Sheikh Karume angeyakubali haya?

 Abeid Amani Karume Rais wa kwanza wa Zanzibar
Abeid Amani Karume Rais wa kwanza wa Zanzibar
Ahmed Rajab       Toleo la 459       25 May 2016

UKITAKA unaweza ukamshambulia Sheikh Abeid Amani Karume kwa mengi. Lakini huwezi kumsema kwamba hakuwa mzalendo wa Kizanzibari. Kuna mambo yaliyopo sasa katika uhusiano wa Zanzibar na Serikali ya Muungano wa Tanzania ambayo Karume angeliyatafsiri kuwa ni ya kuidhalilisha na kuionea Zanzibar.

Karume ana umuhimu mkubwa katika historia ya Zanzibar kwa sababu alikuwa Rais wa mwanzo wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na mwasisi wa chama cha Afro-Shirazi Party (ASP), kimojawapo ya vyama viwili vikuu nchini humo wakati wa ukoloni. ASP iliundwa kwa kuunganishwa jumuiya mbili za kikabila, African Association (Jumuiya ya Wafrika) na Shirazi Association (Jumuiya ya Washirazi).

Chama cha pili kikubwa kilikuwa Zanzibar Nationalist Party (ZNP) au Hizbul Watan, kwa ufupi Hizbu, kilichokuwa chini ya uongozi wa Sheikh Ali Muhsin Barwani. Hiki ndicho chama kilichoshirikiana na chama kidogo cha Zanzibar and Pemba Peoples’ Party (ZPPP) kuunda serikali ya mwanzo baada ya visiwa vya Zanzibar kupewa uhuru na Uingereza, Desemba 10, 1963.

Hiyo ndiyo serikali ambayo siku 32 tu baadaye ilipinduliwa na wanaharakati wa ASP wakishirikiana na wafuasi wa Umma Party, chama kingine kidogo kilichokuwa kikiongozwa na Abdulrahman Babu.

Wanachama wa Umma Party na kiongozi wao walikuwa ni watu walioanzia katika ZNP, wakajiengua baada ya kuzuka tofauti za kiitikadi baina yao na wahafidhina wa ZNP.

ZPPP nacho kilichokuwa kikiongozwa na Sheikh Muhammed Shamte, ambaye baada ya uhuru alikuwa waziri mkuu, kilianzia ASP. Wafuasi wa chama hicho na kiongozi wao walijiengua kutoka ASP baada ya kuzuka mzozano mkubwa baina yao na Sheikh Karume.

Haina haja kwa maudhui niliyoyakusudia kuziingilia sababu au kuzichambua hoja zilizowafanya kina Shamte wajitoe kutoka ASP au kina Babu wajitoe kutoka Hizbu. Kufanya hivyo huenda kukatufanya tupotee njia.

Labda nianze tu kwa kusisitiza kwamba viongozi wote hao wanne niliowataja, Karume, Muhsin, Shamte na Babu, walikuwa wazalendo. Juu ya tafauti zao za kisiasa wote waliiweka mbele Zanzibar. Pumzi zao na nguvu zao walizilenga juu ya mustakbali wa Zanzibar na wote wakiitakia mema nchi yao. Wote wakitaka kuiona Zanzibar huru ikiendelea na kustawi.

Sasa tutawaweka kando kina Muhsin, Shamte na Babu. Tutaendelea na niliyemkusudia, yaani Karume kwa sababu kwanza, yeye ndiye aliyewashinda nguvu wenzake watatu kwa Mapinduzi ya Januari 12, 1964. Pili, ni yeye aliyeamua kuviunganisha visiwa vya Zanzibar na Tanganyika kwa ushawishi wa Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa Tanganyika.

Hatua hiyo ndiyo iliyoichongea Zanzibar ifike hapa ilipo, iwe nchi iliyopoteza mamlaka yake mengi. Miongoni mwa mambo unayoweza kumshambulia Karume ni uamuzi huo wa papara wa kuiunganisha nchi yake na Tanganyika bila ya ridhaa ya wananchi wenzake katika mazingira ya kutatanisha.

Tutakuwa tunaikana historia tusipokubali kwamba Karume alikuwa nalo wazo la kuiunganisha Zanzibar na Tanganyika hata kabla ya uhuru wa Zanzibar. Safari moja aliingia matatani kwa sababu katika kulizungumzia wazo hilo aliugusa ufalme wa Zanzibar kwa kuonyesha kama angependelea nchi iwe jamhuri. Ilimbidi aombe radhi kwa sultani wa siku hizo, Seyyid Khalifa bin Haroub, babu yake sultani aliyepinduliwa 1964, Seyyid Jamshid bin Abdallah bin Khalifa.

Baada ya Mapinduzi yaliyomwangusha sultani na kuifanya Zanzibar iwe jamhuri Karume alilifufua wazo la kuunganisha nchi yake na Tanganyika. Wakati huo alikuwa na sababu zaidi ya moja zilizomtia shime pawepo Muungano wa haraka na Tanganyika. Akiamini kwamba serikali ya nchi hiyo jirani itampa himaya asije kupinduliwa na mahasimu wake walio nje au ndani ya Zanzibar.

Nyerere naye kwa upande wake, ingawa alikuwa na sababu zake za kutaka nchi hizo mbili ziungane, alikuwa pia akihimizwa na madola ya Magharibi, hususan Marekani na Uingereza, afanye kila awezalo aiweke Zanzibar chini ya mbawa za Tanganyika.

Nyerere akafanya aliyoyafanya Muungano ukaundwa Aprili 1964. Waliokuwa naye Karume wakati huo wanasema kwamba hakuielewa vizuri azma ya Nyerere, kwamba yeye Karume akidhania ya kuwa nchi zao zinaungana ziwe katika mfumo wa shirikisho.

Naiwe iwavyo jambo moja ni wazi. Katika miaka yake ya mwanzo Muungano wa Tanzania ulikuwa muungano wa usawa. Ulikuwa ni muungano wa mataifa mawili yaliyokuwa na haki sawa.

Nyerere alikuwa Rais na Karume alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais pamoja na kuwa Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, lililokuwa chombo rasmi cha utungaji sheria. Siku hizo palikuwa hakuna Bunge wala Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Ingawa Baraza la Mapinduzi ndilo lililokuwa chombo cha kutunga sheria wakati mwingine alikuwa ni yeye mwenyewe Karume aliyekuwa akitunga sheria. Tamko lake lilikuwa sheria. Ukweli wa mambo ni kwamba akitawala wa mkono wa chuma.

Nyerere akimwogopa Karume. Yaliyomkuta Amir Jamal alipotumwa na Nyerere kwa Karume yanaeleza mengi.

Jamal, aliyekuwa waziri wa fedha wa Tanzania, alitumwa kwa minajili ya kumshawishi Karume akubali akiba ya sarafu za kigeni (forex reserves) za Zanzibar iingizwe katika Benki Kuu ya Tanzania. Siku hizo akiba ya Zanzibar ya fedha za kigeni ilikuwa ni kubwa kuipita ya Jamhuri ya Muungano.

Karume alimsikiliza Jamal akimweleza aliyoambiwa na Nyerere amweleze. Alipomaliza Karume alimkatalia kinagaubaga.

Ili kumwonyesha Jamal kwamba alikuwa hatanii Karume alimtukana, akamuadhiri kwa kumfokea na kumfurusha kutoka Ikulu ya Zanzibar. Jamal aliondokea patupu. Akafululuzia uwanja wa ndege kupanda ndege ya kumrudisha Dar es Salaam huku akiwa anatetemeka na kuhema. Alipofika Dar ghafla alipata mshtuko wa moyo.

Jamal hakuwa na bahati. Niliwahi kusikia kwamba kuna wakati mwingine Nyerere alimtuma kwa Hastings Kamuzu Banda, aliyekuwa Rais wa Malawi. Banda alipandwa na ghadhabu akamkaripia Jamal na aliporudi Dar Jamal alipata mshtuko mwingine wa moyo.

Nyerere hakuweza kumfanya kitu Karume baada ya kuelezwa na Jamal yaliyomkuta. Hakuwa na la kufanya ila kutafuna meno na kuungulika ndani kwa ndani.

Kumwogopa Karume ndiko kulikomfanya Nyerere amridhie kwa kila alichokitaka. Karume alipomtaka awakamate Bara akina Abdalla Kassim Hanga na Othman Shariff na awarejeshe kwao Zanzibar, Nyerere alimridhia. Alifanya hivyo ingawa lazima alikuwa akijua hatari iliyokuwa ikiwakabili mahasimu hao wawili wa Karume. Baadaye wote wawili waliuliwa Zanzibar.

Wakati wa uhai wake Karume ndiye aliyekuwa akiushika mpini katika Muungano. Muda wote huo Zanzibar ilikuwa na uungwana wake na haiba yake. Kweli Zanzibar chini ya utawala wake ilikuwa Zanzibar ya kikatili lakini ilikuwa na uhuru wake na haikuwa na wa kuiingilia. Ndio maana Karume aliweza kufanya aliyoyafanya bila ya Nyerere kuthubutu kumwingilia kati.

Karume alikuwa kiongozi wa kihistoria, aliyepangika awe na jukumu la kuwa mkombozi. Alipokuwa baharia wakati wa ujana wake alizitembelea nchi nyingi zilizoendelea. Akijua kwamba nchi hizo zimeendelea kwa ujuzi wa watu wao waliosoma. Naye alipokuwa hana budi akiwatumia wasomi lakini, kwa jumla, akiwadharau. Nyerere alikuwa msomi na alikuwa katika fungu la waliodharauliwa na Karume.

Alimdharau kwa usomi wake na wakati huohuo alimtumia Nyerere ili aweze kumlinda na kumpa kinga ya kumnusuru na maadui zake. Nyerere naye, kwa upande wake, alikuwa na ajenda yake kuhusu Zanzibar. Bahati mbaya kwa Zanzibar ajenda hiyo ilikuwa ajenda nzito.

Karume alikuwa mtu jabari, mtu wa ari. Na akiona mbali. Hakukubali hata siku moja yeye au nchi yake ichezewe au hadhi yake au ya nchi yake ishushwe.
Kuna ushahidi kwamba mwishoni mwa maisha yake alikuwa amechoka nao Muungano. Uhusiano wake na Nyerere uliharibika na ilifika hadi viongozi hao wawili wakinuniana na kupigana vijembe.

Nyerere hakuthubutu kumwingilia Karume. Hakuweza kumzuia asiendelee kuyafanya aliyokuwa akiyafanya Zanzibar. Wala hakuweza kumshurutisha azitii amri zake.

Kwa upande wake, Karume aliyakubali na aliyachukua aliyoyataka kutoka kwa Nyerere. Aliyokuwa hayataki, na yalikuwa mengi, alimwachia mwenyewe.
Karume hakulikubali hata Azimio la Arusha lililokuwa fahari ya Mwalimu na dira ya uongozi na sera za Tanzania. Karume alitangaza hadharani kwamba Azimio la Arusha mwisho wake ni Chumbe, kisiwa kilicho umbali wa kilomita kama sita kutoka Unguja na kilomita 30 kutoka mwambao wa Mrima.

Tangu Karume auliwe 1972 kuna mambo yamezuka katika uendeshaji wa Muungano ambayo lau angelikuwa hai, asingeyakubali hata kidogo. La msingi, angelipinga kuunganishwa kwa vyama vya Afro-Shirazi Party (ASP), kilichokuwa kikitawala Zanzibar, na Tanganyika African National Union (TANU), kilichokuwa kikitawala Tanganyika.

Karume alikuwa mtu wa hadhari aliyekuwa daima hadhiri. Kwa hivyo, angepewa shauri ya kukiua chama chake kwa kukiunganisha na TANU angeshuku kwamba hiyo ilikuwa njama ya kuudhoofisha udhibiti wake katika siasa za Zanzibar.

Ya Bara yalikuwa hayamshughulishi. Kwake Bara ilikuwa ni ngao tu ya kumlinda. Mapenzi yake yote na macho yake yote yalikuwa juu ya Zanzibar. Kwa vile mtizamo wake ulikuwa ni huo ni muhali kufikiria kwamba katika uhai wake pangezaliwa Chama cha Mapinduzi (CCM) au chengine kama hicho.

Sambamba na upinzani wake wa kuunganishwa vyama, Karume asingelikubali yaongezwe mambo zaidi katika ile orodha ya awali ya yale yaitwayo “mambo ya Muungano”. Angeng’amua tu kwamba kila mambo yanapozidi kuongezwa kwenye orodha hiyo ndipo Zanzibar inavyozidi kupoteza mamlaka yake ya kujitawala.

Karume angekuwepo hii leo asingelikubali apokonywe wadhifa wake wa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na akubali kupewa uwaziri usio na wizara maalum.

Angeona kuwa nchi yake inaonewa na yeye anadhalilishwa. Asingekubali mwenyewe adhalilishwe wala asingewaachia Wazanzibari wenzake wajidhalilishe.

Chanzo: Raia Mwema

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s