Wanasiasa waisaidie Z’bar inufaike na mafuta, gesi

Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira –  Mhe. Salama Aboud Talib
Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira – Mhe. Salama Aboud Talib

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) hivi karibuni imesema kuwa mafuta na gesi yapo katika visiwa vya Unguja na Pemba. Waziri wa Maji na Nishati wa Zanzibar, Salama Abud Talib alisema kuwa mafuta na gesi vipo Zanzibar na Wizara yake ipo katika maandalizi ya kuandaa sera na kuiwasilisha katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar (BLW).

Mafuta na gesi ni bidhaa muhimu ambayo nchi inayobarikiwa kuwa nayo inakuwa katika nafasi nzuri ya kupiga hatua ya maendeleo kiuchumi na maisha ya wananchi wake.

Suala la mafuta Zanzibar lilianza muda mrefu kwani utafiti wake ulianza tangu wakati wa ukoloni na ushahidi upo hadi sasa kwa kuwapo na mashimo ambayo yalichimbwa kutafuta mafuta katika sehemu mbalimbali za Unguja na Pemba

Hata hivyo, kwa upande mwingine suala hilo limekuwa katika ajenda ya kisiasa kwani katika miaka ya karibuni aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) alipotamka kuwa Zanzibar ina mafuta alipingwa vikali.

Chama cha Mapinduzi (CCM) kinachotawala Zanzibar kilimpinga kwenye mikutano ya hadhara hata katika Uchaguzi Mkuu uliopita uliofanyika Oktoba 25, mwaka 2015 wakati wa kampeni makada wa chama hicho walionyesha kumshangaa Maalim Seif juu ya suala hilo.

Katika mkutano mmoja wa kampeni kiongozi mmoja wa CCM alishangaa kuona picha ya Maalim Seif kwenye gazeti akiwa anatembelea sehemu moja ambayo ilikuwa imechimbwa shimo la kutafuta mafuta.

Licha ya hali hiyo kuna wakati mafuta iliwaunganisha Wazanzibari wote na kuwa wamoja wakidai kwamba suala hilo lisiwe la Muungano. Hata wabunge na wajumbe wa BLW kutoka CCM ambao ni nadra kupinga suala lolote la Muungano waliungana na wenzao kutoka CUF wakitaka mafuta isiwe mali ya Muungano, bali iwe ni sehemu ya upande yaliyopatikana.

Kwa sasa suala hilo linazua maswali kwa wanasiasa kwani wapo wanaosema kwamba limeshakubaliwa kuwa siyo la Muungano na wako wanaosema kwamba haijawa bayana na wazi kwamba mafuta si mali ya Muungano.

Achilia mbali yote hayo mafuta na gesi yanabaki kuwa rasilimali kubwa ambayo kama nchi itavipata na kuyatumia vyema ina nafasi ya kupiga hatua kubwa ya maendeleo na kuingia katika kundi la nchi tajiri.

Sera ya mafuta iwe nzuri Msingi wa kwanza wa jambo lolote katika maisha ya sasa ni kuwekewa sera nzuri ambayo itawezesha utekelezaji wa jambo hilo kufanywa kwa ufanisi na weledi wa hali ya juu.

Kwa hiyo, SMZ ina kazi kubwa mbele yake ya kuhakikisha kwamba inaanda sera za mafuta na gesi ambazo ni nzuri na zinatoa fursa kwa wawekezaji na wananchi kufaidika na rasilimali hizo.

Sera zinazotakiwa zisiwakwaze wawekezaji na kuwanyima fursa ya kuingia katika uwekezaji wa rasilimali hizo, lakini hapana budi wakati huohuo ziwe zinanufaisha Taifa kwa faida ya wananchi wake.

Ni jambo la msingi kwa sera zitakazotengenezwa kwa namna yoyote ile zihakikishe kuwa wananchi wanafaidika na rasilimali hiyo kwa maendeleo yao na kawapunguzia ugumu wa maisha uanaowakabili.

Mchakato ufanywe haraka Saual la Zanzibar kuwa na mafuta ni suala la muda mrefu na sasa limethibitishwa rasmi na Serikali kwa hiyo kuna haja ya kufanywa haraka ili uchimbaji wake uanze mara moja.

Pamoja na kwamba kuna baadhi ya Wazanzibari bado hawaamini kuwa mafuta na gesi vipo Zanzibar kwani wanadai kuwa kama vipo visingeachwa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Sita Zanzibar, Dk Amani Abeid Karume.

Hata hivyo, bila shaka kwa vile Serikali imetamka rasmi kuwa mafuta na gesi vipo Unguja na Pemba hakuna tena suala la ubishi na lililobaki ni kwa Serikali kuchukua hatua ili rasilimali hizo zianze kuwafaidisha Wazanzibari.

Dunia ya sasa mambo yanaenda kwa kasi kwa hiyo hakuna wakati wa kupoteza kwa Serikali ya Zanzibar bali ni kuanza mchakato wa kuyapata mafuta na gesi ili yaongeze kasi ya maendeleo ya Zanzibar.

Vitaleta maendeleo hapana shaka yoyote kupatikana kwa mafuta na gesi Zanzibar kama kutakuwa na mipango mizuri kutaongeza maendeleo ya uchumi katika visiwa hivyo vilivyokuwa vinategemea zao la Karafuu na Utalii katika uchumi wake.

Kwa hiyo, mafuta na gesi yatapanua uchumi wa Zanzibar na ina nafasi kubwa ya kuwa nchi yenye uchumi wa kati baada ya miaka michache ya upatikanaji rasilimali hizo muhimu katika matumizi ya mwanadamu duniani.

Mafuta na gesi ni utajiri uliodhahiri ambao unahitaji mipango kidogo ili kulinufaisha Taifa na kuinua hali ya maisha ya wananchi wake ambao katika nchi nyingi za dunia ya tatu wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha.

Nchi kadhaa duniani zenye utajiri wa mafuta zimepiga hatua kubwa ya maendeleo na wananchi wake wanaishi katika maisha ya raha yasiyo na usumbufu wowote.

Bila umakini tutakwama Pamoja na kwamba mafuta na gesi huleta utajiri katika nchi, lakini ikikosekana mipango madhubuti utajiri huyeyuka na badala yake umaskini hujichimbia miongoni mwa wananchi.

Kuna nchi kadhaa duniani licha ya utajiri wa mafuta wananchi wake hawana maendeleo yoyote na wanaishi katika umaskini uliokithiri na wa kutupwa na faida ya mafuta hayo inakwenda kwa wageni ambao wamewekeza.

Wananchi walio wengi hawafaidiki na rasilimali hizo na badala yake wanaambulia athari za uharibifu wa hali ya hewa unaosababishwa na uchimbaji wa mafuta na gesi na wao wanabaki katika umaskini uliokithiri.

Bila kuwapo mipango mizuri mafuta na gesi yanaweza kuingiza nchi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa kila mmoja naye kupigania kufaidi keki ya rasilimali hizo.

Kwa hiyo, ni muhimu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar isiangalie upande mmoja tu kwa faida ya mafuta na gesi bali ichukue hatua za kuzuia athari ambazo zinaweza kutokea nchini kutokana na rasilimali hizo.

Hayo ni mambo muhimu ya kuzingatia kabla ya kuingia mikataba na kampuni mbalimbali duniani za uchimbaji wa mafuta na gesi ili kuhakikisha kwamba amani na utulivu vinaendelea kudumishwa hata baada ya kuja kwa rasilimali hizo.

Ni dhahiri kwamba kama hakutakuwa na mipango mizuri mafuta na gesi vinaweza visilete utajiri na maendeleo na badala yake vikaleta umasikini na vita na athari kubwa ya mazingira.

Kwa hiyo, mafuta na gesi ni utajiri uliowazi, lakini kama nchi haikuwa makini badala ya kuleta neema na faraja kwa wananchi inakuwa kama laana juu yao na kujuta kwa nini yamegunduliwa katika nchi yao.

Zanzibar inaelekea kupata utajiri wa mafuta na gesi, lakini inapaswa kuwa na hadhari kubwa ili kuhakikisha kwamba rasilimali hizo zinainua maisha ya wananchi badala ya kuyadidimiza zaidi.

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s