Waliopigwa risasi Zanzibar wasimulia kilichotokea

Mkadam Khamis

BAADHI ya wananchi na majeruhi waliopigwa risasi katika tukio la kukamata mifugo Zanzibar, wameelezea kilichotokea huku wakisema walikumbwa na mkasa huo wakiwa katika shughuli zao.

Mmoja kati ya majeruhi hao amesema alikutwa na masahibu hayo akiwa anapita njia huku mwingine akisema alikuwa katika kazi za ujenzi.

Tukio hilo lilitokea Alhamisi iliyopita, wakati vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) vikitekeleza amri ya serikali ya kuondoa mifugo inayozagaa maeneo ya mji. Wakati wa utekelezahji huo, wenye mifugo waligomea hivyo kulazimu askari kutumia risasi za moto.

Mtafaruku huo ulisababisha watu watano kujeruhiwa kwa risasi za moto, wakati askari hao walipotaka kuchukua ng’ombe katika eneo la Tomondo, wilaya ya Magharibi Unguja.

Wakisumilia tukio hilo, wananchi hao walisema askari vikosi vya SMZ wakiongozwa na wafanyakazi wa Baraza la Manispaa, walifika eneo hilo ambalo waliwakuta ng’ombe wakiwa wamefungwa katika malisho na kutaka kuwachukua.

Ali Bakari, mkazi wa eneo hilo alisema askari hao walipokuwa wakitaka kuwachukua ng’ombe hao, wananchi pamoja na wafugaji walikuwa wakiwazuia.

“Wakati mzozo ulipozidi, askari walianza kupiga risasi za moto kwa lengo la kuwatawanya wananchi ili waweze kuwachukuwa ng’ombe, lakini wananchi waligoma kuondoka ndipo zisasi hizo zikawajeruhi watu mbalimbali,” alisema Ali.

Alisema ukamataji wa mifugo haujazingatia maslahi ya wananchi kwa kuwa vikosi hivyo vimekuwa vikitekeleza agizo la Rais kinyume cha alivyosema.

“Nilimsikia Rais kupitia vyombo vya habari akipiga marufuku mifugo kuonekana katika wilaya ya Mjini tu, na hilo tumeliafiki kwa sababu ni kweli mifugo inakera katika maeneo ya mji,” alisema.

MAJERUHI WALONGA

Nao majeruhi, wakiwa katika wodi ya wagonjwa kwenye Hospitali ya Rufani ya Mnazi Mmoja, walisema kitendo cha askari hao kuwapiga risasi kimeaathiri sana.

Omar Khamis (23), ambaye amepigwa risasi katika mkono wake wa kushoto, alisema alifikishwa hospitalini hapo akiwa hana fahamu lakini baada ya kuzinduka alikuwa na maumivu makali.

Alisema alipatiwa matibabu na kutolewa risasi mbili katika mkono wake na sasa anauguza majeraha hayo.

Akizungumzia mkasa huo hadi kujeruhiwa kwa risasi, alisema akiwa katika shughuli zake za ujenzi, alisikia ghasia huku risasi zikiwa zinarindima na alipokuwa akikimbia ghafla risasi zilizokuwa zikipigwa, zilimpata katika mkono wake.

Khamis alisema kuwa ghasia hizo zilizuka baada ya askari hao kuzozana na wananchi na kwamba askari walikuwa wakitaka kuchukua ng’ombe wa wananchi huku wananchi wakipinga.

“Eneo lilipotokea vurugu halikuwa mbali na eneo nililokuwapo ambapo nilikuwa katika kazi zangu za ujenzi. Baada ya kuona risasi zinarindima, nilijaribu kujihami lakini nimejeruhiwa mimi ambaye sina hatia yoyote,” alisema.

Khamis alisema tukio hilo limemsababishia hasara kubwa kutokana na gharama za matibabu kumwelemea yeye na familia yake na shughuli zake za kiuchumi zikisimama.

Majeruhi wengine ambao walizungumza na Nipashe wakiwa katika hospitali hiyo ni Masoud Juma (15) aliyepigwa risasi katika paja la mguu wa kushoto na Salum Masoud (18) katika mkono wa kulia.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, walisema wameshapatiwa matibabu na kila moja alitolewa risasi moja na hali zao zinaendelea vizuri.

Walisema kabla ya kupigwa risasi hizo, walikuwa wakipita njia bila kufahamu chochote kuhusu malumbano yaliyokuwa yakiendelea kati ya askari hao na wananchi.

KAULI YA KAMANDA

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam, alisema jeshi hilo linaendelea kufanya uchunguzi kuhusiana na tukio hilo na kuthibitisha kuwa watu watano wamejeruhiwa kwa kupigwa risasi.

Alisema majeruhi wawili wamelazwa katika Hospitali ya Al-Rahma na watatu katika Hospitali ya Mnazi Mmoja na hali zao zinaendelea vizuri.

Mkadam alisema Jeshi la Polisi linawashikilia watu kadhaa wanaotuhumiwa kunyang’anyana mifugo na kusababisha watu watano kujeruhiwa kwa kupigwa risasi za moto na askari wa vikosi vya SMZ.

Alisema vijana hao waliowakamata ni zaidi ya 10 lakini bado wanaendelea kuwafanyia uchunguzi na kwamba miongoni mwa vijana hao ni wale waliolazwa hospitalini.

Kuhusu askari waliohusika kuwapiga risasi, alisema hawawezi kuwakamata kwa sababu walikuwa katika kazi, kikubwa ni kuwahoji juu ya matumizi ya silaha hizo.

MSIMAMO WA WAZIRI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Haji Omar Kheir, alisema utaratibu unaotumika katika ukamataji wa mifugo ni kufuata sheria ya mifugo ambayo inakataza mifugo kuonekana katika wilaya ya Mjini ili kurejesha nidhamu ya mji na katika hilo hatokuwa na muhali na mtu yoyote.

Alisema wanyama wanachafua mazingira na wanasabisha ajali, hivyo utaratibu huo unaotumika ni wa kisheria.

Waziri huyo alisema mji wa Zanzibar mipaka yake inajulikana na huko hawaruhusu kuonekana wanyama.

“Tokea kazi ya kamata kamata la wanyama, tayari tumeshakamata wanyama 106 kati ya hao kuna punda, mbuzi na ng’ombe na hadi hapa nazungumza walibaki wanyama 96 ambao wafugaji hawajaja kuwakomboa,” alisema Kheir.

“Utaratibu wetu tukimkamata mnyama, faini yake ni Sh. 300,000 kwa sababu tunakerwa na jambo hili. Misafara ya viongozi kadhaa imenusurika kupata ajali kutokana na wanyama.”

MWAKILISHI APINGA

Hata hivyo, mwakilishi wa Jimbo la Kijitoupele (CCM), Ali Suleiman Shihata alisema anaunga mkono agizo hilo la Rais la ukamataji wa mifugo katika Wilaya ya Mjini, lakini si kwa Wilaya ya Magharibi.

“Katika wilaya ya Mjini naliunga mkono kwa asilimia 100 kuwa wanyama wasionekane mjini kutokana na usalama wa wananchi, hasa wanaoendesha vyombo vya usafiri, lakini tafsiri yake imeeleweka tofauti. Mpaka Magharibi mifugo inakamatwa jambo ambalo si sahihi,” alisema.

Alisema katika wilaya ya Magharibi asilimia 90 ya wananchi wake shughuli zao ni za kilimo, uvuvi na ufugaji, hivyo wanapokatazwa kufuga ni kuwakandamiza na kuwaingiza kwenye umasikini.

Shihata alisema wananchi wengi wa wilaya ya Magharibi wamekopa fedha katika taasisi za fedha ili kuendeleza mifugo yao na kujikomboa na hali ngumu ya maisha, hivyo kuwakataza kufuga wakati ndiyo ajira yao wanayoitegemea ni sawa na kuwaonea.

Alipendekeza kuwa ufugaji wa wanyama ukawa huru kwa wilaya nyengine ukiachia wilaya ya Mjini Unguja na kudhibiti mifugo hiyo isiharibu mazao ya wakulima na uharibifu wa mazingira.

Chanzo: Nipashe

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s