Maalim Seif azungumza na Wazanzibari Boston, makala kamili

Na Mwandishi wetu Boston 

Wapenzi wasomaji wetu, kwa muda wa siku kadhaa tulikuwa mfululizo wa makala za “Maalim Seif azungumza na Wazanzibari Boston”. Ifuatayo ni makala kamili kama kuna kipande kilikupita:

Maalim Seif akisalimiana na Wazanzibari.
CUF kuendelea kuigomea serikali ya Zanzibar
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad, ameisitiza kuwa Chama chake kitaendelea kuigomea Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Dkt Ali Mohammed Shein.

Maalim Seif alitoa sisitizo hilo hapo jana alipokuwa akizungumza na Wazanzibari waishio nchini Marekani kwenye mkutano uliofanyika katika jiji la Boston.
“Tutaendelea kuigomea Serikali, na wala hatushirikiani nayo kwa jambo lolote”, alisema Maalim Seif na kuongeza kuwa hatua hiyo tayari imeanza kuiathiri Serikali ya Zanzibar.
Maalim Seif aliwasili jijini Boston jana akitokea jijini Philadelphia ambako alihudhuria Mkutano Mkuu wa Chama Cha Democrats, uliomalizika Alkhamis iliyopita kwa kumpitisha rasmi Bi Hillary Clinton kuwa Mgombea Urais wa Marekani kwa tiketi ya Chama hicho. Uchaguzi Mkuu wa Marekani unatarajiwa kufanyika mapema mwezi Novemba mwaka huu.
Alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege, Maalim Seif anayefuatana na Msaidizi wake Bwana Issa Kheri Hussein, alilakiwa na halaiki ya Wazanzibari wakiongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazanzibari Bwana Sharif Idris pamoja na wanaharakati mbalimbali wa Demokrasia.
Akiwa Philladelphia, Mwanasiasa huyo mkongwe alipata nafasi ya kuhudhuria kwenye Kongamano la Kimataifa juu ya Uongozi Bora ambapo alipata nafasi ya kuonana na viongozi kutoka sehemu mbali mbali duniani wakiwemo Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya Bwana Raila Odinga, Rais Mstaafu wa Zambia Bwana Rupia Banda, Waziri Mkuu wa zamani wa Guinea Bwana Cellou Dalein Diallo, Waziri Mkuu wa Denmark Bwana Lars Løkke Rasmussen na wengineo.
Maalim Seif na ujumbe anaofuatana nao, anaondoka leo nchini Marekani kurejea Uingereza baada ya ziara iliyochukua muda wa wiki moja.
Maalim Seif, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) alikamilisha ziara yake hiyo tarehe 30 Julai kwa kuzungumza na Wazanzibari kwenye Mkutano wa hadhara uliofanyika katika jimbo la Massachusetts.
Mgeni huyo rasmi alikaribishwa kwa risala ya Jumuiya ya Wazanzibari waishio katika jiji la Boston kulikofanyika mkutano huo, Bwana Mohammed Lali, iliyoelezea imani yao juu ya uongozi wa Maalim Seif katika mapambano ya kupigania haki sawa na demokrasia Visiwani Zanzibar.
Akijibu risala hiyo, Mwanasiasa huyo alielezea shukrani zake za dhati kwa imani ya Wazanzibari juu uongozi wake na kuwahakikishia kuwa haki yao itapatikana.
Madhumuni ya Ziara zake.
Maalim Seif, aliyekuwa mgombea wa Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF katika uchaguzi Mkuu uliofanyika mwezi Oktoba mwaka jana, alielezea lengo la mizunguko yake hiyo kuwa ni kukutana na viongozi wa ngazi za juu wa nchi na taasisi alizozitembelea ili kuwapa picha halisi ya hali ya mambo ilivyo huko Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika nyanja za demokrasia na haki za binadamu kufuatia uchaguzi huo.
“Tumekuwa tukiwasiliana ili kuwapa ‘brief’ (maelezo) ya hali halisi ilivyo” aligogoteza Maalim.
Alisema kuwa nchi nyingi kwa kupitia Balozi zao zilikuwa zikitetea demokrasia, na wala siyo chama au kiongozi fulani.
“Nchi nyingi kwa kupitia Balozi zao zilikuwa zinatetea demokrasia, na wala siyo CUF wala Maalim Seif”, alisema gwiji huyo wa siasa, na kuongeza kuwa, “Msimamo huo ndio uliotusukuma kutembelea nchi hizi ili kuwapa ‘utandu na ukoko’, kwani kwa kufanya hivi tunapata nafasi ya kukutana na watunga sera wenyewe” Hii ni kutokana na kuwa Mabalozi wanafanya kazi kutokana na maagizo ya viongozi wa nchi zao, “na kama hamkujikaza swala hili linaweza kusahaulika”, alisistiza.
Migogoro ya Zanzibar.
Katika mkutano huo, mwanasiasa huyo mkongwe alielezea kwa mukhtasari juu ya historia ya migogoro visiwani Zanzibar kwa kusema kuwa migogoro visiwani humo ni tofauti na migogoro katika nchi nyengine ambako huwa inajikita katika misingi ya ukabila au udini. lakini swala la ukabila au udini haliko Zanzibar licha ya kuwa 97% ya watu wake ni Waislamu.
“Mgogoro zaidi ni wa kisiasa tangu zama hizo zinazoitwa za siasa”, alifafanua mweledi huyo, na kuongeza: “Baada ya kuanzishwa kwa vyama vya ASP, ZNP na ZPP, siasa iliwagawa Waznaibari na baadaye yakaja Mapinduzi ya mwaka 1964”
Mapinduzi hayo yalikomesha mfumo wa vyama vingi vya kisiasa, na kuendelea na Chama kimoja mpaka vyama vingi viliporukhusiwa tena mwaka 1992. Hata hivyo Chama tawala kiliukubali mfumo huo kwa vile ulikuja kutoakana na wimbi la mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi ulimwenguni.
“Baada ya kurejeshwa kwa shingo upande, waliukubali kwa shingo upande”, alisema Maalim Seif aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika Serikali ya Zanzibar, na kuongeza “Tulitukanwa na kufanyiwa mambo mengi hata kabla ya kuzaliwa kwa CUF”
Itakumbukwa kuwa Chama Cha Wananchi (CUF) kilitimiza masharti ya usajili wa muda mapema mara tu baada ya vyama vingi kurukhusiwa lakini kikapata wakati mgumu kupata uajili. “Chama chetu kilitimiza masharti mapema, lakini kupata usajili ikawa nongwa”, alisema Maalim na kusisitiza kuwa “Baadaye ikwa hawana budi kutupa usajili, na CUF ikapata usajili namabari mbili baada ya Chama Cha Mapinduzi – CCM”
Mara baada ya hapo zilifuata chuki na uhasama miongoni mwa wananchi badala ya kuwa kitu kimoja kama Wazanaibari. Chuki hizo na uhasama vikaendela na kufuatiwa na machafuka ya kisiasa kiasi kwamba kufikia mwaka 2001, kwa mara ya kwanza kabisa katika historia, Tanzania ikazalisha wakimbizi.
Itakumbukwa kwamba, wafuasi wa CUF walifanya maandamano mnamo mwezi wa Januari 2001, maandamano ambayo yalikabiliwa vikali na vyombo vya dola na kuplekea watu kadhaa kupoteza maisha na wengine kulazimika kuihama nchi na kukimbilia nchini Kenya na Somalia.
Maalim Seif, anayesifika kwa busara na hekima, aliendelea kueleza kuwa hali ya uhasama ikaendelea kuvigubika visiwa hivyo vya marashi ya karafuu mpaka mwaka 2009, ambapo alikutana na Rais wa Zanzibar wa wakati huo Dakta Amani Karume na kufikia maridhiano ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Alisema: “Hali iliendelea kuwa ya uhasama mpaka 2009 tulipokutana na Rais Karume na kufikia maridhiano yaliyoungwa mkono na Baraza la Wawakilishi na wanachi”
Itafaa kukumbusha kuwa tangu kufanyika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, Zanzibar ilikuwa ikikabiliwa na migogoro ya kisiasa iliyofuatiwa na mazungumzo ya upatanishi yakizishirikiahs pande mbalimbali za Kimataifa na kufikiwa miafaka tete ambayo ilivunjika mara tu baada ya chaguzi. Hata hivyo, Maalim Seif na Rais Amani Karume walikutana na kufikia maridhiano ya kizalendo ambayo hayakushirikisha upande wowote wa nje.
Maridhiano hayo yaliyotaka kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa yalipitishwa na wananchi katika kura ya maoni na kuidhinishwa rasmi na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.
Amani na utulivu
Katibu Mkuu wa Chama Cha wanancni (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad, aliendelea kwa kusema kuwa kufuatia maridhiano hayo, uhasama wa kisisasa na jazba zake vilitoweka, na watu wakawa wanaishi kwa amni na utulivu.Uchaguzi wa mwaka 2010 ukapita kwa salama na amani.
Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar iliyofanyiwa marekebisho kutokana na maridhiano hayo, ilikubaliwa kuwa Chama kitakachoshika nafasi ya kwanza katika uchaguzi kitatoa rais wa Zanzibar.
Makamo wa kwanza atatoka katika chama kitakachoshika nafasi ya pili, wakati ambapo makamo wa pili atatoka kwenye chama kilichoshika nafasi ya kwanza.
Aidha kwa mujibu wa Katiba hiyo Wajumbe wa Baraza la Mawaziri walitakiwa watoke kutoka vyama vilivyopata uwakilishi kwenye Baraza la Wawakilishi. “Baada ya uchaguzi tuliunda serikali ya Umoja wa Kitaifa kati ya CUF na CCM, huku CUF ikiwa na Mawaziri 7”, alisema Maalim Seif.
Uchaguzi wa 2015
Uchaguzi wa mwezi Oktoba 2015 ulikuwa wa kihistoria. katika chaguzi zilizotangulia, ushindi ulikuwa kwa tofauti ndogo ya kura. Lakini katika uchaguzi wa 2015, CUF ilipata ushindi wa kishindo: “Tulishinda kwa zaidi ya kura 25,000” alijigamba Maalim Seif.
Alitoa siri ya ushindi huo kuwa ni maandalizi mazuri na chama kuwa madhubuti katika kulinda kura zao: “Tulijidhatiti kulinda matokeo yetu”, alisisitiza.
Zoezi la kuhesabu kura lilienda vizuri mpaka tarehe 27 Oktoba ambapo zaidi ya 34% kwa upande wa uraisi zilikuwa zimeshahesabiwa, hapo mambo yakaanza kubadilika, na vituko kuanza. Kutokana na hali livyokuwa ikiendelea, Maalim Seif akaamua kuyaaanika hadharani matokeo ya uchaguzi kwa mujibu wa takwimu sahihi walizokuwa nazo.
Kwa upande mwengine, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Bwana Jecha Salim Jecha alitoweka na hatimaye kujitokeza kwenye vyombo vya khabari vya serikali akitangaza kufutwa kwa uchaguzi.
“Walimamua kumwamuru Mweyekiti wa Tume ya Uchaguzi afute matokeo ya uchaguzi”, alisema Maalim Seif. Kitendo hicho cha Mwenyekiti wa ZEC kilikwenda kinyume na Sheria na Katiba ya Zanzibar, kwani hakuna kipengele hata kimoja kinachompa mamlaka Mwenyekiti wa Tume kufuta uchaguzi.
“Hakuna kipengele hata kimoja cha sheria kinachoruhusu kufutwa kwa uchaguzi……., hakuna mtu au chombo chochote kinachoweza kufuta uchaguzi wa Zanzibar” Alisisitiza msomi huyo wa Sayansi ya Siasa. Aliendelea kusema kuwa kitendo hicho kiliingiza Zanzibar kwenye mgogoro wa kikatiba.
Baada ya kufutwa kwa uchaguzi.
Kufuatia kitendo cha kufutwa kwa uchaguzi kinyume na sheria, Maalim Seif aliyekuwa Makamo wa Kwanza wa rais alifanya juhudi za kuwasiliana na rais wa Zanzibar wa wakati huo Mheshimiwa Ali Mohammed Shein ili wakutane na kujadili juu ya namna ya kuitoa Zaiznbar kwenye mgogoro huo wa kikatiba.
Baada ya majaribio kadhaa, hatimaye Dkt Shein akakubali kukutana naye na kuanza msusuro wa vikao vya mazungumzo vilivyowashirikisha pia Makamo wa Pili wa rais wa wakati huo Balozi Ali Seif Iddi pamoja na marais wastaafu wa Zanzibar.
Wanasiasa hao waliendelea kujadiliana katika vikao vya faragha kwa wiki kadhaa huku ‘drip’ zikiwa zinamiminika mitaani mpaka wakafikisha jumla ya vikao nane bila mafanikio. Mazungumzo hayo yalivunjika baada ya Serikali kutangaza tarehe ya uchaguzi wa marudio bila maafikiano ya vikao hivyo ambavyo bado vilikuwa vinaendelea.
Mbali na utata wa hatua ya Mwenyekiti ya kuufuta uchaguzi kinyume na sheria, tofauti nyingine zilizojitokeza katika mazungumzo hayo zilikuwa ni kurejewa kwa uchaguzi na uhalali wa kufanya hivyo kisheria, Tume itakayosimamia uchaguzi huo wa marudio; iwe ni ilele ya Mheshimiwa Jecha aliyevuruga mambo, iundwe Tume mpya au uchaguzi usimamwe na Tume huru ya Kimataifa?
Licha ya kutofikiwa kwa makubaliano kwenye mazungumzo hayo, ‘serikali’ iliendelea na mpango wake wa kufanya uchaguzi wa marudio. Tunasema ‘serikali’ kwa vile kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar serikali iliyoingia madarakani kufuatia uchaguzi wa 2010, ilikuwa imeshamaliza muda wake, na haikuwa na mamlaka yoyote ya kisheria.
Hilo alilisistiza kiongozi mwadilifu Maalim Seif kwa kusema kuwa Mawaziri wa CUF wakati huo tayari walikuwa wameshajiondoa kama inavyotakiwa na Katiba ya Zanzibar. Maalim Seif alisisitiza kuwa kile kinachoitwa uchaguzi wa marudio hakikupata ridhaa ya wananchi, na vituo vya kupigia kura vilikuwa vitupu.
“Ni wapiga kura chini ya 15% tu ndio waliojitokeza kupiga kura, kinyume na 57% iliyotangazwa na serikali” alisema Maalim Seif na kusisitza: “Na kwa bahati walifedheheka, kwani Televisheni zilionesha vituo vya kupigia kura vikiwa vitupu”
Baada ya Uchaguzi wa Marudio
Kile kinachoitwa uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar, hakikupata uungwaji mkono tangu ndani hadi nje ya visiwa hivyo. Jamii ya Kimataifa ilikataa kushiriki katika uangalizi wa uchaguzi huo kwa vile haukuwa na mashiko yoyote ya Uhalali.
Na kwa upande wa ndani, Chama Kikuu cha upinzani Cha Wananchi (CUF) ambacho kiliususia uchaguzi huo hakikuitambua serikali mpya iliyoundwa na Mheshimiwa Ali Mohammed Shein, na kikaamua kuisusia kama kilivyoususia uchaguzi wenyewe.
Maalim Seif alisema kuwa wananchi wa Zanzibar wameigomea serkali hiyo na sasa iko taabani, na kusisitiza: “Na wala hatushirikiani nayo kwa jambo lolote lile”
Aliendelea kuelezea kuwa CUF walikaa kimya kwa muda, jambo ambalo liliwafanya viongozi wa chama Tawala cha CCM waamini kuwa wamemaliza Simba wa Nyika. “Tulikaa kimya kwa muda na wao wakadai CUF tumeimaliza……, mpaka tulipoanza ziara za Wilaya mbalimbali Unguja na Pemba zikifuatiwa na kuwatembelea wagonjwa…”
Ni vizuri kukumbusha kuwa Maalim Seif alianza ziara zake hizo kwa kuzitembelea wilaya za Pemba ambako alipokelewa na halaiki ya wananchi waliokuwa wakisema “raisi..raisi…raisi”. Kufuatia ziara hizo aliitwa Makao Makuu ya Polisi Zanzibar na kuhojiwa kwa muda wa masaa kadhaa.
Mgomo wa wananchi umeimarika, na umekuwa ukiitikisa serikali na kupelekea ukamataji ovyo wa wananchi kinyume na sheria: “Wameghumiwa, mgomo wa wananchi umeshika kasi…., wakaanza kukamata watu kinyume cha sheria” alisisitiza Maalim Seif.
Badala ya kushughulikia maendeleo ya nchi, serikali imejikita kwenye mikakati ya kuimaliza CUF na wafuasi wake. Hata hivyo, mikakati hiyo imekuwa ikiwaathiri wananchama wa CCM pia. Alitoa mfano wa sakata la kukamatwa ng’ombe na wenyewe kutakiwa kwenda kuwagomboa.
“Kila wanachofanya ni kuwamaliza CUF, lakini ukweli ni kwamba wenye ng’ombe wengi ni wanachama wa CCM”, alisema . Maalim Seif aliendelea kufafanua juu ya dhulma wanazofanyiwa raia na mali zao na kutoa mfano wa “jumba la treni”, kwa kusema “Watu walihamishwa, kwa ajili ya ukarabati wa jengo lile, na mpaka leo hata ramani haipo”
Itakumbukwa kuwa michoro ya kile kinachodaiwa kuwa ni ramani mpya ya mwonekano wa jengo hilo litakavyokuwa ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii, lakini kwa mujibu wa maelezo ya Maalim Sif, ilikuwa ni kiini macho tu.
Aidha Maalim Seif alifafanua kuwa Mji Mkongwe ni sehemu ya Turathi za Kimataifa. Kwa hivyo uvunjaji wa jengo lolote la kihistoria unapaswa kupata ridhaa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni. Hata hivyo, mpaka wakati tunaingia mitamboni hakuna karatasi yoyote inayoonesha kuwa tayari Serikali ya Zanzibar imewasiliana na kushauriana na shirika hilo. Kwa hivyo ni wazi kuwa uhamishwaji wa wanachi kutoka jengo la treni ulikuwa na malengo ya kisiasa na kuwadhalilisha wananchi.
Upande wa Tanzania.
Kwa vile Tanzania ni Jamhuri ya Muungano nchi mbili huru Tanganyika na Zanzibar, yanayotokea upande mmoja yanaathiri upande mwengine wa Muungano huo kwa njia moja au nyengine. Kwa hivyo, Makamo wa Rais Mstaafu wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, hakusahau kuigusia hali ilivyo nchini Tanzania chini ya Utawala wa Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli.
Maalim Seif aliilezea hali ilivyo nchini Tanzania kisiasa kuwa si yakuridhisha, na serikali iliyopo madarakani inaipelekea nchi pabaya.
Maalim Seif alikosoa hatua ya kuzuiliwa vikao vya Bunge kuonehswa moja kwa moja kwenye televisheni, na kusema lengo lake kuu ni kuua upinzani. Hii ni kutokana na kuwa Bunge lenye mijadala huru ndilo linalojenga upinzani.
Akakosoa hatua ya Wabunge 11 wa upinzani kuzuiliwa kushiriki katika vikao vya Bunge bila ya sababu yoyote ya kimsingi: “Nini kosa lao?, alihoji Maalima Seif, na kujibu mwenyewe kuwa: “Kosa lao kubwa ni kuikosoa Serikali”.
Alielezea masikitiko yake kuwa majimbo ambayo Wabunge wao wamezuiliwa yatakosa uwakilishi Bungeni kwa muda mrefu kwani wengine wamefungiwa mpaka mwezi wa Januari mwakani.
Akijibu swali iwapo kuna Mbunge yeyote wa CUF kati ya 11 waliofungiwa, Maalim Seif mwenye upeo wa kuona mbali alisema kuwa hakuna Mbunge yeyote kutoka chama hicho kati ya hao walioathirika na hatua hiyo na kusisitiza: “Nia ni kuugawa upinzani, ili waseme kuwa CUF ni wasaliti”
Alifafanua kauli hiyo kwa kusema kuwa kuna Wabunge wengi wa CUF ambao ni wasemaji wazuri na wakosoaji wakubwa wa Serikali, lakini hawakufungiwa ili watu wenye nyoyo dhaifu waone kuwa CUF ni wasaliti, au vibaraka.
Aidha, mwanasiasa huyo shupavu, aliifananisha hali ilivyo Bungeni na uwanja wa vita kutokana na kuwepo kwa askari wengi ambao mara kadhaa wamekuwa wakiingia ndani ya Bunge.”Ukienda Bungeni utadhani uwanja wa vita”, alisema.
Alitoa mfano wa nchi kama Uturuki ambako kumetokea mitafatuku Bungeni, lakini hakuna Polisi aliyeingia ndani ya Bunge. Halkadhalika Maalim Seif alielezea wasiwasi wake mkubwa juu ya matumizi mabaya ya Sheria ya Mtandao (Cyber Act) nchini Tanzania.
Aliendelea kwa kuelezea kutoridhishwa kwake na jinsi rais Magufuli anavyoingilia kazi za Mawaziri wake, akitoa mfano wa matamshi ya vitisho aliyoyatoa Mheshimiwa Magufuli dhidi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kukhusu tangazo lao la kutisha mikutano ya nchio nzima mnamo tarehe mosi Septemba. “Swali kama hilo umwachie Waziri wako wa Mambo ya Ndani kuingiulia”, alisema Maalim.
Kukhusu amri ya kuhamia Dodoma, Maalim Seif alisema kuwa hakuna umuhimu wowote wa kuhamia Dodoma kwa lazima, na kukosoa kauli za vitisho za rais Magufuli dhidi ya watendaji amabao hawataki kuhamia Dodoma waache kazi, na kuelezea khofu yake kuwa hakuna maandalizi ya kutosha.”Maandalizi gani yamefanywa?” Alihoji Maalim Seif.
Alielezea wasiwasi wake juu ya upatikanaji wa huduma muhimu katika mji wa Dodoma: “Sote Dodoma tunaijua…, kuna watu wana watoto wanakwenda shule, halafu uwaambie wahame kwa ghafla, rais anapohama ni lazima Mabalozi wamfuate, watakaa wapi Mabalozi?” alihji Maalim Seif.
“Kwa hiyo, hivyo ndivyo Tanzania inavyoendeshwa, ninaposema uvunjaji wa haki za binadamu, siyo Zanzibar tu, bali ni Tanzania kwa ujumla” alisema na kuonya kuwa Visiwani kukichafuka, Bara pia kutaathirika”
Akijibu swali kukhusu Masheikh wa UAMSHO walioko gerezani Tanzania Bara, Maalim Seif alijibu kwa kusema: “Hatukuona sababu yoyote ya kupelekwa Bara”, na kuendelea kuwa Mahakama ya Zanzibar ina mamlaka ya kisheria kuwahukumu watu wote wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali, bila kuwajibika kuwapeleka Bara.
Aliongeza kuwa: “Kama wana makosa, wangeshtakiwa Zanzibar”, akisistiza: “Huu ni udhaifu wa serikali iliyopo, kila lisemwalo na Bara, wao hewallah” Ni vizuri kukumbusha kuwa, Masheikh kadhaa wa Jumuiya ya UAMSHO kutoka Zanzibar walikamatwa na kupelekwa Bara bila kufunguliwa mashtaka katika Mahakama za Zanzibar, jambo ambalo lilizusha mjadala wa kisheria.
Masheikh hao wanatuhumiwa kwa makosa ya kile kinachoitwa ugaidi, na kwa muda wa miaka kadhaa sasa wako rumande na wamenyimwa dhamana kwa madai eti upepelezi bado unaendelea. Hata hivyo Wazanzibari wanaamini kuwa Waumini hao hawana hatia yoyote sipokuwa msimamo wao imara wa kutetea hadhi ya Zanzibar ndani ya Muungano wa Tanzania, khususan ikizingatiwa kuwa walikuwa msitari wa mbele katika kutetea mamlaka kamilii ya Zanzibar wakati wa mchakato wa Katiba mpya iliyofeli ya Tanzania.
Hitimisho
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, jana aliwasili Zanzibar akitokea Ughaibuni baada ya kukamilisha awamu ya pili ya ziara yake ya Mataifa mbalimbali Ulimwenguni.
Katika awamu hiyo ya pili, Maalim Seif alitembelea Marekani na kupata nafasi ya kuzungumza na Wazanzibari katika jimbo la Massachusetts. Ifuatayo ni sehemu ya mwisho ya mfululizo wa makala zetu za “Maalim Seif azungumza na Wazanzibari Boston”
Akiwa mwishoni mwishoni mwa hotuba yake, Mwanasiasa huyo Mkongwe alikariri msimamo wa CUF wa kutoitambua serikali ya Zanzibar iliyoko madarakani kwa vile haikupata ridhaa ya wananchi, akisisitiza kuwa serikali hiyo pia haitambuliki Kimataifa.
“Hatuitambui serikali ya Dakta Sheni, na hakuna taifa hata moja linaloitambua”, alisisitiza. Maalim Seif alielezea kwamba, wakati wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, wafanyazi wa serikali walikuwa wakipokea mishahara yao kwa wakati. Lakini matokeo ya serikali hiyo kugomewa na wanchi na kutengwa kimataifa, kumezidisha hali ya kiuchumi kuwa mbaya kiasi kwamba serikali inashindwa kuwalipa mishahara wafanyakazi wake kwa wakati.
“Tulifikia hatua nzuri, kiasi kwamba tarehe 22-23 watu walikuwa wameshapata mishahara yao. Sasa hali imezidi kuwa mbaya kiuchumi kiasi kwamba inafika mpaka tarehe 3 watu hawajalipwa”, alisisitiza.
Kama Wahenga walivyosema: “Baada ya dhiki faraja”, Maalim Seif naye aliwataka Wazanzibari kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha mpito, akiwahakikishia kuwa serikali iliyopo madarakani haitodumu.
“…. Wananchi wavumiliye, na mwisho serikali hii itaondoka madarakani”, alisihi, na kutamba: “Tutaendelea kufanya wajibu wetu na hatuchoki. Wala wasidhani kuwa tutarudi nyuma kwa kutukamata”.
Aidha alikariri wito wake kwa jamii ya Kimataifa wa kuendelea kuibana serikali akisema: “Tunaiomba Jamii ya Kimataifa waendelee kuibana serikali…….., na Inshallah itaondoka” alisema huku akijibiwa kwa akauli za “Amin”
Kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi. Kwa hivyo, kukhusu vitisho vilivyotolewa dhidi yake vya uwezekano wa kukamatwa, Maalim Seif aliyewahi kuwekwa gerezani kwa miaka kadhaa alisema kuwa kukamatwa kwake siyo mwisho wa harakati za Wazanzibari kudai haki yao, akisisitiza: “Kuna Maalim Seif zaidi ya mmoja”
Aliongeza kwa kuwaonya viongozi wa Zanzibar dhidi ya kuchukuwa khatua kama hiyo kwa kusema: “….Washukuru sasa hivi kuna mtu ambaye angalau anaweza kusema na watu wakamsikiliza….”
Kukhusu suluhisho la mzozo wa sasa wa kisiasa Visiwani Zanzibar, Maalim Seif alitoa rai ya kuundwa kwa serikali ya mpito itakayosimamiwa na watu wanaoheshimika na ambao hawaelemei upande wowote wa kisiasa. Jukumu kubwa la serikali hiyo ya mpito litakuwa kufanya marekebisho ya sheria za uchaguzi visiwani humo: “Khaswa khaswa Tume ya Uchaguzi”, aligogoteza.
Mahakama Ya Kimataifa:
Ni vizuri kukumbusha kuwa katika awamu yake hii ya pili ya ziara zake za Kimataifa, Maalim Seif na ujumbe aliofuatana nao walifika jijini The Hague, Uholanzi, na kufikisha malalamiko ya Wazanzibari.
Alipoulizwa iwapo khatua hiyo ina umuhimu wowote, khususan kwa vile viongozi wengi wa Kiafrika wamekuwa wakitoa wito wa kujitoa kwenye mkataba wa Kimataifa unaokhusiana na mahakama hiyo, Maalim Seif alisema: “Azimio lenyewe halikupita kwenye Mkutano wa Kilele wa Umoja Wa Afrika uliopita”
“Tumejidhatiti kikweli kweli kwa hili, kama wanadhani tunatania, wasubiri”, alisistiza na kuongeza: “Tumepata Wakili mahiri, na anasubiri tumpatie vielelezo zaidi tu…, kwa hivyo tuko ‘serious’ kwa hili”
Akijibu swali kukhusu kile kilichoandikwa na baadhi ya magazeti ya Tanzania kuwa Mahaka hiyo ya Uhalifu (ICC) imeitaka CUF kukanusha madai yake, msaidizi wa Maalim Seif aliyefuatana naye kwenye mkutano huo Bwana Issa Kheri Hussein, alitupilia mbali uzushi huo na kusema kuwa hiyo ni propaganda tu.
Aidha alisema kuwa hizo ni mbinu za kuitafuta CUF itoe maelezo kukhusu kile kinachoendelea The Hague kwa vile bado watu hawajui khaswa kinachoendelea na madai yaliyomo katika shauri hilo.
Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s