Siku Kumi Za Mwisho Za Ramadhaan

laylatul_qadr

((عن عائشة رضي الله عنها أن النبي صلى الله عليه وسلم ” كان إذا دخل العشر أحيا الليل وأيقظ أهله وشد مئزره)) البخاري ومسلم   زاد مسلم وجَدَّ وشد مئزره .

((Bibi ‘Aaishah رضي الله عنها  amesema “Zilipokuwa zikiingia siku kumi za mwisho (za Ramadhwaan), Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akiuhuisha usiku kwa kufanya ibada, akiamsha ‘ailah (familia) yake usiku, na akikaza Izaar yake (shuka inayovaliwa kiunoni [makusudio hapa ni kuwa alikuwa akijibidiisha sana]) [Al-Bukhaariy na Muslim] Muslim akazidisha, akijitahidi na akikaza Izaar yake]

Hadiyth hii ni uthibitisho kuwa siku kumi za mwisho za Ramadhwaan zina fadhila khaswa na kubwa kuliko siku zozote nyingine ambazo Muislamu inampasa aongeze twa’aa na vitendo vya ibada kama kuswali, kufanya dhikr (kumkumbuka Allaah سبحانه وتعالى kwa Tasbiyh, Tahmiyd, Tahliyl, Takbiyr) na kusoma Qur-aan.

Bibi ‘Aaishah رضي الله عنها ametuelezea kuhusu Mtume wetu صلى الله عليه وآله وسلم kama mfano bora kabisa kwa sifa nne zifuatazo:

 1)     Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa “akiuhuisha (akikesha usiku) katika ibada”

         Ina maana kwamba, alikuwa halali usiku. Kwa hiyo yeye Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  alikuwa akikesha usiku mzima kufanya ibada na akiifufua nafsi yake kwa kutumia usiku wake kukaa macho na kuacha kulala. Hii ni kwa vile kulala usingizi ni mauti madogo. Maana ya “akihuisha (akikesha usiku)” ni kwamba yeye Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akitumia wakati huo katika hali ya Qiyaam (kusimama kuswali usiku) na kufanya vitendo vya ibada ambavyo vinafanywa kwa ajili ya Allaah سبحانه وتعالى  Mola wa Ulimwengu.  Inatupasa tukumbuke siku kumi za mwisho za Ramadhwaan ni chache zilizokadariwa kwa nambari.

Ama  kuhusu ilivyoripotiwa katika Hadiyth ya ‘Abdullaah ibn ‘Amr kwamba imekatazwa kukesha usiku mzima katika Swalah, hii inahusu mtu anayefanya hivyo kwa mfululizo wa siku zote za mwaka.

 2)     Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa “akiamsha ‘ailah (familia) yake”  

Ina maana kwamba ni wake zake صلى الله عليه وآله وسلم waliotwaharika, Mama wa Waumini, ili nao wanufaike katika ibada njema hizo za dhikr (kumkumbuka Allaah) na vitendo vyote vingine vya ibada katika siku hizo zenye baraka nyingi.

 3)     Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa “akifanya bidii”

Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akijizuia na akijitahidi sana katika ibada, akiongeza vitendo vyema zaidi kuliko alivyokuwa akifanya siku ishirini za mwanzo (wa Ramadhwaan). Akifanya hivi kwa sababu Laylatul-Qadr inatokea katika usiku mmoja wa siku hizo kumi.  

 4)     Mtume صلى الله عليه وآله وسلم “akikaza izaar (shuka) yake”

Alikuwa akijihimiza na kufanya bidii kubwa katika jitihada ya kufanya ibada nzito. Inasemekeana vile vile kuwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akijitenga na wake zake. Hii ni kauli iliyo sahihi zaidi kwa vile inakubaliana na ilivyotajwa kabla katika Hadiyth ya Anas رضي الله عنه “Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akikunja kitanda chake na akijitenga na wanawake (yaani wake zake)” [Tazama  Latwaaif-ul-Ma’aarif, Ukurasa  219]

Vile vile Mtume  صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akifanya I’tikaaf katika siku za mwisho za Ramadhwaan na watu wenye kuwa katika hali ya I’itikaaf hujizuia na jimai (tendo la ndoa) na wake zao.

Kwa hiyo enyi ndugu Waislamu, jitahidini kujizoesha na kuwa  katika sifa na khulka hizi. Na zingatieni Swalah za usiku (Tahajjud) pamoja na Imaam hata baada ya kuswali Taraawiyh (ambayo inaswaliwa katika nyakati za mwanzo za usiku) ili jitihada zenu katika siku hizi kumi za mwisho zipindukie siku ishirini za mwanzo na ili mpate kufaulu kupata sifa ya “kuuhuisha usiku kwa ibada” kwa kuswali. 

Na ni lazima muwe na subira katika twa’a ya Allaah سبحانه وتعالى  na ibada za usiku  kwani hakika Tahajjud (Swalah ya usiku) ni ngumu lakini thawabu zake ni kubwa sana. Naapa kwa Allaah, ni fursa kubwa katika maisha ya Muislamu na vile vile ni faida kubwa kuitumia fursa hii kwa yule aliyejaaliwa kupewa na Allaah سبحانه وتعالى (kuwa hai na uzima). Kwani binaadamu hawezi kujua kama ataweza kuchuma tena thawabu nyingi kama hizi, ambazo zitamfaa katika maisha yake ya dunia na ya Aakhirah. 

 Salafus-Swaalih (Wema waliotangulia) wa Ummah huu walikuwa wakijitahidi katika ibada za masiku haya kwa kuzirefusha Swalah za usiku. As-Swaa’ib bin Yaziyd amesema, “‘Umar bin Al-Khattwaab alimuamrisha Ubay bin Ka’ab na Tamiym Ad-Daariy kusimamisha (kuongoza) watu katika Swalah kwa Raka’ah kumi na moja. Imaam alikuwa akisoma ayah mia moja hadi ilibidi tuegemee mkongojo kwa sababu ya kisimamo kirefu, na tulikuwa hatupumziki hadi inapoanza kuingia Alfajiri”.  [Tazama Al-Muwattwa, Mjalada 1, Ukurasa 154]

‘Abdulllaah bin Abu Bakr amesema “Nimemsikia baba yangu (Abu Bakr) akisema, wakati wa Ramadhwaan, tulikuwa tukichelewa  kumaliza Swalah za usiku (hadi karibu na Alfajiri) hata tukiwahimiza watumishi kutuwekeasuhuur (daku) kwa kuogopa Alfajiri isitufikie”  [Muwattwa ya Imaam Maalik, Mjalada 1, Ukurasa 156]

Nafsi ya Muumini inapambana na jitihada mbili katika Ramadhwaan; Jitihada ya mchana kwa kufunga na jitihada ya usiku kwa Qiyaam (Swalah ya usiku). Kwa hiyo yeyote atakayejumuisha jitihada mbili hizi na akatimiza haki zake, basi yeye atakuwa miongoni mwa wenye subira kama Alivyosema Allaah سبحانه وتعالى

((إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُم بِغَيْرِ حِسَابٍ))

((Hakika wenye subira watapewa ujira wao bila ya hisabu)) [Az-Zumar: 10] 

Siku kumi hizi ni za mwisho katika mwezi mtukufu huu na vitendo vya Muislamu vinahesabika zaidi vile vya mwisho.  Kwani huenda akafaulu kukutana na usiku wa Laylatul-Qadr wakati akiwa amesimama katika Swalah ikawa ni fursa nzuri ya kufutiwa madhambi yake yote na Allaah سبحانه وتعالى. 

Ni wajibu wa kila mtu kuamsha, kushawishi, kuhimiza na kushurutisha ‘ailah (familia) yake kutenda vitendo vya ibada khaswa katika nyakati hizi tukufu, kwani hakuna atakayedharau kufanya hivi ila yule aliyenyimwa fadhila hizi.  Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba wakati wengine wako katika ibada khaswa za masiku haya kumi, wengine wanatumia wakati wao katika vikao vya maasi. Hakika hii ni khasara kubwa. Tunamuomba Allaahسبحانه وتعالى Atuhifadhi na Atuhidi. 

Kwa hiyo Muislamu atakayejishughulisha na kutenda vitendo vyema na ibada katika siku kumi hizi za mwisho atakuwa amejiingiza katika milango ya kuchuma mema yaliyobakia katika mwezi huu mtukufu. Ni khasara kwa mtu aliyeanza mwezi wa Ramadhwaan kwa kusimama kwa nguvu kuswali, kusoma Qur-aan na dhikr, kisha siku za mwisho akawa na ‘ajzi (akawa mzito na mvivu) katika kufanya ibada, wakati hizi siku za mwisho ndio siku zilizokuwa muhimu na zenye uzito wa thawabu ya kusimama kuswali na mengineyo kuliko zote. Hivyo kila mmoja inampasa aongeze bidii zaidi na kujitahidi kwa kadiri awezavyo kuongeza vitendo vyema na ibada katika kumalizia mwezi mtukufu huu. Na kukumbuka kuwa ‘amali za mtu zinahesabika zile za mwisho.

 DU’AA YA LAYLATUL-QADR

Katika siku hizi kumi za mwisho ni vizuri sana kuisoma Du’aa hii kila mara khaswa katika usiku wa Laylatul-Qadrkama ilivyothibiti katika Hadiyth ifuatayo:

(عن عائشة رضي الله عنها أنها قالت يا رسول الله أرأيت إن وافقت ليلة القدر ما أدعو قال تقولين اللهم إنك عفو تحب العفو فاعف عني)) ابن ماجه و صححه الألباني

((Kutoka kwa Bibi ‘Aishah رضي الله عنها kwamba alisema “Ewe Mtume صلى الله عليه وآله وسلم je, nitakaposimama usiku waLaylatul-Qadr niombe nini?” Akasema, “Sema Ee Allaah Hakika Wewe Ndiye Mwenye Kusamehe Unapenda Kusamehe basi Nisamehe”)) [Ibn Maajah na kaisahihisha Al-Albaaniy]

MATAMSHI YAKE

Allaahumma Innaka ‘Afuwwun Tuhibbul-‘Afwa Fa’afu ‘Anniy

Chanzo: Alhidaaya

Imeandikwa na: Dkt. Shaykh Swaalih Ibn Fawzaan Al-Fawzaan

 Na kufasiriwa na: Ummu Iyyaad 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s