MAHOJIANO MAALUMU: Jussa asema CUF iko ngangari

Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF, Ismail Jussa Ladhu
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF, Ismail Jussa Ladhu

WAKATI mgogoro baina ya Chama Cha Wananchi (CUF) na Prof. Ibrahim Lipumba kuhusiana na nafasi ya uenyekiti ukiendelea kunguruma, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa chama hicho, Ismail Jussa Ladhu, amesema chama hicho bado ni ‘ngangari’ na kamwe hakiwezi kupasuka

Uongozi wa CUF na Lipumba umeingia katika mvutano unaodaiwa kutishia uimara wa chama hicho, hasa kwa upande wa Bara. Lipumba aliyewahi kuandika barua ya kujiuzulu na kisha kujiweka kando muda mwanzoni mwa Agosti, mwaka jana, kutokana na kile alichoeleza kuwa ni kutounga mkono kupokewa kwa Edward Lowassa ndani ya kambi ya muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Pamoja na kutangaza kuachi ngazi, Lipumba alirejea kwa aina yake na kusisitiza kuwa ndiye mwenyekiti halali baada ya kughairi na kuandika barua ya kutengua uamuzi wake wa awali.

Lowassa aliyejiunga Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akitokea CCM, aligombea urais akiwakilisha pia Ukawa ambao pia huundwa na Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.

CUF ambayo ilishiriki uchaguzi mkuu bila Lipumba na kupata mafanikio makubwa zaidi ikiwamo kuwa na wabunge 10 wa upande wa Tanzania Bara kutoka wawili waliokuwa nao kabla, inasisitiza kuwa kwa mujibu wa katiba yao, Lipumba si mwenyekiti tena.

Mgogoro huo ulishika kasi zaidi baada ya CUF kutangaza kumvua uanachama Lipumba huku ikimtuhumu kuwa amebadilika sasa anakihujumu chama huku Msajili wa Vyama vya Siasa, Francis Mutungi, akitangaza kumtambua Lipumba kuwa ndiye mwenyekiti halali. Mvutano huo ndio uliobua hofu kwa badhi ya watu kuwa sasa, CUF inaelekea kugawanyika makundi mawili, yaani Bara na visiwani, Zanzibar.

Hata hivyo, akohojwia na Nipashe juzi, Jussa alisisitiza kuwa CUF haiwezi kugawanyika na kwamba kinachotokea ni jitihada kuwatoa kwenye “mstari”, kwa maana ya kusahau ajenda yao ya kupigania haki.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo maalumu na Jussa yaliyofanyika mjini Zanzibar juzi:

SWALI: Hivi sasa CUF haiko kwenye Serikali ya pamoja na CCM visiwani Zanzibar baada ya kususia uchaguzi wa marudio. Je, unadhani kufanya hivyo kumeiinua CUF au kumeiyumbisha? Kwani hamna mjumbe hata mmoja ndani ya Baraza la Wawakilishi.

JUSSA: Ni muhimu kwanza tuelewe msingi wa kuwapo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar. Na mimi nilikuwa mmoja wa waasisi wa suala hili. Hatukukubaliana kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kuiingiza katika katiba kwa madhumuni ya kwamba mmoja atatawala kwa mabavu na kila siku kupora ushindi wa mwenzake halafu amwalike yule aliyempora katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Kufanya hivyo tutakuwa tunaitukana demokrasia na kuifanya haina maana. Msingi wa Serikali yoyote halali katika dunia hii lazima utokane na ridhaa ya watu na katiba yetu ya Zanzibar inatambua hilo. Ibara ya tisa inasema mamlaka ya nchi ni ya wananchi na serikali na vyombo vyake vyote vitapata uhalali wake kutokana na wananchi.

Kwa msingi huo, ni kwamba kusema kuwa CUF kutokuwamo katika Serikali kumeiinua au kuiyumbisha lazima tutambue kuwa lengo la CUF lilikuwa kuwapa nafasi wananchi wa Zanzibar kuchagua serikali wanayoitaka ni pamoja na kuwapo kwa GNU (Serikali ya Umoja wa Kitaifa).

Lakini tulipaswa kuwapa nafasi nani wa kuiongoza serikali ya GNU, chama kinachotoa rais ndicho kinachoamua sera gani ziongoze serikali hiyo kwa kiasi kikubwa.

Kwa hiyo wananchi wanapochagua chama hawachagui mtu kwa sababu ya kumpenda. Wanachagua sera anazoziwakilisha. Sasa CUF kukubali tu kwamba kila miaka mitano iende katika uchaguzi ishinde halafu iporwe ushindi nayo ikubali kwa sababu imepewa nafasi katika Serikali hayakuwa malengo.

Hiyo itakuwa kuwadhulumu na kuwasaliti wananchi wa Zanzibar ambao ndio wenye mamlaka ya kuchagua sera gani ziwaongoze.

Kwa hiyo mimi ukiniuliza nasema inawezekana kwa mtazamo wa maslahi binafsi kwamba kuna watu wamepoteza nafasi.

Lakini kwa maslahi ya nchi na wananchi, msimamo waliouchukua CUF umekuwa na manufaa katika kuifanya dunia ifahamu kuwa kinachoendelea Zanzibar hakikubaliki na kuna haja ya kufanya marekebisho ya msingi ili uamuzi wa watu uheshimiwe.

Hilo nadhani tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana maana wananchi hadi leo ari yao imekuwa kubwa zaidi kuliko ilivyokuwa hata kabla ya uchaguzi wa mwaka 2015.

Na tumeona katika uchaguzi huo wananchi wengi wameiunga mkono CUF na hilo lilijidhihirisha katika matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25, 2015. Haijawahi kutokea katika visiwa vya Zanzibar kwa chama kimoja kushinda kwa zaidi ya kura ishirini na tano elfu. Na tulimshinda Dk. Ali Mohamed Shein kwa kura zaidi ya ishirini na tano elfu.

Katika viti vya uwakilishi, CUF imeongeza na kila uchaguzi imekuwa ikiongeza viti. Hilo wananchi na dunia wanalitambua. Hiyo imezidi kutuongezea nguvu na ari ya watu kupambana wakiamini kwamba hatimaye haki itashinda.

Hata suala la diplomasia na jumuiya ya kimataifa, CUF imejenga heshima kubwa zaidi na imekubalika zaidi, hasa ilipoonekana imeshinda lakini ikaamua kuwatuliza watu wake ili nchi ibaki katika hali ya amani na utulivu na ikatafuta njia za kidiplomasia na kistaarabu katika kupigania haki yake na uelewa na maarifa ya kisiasa kwa wananchi wa Zanzibar yameongezeka zaidi hivi sasa kuliko ilivyokuwa mwanzo.

Kwa hivyo, nadhani kuwa CUF imejenga heshima kubwa na imeonyesha kwa wananchi na jumuiya za kimataifa kuwa hatupo kwa ajili ya vyeo.

Ingekuwa tupo kwa ajili ya ubinafsi na vyeo basi tungeweza kuridhia, tungeingia katika uchaguzi wa marudio na Maalim Seif angeendelea kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na baadhi yetu tungeendelea kuwa wawakilishi na mawaziri.

Lakini je, hayo ndiyo maslahi ya wananchi wa Zanzibar wanayoyataka? Kama tumeshindwa kufanya mabadiliko ya msingi katika kipindi cha miaka mitano ya GNU pia tusingeweza kufanya chochote sasa… tungeendelea kupata mishahara na hadhi sisi binafsi lakini wananchi wa Zanzibar wangeendelea kuathirika katika mfumo ambao GNU ingekuwa haiundwi kwa sababu ya maamuzi ya wananchi lakini kwa sababu ya kupora madaraka kwa CCM. Kwa hiyo sisi CUF hatukuyumba na tupo imara

SWALI: Kwa mwenendo wa sasa wa kisiasa Zanzibar, unadhani bado kuna uwezekano wa kufanyika kwa uchaguzi mwingine huru kabla ya 2020?

JUSSA: nadhani uwezekano huo upo kwa sababu Serikali inayoitwa halali wakati si halali ipo ipo tu. Ukitazama shughuli nyingi za kiuchumi zimeathirika.

Shughuli nyingi za kiserikali haziendi kutokana na ukosefu wa mapato. Jumuiya ya kimaitaifa imejitenga na Zanzibar na wafanyakazi serikalini wanasikitika, wanaikumbuka GNU. Kwa hiyo wananchi wengi wanasikitikia hali iliyopo sasa ambayo ni ya mivutano… haiwezi kuifanya nchi ikaendelea mbele na hata hao wanaojiita Serikali hawawezi kufanya shughuli zao.

Wananchi wamewagomea na kuwasusia. Kwa hiyo sidhani kwamba tutaweza kuendelea na jambo lolote.

Kwa sababu ya shinikizo kubwa ambalo lipo, nadhani kuna uwezekano juu ya utashi wa kisiasa utakuwapo kufanya uchaguzi huru na wa amani… na kutoa nafasi kwa wananchi kuchagua viongozi wanaowataka. Na matokeo ya uchaguzi huo yawe ndiyo msingi wa kuunda Serikali mpya ya Umoja wa Kitaifa ambayo ridhaa yake, uhalali wake na muundo wake unatokana na matakwa ya wananchi wa Zanzibar.

SWALI: Kugomea kwenu uchaguzi wa marudio kumewapa nafasi CCM kurejesha majimbo ya Pemba ambayo hawajawahi kushinda kwa kiwango cha sasa tangu kurejeshwa vyama vingi mwaka 1995. Je, hauoni uamuzi huo umewapa nafuu kubwa wapinzani wenu kiasi kwamba hamtaweza kukomboa tena majimbo hayo katika uhaguzi ujao?

JUSSA: Sioni hivyo na CCM yenyewe haiamini hivyo kwa sababu Pemba ni Pemba. Waswahili wana msemo kuwa Pemba peremba, ukija na joho utarudi na kilemba.

Wananchi wa Pemba wanajulikana kwa msimamo wao katika kile ambacho wanakiamini na hilo limedhihirika tokea mwaka 1995, wakati wa uchaguzi wa mwanzo hadi leo. Na CCM kupora majimbo Pemba si mara ya kwanza.

Uchaguzi wa mwaka 2000 walijitangazia kuwa wameshinda majimbo matatu lakini ulipokuja uchaguzi mdogo mwaka 2003 hawakupata jimbo. Kwa hiyo CCM hawajawahi kushinda uchaguzi wowote uliokuwa huru na wa haki kisiwani Pemba.

Naamini tukifanya uchaguzi wowote, leo hii majimbo yote yatarudi kwa CUF tena kwa kura nyingi. Hata Unguja CUF itapata majimbo mengi zaidi.

SWALI: Kuna mapendekezo kuwa CUF na CCM zirudi mezani ili kujadiliana juu ya hali ya Zanzibar ili kurejesha umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi… yaani Zanzibar kwanza, vyama vyenu baadaye. Je, hili unalizungumziaje?

JIBU: Hoja ya mazungumzo ya CUF siku zote imekuwa mstari wa mbele. Haijawahi kukataa hata siku moja mazungumzo kwa sababu tunaamini kuwa siasa inafanywa kwa mazungumzo, si kwa kutumia mabavu na vitisho… hayo yamepitwa na wakati katika dunia ya leo.

Pamoja na kuamini kuwa tumeshinda kihalali katika uchaguzi wa Oktoba, mwaka jana, bado CUF imenyoosha mkono na kutoa mapendekezo kupitia kiongozi wetu Maalim Seif, hasa akiwa katika ziara nchi za nje kutaka yafanyike mazungmzo yatakayowezesha kuundwa kwa Serikali ya Mpito na baadaye kukubaliana kufanyika uchaguzi mwingine.

Kwa hivyo, CUF ipo wazi kwa mazungumzo… wananchi wamekasirishwa na kitendo kilichofanyika kwa sababu hawakutarajia Zanzibar kurejeshwa ilikotoka. Hawaipi ushirikiano Serikali. Bila shaka pana haja ya mazungumzo lakini ili yafanyike panahitajika kwanza kutambua tatizo kwa pande zote mbili zinazohasimiana.

Pili kuwe na utashi wa kuona kuwa mazungumzo hayo yanaleta tija ndiyo maana CUF tunasema kwamba mazungumzo kati ya CCM na CUF tumeshafanya mengi hayaonekani kwamba yanachukuliwa kwa umakini. Kuna haja ya kuwa na mpatanishi ambaye atasimamia mazungumzo hayo na awe mtu anayeheshimika na mwenye uadalifu na atoke nje ya Tanzania au nje ya Afrika.

Zanzibar ni yetu sote. Kuendelea kuvutana hakuwanufaishi wananchi wetu lakini kunahitajika CCM nayo kuacha kiburi na kutambua kwamba haina hatimiliki ya kuongoza Zanzibar … na wenye hatimiliki ni wananchi wa Zanzibar.

Lakini kwa upande wa Bara, nao wanapaswa kutambua kuwa hali inayoendelea sasa haina maslahi hata katika Muungano. Muungano hauwezi kujengwa kwa kuidhoofisha Zanzibar. Tunapaswa tushirikiane ili Zanzibar iwe imara, yenye umoja na mshikamano.

SWALI: Hivi sasa chama chenu kinadaiwa kuwa katika tishio kubwa la mpasuko, hasa Bara kutokana na mgogoro unaoendelea na Prof. Lipumba anayesisitiza kuwa yeye ni mwenyekiti halali. Hili unalizungumziaje?

JIBU: Sioni kama tuna tishio kubwa la mpasuko. Haidhuru hawa wanaosimamia hili wanapenda ionekane hivyo na ndiyo picha inayojaribu kujengwa ili kuhakikisha hilo unalolisema… inaonekana kwamba fikira zetu za kisiasa zipo katika ukale wa kudhani kwamba kudhoofisha mpinzani wako ndiyo manufaa yako na nchi.

CUF ni taasisi muhimu sana katika nchi hii. Kwa hiyo mtu yeyote anayedhani kwamba anaidhoofisha CUF atanufaika anajidanganya. Lakini CUF haiwezi kutishiwa kwa matishio madogo madogo kama haya. Imeonekana wazi kwamba Msajili wa Vyama vya Siasa ametumika waziwazi kumpa uhalali mtu ambaye ameshafukuzwa katika chama.

Mkutano Mkuu wa Taifa umemkataa na kukubali kujiuzulu kwake. Baraza Kuu la Taifa limemsimamisha na hatimaye kumfukuza uanachama. Bado Msajili amemng’ang’ania na kumpa uhalali… na watu wengi wanaamini kuwa anatumiwa na CCM kutaka kuivuruga CUF…. CUF ina uimara wa katiba yake.

Tulipambana na njama kama hizi tokea mwaka 1994 … tulishapambana mara nyingi kwa njama kama hizi. Na tutapambana na njama hizi … na tutamshinda kama tulivyowashinda wengine kwa sababu kwetu sisi cha msingi ni katiba yetu na msingi wa kuanzishwa CUF si mtu. Wale wanaosema kwamba Lipumba kwanza chama baadaye watafute pa kumpeleka.

Kwetu sisi chama kwanza watu wengine wote baadaye. Na yaliyojitokeza tunaamini kwamba tutachukua hatua za kisheria na tutafuzu na hatimaye chama kitarudi katika uimara wake.

Na mgogoro huu haujakiathiri chama … na chama kimepata kutajwa sana kuliko wakati mwengine wowote na wataalamu wa mambo ya uenezi wanasema unapotajwa hata kwa nia ya kuchafuliwa lakini kwamba unasikika peke yake, watu wanataka kujua ni nani hawa CUF? Wana kitu gani? Kwa nini wanaandamwa kwa kiasi hiki? Kwa hiyo sisi suala hili limetusaidia kwa kiasi kikubwa na nadhani baada ya suala hili kumalizwa, itatoka CUF ikiwa imara zaidi na tena inayotambulika zaidi.

SWALI: Kuna madai kwamba licha ya mafanikio yenu katika uchaguzi mkuu uliopita kupitia Ukawa, upo uwezekano mkapotea kabisa Bara katika uchaguzi ujazo kwa sababu hakuna jitihada za kutosha kuimarisha chama chenu mikoa ya Bara. Hili nalo likoje?

JIBU: Sisi msimamo wetu uko palepale. CUF inautambua na kuheshimu Ukawa. Waliokuwa wanaupiga vita Ukawa ni vibaraka wa CCM … suala la kusema kuwa tunawezaje kuimarisha chama, niseme kwamba kama kuna mtu wa kulaumiwa na katika hili huwa nashangaa kusema kuwa Lipumba anataka kuimarisha chama… tokea mwaka 1999 alipochaguliwa mwenyekiti mpaka mwaka 2015 alipojiuzulu, kwa nini alishindwa kuimarisha chama na badala yake CUF kila uchaguzi ilikuwa asilimia (ya ushindi) inapungua badala ya kuongezeka?

Kupitia Ukawa tumeweza kupata viti 10 vya kuchaguliwa majimboni Bara na utakuta kura za CUF katika nafasi ya ubunge zimebakia pale pale… ndio maana hata katika mgawanyo wa ruzuku hatukuathirika. Lengo la mgogoro wa Lipumba ni kutuondosha katika msingi wa kuimarisha chama. Lakini tunawaambia hawatafanikiwa.

SWALI: Kuna madai kuwa kitendo chenu cha kuhangaishwa na mvutano uliopo na Lipumba kumewafanya kuimarisha chama chenu? Je, kuna ukweli gani kuhusiana na hilo?

JIBU: Kwa upande mmoja ni kweli na mimi naamini kuwa ndilo lengo la hao wanaotumiwa. Suala kubwa ni la kupigania haki ya ushindi kwa Zanzibar na limeshughulisha mno watawala hasa baada ya jumuiya za kimataifa kusimamia kidete kutaka suala la Zanzibar kuchukuliwa hatua, Kwa upande mwingine ni kweli kama si suala la Lipumba tungekuwapo katika wilaya mbalimbali tukifanya shughuli za kuimarisha chama. Lakini wasidhani kwamba wanaweza wakatuondosha katika kuimarisha chama. Tumejipanga vizuri na hatuna wasiwasi katika hilo.

SWALI: Hivi unajisikiaje kuona Lipumba, ambaye ni Mwenyekiti wenu aliyewaongoza vyema kwa zaidi ya miongo miwili, sasa mkikwaruzana naye kiasi cha kuumbuana hadharani? Kwa nini hamkutafuta mbinu sahihi ya kuzima msuguano huu mapema?

JIBU: Si kama nasikitika lakini kwa Watanzania, watakumbuka kwamba tunayajua mengi ya Lipumba. Pamoja na kututenda katika mambo mengi sana…mambo mengine mengi lakini yote tuliamua kunyamaza kimya. Pamoja na kuamua kujiuzulu, tukasema kuwa tutaendelea kuheshimu mchango wake katika kukijenga chama, tukawaomba wanachama wampe heshima hiyo na kwa muda mrefu hatukuyazungumza hayo kwa sababu tulitaka kuona tunaheshimiana.

Pamoja na hayo tunaona mwezetu hakuitaka heshima. Kwa sababu huwezi wewe ukajiuzulu, ukahamisha vitu vyako vyote ofisini, lakini baada ya miezi 10 ukarudi unasema unatengua uteuzi na kwa staili hii, kwa sababu kama alikuwa na nia njema angewafuata viongozi wa chama na kufuata utaratibu. Lakini ametaka kurudi kutumia mlango wa nyuma na kutumia mabavu.

SWALI: Kuna hofu kuwa kufikia 2020, mvuto wa Maalim Seif visiwani Zanzibar utakuwa umepungua kutokana na sababu za kiumri. Unasemaje kuhusu hili?

JIBU: Kwanza suala la Maalim Seif na mvuto kila uchaguzi ukimalizika watu wanazungumzia kumalizika mvuto wake. Lakini kila uchaguzi unapokuja mvuto wake unaongezeka ndiyo maana anapata kura nyingi na kama umri ni kigezo. Dk. Shein ni mdogo kwa Maalim Seif kwa miaka mitano kwa hivyo tungetegemea angepata kura nyingi zaidi katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana amemshinda Dk. Shein kwa kura nyingi kwa hivyo umri si kigezo, haiba, mvuto,uzoefu, maarifa,uzoefu na sera anazozisimamia ndiyo zinazopimwa na wapiga kura.

Uchaguzi Zanzibar unaweza kufanyika muda wowote kabla ya mwaka 2020 na bado Maalim Seif ni hazina kwa CUF na pamoja na umri wake mkubwa vijana wengi wanaimani na yeye kwa sababu amejenga heshima kubwa,haiba,uaminifu na jina lake limekuwa likiheshimika ndani na nje ya nchi. Na hii si rahisi katika Afrika hii kupata kiongozi ambaye anaporwa ushindi wake kwa miaka mitano mfululizo na bado akatuliza watu kwa kutaka amani na usalama katika nchi yake.

Maalim Seif ataendelea kuitesa CCM kwa sababu hawajapata mtu yoyote ambae anafikia haiba, uwezo na mvuto alio naondiyo maana mara nyingi hata hizi ajenda za Maalim Seif kuwa apumzike zinatoka CCM zaidi na CUF wameridhika naye.

SWALI: Baada ya kushika nafasi mbalimbali ndani ya CUF, sasa una ndoto zipi za kisiasa ambazo bado unataka kuzitimiza?

JIBU: Ndoto zangu kuona CUF inashika madaraka kwa upande wa Zanzibar na kuona Ukawa kwa pamoja tunaiangusha CCM katika Mungano. Sina ndoto binafsi kwa sasa hivi.

Ndoto yangu kubwa kupitia CUF kufanya kila linalowezekana kuhakikisha Maalim Seif anashika hatamu kuiongoza Zanzibar. Tunamwamini yeye zaidi tukiamini kwamba ametushinda sote kwa haiba, uzoefu, maarifa na uzoefu.

SWALI: Tugusie uchumi kidogo. Ni mambo gani matatu muhimu ambayo unadhani yakifanyika Zanzibar itapiga hatua kwa kasi zaidi kiuchumi kuliko ilivyo sasa?

JIBU: Kwanza ni kuona kwamba tunaitangaza Zanzibar kuwa ni bandari huru kwa sababu hapa ilipo inaweza kuwa ni mlango wa kuingilia na kutokea katika Afrika Mashariki na Afrika kwa jumla.

La pili kuweka miundombinu ya kisasa kuongeza huduma za bandari na viwanja vya ndege. Tuweke kodi za chini kabisa ili kuvutia kiasi kikubwa cha bidhaa ambazo zinatumika Afrika Mashariki na Kati zipitie Zanzibar.

La tatu ambalo ni kubwa zaidi ni jinsi gani ya kubadilisha mitaala ya elimu ili kuzalisha wanafunzi wa daraja la juu zaidi na hatimaye kuifanya Zanzibar ijitegemee kiuchumi ili kupiga hatua za kimaendeleo.

Chanzo: Nipashe

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s