Lipumba: Magufuli chanzo uhaba wa sukari

Aliyekuwa mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba
Aliyekuwa mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema Rais John Magufuli ndiye aliyesababisha sukari kuadimika, baada ya kuzuia vibali vya kuagiza bidhaa hiyo nje ya nchi.

Alisema takwimu za hali ya sukari nchini zilizopo katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi mwaka 2016/17 iliyosomwa na waziri wake, Mwigulu Nchemba zinaonyesha nchi ina uhaba wa sukari na zinapingana na maelezo ya Rais kwamba nchi ina sukari ya kutosha.

Profesa huyo aliyejikita katika masuala ya uchumi, katika mkutano wake na wanahabari jana aliouita ‘sakata la sukari nchini’, aliponda operesheni ya kuwakamata wafanyabiashara walioficha sukari, kwamba haiwezi kumaliza tatizo lililopo kwa sababu mahitaji ya sukari nchini ni tani 420,000 wakati inayokamatwa haifiki hata tani 10,000.

“Rais anapaswa kujua jinsi uchumi wa soko unavyokwenda. Nilivutiwa sana na hotuba yake ya kufungua Bunge ila utendaji na maamuzi yake ya sera kwenye majukwaa ya siasa vinanipa wasiwasi mkubwa,”

alisema Profesa Lipumba ambaye amewahi kuwa mshauri wa Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi katika masuala ya uchumi. Februari 18, mwaka huu katika hotuba yake ya kuwashukuru wasanii, wanahabari na makundi mbalimbali yaliyoshiriki kwenye kampeni za urais CCM, Rais alipiga marufuku uagizaji wa sukari kutoka nje na kumuagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kusimamia utoaji wa vibali vya kuagiza bidhaa hiyo ambayo sasa imepanda bei maradufu, kutoka Sh1,800 kwa kilo hadi Sh3,500.

Hata hivyo, Aprili 27 mwaka huu wakati akihitimisha mjadala wa bajeti ya ofisi yake, Majaliwa alieleza uamuzi wa Serikali kuagiza tani 100,000 za sukari nje ya nchi kutokana na bidhaa hiyo kuadimika nchini, huku akifafanua kuwa mpaka wakati huo katika maghala kulikuwa na tani 37,000 tu.

Juzi, Majaliwa alisema Serikali imeagiza tani 70,000. Siku moja baadaye Rais aliapa kupambana na wafanyabiashara wa sukari wasiozidi 10, waliohodhi bidhaa hiyo na kutaka wakamatwe kwa maelezo kuwa wameficha kwa makusudi ili wananchi wahangaike.

Profesa Lipumba alisema Rais Magufuli alitoa tamko la kusitisha uingizwaji wa sukari bila kushauriana na watendaji wa Bodi ya Sukari na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na kumtaka kuzipa fursa taasisi na wizara husika kutekeleza majukumu yao, badala ya kufanya maamuzi katika majukwaa ya kisiasa.

 Alibainisha kuwa bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvivi, imeelezwa kuwa mahitaji ya sukari nchini ni tani 420,000 kwa matumizi ya kawaida na tani 170,000 kwa matumizi ya viwandani.

“Hotuba inaonyesha mpaka kufikia Machi mwaka huu uzalishaji ulifikia tani 290,112 ikilinganishwa na matarajio ya tani 288,802, kwamba viwanda vilivyopo nchini havizalishi sukari ya matumizi ya viwandani, hivyo sukari iliyotarajiwa kuagizwa kutoka nje ni tani 131,198 kwa matumizi ya kawaida na tani 170,000 kwa matumizi ya viwandani,” alisema.

“Jumla ni tani 301,198. Rais katika ule mkutano wake alisema viwanda vya ndani vinashindwa kuuza sukari kwa sababu ya sukari inayoagizwa nje. Hivi sasa viwanda vinaeleza havina sukari na uzalishaji utaanza Julai, ila Rais anasisitiza sukari imefichwa,” alihoji.

Profesa Lipumba ambaye amewahi kuwa mshauri wa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni katika masuala ya uchumi, alisema kitabu cha bajeti kinaeleza hadi Machi 29, mwaka huu, wazalishaji walikuwa na tani 17,996 huku wasambazaji wakubwa na wa kati wakiwa na tani 14,652 na kufanya jumla ya sukari yote iliyokuwapo kuwa tani 32,652.

“Ikiwa matumizi ni tani 420,000 kwa mwaka maana yake kila mwezi tunatumia tani 35,000 na msimu wa uzalishaji sukari viwandani umemalizika viwanda vimefungwa. Hiyo iliyofichwa hata tani 10,000 haifiki, sasa kwa hali hii nani wa kulaumiwa,” alihoji Lipumba.

Alisema hata Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ilimuomba Rais kuruhusu kutoa vibali vya kuagiza sukari ili kukabiliana na upungufu wa bidhaa hiyo, lakini ombi hilo liligonga mwamba. “Rais aombe ushauri kuhusu changamoto na taratibu za kujenga uchumi wa soko shirikishi.

Uzoefu wa Rais Benjamin (Mkapa­Rais wa Awamu ya Tatu) wa kujenga utawala wa Serikali utamsaidia,” alisema profesa huyo. Huku akiponda kitendo cha Serikali kupanga bei elekezi ya sukari kuwa Sh1,800, wakati si kazi yake na ikiwa haijulikani bei hiyo ni ya rejareja, jumla au kiwandani, Profesa Lipumba alisema wakuu wa mikoa, wilaya na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), wanafanya msako wa sukari iliyofichwa bila kuelewa uhalisia wa kutoweka kwa bidhaa hiyo.

Mchumi huyo alisema sheria haimpi mamlaka Rais au Serikali kupanga bei ya sukari, na kusisitiza kuwa vitisho dhidi ya wafanyabiashara havijengi taswira ya Serikali kuithamini na kuishawishi sekta binafsi kuwekeza nchini. Alisema vitisho na ubabe wa Rais vinaweza kuwaogopesha mawaziri na watendaji serikalini wasimueleze bayana, hali halisi ya masuala mbalimbali yanayoendelea nchini.

“Ubabe huu unanikumbusha andiko la mwana habari maarufu baada ya uteuzi wa Rais Magufuli kuwa mgombea urais wa CCM maana aliuliza ‘nani atakayemfunga gavana Rais Magufuli’?” alisema.

Makonda ataka vibali vya sukari

Wakati huohuo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameiagiza Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), kupitia nyaraka za uingizaji wa tani 5,800 za sukari za Kampuni ya Mohamed Enterprises.

Agizo hilo linafuatia Makonda kubaini sukari ya viwandani katika ghala la kampuni hiyo, lililopo maeneo ya Kiwalani, Manispa ya Ilala juzi.

“Nahitaji kujua sukari hii zaidi ya mifuko 100,000 imekuja lini hapa. Kwa sababu hii kampuni ina kibali cha kuibadilisha sukari ya viwandani kuwa ya matumizi ya nyumbani na ukizingatia huko nje kuna uhaba wa bidhaa hii,” alisema Makonda. Kwa mujibu wa Makonda, aliitaka TFDA, kumpa mrejesho ndani saa 24, ili taratibu zingine zifuate.

Mwenyekiti wa kampuni hiyo, Gullam Dewji alisema uwapo wa idadi ya sukari umetokana na kufungwa kwa kiwanda cha soda kwa muda, ambacho hata hivyo kimeanza kufanya kazi hivi karibuni.

“Ni kweli tunabadilisha sukari kwenda katika matumizi ya kawaida, lakini hizi tani zilikuwa maalumu kwa ajili ya kiwanda cha soda. Kuhusu nyaraka kesho tutawapatia,” alisema Dewji.

DC Babati atoa siku tatu

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Babati, Crispin Meela alifanya ziara ya ghafla kwenye kiwanda cha sukari cha Manyara Sugar, na kutoa siku tatu apate maelezo ya kitendo cha tani 181.3 za sukari kuhifadhiwa ghalani kwa madai ipo kwenye hatua za utengenezwaji.

Meela alifunga ghala hilo na kuondoka na funguo hadi mkurugenzi wa kiwanda hicho atakapokamilisha maelezo ya kuweka sukari ndani bila sababu za msingi.

“Maeneo ya viwanda ni mali ya wananchi na waliwapatia ninyi ili waweze kufaidika na kazi mnazozifanya ikiwamo kiwanda cha sukari, sasa leo mnafungia sukari ndani halafu wao wanapata taabu ya kununua sukari Sh 3,000 kwa kilo, huu si uungwana,” alisema.

Alisema ataagiza TFDA kuipima sukari hiyo ili wabaini kama inafaa kwa matumizi ya binadamu, ili isambazwe kwenye mkoa wa Manyara kwa bei elekezi. Msimamizi wa Manyara Sugar company Ltd, Sureshi Hiran alisema sukari hiyo iliyozalishwa Aprili ni daraja la tatu na bado ipo katika hatua ya mchakato wa utengenezaji.

“Sukari hii tuliiweka hapa kwa kuwa bado haina ubora wa kutosha, ni ya daraja la tatu ili iwe na ubora tunasubiri tuvune miwa ili tuchanganye na daraja la kwanza iwe sukari kamili kwa ajili ya kuuzwa, lakini tatizo msimu wa kuvuna miwa bado,” alisema Hiran.

Hata hivyo, Meela alipinga maelezo hayo akidai yanaashiria uhujumu wa uchumi. Wakati huo uo, hofu imetawala kwa wafanyabiashara wa sukari katika maduka ya jumla, baada ya wenzao kukamatwa wakidaiwa kununua bidhaa hiyo kutoka kwa mfanyabiashara Harun Zacharia, ambaye amekuwa akidaiwa kuficha sukari.

Hivi karibuni Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) ilitangaza kumshikilia mfanyabiashara huyo kwa tuhuma za kuficha sukari, ikiahidi kumfungulia kesi ya kuhujumu uchumi.

Baadhi ya wafanyabishara katika eneo la Manzese, walidai hawatamani kuuza tena sukari kwenye maduka yao kwa sasa kutokana na usumbufu ambao wameshuhudia ukiwakumba wenzao kadhaa. “

Ninachokiona mimi ni kama vile wito wa Rais Magufuli wa umeeleweka visivyo, kwa sababu inashangaza mfanyabishara anakamatwa kwa kuwa na sukari ambayo amenunua kihalali, imetushtua na kutuogopesha,” alisema Festo Tesha.

Mary Barnaba ambaye amekutwa na amri ya kuzuiliwa kuuza sukari yake, alisema alifika Mkuu wa Wilaya wa Kinondoni Ally Hapi akiwa na maofisa wa polisi na kuwataka wasiuze bidhaa hiyo hadi upelelezi utakapokamilika.

Chanzo: Mwananchi

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s