Alama za dola ya kipolisi hazifichiki

IGP Ernest Mangu akimuelezea Balozi Seif Ali Idd mikakati ya Jeshi la Polisi katika ulinzi wa raia na mali zao
IGP Ernest Mangu akimuelezea Balozi Seif Ali Idd mikakati ya Jeshi la Polisi katika ulinzi wa raia na mali zao
Ahmed Rajab     Toleo la 462     15 Jun 2016

KUNA mambo kadhaa ya utawala wa Awamu ya Tano yenye kutia wasiwasi. Huu ni wasiwasi wa kwamba Tanzania inazidi kuwa na sura ya dola ya kipolisi. “Dola ya kipolisi” ni matamshi yanayoielezea serikali yenye kutumia mabavu katika uendeshaji wake.

Ninavyoandika makala haya nasikia kuwa Zitto Kabwe, kiongozi na mbunge wa ACT-Wazalendo, amekuwa akisakwa na polisi wikiendi iliyopita huku Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, akiwa ameshikiliwa na polisi siku ya Jumapili kwa muda wa saa mbili mjini Mwanza.

Hivi karibuni, Jeshi la Polisi la Tanzania lilipiga marufuku mikutano ya hadhara na maandamano ya vyama vya siasa. Polisi imesema iliyapiga marufuku maandamano hayo kwa sababu yanahatarisha usalama na amani ya taifa.

Ingawa hatua hizo zinaviathiri vyama vyote vya siasa ni wazi kwamba vilivyokusudiwa ni vile vya upinzani. Kuna tetesi kwamba amri hiyo ilitoka juu katika serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Baadaye polisi walitumika kuusambaratisha mkusanyiko wa wafuasi wa Chadema huko Kahama, mkoa wa Shinyanga. Polisi walidai kwamba hao wapinzani walikusanyika kujiandaa kuhudhuria mkutano wa hadhara wa Chadema licha ya kwamba mikutano aina hiyo imepigwa marufuku.

Imeripotiwa kwamba polisi walitumia nguvu na mabomu ya kutoa machozi hadi kwenye hospitali moja ya karibu na palipopangwa kufanywa mkutano bila ya kujali usalama wa wagonjwa. Huu ni uungwana? Na hii ndiyo iitwayo “Tanzania kisiwa cha amani”?

Wakithibitisha kwamba hawakuwa wakifanya utani kwa kupiga marufuku mikutano, polisi waliwafikisha mahakama ya Shinyanga wafuasi 22 wa Chadema kwa mashitaka ya kukusanyika kinyume na sheria.

Mfano mwingine ni pale kiongozi anapokuwa na uhuru wa kutumia neno lolote, kama vile “bwege”, “malofa” dhidi ya wapinzani au watawaliwa. Lakini neno lilelile likitumiwa na mtu mwenye kuukosoa utawala au mtawala basi humchongea asailiwe na polisi au hata ahukumiwe kifungo gerezani.

Hayo ndiyo yaliyomfika kijana mmoja, Isaac Ababuki, aliyehukumiwa na mahakama ya Arusha kifungo cha miaka mitatu gerezani pamoja na faini ya shilingi milioni tano za Tanzania. Baada ya wakili wake kulalamika na kukata rufaa Ababuki akapunguziwa adhabu kwa kuamriwa alipe faini ya shilingi milioni 3. Akishindwa kulipa itambidi atumike kifungo cha gerezani.

Alihukumiwa chini ya sheria ya mtandao kwa shtaka la kumtukana Rais John Magufuli katika ukurasa wake wa Facebook. Ababuki aliandika humo kwamba huwezi kumlinganisha Magufuli na Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa Awamu ya Kwanza, kwa sababu Magufuli ni “bwege”.

Wakati wa kampeni ya uchaguzi wa Oktoba mwaka jana, Balozi Seif Ali Idi, alimwita “bwege” hadharani Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Katibu Mkuu wa chama cha CUF. Hatukukisikia chombo chochote cha dola kikimchukulia hatua kwa kumkashifu kiongozi aliyemzidi cheo serikalini.

Aliyoyasema ni haya: “Tangu uchaguzi wa 1995 Seif amekuwa akilalamika kuwa anashinda lakini anapokonywa ushindi wake basi kila siku unapokonywa wewe tu? Basi bwege.”

Na ilisadifu kwamba hata katika uchaguzi huo wa 2015 alipokonywa ushindi, safari hii kwa uwazi kabisa hata ulimwengu mzima ukashtushwa, ukiwa pamoja na Muungano wa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika ya SADC, jumuiya ambazo zina uzoefu wa kuwalinda viongozi wa Kiafrika inapohusika na uchaguzi. Hata hizo nazo ziliupinga uamuzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kuufuta uchaguzi huo.

Hii inakuwa kama nchi inaishi katika ile mwandishi wa Kiingereza George Orwell aliloliita “Animal Farm” (“Shamba la Wanyama”). Katika riwaya yenye jina hilo, nguruwe wenye kuidhibiti serikali wanatangaza kwamba “wanyama wote ni sawa lakini baadhi (yao) wana usawa zaidi ya wengine”.

Itaendelea …

Chanzo: Raia Mwema

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s