Mihangwa si wa kufanya utundu huu

Rais wa zamani wa Zanzibar, marehemu Aboud Jumbe Mwinyi
Rais wa zamani wa Zanzibar, marehemu Aboud Jumbe Mwinyi

Na. Ahmed Rajab

WAANDISHI wa habari tuna wajibu mkubwa. Tuna wajibu kwa jamii, tuna wajibu kwa ukweli na tuna wajibu kwa historia.Tusipokuwa makini tunaweza tukachochea mambo yanayoweza kuifanya historia isituonee huruma, ituhukumu kwa ukali.

Kuna tofauti kubwa mwandishi anapoeleza fikra zake au uchambuzi wake na ukaupinga kwa sababu hukubaliani nao na pale anapoandika jambo akalifanya ni la hakika ilhali ni la kuzua.

Joseph Mihangwa ni mwandishi aliyebobea kwa uchambuzi na kwa uandishi wenye kufichua mengi.  Unaweza ukaukubali uchambuzi wake au unaweza ukaupinga. Lakini vyovyote ufanyavyo huwezi kumnyima heshima yake ya uandishi.

Yeye si miongoni mwa wenye kutafsiri makala yaliyoandikwa katika magazeti ya nje na kuyachapisha katika magazeti ya Tanzania bila ya kutuongezea “faida”. Kwa sababu ya huo uzoefu wake nilishangaa nilipomsoma hivi karibuni (Raia Mwema, Septemba 22, 2016) akimtuhumu Bashir Kwaw-Swanzy kwamba alikuwa “wakala” wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA).

Kwaw-Swanzy (ambaye Mihangwa ameshika kumuandika “Swanzy”) alikuwa Mghana aliyewahi kuwa mwanasheria mkuu wa Kwame Nkrumah, Rais wa kwanza wa Ghana, na baadaye akawa mwanasheria mkuu wa Sheikh Aboud Jumbe, Rais wa pili wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na makamu wa Rais wa Tanzania.

Katika makala yake Mihangwa ameandika yafuatayo:

“Inafahamika, Swanzy alikuwa wakala wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) aliyetumiwa kuangusha Serikali ya mwanaharakati dhidi ya ukoloni mkongwe na ukoloni mamboleo, Rais Kwame Nkrumah wa Ghana mwaka 1966; na inadhaniwa alitaka kutumika kwa mgogoro wa Zanzibar kuvuruga harakati za ukombozi barani Afrika ambapo Tanzania ilikuwa Mwenyekiti wa harakati hizo.”

Mihangwa hapo amejaribu kujikinga kwa kutumia maneno mawili: “Inafahamika” na “inadhaniwa”. Lakini hata kwa kutumia kinga hizo ni wazi kwamba ama kalamu ilimteleza au akifanya utundu wa kusudi wa kumpaka tope Kwaw-Swanzy.

Aghalabu watu wakitajiwa kuwa “fulani ni jasusi wa Marekani” mara moja huiamini shutuma hiyo na wao huanza kuisambaza.

Nilipomsoma Mihangwa nilijiambia kuwa haiwezekani kwamba Kwaw-Swanzy alikuwa jasusi wa CIA. Mihangwa ametumia neno “wakala” likiwa tafsiri ya neno la Kiingereza “agent” ingawa Waswahili tunalitumia neno “wakala” katika shughuli za kibiashara.

Akichokusudia kusema ni kwamba Kwaw-Swanzy alikuwa jasusi wa CIA.

Swali linalozuka hapo ni kwamba kama kweli alikuwa jasusi wa waliosaidia kupindua kwa nini Kwaw-Swanzy naye alifungwa jela katika mazingira magumu na kwa muda mrefu baada ya majeshi ya Ghana kumpindua Nkrumah Februari 24, 1966?

Siku tatu kabla ya kupinduliwa, Nkrumah aliondoka Ghana kuelekea China na Vietnam katika jaribio la kutafuta amani ya Vietnam.  Hakuwa ametumwa na mtu, serikali wala taasisi yoyote ile.  Ilikuwa ni jukumu alilojitwika kwa hiari yake akijitolea kutafuta amani.

Siku hizo Vietnam ilikuwa imegawanyika sehemu mbili. Vietnam ya Kaskazini ilikuwa na utawala wa kikomunisti ukiongozwa na Ho Chi Minh. Vietnam ya Kusini ilikuwa kama mtoto wa kambo wa Marekani ikiongozwa wakati huo na waziri mkuu Nguyen Cao Ky.

Katika mkesha wa kuamkia Februari 24, siku Nkrumah alipopinduliwa, kulizuka mapigano makali Vietnam.  Mapigano hayo yanajulikana kama “Mapigano ya Suoi Bong Trang” na yalikuwa baina ya majeshi ya Marekani na ya Australia kwa upande mmoja.

Upande wa pili kulikuwa majeshi ya wapiganaji wakombozi wa Vietnam ya Kusini au Viet Cong, kama walivyokuwa wakiitwa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi. Wapiganaji wa Viet Cong wakisaidiwa na wanajeshi wa Vietnam ya Kaskazini.

Nkrumah aliarifiwa kuwa amepinduliwa mara tu ndege yake ilipotua Beijing akiwa safarini kuelekea Hanoi.  Wachina wakamchukua wakamficha, wakautengua ujumbe wake wa kuleta amani na halafu baada ya muda walimruhusu afunge safari ya kurudi Afrika kwa kupitia Moscow.

Wakati huo Rais Ahmed Sékou Touré wa Guinea alikwishatangaza kuwa Nkrumah, Rais wa Ghana, pia ni Rais mwenza wa Guinea.  Kwa hivyo, kutoka Moscow Nkrumah alikwenda Conakry, Guinea, ambako Sékou Touré alimuweka katika nyumba iliyoitwa Sylia Villa. Nkrumah alikuwa na wadhifa wa urais mwenza wa Guinea kwa muda mfupi.

Ingawa Nkrumah alipinduliwa na majeshi yaliyoongozwa na Emmanuel Kwasi Kotoka, hata hivyo haikuchukua muda ila ulimwengu ulijua ya kwamba waandalizi wa mapinduzi hayo walikuwa majasusi wa Kimarekani waliokuwa watumishi wa shirika lao la ujasusi la CIA.

Huenda palikuwa na mkono mwingine katika njama hiyo.  Nyaraka rasmi za shirika la ujasusi wa ndani ya nchi la Uingereza (MI5) zimeonyesha kwamba kulikuwako jasusi wa Kiingereza aliyejulikana kwa jina la “Swift” aliyejipenyeza na kukubalika katika duru za ndani za serikali ya Nkrumah.  Yumkini huyu naye alisaidia kuyafanya mapinduzi dhidi ya Nkrumah yafanikiwe.

Nkrumah alipopinduliwa, Kwaw-Swanzy, aliyekuwa waziri na mwanasheria wake mkuu, alitumbukizwa gerezani mjini Accra.  Aliselelea ndani humo kwa muda mrefu.

Huko jela alitokewa na miujiza.  Alioteshwa ndoto iliyomfanya asilimu na akapewa jina la Bashir akaliacha alililokuwa nalo la Edward. Safari moja tukiwa nyumbani kwake katika mtaa wa Golders Green, kaskazini mwa London, alinihadithia yaliyomkuta jela hata ikambidi abadili dini.

Kama nilivyoeleza katika sehemu ya tatu ya makala manne niliyoyaandika juu ya Jumbe (Raia Mwema, Septemba 1, 2016) nilimuomba Kwaw-Swanzy aandike makala kuhusu kadhia hiyo. Tuliyachapisha masimulizi hayo katikaAfrica Events, jarida ambalo nilikuwa mmoja wa wahariri wake.

Ingelikuwa Kwaw-Swanzy ni kibaraka wa Marekani au jasusi wa CIA sina shaka yoyote kwamba ningelizipata habari hizo siku hiyo niliyokwenda kumuona.  Mtu ambaye angeliniambia angekuwa marehemu Kofi Buenor Hadjor, aliyewahi kuwa msaidizi wa Nkrumah wa mambo ya habari na aliyeandika vitabu kadhaa kumhusu Nkrumah.

Kofi Hadjor akijua kwamba nilikuwa nakwenda kumuona Kwaw-Swanzy na baada ya kuonana naye nilimtajia kwamba nilishaonana naye.  Hakuwahi hata mara moja kunambia kwamba Kwaw-Swanzy alikuwa jasusi wa Marekani wala hakusema lolote baya la kumfanya mtu amtilie shaka Kwaw-Swanzy kuwa alikuwa jasusi. Na Kofi hakuwa na tabia ya kubania mambo.

Kofi na mimi tulitoka mbali.  Wakati mmoja tukifanya kazi idara moja ya shirika la Unesco la Umoja wa Mataifa na mkuu wetu wa kazi alikuwa mmoja, Alex Quarmyne, Mghana mwenzake.  Lakini Kofi alikuwa Dar es Salaam akiwa Mkurugenzi wa Chuo cha Uandishi Habari cha Tanzania (TSJ)  na mimi nilikuwa Nairobi nikisimamia miradi ya magazeti ya vijijini ya Kenya na redio jamii ya Homa Bay, magharibi mwa Kenya.

Niliporudi London baada ya kipindi cha miaka mitatu nilimkuta Kofi tayari ameshajijenga katika duru zangu. Alishawahi kuwa mhariri wa jarida la New African ambalo nikiliandikia mara baada ya mara na nilipoanzisha jarida la Africa Events, Kofi alikuwa akiendesha taasisi iliyokuwa ikiitwa Third World Centre na iliyokuwa katika jengo aliloliita Nkrumah House katika mtaa wa Old Street, katikati mwa London.

Siku hizo tukionana takriban kila siku kwa sababu jengo la Nkrumah House lilikuwa mwendo wa dakika kama tatu hivi kutoka Banner House, kulikokuwako Africa Events.

Siku Nkrumah alipopinduliwa ilikuwa siku ya maajabu mjini Accra.  Watu walimiminika barabarani wakiyashangilia mapinduzi kwa kuzivunja sanamu na picha za Nkrumah.

Kila kitu kilichokuwa na isimu yake kilibadilishwa jina, majengo, barabara, vyuo vikuu pamoja na ile Taasisi ya Itikadi iliyokuwa Winneba na iliyokuwa ikiwapa mafunzo ya kijeshi wapiganaji wakombozi kutoka nchi za kusini mwa Afrika.

Kwa ghafla moja jina la Nkrumah lilianza kunuka.  Hata wale waliokuwa rafiki zake nao pia haraka haraka walianza kuyasahau mema yake.  Baadhi yao walikuwa mawaziri wake, kwa mfano Alex Quaison-Sackey,  aliyekuwa waziri wa mambo ya nje na aliyekuwa pamoja na Nkrumah Beijing walipoarifiwa kwamba walikuwa wamepinduliwa.

Nkrumah ameandika kwenye kitabu chake “Dark Days in Ghana” (Siku za Giza katika Ghana) kwamba walipopinduliwa Quaison-Sackey aliingiwa na hofu kubwa na akaanza kuharisha, “aliingia msalani kama mara ishirini siku ile.”

Quaison-Sackey halafu alimlaghai Nkrumah.  Baada ya kushauriana naye alimwambia kwamba lazima ende kwa haraka kwenye mkutano wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) Addis Ababa kwenda kukikalia kiti cha Ghana.

Lakini badala ya kuitimiza ahadi hiyo alifululiza moja kwa moja kurudi Ghana. Alipowasili uwanja wa ndege wa Accra alitangaza kwamba anayaunga mkono mapinduzi na akawaambia waandishi wa habari kuwa akiona raha “kuinusa hewa ya uhuru.”

Quaison-Sackey hakuwa waziri pekee aliyemsaliti Nkrumah baada ya mapinduzi. Mwengine alikuwa Kwaku Boateng, aliyekuwa waziri wa elimu ya juu.

Mtu mwingine aliyemgeuka Nkrumah alikuwa John Tettegah, aliyekuwa katibu mkuu wa Chama cha Wafanyakazi (TUC) na ambaye baadaye alikuwa balozi mjini Moscow wakati wa utawala wa Jerry Rawlings. Aliwahi pia kuwa balozi katika Nigeria na Zimbabwe.

Tettegah ni mtu aliyekuwa karibu sana na Nkrumah na alikuwa na siasa kali za mrengo wa kushoto.  Nilijuana naye nikiwa kijana kabisa, tena kwetu Zanzibar.

Alikuwa mmoja wa wageni waheshimiwa kutoka nchi za nje waliokuja kuhudhuria sherehe za mwanzo za May Day kufanywa Visiwani baada ya Mapinduzi ya 1964.  Mimi nilikuwa miongoni mwa vijana waliokuwa wakiwasaidia wageni hao.  Miaka kama 25 baadaye nikakutana naye tena London na tukaanza kuwasiliana.

Nkrumah alipopinduliwa Tettegah alikuwa miongoni mwa watu wake wa karibu waliokuwa wakimponda hadharani.  Kwa mfano, aliwaambia waandishi wa habari kwamba alikuwa “na furaha isiyo kifani kwa kupinduliwa kwa utawala wa mabavu wa Nkrumah.”

Katika miaka ya mwisho ya 1980 gazeti moja lililokuwa likichapishwa Paris liliandika kwamba Tettegah alifichuliwa na Warusi kwamba alikuwa akitumiwa na shirika la ujasusi la Marekani, CIA.

Katika orodha ya Waghana wanaoshutumiwa kumwendea kinyume Nkrumah au kutumiwa na CIA sikuwahi hata mara moja kuliona, au kulisikia likitajwa, jina la Kwaw-Swanzy.  Ndipo niliposhituka niliposoma kwenye makala ya Mihangwa kwamba Kwaw-Swanzy alikuwa jasusi wa CIA aliyetumika kuiangusha serikali ya Nkrumah.

Wiki iliyopita nilimpigia simu mwandishi mkongwe kutoka Ghana Cameron Duodo, aliyekuwa akiwajua Nkrumah na Kwaw-Swanzy. Nilipomtajia maneno aliyoyaandika Mihangwa alikasirika na kusema:  “Absolute nonsense” (Upumbavu mtupu). Amekanusha kabisa tuhuma hizo na amenambia hakuwahi kamwe kuzisikia.

Aliongeza kwamba Kwaw-Swanzy alitoka sehemu moja na Nkrumah lakini muhimu alikuwa akimuunga sana mkono.  Na, kama nilivyokwishataja, alifungwa baada ya Nkrumah kupinduliwa.

Kwa hivyo, ndiyo hayo.  Sijui alikuwa na madhumuni gani Mihangwa ya kumpaka tope Kwaw-Swanzy.

Nisitosheke. Nikamwandikia baruapepe Mghana mwengine, mwanaharakati Napoleon Abdulai, ambaye karibuni hivi alistaafu kazi Umoja wa Mataifa. Abdulai alikuwa akimjua sana Kwaw-Swanzy na nilimuuliza kama kweli alikuwa jasusi wa CIA au kibaraka wa Marekani. Jibu lake lilikuwa: “No, no, no. Not true” (Siyo, siyo, siyo. Si kweli”.

Baada ya muda mchache akaniletea baruapepe nyingine akinieleza kuwa Kwaw-Swanzy alimpatia nyaraka zake zote na hakuona chochote katika nyaraka hizo zilizomfanya amtilie shaka. Alimaliza kwa kuandika: “Akinipenda na akiipenda CPP” (yaani Convention People’s Party, chama cha Nkrumah), chama ambacho zamani Abdulai akikiunga mkono.

Nilijaribu kumpigia simu mwanawe Nkrumah anayeishi Cairo, Gorky Gamal Nkrumah.  Bahati haikuwa yangu, sikumpata.  Mjini Accra, bintiye Nkrumah, Samia, aliyerithi uongozi wa CPP, pia sikujaaliwa kumpata lakini watu kadhaa walio karibu naye au waliokuwa karibu na babake wamesema kwamba hawakupata kusikia kuwa Kwaw-Swanzy alikuwa jasusi wa Marekani.

Mwisho mwanaharakati mmoja wa CPP na msaidizi mkuu wa Samia Nkrumah aliweka tangazo maalum kwenye mtandao wa ndani wa chama chao (wenyewe wanauita “jukwaa”) akiuliza iwapo kuna aliyewahi kuzisikia hizo shutuma dhidi ya Kwaw-Swanzy.

Hadi leo Jumapili ninapoyahitimisha makala haya hakuna aliyesema kwamba shutuma hizo zina ukweli wala hakuna aliyesema kwamba alishawahi kuzisikia.

Kwa hivyo, nimeridhika kwamba shutuma hizo hazina msingi, zilikuwa za upotoshaji. Hapo ndipo linapozuka swali jingine: kwa nini? Kwa lengo gani?

Dhamira halisi ilikuwa kumpaka tope Kwaw-Swanzy au kumpaka tope Sheikh Aboud Jumbe? Au ilikuwa kuzipaka tope jitihada za Jumbe zilizokuwa zikipigania papatikane Muungano wenye muundo wa serikali tatu?

Chanzo: Raia Mwema

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s