SMZ yafanyia mabadiliko Sheria ya ZEC

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema imeamua kuifanyia mabadiliko Sheria Namba 9 ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) ikiwamo muundo wake na pamoja na utendaji wake wa kazi kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Hayo yalitangazwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Vuga Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja jana.

Waziri Aboud alisema mabadiliko hayo yametokana na kasoro zilizojitokeza katika sheria iliyopo, ndiyo maana serikali imeamua kubadilisha muundo wa upatikanaji wa viongozi wake pamoja na kuweka adhabu.

“Muswaada wa kufuta sheria namba 9 ya 1992 na kutunga sheria mpya ili kuweka mfumo bora zaidi wa usimamizi na utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar umeandaliwa tayari,” alisema Waziri Aboud akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wake, Joseph Meza.

Aidha, alisema sababu nyingine zilizosababisha kufanyika kwa mabadiliko ya sheria hiyo ni kuondoa mgongano uliopo baina ya Sheria ya Tume, Sheria ya Uchaguzi na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Alisema mpaka sasa hakuna mfumo wa kisheria unaoiwezesha Tume ya Uchaguzi kuunda kamati za ushauri kwa masuala ya uchaguzi pamoja na kutokuwapo mfumo wa kisheria wa uendeshaji wa Ofisi za Wilaya za Tume ya Uchaguzi Zanzibar.

Waziri Aboud alisema mabadiliko hayo ya Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar yatasaidia Zec kuijengea uwezo mkubwa katika utekelezaji wake wa majukumu na kufikia viwango vya ubora katika kusimamia majukumu yake.

Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Katiba na Sheria ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), Machano Othman Said, alisema wakati umefika kifungu cha 119 cha Katiba ya Zanzibar kifanyiwe marekebisho ili wajumbe wa Tume ya Uchaguzi wateuliwe na Rais bila ya kupitia vyama vya siasa Zanzibar.

Alisema hatua ya Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi kuteuliwa na Rais kupitia vyama vya siasa wamekuwa wakitetea maslahi ya vyama vyao badala ya kusimamia Sheria ya Uchaguzi Zanzibar.

Aidha, mabadiliko hayo ya Sheria ya Uchaguzi yanakuja huku Zec ikiwa na mgogoro mkubwa na Chama cha Wananchi (CUF) baada ya kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana kwa madai ya kufanyika udaganyifu kabla ya kutangazwa matokeo yake.

Hatua hiyo ilisababisha CUF kususia uchaguzi wa marudio na hivyo kukwama kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) baada ya vyama vingine vilivyoshiriki kushindwa kufikisha masharti ya kuingia katika serikali ya pamoja kwa kutopata asilimia 10 ya matokeo ya urais wa Zanzibar.

Chanzo: Nipashe

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s