CAG abaini ufisadi wa bilioni 1.4/- Baraza la Wawakilishi Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akiwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu es Hesabu za Serikali Bi Fatma Mohamed Said
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akiwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu es Hesabu za Serikali Bi Fatma Mohamed Said

KASHFA nzito ya ufujaji wa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDF) imeibuliwa visiwani humu na miongoni mwa walioguswa ni Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi (BLW), wakiwamo waliokuwa Wawakilishi wa Chama cha Wananchi (CUF) visiwani hapa.

Kashfa hiyo imeibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar (CAG), Fatma Mohamed Said, katika ripoti yake ya mwaka wa fedha 2011 / 2015 katika matumizi ya CDF kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya CAG iliyowasilishwa katika Baraza la Wawakilishi mjini Zanzibar jana na Waziri wa Katiba, Sheria ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, imeeleza kuwa kati ya Sh. bilioni tatu, Sh. bilioni 1.4 zimetumika bila ya kuwa na vielelezo vya matumizi yake, jambo ambalo ni kinyume cha Sheria ya Fedha namba 12 ya mwaka 2005 pamoja na Sheria ya Mfuko huo namba nne ya mwaka 2012.

Majimbo ambayo yamezitumia kinyume cha sheria baada ya kuingiziwa fedha hizo na Hazina kupitia Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ni Kwahani (Sh. milioni 30), Rahaleo (Sh. milioni 30), Mji Mkongwe (Sh. milioni 10), Mpendae (Sh. milioni 30), Amani (Sh. milioni 30), Kikwajuni (Sh. milioni 30), Kwamtipura (Sh. milioni 30), Jang’ombe (Sh. milioni 30), Chumbuni (Sh. milioni 30), Magomeni (Sh. milioni 10) na Bububu (Sh. milioni 30).

Mengine ni Dimani (Sh. milioni 30), Fuoni (Sh. milioni 30), Kimbesamaki (Sh. milioni 10), Magogoni (Sh. milioni 30), Mwanakwerekwe (Sh. milioni 30), Mfenesini (Sh. milioni 30), Koani (Sh. milioni 30), Uzini (Sh. milioni 30), Chwaka (Sh. milioni 30), Muyuni (Sh. milioni 30), Muyuni (Sh. milioni 30), Makunduchi (Sh. milioni 30), Kitope (Sh. milioni 30), Bumbwini (Sh. milioni 10), Donge (Sh. milioni 30). Mkwajuni (Sh. milioni 30), Matemwe (Sh. milioni 30), Chaani (Sh. milioni 30), Nungwi (Sh. milioni 30) pamoja na Tumbatu (Sh. milioni 30).

Kisiwa cha Pemba, majimbo hayo ni Micheweni (Sh. milioni 30), Mgogoni (Sh. milioni 30), Konde (Sh. milioni 30), Tumbe (Sh. milioni 30), Chake Chake(Sh. milioni 30) Chonga (Sh. milioni 30) Wawi (Sh. milioni 30), Ziwani (Sh. milioni 30), Weye (Sh. milioni 30) Ole (Sh. milioni 30), Mtambwe (Sh. milioni 30), Kojani (Sh. milioni 30), Gando (Sh. milioni 30), Mkoani (Sh. milioni 10), Chambani (Sh. miliomi 30), Mkanyageni (Sh. milioni 30), Mtabile (Sh. milioni 30) pamoja na Kiwani (Sh. milioni 30).

Ripoti hiyo imeleeza kuwa fedha hizo walipewa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kufanikisha miradi ya maendeleo ya majimbo, lakini zimetumika bila ya kuonekana vielelezo vya matumizi yake wakati wa ukaguzi mwaka jana.

“Kufanya hivyo ni kwenda kinyume cha kifungu cha 26 cha Sheria Namba Nne, ya mwaka 2012 ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo pamoja na Sheria ya Fedha Namba 12 ya mwaka 2005,” alisema CAG katika ripoti yake yenye kurasa 182.

Aidha, alisema wamegundua mambo sita katika ukaguzi huo ikiwamo ukiukwaji wa sheria mbalimbali katika utekelezaji wa miradi ikiwa ni pamoja na Sheria ya Fedha namba 12 ya mwaka 2005, Sheria ya Manunuzi na Ugavi Namba tisa ya mwaka 2005 pamoja na Sheria ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo Namba nne ya mwaka 2012.

Aliyataja mambo mengine pamoja na kukosekana taarifa na kumbukumbu za vikao vya kamati za maendeleo ya Mfuko wa Jimbo, kukosekana vielelezo vya matumizi ya fedha katika utekelezaji wa miradi na kukosekana kwa kumbukumbu za hesabu yakiwamo madaftari ya kuhifadhi taarifa muhimu za upokeaji na utoaji na uhifadhi wa vifaa vya miradi ya maendeleo katika majimbo.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa matatizo ya kutokuelewana kwa Wajumbe wa Kamati za Maendeleo na Wenyeviti wa Kamati, kumeathiri utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika majimbo kupitia fedha hizo.

Hata hivyo, ripoti hiyo imeleeza kuwa tangu fedha hizo kuanza kutolewa, kila mjumbe amenufaika na Sh. milioni 60 ambazo zilikuwa zikitolewa kwa madhumuni ya kuharakisha miradi ya maendeleo majimbo ya Visiwa vya Unguja na Pemba.

Imedaiwa katika ripoti hiyo kuwa Sh. milioni 20 kila jimbo ziliingizwa, lakini majimbo 34 kati ya 50 fedha hizo zilikuwa hazijatumika mpaka ukaguzi unakamilika huku wananchi wakiendelea kuandamwa na kero mbalimbali katika majimbo yao.

Ripoti hiyo imesema kuna miradi imeshindwa kuendelezwa na kukamilika licha ya fedha kutolewa na vifaa kununuliwa katika majimbo mbalimbali ya Unguja na Pemba, lakini kuna baadhi ya majimbo yamefanya vizuri katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Hata hivyo, akijibu hoja ya BLW baada ya kuchangiwa kwa ripoti hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud, alisema serikali itawataka wajumbe wote walioguswa katika matumizi mabaya kutoa maelezo kabla ya kuchukua hatua za kisheria.

Alisema sheria inambana kila mtu anayetumia fedha za umma kinyume cha taratibu na kwamba serikali itahakikisha ripoti hiyo inafanyiwa kazi ili malengo ya kuanzishwa kwa mfuko huo yaendelee kuonekana na kuleta tija kwa wananchi wa Zanzibar.

Alisema fedha ambazo hazijatumika katika majimbo tangu kuingizwa, zitarejeshwa serikalini, huku akieleza kuwa ni jambo la kushagaza mwakilishi kutochukua fedha za maendeleo ya jimbo wakati wananchi wake wanakabiliwa na kero.

Chanzo: Nipashe

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s