Hotuba ya Zitto Kuzindua “Operesheni Okoa Demokrasia Nchini”

ZZ Kabwe

Ndugu Wananchi mnajua mara baada ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar kufutwa chama chetu kiliweka msimamo wa wazi kwamba kinatambua ushindi wa Maalim Seif Sharif Hamad kama Rais aliyechaguliwa na Wazanzibari na anayepaswa kula kiapo na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Tuliandika pia masuala 10 muhimu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuyafanyia kazi, na moja ya jambo tulilomtaka Rais Magufuli Kulifanyia kazi ni suala la demokrasia ya Zanzibar. Rais hakusikia wito wetu na aliruhusu ufutwaji usio halali, kisiasa wala kisheria wa uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 25, 2015.

Tunarudia kusisitiza kuwa Chama chetu cha ACT Wazalendo hakiutambui uchaguzi wa marudio wa Zanzibar uliofanyika mwezi Machi mwaka 2016 pamoja na matokeo yake yote. Kwa maana hiyo hatutambui Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Baraza la Mawaziri la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na Pia Rais wa Zanzibar.

Wananchi, Hivi karibuni kumekuwa na kuongezeka kwa sintofahamu huko Zanzibar kufuatia Mgombea Urais aliyeshinda na kunyanganywa ushindi wake kwenda kwa wananchi kuzungumza nao. Hali hii imepelekea jeshi la polisi kumhoji Maalim Seif na siku mbili baadaye Dkt. Shein kutamka kuwa hamwogopi Maalim Seif kwa sababu “Hana vifaru na mizinga”.

Tunalaani kauli hii ya Dkt. Shein ya kutisha kwa vifaru na mizinga. Kamwe huwezi kuzima haki za Wananchi kwa vifaru na mizinga. Dkt Shein akumbuke kuwa Sultan alikuwa na jeshi, vifaru na mizinga na ulinzi wa Dola kubwa kama Uingereza lakini aliangushwa na wananchi wa Zanzibar mwaka 1964.

Dkt Shein akumbuke kuwa nchi kadhaa duniani zilikuwa na madikteta wenye vifaru na mizinga lakini waliondoka. Dkt Shein afute kauli yake hii na kuacha vitisho badala yake aanze mchakato wa kupata maridhiano ya jamii ya Zanzibar. Hatutaki kurithi damu, tunataka kurithi nchi yenye amani, haki na demokrasia.

Wananchi, sisi ACT Wazalendo, tunajua hali mbaya ya kisiasa iliyopo Zanzibar na mkwamo uliopo hivi sasa Kisiasa, Kijamii na Kiuchumi. Hata hivyo ni lazima tupate jawabu kupitia sanduku la kura.

Tunapendekeza kuwa Vyama vikuu vya siasa Zanzibar vikubali ‘kufa kidogo’ yaani ‘to die a little’, kwa vyote kukubali kuwa Chaguzi zote Mbili, wa Mwaka 2015 na ule wa mwaka 2016 zilikuwa batili, zifutwe na Uchaguzi Mkuu mpya uitishwe.

Uchaguzi huo utanguliwe na Serikali ya Mpito itakayohusisha vyama vyote vya siasa na baadhi ya wanajamii wanaoheshimika na Wazanzibari wote ili kujenga kuaminiana. Tunadhani hii itatupa nusra kwa Zanzibar.

Tunawaomba Wazanzibari watumie mwezi mtukufu wa Ramadhani kutafakari maoni haya na wote kwa pamoja baada ya Ramadhani kuja na jawabu ya hali ya kisiasa.

Tunatamani Zanzibari irudi kwenye hali ya kawaida na ishamiri. Zanzibar ikiingia kwenye mtafuruku Tanzania nzima itakuwa kwenye mtafaruku. Ni dhahiri kuwa Rais Magufuli ameshindwa kutoa uongozi kwenye suala hili na hivyo ni wajibu wa Wazanzibari wenyewe kukaa na kupata mwafaka wa kijamii na kusonga mbele.

Zitto Ruyagwa Kabwe

Dar es Salaam

Juni 5, 2016

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s