namna ya kipekee, chuki dhidi yake zinavyokuzwa. Zipo chuki dhidi yake kwa sababu tu wananchi wanajua hawakumchagua kuwaongoza.

Wananchi wanabaki na imani hiyo hata wafanyweje. Wameshatumiwa vifaru na kuoneshwa silaha nzito kwenye magari ya deraya; wameshashuhudia gwaride la askari waliovalia kivita; wameshaona ndege za kivita zikirandaranda angani; wameshapata majumbani mwao ugeni wasiouridhia wa askari tofauti wa serikali.

Wananchi wa Zanzibar, kote Unguja na Pemba, wameshajionea wakisakamwa na askari wa halali kisheria na wahuni ambao wanapita mitaani wakiwa wamevaa soksi usoni na kubeba silaha yakiwemo marungu na mapande ya nondo.

Wazanzibari wameshakabiliana na misukosuko ya kunyang’anywa mifugo yao kwa sheria za kubuniwa ndani ya Mkoa wa Mjini Magharibi. Wameshalazimishwa kuhonga askari waliopachikwa jina la “mazombi” ambao hupita wakipora vitu kama chipsi-kuku ambavyo wananchi wanauza ili kupata riziki ya siku. Haya yameonekana hata kwenye masoko.

Wananchi wameshaishi maisha ya kulazimika kuhama kwenye maeneo ya biashara ndogo na kubwa zinazojenga uchumi wa familia zao na kusukumwa maeneo yasiyovutia wateja; na kubanwa hata anayeuza njugu (karanga) na machungwa aliyovuna kwenye michungwa yake miwili akate leseni isiyopungua Sh. 150,000.

Katika kadhia ya kudhibiti madaraka yasiyowastahili, CCM wameshawezesha watendaji kadhaa serikalini na katika taasisi zake, wanaoonekana kwa hisia tu kuwa si watiifu kwa mabwana CCM, kuandamwa na hatimaye kuhamishwa au baadhi yao kusimamishwa kazi kwa kutungiwa tuhuma.

Wala hawaandikiwi rasmi tuhuma, na hata hawapelekwi mahakamani.

Baadhi ya watendaji kwa ngazi ya makatibu wakuu na wakurugenzi, kwa kuwa tu walifanya kazi pamoja na aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif, wametelekezwa katika hali inayoonesha serikali inadharau utaalamu katika utumishi wa uuma. Baadhi hawajapangiwa kazi.

Hapa nisikitike kwamba mfumo huu wa kijahili unatumiwa kuua hata taasisi zenye mchango muhimu katika jukumu la serikali la kikatiba la kukuza sekta za kiuchumi kama msingi wa kusukuma mbele maendeleo ya nchi, kama vile benki.

Nagusia kilichofanywa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ).
Juma Amour, Mtendaji mkuu aliyeijenga benki na kuiokoa na hatari ya kufa kwa sababu ya kufisidiwa na wakubwa, mwishoni miaka ya 1990, ameondolewa kifedheha, na kuwekwa anayeitwa Juma Ameir, ambaye wajuzi walimtaja kama asiye na uzoefu wa kiwango kinachotakiwa nafasi hiyo.

Hali iliyopo Zanzibar ni ya mamlaka iliyojipa ridhaa kubomoa msingi wa nchi kuendeshwa kwa maridhiano ya umma. Inaongozwa kishetani. Kisa? CCM tu itawale. Hapana. Pamoja na kumpamba Dk. Shein, Wazanzibari hawatasahaulishwa haki yao. CCM wajue hawataizuia, sembuse kupata namna ya kuiua.

Chanzo: MwanaHalisi

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s